NCHI SASA NJIA PANDA


Nchi inapita katika kipindi kigumu kwa sasa kulingana na matukio mbalimbali yanayotokea wakati tukielekea katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Kulingana na hali hiyo, lugha yenyepesi inayoweza kutumika katika kufafanua ni kusema kwamba, nchi ipo njia panda.

Baadhi ya mambo hayo ni yale yaliyotokea na kuigusa nchi kama taifa, huku mengine yakigusa maisha ya wananchi moja kwa moja.


Katiba mpya
Rais Kikwete akipokea nakala ya Katiba Inayopendekezwa kutoka kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel Sitta
Moja ya mambo yanayoumiza vichwa vya Watanzania ni kuhusu upatikanaji wa Katiba mpya, ambapo hadi sasa hakuna anayejua iwapo Katiba hiyo itapatikana au laa, hasa kutokana na kutojulikana kwa hatima ya kura ya maoni.
Kura hiyo ni muhimu kwa ajili ya kupitisha au kutopitisha Katika mpya, kwani awali Serikali ilisisitiza kuwa kura hiyo itafanyika Aprili 30, jambo ambalo ni tofauti na sasa.

Msimamo huo wa serikali ulitolewa kwa nyakati tofauti na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwamo Rais, Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Wakati Serikali ikiwa na msimamo huo, vyama vya upinzani chini ya Mwamvuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walisema muda wa uandikishaji ili Katiba hiyo ipigiwe kura hautoshi.
Viongozi wa Ukawa walipendekeza kura ya maoni ifanyike baada ya uchaguzi mkuu, ushauri ambao ulipingwa na baadhi ya viongozi wa Serikali wakisisitiza kura ya maoni ipo palepale kulingana na tarehe iliyotangazwa.

Baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu, hatimaye wakati Pinda akiahirisha mkutano wa 19 wa Bunge, alisema msimamo juu ya hatima ya kura ya maoni utatolewa na Tume ya Uchaguzi (NEC).
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Aprili Mosi alitangaza kuahirishwa kwa kura ya maoni bila kusema ni lini kura hiyo itafanyika.

Shule kufungwa kwa kukosa chakula
Ni jana tu gazeti hili liliripoti taarifa ya shule kadhaa za sekondari nchini kuwa zimefungwa kutokana na ukosefu wa chakula uliosababishwa na wazabuni kugoma kupeleka chakuka shuleni, kutokana na Serikali kushindwa kuwalipa fedha zao.

Shule zilizoathirika ni zile za bweni zinazohudumiwa chakula na Serikali ambazo wanafunzi wanakaa mbali na maeneo zilipo shule hizo. Hivi karibuni wanafunzi wa kidato cha sita wanatarajiwa kufanya mtihani wa taifa.

Shule ambazo zimeshafungwa ni pamoja na Kazima, Tabora wavulana, Tabura wasichana na Milambo, zote za mkoani Tabora.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia, Serikali imekuwa ikituma fedha za chakula shuleni kila mwezi, hivyo hakuna sababu ya shule kufungwa kwa kukosa chakula.


Migomo ya madereva
Licha ya kuwa migomo ni jambo la kidemokrasia, jamii ya Watanzania haikuzoea kuona migomo haswa inayohusisha sekta ya usafiri, tofauti na usafiri wa reli.

Migomo iliyozoeleka katika miaka ya hivi karibuni ni ya wanafunzi, madaktari, mahabusu, tofauti na matukio yanayojiri sasa.
Wiki iliyopita taifa lilitikiswa, kutokana na mgomo wa madereva, ambapo hali ilikuwa tete na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Hali hiyo ilijitokeza baada ya madereva wa mabasi ya abiria ya mikoani na daladala katika jiji la Dar es Salaam, kugomea sheria mpya inayowataka waende kusoma baada ya leseni zao za udereva kufikia mwisho, ili wapatiwe leseni mpya.
Sehemu ya abiria waliokwama usafiri kwenye kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Ubungo. ©Mtanzania
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka, alifanikiwa kumaliza mgomo huo baada ya kutangaza kufuta sheria hiyo huku Kamanda wa Polisi Kanda Maalimu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akisema hata tochi zinazotumiwa na askari wa usalama barabarani hazitawahusu madereva.
Hata hivyo jambo la kushangaza, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe, wakati juzi akizindua tochi mpya alibeza kauli ya kupiga marufuku tochi akisema. “Kauli ile ni siasa za Kova,” alisema.

Mgomo wafanyabiashara
Sehemu ya maduka yaliyofungwa Kariakoo. ©Kings FM
Kwa takribani mwaka mzima sasa wafanyabishara wamekuwa wakikosesha taifa mapato kutokana na migomo ya mara kwa mara.

Awali ilielezwa chanzo cha migomo hiyo ni matumizi ya mashine ya EFDs, lakini kila siku zilivyosogea sababu ziliongezeka.

Sababu hizo ziliongezeka hadi kufikia uingizwaji wa mizigo nchini na namna wafanyabiashara wakubwa wanavyokwepa kodi, huku wale wadogo wakikamuliwa.

Badala ya kufikiria namna bora ya kumaliza mgogoro na wafanyabiashara, Serikali ilimkamata Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyabiashara, Jonson Minja na kumzuia asifanye mikutano na wenzake.

Kufanya mikutano hiyo kunatafsiriwa kuwa ni kuhamasisha migomo, hatua ambayo haikusaidia serikali kudhibiti migomo hiyo zaidi ya kuichochea.


Daftari la wapiga kura

Nembo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi. ©BBC
Uboreshaji wa Daftari la Wapiga Kura unaofanywa kwa kutumia mashine za Kielektroniki za Biometric Voter Registration (BRV0 ni wazi kuwa umebaki gizani, kwani hadi sasa haujulikani utamalizika lini kutokana na upungufu wa mashine hizo.

Kwa mkoa mmoja tu wa Njombe uandikishaji ulianza Februari 23, ukachukua zaidi ya miezi miwili na mpaka sasa ratiba ya uandikishaji katika mikoa mingine haijulikani licha ya kuwa Oktoba mwaka huu nchi inaingia katika uchaguzi mkuu.

Moja ya kikwazo cha kufanikiwa kwa zoezi hili ni ukata wa Serikali, kwani awali Tume ya Uchaguzi ilitaka BVR 15,000 serikali ikasema inaweza kununua mashine 8,000 huku taarifa za mwisho zikieleza kuwa mashine zilizokuwa zimenunuliwa ni 250 tu.

Shilingi ya Tanzania kuporomoka
Kwa takribani miezi mitano sasa, shilingi ya Tanzania imeporomoka dhidi ya dola ya Marekani kutoka Sh1,500 kwa dola moja hadi Sh1,900.

Hali hiyo inafanya ugumu wa maisha kuongezeka kwani bidhaa nyingi ambazo zinatumika nchini zinaunzwa kwa bei ya juu kutokana na gharama ya ununuzi wa dola kuwa juu.
Siasa za uhasama Zanzibar

Zanzibar ni sehemu ambayo kwa muda kumekuwa na siasa za ushindani, jambo ambalo kwa miaka ya nyuma lilifanya watu kupoteza maisha.

Baada ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kuanza kazi, ilionekana kuwa siasa za chuki na uhasama zimkwisha na watu kuishi kama ndugu.

Tukio la hivi karibuni la wafuasi wa Chama cha CUF kushambuliwa na baadhi yao kuumizwa vibaya walipkuwa wakitoka katika mkutano wa kisiasa, inatonesha vidonda vilivyokuwa vinaelekea kupona visiwani humo.

Mauaji ya polisi
Mauaji ya polisi yanayofanywa na raia ni jambo jingine linalofikirisha wananchi na hatima ya usalama wao.

Tukio la mwisho ni lile lililotokea Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani, ambapo polisi wawili waliuawa na watu wasiojulikana kisha wakapora bunduki.

Taukio hilo lilikuja wakati bado Watanzania wakiwa na kumbukumbu ya tukio jingine la polisi kupambana na kundi la vijana katika mapongo ya Amboni mkoani Tanga.
Watu hao walidaiwa kuwa na silaha ambazo zilikuwa zimeporwa katika matukio mbalimbali ambayo polisi walivamiwa.

Vituo kuvamiwa na silaha kuibwa
Februari mwaka huu, watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi, walivamia na kuvunja stoo (amari) ya Kituo Kidogo cha Polisi Mngeta, Kilombero na kuiba bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 30.
Kituo hicho ni cha tatu kuvamiwa mwaka huu baada ya Kituo Kikuu cha Polisi Rufiji, Mkoa wa Pwani na Bukombe kuvamiwa na majambazi na kuua polisi wawili na kupora bunduki saba na risasi 60.

Mwaka jana majambazi walivamia Kituo cha Polisi Mkamba, wilayani Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja na mgambo wawili kisha kupora bunduki tano na risasi 60.

Kadhalika, Juni mwaka jana, majambazi yalivamia Kituo cha Polisi Bukombe na kuua askari wawili na kupora bunduki 10 na risasi kadhaa.

Bado haijajulikana silaha hizo zinazoporwa zinapelekwa wapi, huku kasi ya upatikanaji wake ikiwa haiendani na ile ya upotevu wake.

Watoto kuhifadhiwa kambini
Kumekuwa na matukio kadhaa ya watoto kubainika wakiwa wamefichwa maeneo kadhaa lakini tuki la karibuni ni lile la watoto takribani 17, waliopatikana mkoani Kilimanjaro ikidaiwa wametoka katika mikoa mbalimbali nchini.

Watoto hao walikuwa na miaka kati ya miwili na 13 ikadaiwa kuwa waliwekwa katika eneo hilo ili kufundishwa masomo ya dini.

Undani na ukweli wa suala hilo bado haupo wazi sana, huku jamii ikiwa imebaki na maswali mengi juu ya matukio ya aina hiyo.

Viongozi wa dini kukinzana
Katika hali isiyokuwa ya kawaida tangu mwaka jana kumekuwa na mikinzano kati ya viongozi wa dini na wale wa serikali.

Ili kupata nguvu, viongozi wa kikirsto waliungana na kuanza kutoa matamko ya pamoja dhidi ya Katiba tangu mchakato ulivyokuwa katika Bunge Maalumu la Katiba na kuendelea hadi Katiba inayopendekezwa ilipokabidhiwa kwa Rais Jakaya Kikwete.
Hali hiyo imeendelea katika masuala mbalimbali ikiwamo lile la Mahakama ya Kadhi, huku wale wa kiislamu nao wakitoa hoja zao.

Viongozi wa dini wameendelea kusigana, ambapo wakati maaskofu wanapinga uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, kwa upande wao masheikh na maimamu wamekuwa wakitoa matamko wakiwataka maaskofu kutoingilia suala hilo kwa kuwa haliwahusu.

Ni hivi juzi tu Rais Kikwete akiwa mkoani Shinyanga katika misa ya kusimikwa kwa Askofu mpya wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, Liberatus Sangu, aliwataka viongozi wa dini kutoingilia masuala ya siasa.

Rais Kikwete alifika mbali na kuwataka viongozi hao kuwakataa watu wanaofika kanisani na kutaka kufanya siasa huko. Yote hayo ni kujaribu kulinusuru taifa na mpasuko wa kidini.

Vikundi vya kihalifu
Vikundi mbalimbali vya kihalifu vimekuwa vikiibuka kila mara, ikiwamo vikundi vya panya rodi, mbwa mbitu na vingine.

Makundi hayo yamesumbua jiji la Dar es Salaam na kuwafanya wananchi waishi kwa hofu, huku vyombo vya dola vikihangaika kudhibiti hali hiyo. Hali hiyo inadaiwa kuchochewa na ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira.

Mauaji ya albino
Msichana Kulwa Lusana ( 16 ) mwenye ulemavu wa ngozi (Albino ) mkazi wa kijiji cha Mbizi, Kata mpya ya Mbega iliyozaliwa kutoka Kata ya Segese wilayani Kahama mkoani Shinyanga, akiwa amelazwa katika wodi ya majeruhi katika hospitali ya wilaya ya Kahama  baada ya kufanyiwa ukatili na unyama kwa kukatwa mkono wake wa kulia ©Global Publishers

Mwaka 2008 ndipo mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yalipoibuka, serikali ikajitahidi kwa kadri iwezavyo kumaliza hali hiyo.
Mwaka huu matukio hayo yameibuka tena na tayari watu kadhaa wenye ulemavu wa ngozi wamepoteza maisha.

Ajali za barabarani
Ajali za barabani ni jinamzi jingine linaloikabili nchi, sababu zikielezwa kuwa ni uzembe wa madreva na miundombinu mibovu ya barabara.

Moja ya ajali iliyosikitisha ni ile ya juzi iliyotokea katika eneo la Ruaha Mbuyuni kilomita 10 kutoka Morogoro Mjini, ambapo watu 18 waliteketea baada ya basi kuwaka moto.

Ajali hiyo ilihusisha basi la Kampuni ya Nganga lenye namba za usajili T 375 DAH kugongana uso kwa uso na gari la mizigo (Fuso) lililokuwa likitokea Morogoro kwenda Iringa.

Mwarobaini wa tatizo hili bado haujapatikana, licha ya madereva kudhibitiwa kwa kutakiwa kutembea mwendo usiozidi Km 80 kwa saa.
Mojawapo ya ajali za barabarani. Picha ya Maktaba.
Wafadhili kugomea bajeti
Suala la bajeti nalo ni pasu kichwa, ambapo miradi mingi ya Serikali imeonekana kukwama kutokana na wafadhili kugomea kuchangia bajeti ambayo kwa kiasi kikubwa fedha zao hutumika katika miradi ya maendeleo.

Miradi mbalimbali ikiwamo ile ya maji na barabara inaelezwa kusuasua kutokana na ukosefu huo wa fedha, sababu kubwa ikiwa ni wafadhili hao kukerwa na kashfa ya Escrow.

Kashifa zinazolikabili taifa Mpaka sasa kashfa ya Uchotwaji wa Sh bilioni 306 kwenye akaunti ya Tegeta, inaelezwa kuwa moja ya vitu vilivyoisumbua sana serikali.

Nyingine ni ile ya Mradi wa Mwambani ya Economic Corridor ambayo inadaiwa kuwa zabuni yake imetolewa kinyemela.

Zabuni hiyo ni ya Sh trilioni 54, fedha ambazo ni takribani bajeti ya Tanzania kwa miaka mitano.

Majanga ya asili
Sehemu ya makazi ya watu yaiwa yamezingirwa na maji. ©Taarifa
Majanga ya asili ya mafuriko, mvua za mawe na njaa ni kati ya vitu ambavyo vinawakabili wananchi walio wengi.

Baadhi ya mikoa tayari wawakilishi wake bungeni wamesikika wakisema hali ya chakula ni mbaya kutokana na ukosefu wa mvua.

Askari wa kikosi cha Zimamoto na Uokoaji akifaulisha wananchi waliokwama juu ya paa kutokana na mafuriko jiji Mwanza. ©GSengo Blog

Migogoro ya wafugaji na wakulima
Licha ya kuwa haifanani na miaka kadhaa iliyopita, bado jamii ya wakulima na wafugaji haijaweza kuishi vizuri katika maeneo kadhaa.

Hali hiyo inazorotesha uzalishaji pamoja na kuchochea uhasama miongoni mwa jamii.
Mfugaji jamii ya wasukuma akijaribu kuokoa mali zake wakati makazi yakichomwa kutokana na mgogoro baina ya wakulima na wafugaji mkoani Morogoro ©PINGO's Forum.
Wasomi wanena
Akizungumza na MTANZANIA, mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Ruaha cha Iringa, Profesa Gaudence Mpangala alisema Serikali imekuwa na uamuzi wa kulazimisha mambo, bila hata kuwahusisha wadau hali inayosababisha kukwama kwa utendaji wake.

“Chimbuko la matatizo yote haya ni Serikali kulazimisha uamuzi. Kwa mfano katika mchakato wa Katiba, mchakato ulianza vizuri na wananchi walishiriki kutoa maoni, lakini baadaye CCM waliyachakachua na kuunda Katiba inayopendekezwa.

“Wananchi na wadau wengi waliikosoa Katiba inayopendekezwa, lakini Serikali ikalazimisha. Wakristo, Waislamu na hata wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba, walikosoa, lakini, Serikali ikalazimisha.

“Hili ndilo tatizo la kupindisha demokrasia kwa masilahi ya wachache. Mchakato wa Katiba ulipaswa kuahirishwa ili tujipange vizuri, lakini walikataa wakang’ang’ania kura ya maoni ipigwe, sasa imeshindikana.

“Ilionekana Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshindwa kununua vifaa vya BVR kwa kukosa fedha. Hiyo ni kutokana na mipango mibovu ya Serikali kwa sababu walitumia fedha nyingi kwenye Bunge Maalum la Katiba wakasahau mchakato huu,” alisema Profesa Mpangala.

Alitaja kashfa ya akaunti ya Tegeta Escrow akisema Serikali haikuonyesha dhamira ya kuwawajibisha waliotajwa kuhusika.

“Katika kashfa ya Escrow nchi wahisani hazikufurahishwa na hatua za Serikali ndiyo maana zikachelewesha misaada. Matokeo yake sasa hata shule za Serikali zinakosa ruzuku na zinafungwa kwa kukosa chakula, sijawahi kuona jambo kama hili,” alisema.

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi aliunga mkono hoja ya Profesa Mpangala akisema Serikali haiwashirikishi wananchi katika uamuzi wake.

“Haya yanayotokea nchini kama mgomo wa madereva na mgomo wa wafanyabiashara kwa mashine za EFD ni matokeo ya Serikali kutowashirikisha wadau kwenye uamuzi wake,” alisema na kuongeza:
“Nimefanya utafiti wa mashine hizo kwa kuzungumza na wafanyabiasha na serikali, kila mtu anavutia kwake, lakini kuna kukosekana kwa ‘good participatory approach’ (mfumo mzuri wa ushirikishwaji).”

Akizungumzia tatizo la kushuka kwa thamani ya shilingi kulinganisha na Dola ya Marekani, Profesa Ngowi alisema linatokana mahitaji ya dola katika soko la dunia.

Aliongeza kuwa, shilingi ya Tanzania inapoteza thamani kwa sababu hatuzalishi bidhaa za kuuza nje, badala yake tunanunua karibu kila bidhaa nje ya nchi.

“Tunanunua kila kitu nje ya nchi kwa sababu hatuzalishi. Ukienda kwenye maduka makubwa utakuta mazao ya kilimo yanauzwa kutoka nje ya nchi, lakini sisi tunalima mazao ya chakula. Tunanunua mpaka huduma kutoka nje ya nchi. Hali ikiendelea hivi tutalazimika kutumia sarafu ya dola moja kwa moja,” alisema Profesa Ngowi.

Naye Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Benson Bana alisema watendaji wa Serikali ni wazembe ndiyo maana wanashindwa kufanya uamuzi sahihi.
“Huu ni uzembe wa kufanya uamuzi, ufanyaji maamuzi ni taaluma na si kila mtu anaweza. Katika zama hizi, Watanzania wameelimika, wanahoji kila linalotokea. Watendaji wazembe ndiyo wanaiweka Serikali lawamani, huwezi kufanya uamuzi halafu kesho yake utolewe kwa shinikizo,” alisema Profesa bana.

Kuhusu kuahirishwa kwa kura ya maoni, Profesa Bana alisema anaiunga mkono Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kusitisha kura hiyo kwa sababu isingeweza kufanya.

“Suala la kutangaza tarehe ya kura ya maoni lilifanywa na Waziri wa Sheria na Katiba na Rais Jakaya Kikwete, lakini NEC hawakutangaza kwa sababu walijua hali hairuhusu. Lilikuw ani shinikizo tu, huu nao ni udhaifu,” alisema Profesa Bana.

Akizungumzia hali ya uchumi, Waziri wa fedha, Saada Mkuya alisema Serikali inafanya jitihada za kuhakikisha thamani ya shilingi haishuki na tayari imekamilisha mazungumzo na wahisani ili watoe misaada.

“Dola ya Marekani inapanda kwa sababu uchumi wa Marekani nao unakua na kwa kuwa hatuzalishi bidhaa za kuuza nje. Lakini kasi yake siyo kubwa kwama sarafu za nchi nyingine. Kwa sasa tunafanya jitihada ikiwa pamoja a kukuza utalii na tujitahidi kuzalisha,” alisema Mkuya na kuongeza:
“Tumeshazungumza na nchi wahisani na wameshakubali kutoa misaada. Mpaka sasa nchi za Sweden, Canada na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) wameshaonyesha nia ya kutoa misaada ya kibajeti”alisema.

Kuhusu kuahirishwa kwa kura ya maoni, Mkuya alikanusha kuwa ukosefu wa fedha ndiyo umeathiri, akisema tayari Serikali imeshatoa Sh bilioni 72 kwa ajili ya kununulia vifaa vya kielectroniki (BVR).
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (bara), John Mnyika alisema mkwamo unaoendelea nchini ni matokeo ya udhaifu wa Serikali, uzembe wa Bunge na ufisadi.

“Kwa mfano katika suala la BVR, hilo ni bomu la udhaifu na ufisadi ambao hatimaye litakuja kulipuka kutokana na yaliyojiri katika zabuni na utoaji wa fedha za mchakato huo,” alisema na kuongeza:

“Migomo ya makundi mbalimbali katika jamii kama madereva, wafanyabiashara na wengineo ni ishara ya wananchi kuchoka dhidi ya uongozi uliopo katika kushughulikia masuala ya msingi yanayoikabili nchi…” alisema Mnyika.

Chanzo: Gazeti Mtanzania
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.