HOJA: MAMBO MAKUU MATATU YA KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA MAOMBI (Sehemu ya mwisho)

Jumapili iliyopita (soma hapa) tuliendelea na mada yetu ambapo tulianza uchambuzi wa kipengele cha 3 za ujumbe kinachosema kuhusu “kuuona utukufu wa Mungu”. Humo nilifafanua maana ya kipengele na kisha nikaanza kusimulia sehemu ya ushuhuda wangu binafsi, sehemu ambayo 
inaendelea katika toleo hili pia”

Askofu Sylvester Gamanywa

Mwendeleo wa sehemu
ya ushuhuda wangu binafsi

Baada ya kuisikia sauti hii, nilisisimka pale mahali nilipokuwa nimketi na kuamka kisha nikaondoka huku nikiwa natafakari ujumbe ule niliopokea. Kwa mara yangu ya kwanza, niliweza kutambua bila shaka kwamba hiyo ilikuwa ni sauti ya Roho Mtakatifu akiwasilisha ujumbe wa Yesu Kristo kwangu. Isingeliwezekana kuwa ni mawazo yangu kwa sababu naifahamu sauti ya mawazo yangu. Pia naliikumbuka siku ile niliyoweka nadhiri yangu mbele za Mungu kule porini.
 
Ni kweli, Mungu alisikia dua yangu na alinitoa kule porini kwa miujiza yake. Ni kweli baada ya kutoka huko nilijifanya kutoa sadaka kwa maskini na kutoa shukrani kwenye ibada ya dini. Lakini baada ya hapo sikukumbuka suala la “kiapo changu cha kumtumikia Mungu”. Niliendelea na maisha yangu ya dhambi kama kawaida na kusahau yote yalikuwa yamekumba wakati uliopita.
Hata haikuchukua miezi zaidi ya mitatu, nilikutana na Injili ya wokovu na kuamua kutubu na kumpokea Kristo kuwa Mwokozi wangu binafsi. Suala la wokovu wangu na lenyewe lilikuwa na kishindo chake katika mji ndogo niliokuwa ninaishi. Hilo sina muda wa kulishuhudia mahali hapa sasa hivi.

Lakini baada ya kuokoka hakikuchukua muda mrefu nilifundishwa habari za kumpokea Roho Mtakatifu na nikashuhudia tukio jingine la kishindo cha kiroho katika maisha yangu. Hilo ni tukio la kumpokea Roho Mtakatifu. Nalo hilo lina masimulizi yake pia. Hoja yangu ya sasa ni kukupa picha ufupi yaliyojiri tangu siku nilipoweka nadhiri yangu mbele za Mungu na jinsi Mungu alivyoniokoa kwenye mazingira magumu, lakini anaenda mbele zaidi akaniokoa katika kongwa la dhambi.
Na sasa baada ya kuokolewa na kujazwa Roho, ndipo Mungu anazungumuza rasmi kwa mara ya kwanza akinikumbusha mahali aliponitoa na kiapo nilichoweka na kwamba yeye amefanya sehemu yake na kwamba sasa ilikuwa ni wajibu wangu “kutimiza nadhiri yangu kwake”.
Haya ushuhuda huu una uhusiano gani na mada hii katika kipengele cha “kuuona utukufu wa Mungu”? Uhusiano upo tena mkubwa sana. Siwezi kukufundisha habari za “kuuona utukufu wa Mungu” kama mimi binafsi ningekuwa sijawa kuuona katika dhahiri katika maisha yangu.
Pili, “kuuona utukufu wa Mungu” hauishii kwa mtu binafsi anayehusika, bali na hata wengine wanaomzunguka na wanaomfahamu. Nilisema kwamba, “kuuona utukufu wa Mungu” ni “kuyaona kwa dhahiri matendo ya Mungu” ambayo hushuhudiwa kwa na wengine katika mahali husika.
Mathalan, Tukio la kuokoka kwangu licha ya kwamba “niliuona utukufu wa Mungu” kibinafsi, ambao ni “kuondolewa  madhambi” yangu yote niliyokuwa nimewahi kuyafanya huko nyuma; ndugu, jamaa na marafiki zangu wote, walishuhudia “badiliko la kitabia” ambalo ni matokeo ya kuokoka kwa nguvu za Bwana Yesu. Kana kwamba hii haikutosha, hata tukio la “ujazo wa Roho Mtakatifu” liliponitukia halikuishia kuwa siri yangu binafsi, bali lilikuwa na kishindo kama kile kile cha siku ya Pentekoste ambapo maelfu ya watu walikusanyika ili kushuhudia kilichowatokea mitume wa Yesu Kristo.Tumtafute Mungu ili sisi kujua
tumfanyie nini na si yeye atufanyie nini

Kumbuka kwamba kiini cha mada ni “mambo yanayostahili kupewa kipaumbe katika maombi yetu kwa Mungu”. Yaliyotangulia mawili ambayo ni “kupata kibali cha Mungu” na “kupokea hekima ya Mungu” yote yalitupa picha ya umuhimu wake. Hili la kuuona utukufu wa Mungu ndilo linapiga muhuri wa yale yaliyotangulia, au kuyathibisha yale yaliyotangulia.

Japokuwa ninalosema hapa si jambo geni kwangu, na wala si ufunuo mpya kabisa kwangu, lakini najisikia kusema kwamba, nimefunuliwa kwa upya kuhusu hoja hii. Hoya ya kumwomba Mungu atuonyeshe anataka tumfanyie nini, badala ya sisi kung’ang’ania kumtaka Mungu atutendee nini.
Kuna siri gani katika hoja hii? Kuna siri kubwa kupita kawaida. Laiti wacha Mungu wote tungeliupata ufunuo huu.! Latini kila binandamu aliye hai angeliupata ufunuo huu.  Dunia ingebadilika na kuvunja rekodi ya mabadiliko. Lakini tumefungwa akili zetu hatuoni yatupasayo kuomba mbele za Mungu. Naweza kusema kwamba, ni Ibilisi tu ndiye amepofusha fikira zetu, kwa sababu ya ubinafsi wetu, tunazidi “Kuzunguka kwenye jangwa la maombi yasiyojibiwa” kwa sababu tu “hatujui kuomba jinsi itupasavyo”!

Ninasikitika sana kwamba, hata sisi watumishi tumechangia kwa kiasi kikubwa kuwapotosha wafuasi kwa kuwafanya waendelee kujenga mtazamo wa kumwomba Mungu mambo yao binafsi tu badala ya kuwaelekeza kumwomba Mungu awafunulie anawataka wamfanyie nini Mungu.

Mara nyingi tumeweka mkazo zaidi kuwafundisha watu wamtolee Mungu fedha na mali zao kwa ajili ya kazi yake. Ingawa hili nalo ni mapenzi ya Mungu wafuasi kulijua, lakini tulipaswa kuwaekeza wajifunze kumtafuta Mungu ili awaambie anawataka wamfanyie nini, na sio tu kumtolea fedha na mali. Sisi wote ni mashahidi kwamba, wako watu wanamtolea Mungu lakini hawaoni matokeo ya kutoa kwao kwa sababu hata katika kutoa kwenyewe hawatoi kwa njia iliyo sahihi mbele za Mungu. Tunashindwa kuwaambia kwamba Mungu hana shida na fedha na mali zao, bali anataka kujenga mahusiano ya kibinafsi kati yake na wao, na kwamba matoleo ni matokeo.

Ninatamani Mungu anipe fursa nyingine tena, upako mwingine tena, nguvu nyingine tena, ili nipate kibali mbele zake tena, nipokee hekima yake tena kwa ajili ya kuwahamasisha, kuwaelemisha, kuwarejesha kiimani watu katika kujitoa wao wenyewe WAMTAFUTE MUNGU ILI KUJUA KUTOKA ANAWATAKA WAMFANYIE NINI NA SIO YEYE AWAFANYIE NINI!
MwishoShare on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.