HOJA: MAMBO MAKUU MATATU YA KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA MAOMBI (2)

Jumatatu iliyopita niliwasilisha mada mpya (soma hapa) yenye ujumbe wa mambo makuu matatu ambayo nilibaini kwamba yanastahili kupewa kipaumbele wakati tunapowasiliana na Mungu katika sala kama kichwa cha habari kinavyosema hapa juu. Aidha, tulifanikiwa kupitia mambo mawi­­­li na kubaki moja tu. Mambo mawili tuliyojifunza yalikuwa ni “Kutafuta kibali cha Mungu” na la pili lilikuwa ni “kupokea hekima ya Mungu”. Leo tunachambua jambo la tatu ambalo ni “kuuona utukufu wa Mungu”:

Askofu Sylvester Gamanywa

“Kuuona utukufu wa Mungu”­­

Mpendwa msikilizaji, leo tunaendelea na uchambuzi kuhusu kipengele cha tatu kinachohusu “Kuuona utukufu wa Mungu” Vipengele viwili tulivyokwisha kuvipitia cha kwanza kilikuwa “Kupata kibali mbele za Mungu” na cha pili ni “Kupokea hekima ya Mungu”. Leo tunamalizia kipengele cha “Kuuona utukufu wa Mungu”

Kwa tafsri nyepesi ya msamiati wa “utukufu wa Mungu” maana yake ni “uwepo wa Mungu”, “Utendaji wa Mungu unaoweza kuonekana kwa macho”. Japokuwa Mungu Baba haonekani waziwazi kwa sura tukamwona kwa macho ya nyama, mara nyingi amejidhirisha kwa njia nyingi ili kujitambulisha kwamba yupo. Ni kila njia aliyoitumia kujidhihirisha, binadamu wa kizazi cha wakato huo walimtambua na kumtukuza kwa sababu “waliuona utukufu wake”!

Utukufu wa Mungu unawakilisha uwepo na utendaji wa Mungu ukionesha uwezo na mamlaka yake katika ulimwengu wa asili. Ujumbe wa leo unaotuongoza unapatika kwa YH 11:40

“Yesu akamwambia, Mimi sikukuambia ya kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?” (YN. 11:40)

Maneno haya Yesu alimwambia Mariamu wakati wa kifo cha Lazaro aliyekuwa amekaa kaburi ni siku nne. Na Yesu alipokuja msibani hapo, akina Martha na Mariamu walimwambia kama Yesu angeliwahi kufika wakati Lazaro anaumwa na hajafa, angelimuepusha huyo kama yao na kifo. Ni kutokana na Mazunguzo hayo, Yesu alimuuliza swali gumu: sikukwambia ya kuwa ukiamini “Utauona utukufu wa Mungu”?

Tendo la Yesu kumfufua Lazaro aliyekuwa kaburini siku nne, liliudhihirisha utukufu/uwepo/utendaji wa Mungu uzidio uwezo wa kibinadamu. Wote waliokuwepo  msibani walijua kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu. Unajua kwamba, tukio/tendo moja la Mungu linatosha kubadili “mitazamo hasi” dhidi ya Mungu na kuleta mabadiliko makubwa kwa maisha ya watu katika muda mfupi sana

Msomaji mpendwa, tunaweza kuomba dua nzito kwa Mungu, na kupokea hekima ya Mungu kwa mambo magumu, lakini, hakuna jambo lenye faraja na kutia hamasa kama wakati Mungu mwenyewe anapoamua kujidhihirisha waziwazi kwa kufanya mambo ambayo kila binadamu akiyaona anatambua huyu ni Mungu, na si mkono wa binadamu.

Sehemu ya ushuhuda wangu binafsi
kuhusu “kuuona utukufu wa Mungu”

Kuisikia sauti ya Mungu kwa mara ya kwanza. Nilikuwa na muda mfupi baada ya kujazwa Roho Mtakatifu. Nakumbuka nilikuwa bado naishi katika mji mdogo wa Same, majira ya saa 4.00 asubuni nikiwa nimeketi kwenye kituo cha mabasi. Siku nasafiri bali ilitokea tu kwamba nikajipumzisha mahali hapo nikitazama wasafiri wanaopanda mabasi ya kwenda Mjini Moshi na wengine wakiteremka.
Nikiwa nimetulia, mara nikahisi “sauti ndogo ya utulivu” ikisema name kutokea ndani ya roho yangu. Ni sauti niliyoweza kuitambua na kuitofautisha na “mawazo ya kawaida ya moyo wangu.” Kwa kawaida “mawazo ya kibinadamu moyoni yanapojifunua hutambulika kuwa ni mawazo yangu kwa sababu yanabeba utambulisho wangu. Natambua ni “mimi ninayewaza” na sio “nafsi nyingine inayowasiliana nami” Ile “Ile sauti ndogo ya utulivu” kutokea rohoni mwangu niliitambua kwamba “sio mawazo yangu mwenyewe” kwa sababu ilianza kwa kuniuliza swali ikisema:
“Sylvester! Unakumbuka siku ile ulipokuwa msituni ukiwa kwenye shida ngumu ukaniomba nikuokoe kutoka huko, na ukaniapia kwamba nikutoa huko, utanitumikia?” Duuh! 
Kwanza nilishtuka kwa swali hili. Lakini ghafla mara hiyo hiyo mawazo yangu sasa yakavuta kumbukumbu nyakati za nyuma kabisa, wakati bado sijaokoka. Enzi hizo nilijikuta katika mazingira magumu, tena maporini kwenye misitu ya Upareni,  nikiwa porini kwenye mazingira magumu ambapo nilikuwa nimekwama vibaya sana kimaisha. 
Niko ugenini na sina njia wala msaada wa kurudi nyumbani nilikotoka. Wenyeji wangu nao wakawa wananibeza wakisema, siwezi kurudi tena nilikotoka kwa sababu walikuwepo “wanyika” (watoka-mbali) ambao walifika upareni kwao wakashindwa kurejea makwao na wakajikuta wamelowea na kuzeekea huko. Nafsi yangu ilikataa kabisa nikijiapiza lazima miye nitatoka huko na kurudi nyumba! Ni katika majira hayo ndipo nilijikutana nikiomba Mungu nisiyemjua na kumwambia:

 “kama kweli we Mungu upo, na unanisikia, ninaweka nadhiri yangu ukiweza kunitoa katika shida hii nikarudi nyumba nilikotoka; hakina huko niendako kwanza nitatoa sadaka ya shukrani; pili nitatoa msaada kwa maskini; na tatu nitakutumikia.”  Kwa kadiri ya kumbukumbu zangu hii ilikuwa ni sala yangu ya kwanza kwa Mungu tangu kuzaliwa kwangu!
Ghafla nilijikuta nikiitikia ile “sauti ndogo ya utulivu” kutoka moyoni mwangu “Naam Bwana!”; na hasa baada ya kukumbushwa nadhiri yangu ya siku ile, na jinsi nilivyosali sala ngumu, mpaka nikafunga fundo la “mkongwe mwitu” nikimwapia Mungu kuwa nitamtumikia kama akiniokoa kutoka kwenye mazingira yale. Kisha ndipo nikaisikia sauti ile ile ikiendelea kusema nami waziwazi, lakini kutokea ndani yangu:
“Nilisikia toba yako, nikajibu sala yako. Nilikuwezesha kutoka kwenye mazingira yale magumu ukarudi mjini toka maporini. Kwa kuwa ulikuwa unaishi katika dhambi usingeweza kunitumikia katika maisha ya dhambi; kwa hiyo nikaamua kukuokoa kutoka dhambini, na nimekujaza Roho wangu, na sasa ni zamu yako kutimiza ahadi yako, ya kunitumikia.” Mwisho wa sauti ile ndogo ya utulivu.

Itaendelea toleo lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.