KWA TAARIFA YAKO YNA WA THE PROMISE AWEKA MSIMAMO MPYA KUHUSU UIGIZAJI, MUNGU NA FAMILIA KWANZA

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu


Jericho (Angelo) akiwa na Kristine (Yna)


KWA TAARIFA YAKO hii leo tupo kwa muigizaji maarufu nchini kupitia tamthilia ya The Promise, Timeless na nyinginezo ambaye pia ameokoka na ni mke wa mtu. Hii leo kwa mara nyingine nataka nikujulishe kama hufahamu msimamo mwingine mkali uliotolewa na mwanadada Kristine Hermosa almaarufu kama Yna au Ara majina aliyotumia kwenye tamthilia hapo juu.

KWA TAARIFA YAKO kama unavyofahamu kwamba mwanadada huyu aliigiza tamthilia ya mwisho mnamo mwaka 2010 akiwa na mwigizaji mwenzake waliyepata naye umaarufu Jericho Rosales ama mwite Angelo Buenavista. Baada ya tamthilia hiyo ndipo Kristine alipofunga ndoa na mwigizaji mwingine ambaye pia ameokoka aitwaye Oyo Boy Sotto mtoto wa waigizaji nguli nchini Ufilipino. 

KWA TAARIFA YAKO Yna aliamua kuachana na mambo ya uigizaji kwanza ili kujenga familia yake ambapo mwaka 2011 alijifungua mtoto wa kwanza wakike aitwaye Ondress na mwaka jana tena Mungu akambariki mtoto wa pili wa kiume aitwaye Kaleb Hans bila kumsahau mtoto wake mwingine aliyemuasili kutoka kituo cha watoto yatima aitwaye Kiel Kristian. Mashabiki waliowengi wa mwigizaji huyo walikuwa wakimtumia meseji za kumtaka arejee kwenye runinga tena kwakuwa wanamkumbuka sana, lakini mwigizaji huyo anadaiwa kujikita zaidi katika kulea familia yake na kufanya matangazo ya runinga ya kampuni mbalimbali bila kurejea kwenye uigizaji.


Kristine akiwa na familia yake


KWA TAARIFA YAKO kama hujui mwezi uliopita mwanadada huyo akaamua kufunguka na kuweka wazi kwamba hayuko tayari kwasasa kuigiza tena tamthilia kwakuwa zinachukua muda mwingi na kwayeye hatoweza tena kwasababu anahitaji muda wa kukaa na familia yake na watoto wake wadogo lakini pia akasema hatokubali kushiriki kwenye maigizo ambayo atahitajika kubusiana na mwigizaji mwenzake kama ilivyokuwa kwa tamthilia ya The Promise na nyinginezo. Kubwa zaidi amesema yupo tayari kupokea ofa ya kuigiza mchezo wowote wenye kujenga jamii na sio kubomoa, anataka watu wajifunze kupitia atakachoigiza na sio tamthilia za kimapenzi 

KWA TAARIFA YAKO mwigizaji huyu ni mmoja kati ya waigizaji wanaodaiwa kuwa warembo sana na kujitunza vyema mbele ya jamii lakini kubwa zaidi ni tabia yake ya kumpenda Mungu. Baada ya tamthilia yao ya The Promise kuwapa umaarufu si waigizaji pekee bali hata nchi ya Ufilipino. Tamthilia hiyo imeanza kurekodiwa upya kwa usasa zaidi ikiwa na waigizaji wapya nafasi ya Yna ikichezwa na mwigizaji chipukizi Kathryn Bernardo almaarufu kwenye tamthilia ya Mara Clara huku nafasi ya Angelo ikishikwa na Daniel Padilla bila kusahau nafasi nyingine muhimu ni kwa mwanamama Claudia Buenavista imeshikwa na binti matata Angelica Panganiban huku Amor Powers imeshikwa na mwanadada Jodi Sta Maria ambaye kwenye The Promise ya kwanza aliigiza kama mdogo wake Angelo.


Angalia trailer ya The Promise ilivyoigizwa upya ikiwa katika lugha ya Tagalog ya Ufilipino


Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO hii leo, vinginevyo tukutane wiki ijayo….
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.