HOJA: MAMBO MATATU YA KUPEWA KIPAUMBELE KATIKA MAOMBI - ASKOFU GAMANYWA

Mambo makuu matatu ya
kupewa kipaumbele katika maombi

 
Wakati tunapoadhimisha kifo na kufufuka kwa Bwana Yesu, nimeona leo nikuwasilishe ufunuo ambao nimeupata wa kutusaidia kuboresha imani zetu na hususan tunapokuwa katika kumtafuta Mungu kwa njia ya maombi. Mambo haya matatu muhimu ni “kibali cha Mungu”, pili, “Hekima ya Mungu” na tatu, “kuuona utukufu wa Mungu”. Mambo haya nimewashirikisha waombaji wengu ambao tunakutana kwenye kipindi cha TUMAKE PAMOJA kila saa kumi na moja alfajiri kupitia WAPO RADIO.


 

Utangulizi

 

Mara nyingi tumekuwa na juhudi katika kumwomba Mungu, na hata kuwa na mifungo mingi kwa ajili ya kuutafuta uso wa Mungu. Lakini sisi wote ni mashahidi kwamba, matokeo ya majibu ya maombi ni kidogo kuliko vile tunavyokuwa tumejitoa wenyewe mbele za  Mungu. Wengi tunabaki kuamini kwamba Mungu amesikia na kupokea sala zetu, na kwamba atajibu kwa wakati wake. Ni kweli. Lakini si mara zote tunapoomba kwa ni kanuni ya Mungu kunyamaza kimya na kutuacha kwenye giza tusijue mapenzi yake ni nini kutokana na yale tuliyomwomba.

Kutokana na changamoto za kuomba tusipate majibu kama tulivyotarajia, na kwa wakati tuliotarajia kupata majibu, ndipo mimi mwenyewe kwa neema yake Bwana aliamua kushusha ujumbe huu, unaohusu vipaumbele 3 muhimu vya kutuongoza katika maombi yetu.  

 
Kutafuta kwanza kupata

“kibali mbele za Mungu”

 

Jambo la kwanza ambalo nataka kuliweka bayana ni hili; “maombi” ni “mawasiliano kati yetu na Mungu”. Na mawasiliano hufanyika pale ambapo tayari kuna “mahusiano mazuri”. Kuomba si shughuli ambayo mtu anaifanya kama kutimiza wajibu wa kidini tu. Ni msukumo wa kiroho ndani ya mtu ambaye tayari ana mahusiano na Mungu na anawajibika kuyaboresha kwa mawasiliano, ambayo tunaita “Maombi.”

 

Katika msingi huu, tunapokwenda mbele za Mungu kuomba, tujue tunakwenda kwenye mawasiliano na Mungu, na kwa hiyo lazima tujue tunakwenda kuzungumuza nini, na tuna picha gani kuhusu mtazamo wake juu ya mambo yale tunayokenda kuongea naye.

 

Mtunga Zaburi, ambaye alikuwa mzoefu wa kuutafuta uso wa Mungu, alifunuliwa moyoni kwamba, kabla ya kuwasiliana na Mungu kuhusu mambo yake binafsi, ni muhimu atafute msaada wa Mungu katika mambo ambayo tunakwenda kuyasoma hapa chini:

 

“Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.” (ZAB. 19:14)

 

Hapa, mtunga Zaburi alitafakari sana akitafuta na kujenga mahusiano ya karibu na Mungu. Kwa uzoefu wake binafsi aliokuwa nao aligundua kwamba, vitu viwili vinavyoweza kuimarisha mahusiano yake na Mungu, ni “maneno ya kinywa chake” na pili, “Mawazo ya moyo wake”.

 

Kama unavyojua mchakato wa vitu hivi viwili vinategemeana. Huwezi kusema neno kabla kuliwaza kama wazo. Japokuwa si kila wazo lazima lisemwe, lakini likibaki moyoni maana yake limekubalika nafsini mwako. Kwa hiyo wazo hilo Mungu analiona hataka hujalisema, ili mradi tu umelihifadhi moyo wako. Kama ni wazo baya, linaunajisi moyo wako!

 

Ndiyo maana mtunga zaburi akaona ilia pate kufanikiwa, na kufanikishwa na Mungu, lazima maneno ya kinywa chake, pamoja na mawazo yaliyomo moyoni mwake, vyote vipate kibali, vikubalike, vionekane vinastahili na kulinagana na mapenzi ya Mungu! Haya ni maombi mazito na yenye mantiki ya kiroho.

 

Kumbuka hapa kinacholengwa sio kila neno au wazo la mtu vikubaliwe na Mungu; bali ni maneno yale tu ambayo yanalingana na Neno la Mungu na yanakidhi mapenzi yake Mungu; hali kadhalika na mawazo yaliyokomo mioyoni. Upande wa pili wa maombi haya ni sawa na kusema, “maneno yote na mawazo yote yasiyo na kibali, mbele za Mungu yafutwe, yasiwepo kabisa, maneno hayo yasisemwe, na mawazo hayo yasitunzwe mioyoni.” Kimsingi, haya ni maombi ya kumtaka Mungu afanye ukaguzi wake ndani yetu, azijaribu nia zetu, na kutuonesha mawazo yasiyofaa yaondolewe ili yasije kuzaa maneno yasiyofaa.

 

Mpendwa msomaji wangu, kikwazo kikubwa cha kutokujibiwa kwa sala na dua zetu nyingi, ni kwa sababu, ya akiba mbovu ya mawazo yaliyomo mioyoni mwetu hayajapata kibali mbele za Mungu! Na pia ni kwa sababu maneno mengi yatokayo vinywani mwetu haya kibali mbele za Mungu!

 

Tumekuwa tukijehisabia haki kwa madai kwamba, tukiomba lolote ni lazima tupate kwa sababu ni ahadi ya Yesu Kristo kwetu. Lakini tumesahau kwamba, sala na dua zetu lazima vitokane na maneno yenye kibali mbele za Mungu, na pia mioyo yetu imetunza mawazo yenye kibali mbele za Mungu!

 

Kuanzia leo, hebu sala zetu na dua zetu mbele za Mungu zilenge kumsihi Mungu afanye ukaguzi wake kwa njia ya Roho Mtakatifu na kutufunulia hazina mbovu ya mawazo yaliyomo mioyoni mwetu, na maneno yasiyofaa yatokayo vinywani mwetu. Kumbuka sio kwamba Mungu hayajui wal kuyaona, ni sisi ndio wenye tatizo la kuyapambanua na kuyatambua kazi ambayo tunahitaji msaada wa Mungu.

 

Kumbuka kupata “kibali mbele za Mungu”, ni “kukubalika mbele za Mungu na wanadamu”. Kibali cha Mungu ni ufunguo wa mambo yote tunayohitaji kufanishwa katika maisha yetu. Kibali cha Mungu hurahisisha mambo ambayo yangechukua muda mrefu. Kibali cha Mungu ni kinga dhidi ya kuingizwa kwenye njia haramu za rushwa na hongo ili kupata haki na mahitaji yetu. Kibali cha Mungu ni kutambulishwa na Mungu kwa watu wakupokee kwa sababu Mungu yuko upande wako kila uendapo!

 

Kupokea hekima ya Mungu

 

Mpendwa msomaji wangu, sasa tunaingia kwenye kipengele cha pili ambacho ni muhimu kati ya vipaumbele 3 vya kutongoza katika kumwomba Mungu ni “hekima ya Mungu”:

 

“Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote, kwa ukarimu, wala hakemei; naye atapewa.” (YAK. 1:5)

 

Mpendwa msikilizaji, hii si mara ya kwanza kuzungumuzia habari za hekima ya Mungu. Lakini pia najua sio watu wote mnaosoma mada hii mmefikiwa na jumbe zote zilizopita! Kwa mujibu wa Biblia “Hekima ni uwezo wa kimungu wa kutambua na kupambanua mambo yenye utata, na kupata ufunuo wa kuleta ufumbuzi wa tatizo lililopo, au kuepusha kutokea kwa matatizo yatokanayo na waathirika kutokuwa na uwezo wa kuyazuia”!

 

Ndiyo maana maandiko tuliyosoma yanaweka waziwazi kwamba, mtu akijikuta yuko njia panda, amesongwa na mambo, amebanwa kiasi ambacho haoni mlango wa kutokea, maana yake hapo, AMEFIKIA UKOMO WA KUFIKIRI na pia HAKUNA BINADAMU aliye na uwezo wa kumsaidia kutokana katika mazingira hayo. Kama huyo mtu ni mcha Mungu, anashauriwa na maandiko kumwomba Mungu dua ya “kupewa hekima” ya kumtoa katika mazingira tata aliyomo.

 

 

 

 

 

Ndiyo maana kila mtu wa Mungu ambaye tayari anaishi chini ya mamlaka ya Yesu Kristo, anahimizwa kumpokea na kujazwa Roho Mtakatifu. Kwa sababu Roho akiwa ndani yake, ni rahisi kuomba “karama ya Neno la Hekima” akapokea kutoka kwa Roho Mtakatifu papo kwa papo. Lakini sio wacha Mungu wengi ambao wamempokea Roho Mtakatifu, na hata waliompokea Roho Mtakatifu sio wengine ambapo wamejifunza na kupata uzoefu wa kupokea maongozi ya huyo Roho akiwasaidia kutatua mambo yaliyoshindika kwa akili za kibinadamu, na kuwaepusha na kuwakinga na matatizo yalioko mbele yao

 

Ujumbe wa leo unalenga kumhamasisha kila mcha Mungu anapojikuta katika mazingira yenye utata, na haoni njia salama ya kutokea; ajue kwamba iko fursa ya kumwomba Mungu hekima ya kumtoa kwenye mazingira hayo! Ndiyo maana Yesu katika kuwafundisha wanafunzi wake jinsi ya kuomba, aliweka kipengele cha kuomba, “Usitutie majaribu bali utuokoe na Yule mwovu.”. Hapa Yesu alimaanisha kwamba, katika sala zetu, tuombe “Hekima ya Mungu” ya kutusaidia kupambanua, na kugundua mapema hila za Ibilisi na mawakala zake, na kuepuka kabla ya kutumbukia na kupata madhara.

 

Kimsingi, hekima ni uwezo wa kuona tatizo lililofichika na jinsi ya kuliepuka; au hata kama tayari umeshaingia katika tatizo, bado “Hekima ya Mungu” inakupa njia ya kutoka na kukomesha madhara yaliyokusudiwa na Ibilisi dhidi yako.

 

Lakini, pia hekima, sio kwa ajili ya matatizo peke yake, bali hata kwenye ubunifu wa mambo mapya ambayo yanaleta maendeleo ya kiuchumi na kubadilisha maisha ya wengi. Kwa njia ya karama ya neno la hekima unaweza kupokea “wazo jipya” lenye mvuto maalum na ukapewa mkakati wa kulitekeleza likaleta matokeo makubwa kuliko wengi wenye uzoefu wa miaka mingi katika sekta husika.

 

Mpendwa msomaji wangu, unapoona  mtu, au familia fulani, au taasisi shirika kampuni huduma dhehebu fulani lina mgogoro na faraka, ujue kwamba kilichokosekana hapo ni “mtu mwenye hekima ya Mungu ya kutatua mgogoro huo.” Ni hekima ya Mungu iliyokosekana hapo. Na ufumbuzi wake lazima awepo “mtu wa Mungu” mwenye mahusiano na Mungu wa kumwomba Mungu dua ya kupokea Neno la Hekima la kutatua mgogoro huo. Vinginevyo mfarakano huo mwisho wake msambaratiko na maono yake kufikia ukomo wake kabla ya wakati.

Itaendelea....

 

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.