KWA TAARIFA YAKO: SAFARI YA GOSPEL KITAA HADI HIVI SASA

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu

Januari 2012, wafuasi wakiwa 600
Gospel Kitaa, ambayo imeanza mwaka 2011, imekuwa na lengo hasa la kuwavuta vijana na kuwafanya wawe watumishi wa Mungu, kwa namna ambavyo anapenda wamtumikie. KWA TAARIFA YAKO jina la Gospel Kitaa lililenga hasa jamii ya watu mbalimbali, kwanza Gospel ikilenga kuwavuta wale wote wanaopenda na wasio na mashaka na injili, na pia neno Kitaa likiwalenga vijana moja kwa moja, ambao hufika kutazama kinachojiri "kitaani".

Kwa mwendo wa kusuasua na kama mzaa ndivyo ambavyo blogu hii ilianza, ikiendeshwa na Ambwene M. Mwamwaja, kabla ya kuungana naye Elie J. Chansa, na kisha Silas E. Mbise, na hivi karibuni Boniface Kazi. KWA TAARIFA YAKO Team GK wanaoonekana ni hao 4, ila pia kuna wale ambao hawaonekani, mmojawapo ni wewe unayetembelea tovuti kila siku :-) .

Mwenendo


Mwaka 2011 mwezi Aprili ndio ambapo habari ya kwanza iliandikwa kwenye blog hii, ambayo ilikuwa inamhusu mwimbaji Joyce Mlabwa, ambaye alikuwa ametoa toleo lake la pili la album ya picha za sauti. (bofya hapa kusoma) Kipindi hicho blog ikifahamika kama gospelkitaa.blogspot.com

Mwezi Aprili ulishuhudia habari moja tu ikiandikwa, kisha ikifuatiwa na habari mbili kuandikwa mwezi Mei, kisha kufuatiwa na miezi 4 ya ukimya kutokana na majukumu mengine ya kujenga taifa. Hata hivyo nguvu iliongezwa mara baada ya timu kuongezeka, baada Elie kujunga na GK, ambapo mwaka 2012 ukashuhudia jumla ya habari 750 zikiandikwa, kulinganisha na habari 18 kwa mwaka 2011.

KWA TAARIFA YAKO, GK ambayo ilizaliwa jijini Manchester Uingereza ambako wazo la Ambwene kuwa na blog ya kuandika habari za Kristo lilikamilika kwa vitendo akisaidiwa na rafiki yake Dkt Mbonea Mrango. Ila KWA TAARIFA YAKO makao makuu ya Gospel kitaa yalikuwa Kurasini kwenye majengo ya WAPO Radio FM ambako timu nzima ilikutana hapo, iliendelea kufanya vema, na kuanza kupata wadau mbalimbali ambao pia walikuwa wakiisikiliza WAPO Radio FM kwa njia ya mtandao, mara tu ilipoanza. Na hicho ndio chanzo cha mitandao mingine mingi kunakili ratiba ya vipindi kama ilivyoandikwa, ikiwemo mitandao ambayo haiandiki kuhusu habari za injili.

Julai 2014, wafuasi 9000
Uanzishwaji wa ukurasa wa facebook ulifanikisha kueneza injili kwa watu wengi zaidi, ambapo wafuasi walianza kufuatilia mtandao huu kutoka kila kona ya dunia. Ufuatiliaji wa habari za makanisa mbalimbali bila ya kubagua imekuwa sababu nyingine ya GK kupata mashiko, ambapo pamoja na kukua kwake, changamoto nazo zilizidi kukua, ikiwemo ile ya kufuatilia habari kwa muda mrefu na kisha mara baada ya kuandika, watu wengine kuinakili kama ilivyo na kuifanya yao (bila kueleza chanzo chao). KWA TAARIFA YAKO hilo ndilo lililopelekea kuanza mfumo wa kuweka alama kwenye picha na video ambazo GK imezipiga. Tazama baadhi ya video hizo kwa kubofya hapa.

Kwa kadri siku zilivyokuwa zinaenda na changamoto kuzidi, ndivyo ambavyo kumekuwa na mabadiliko kadha wa kadha ili kuendana na teknolojia, kuwezesha kufikisha injili katika viwango vya juu. Mwaka 2013 ulishuhudia mabadiliko ambayo kwa KWA TAARIFA YAKO hata mitandao mingine ililazimika kuiga mfano, ambapo Gospel Kitaa ilihama kutoka www.gospelkitaa.blogspot.com kwenda www.gospelkitaa.co.tz/ ukiuliza waendeshaji, safari kwao bado kufika mwisho.

Ni mengi yangewezwa kuzungumzwa kuhusu safari ya GK hadi kufikia hivi sasa, ila kiufupi. Tunaamini kwamba kuna mahala mtu huguswa na kile ambacho huwa tunakichapisha hapa, aidha kwa utafiti wetu, ama kupitia walimu mbalimbali na wahubiri ambao hutuma mafundisho yao kwa ajili ya kukufikia. Kama ambavyo hatutozi kwa ajili ya kuweka mafundisho kutoka kwa mtu yeyote, ndivyo tunaamini kwamba mafundisho yanafanyika baraka kwako. Maoni yako ni muhimu kama kuna mafundisho uliyoguswa nayo, jambo ambalo pia linamtia moyo mwalimu kuendelea kufundisha. Kama ungependa kuwa sehemu ya Team GK kwenye mkoa wowote uliopo, milango yetu iko wazi kwa ajili ya kumtwalia BWANA Yesu utukufu.

Ila kama ulikuwa hujui, KWA TAARIFA YAKO Team GK na majukumu yao ni kama ifuatavyo. Ambwene Mwamwaja; Mkurugenzi/Mwandishi mwandamizi, Elie Chansa; Mhariri/Mpiga picha mkuu, Silas Mbise; Mratibu/Mwandishi Mpiga picha, Boniface Kazi; Mpiga picha/Graphics

Katika yote tunayofanya na kupitia, tunamshukuru Mungu kwa kutuwezesha kueneza Injili kwa mfumo wa dijitali. Pamoja na yote, KWA TAARIFA YAKO mtandao huu usingefaa kitu kama haukupata watembeleaji wa kila siku kama wewe. Ahsante sana, endelea kueneza ujumbe kwa wengine injili na izidi kusonga mbele.

Hiyo ndio KWA TAARIFA YAKO, vinginevyo tukutane wiki ijayo...
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.