SOMO: MAMBO MAWILI MATATU YA KUFANYA ILI KUVUKA NYAKATI NGUMU



MAMBO MAWILI MATATU YA KUFANYA ILI KUVUKA NYAKATI NGUMU;

1. Iongeleshe hiyo hali/ jambo/ jaribu/ tatizo/ changamoto/ uhitaji.
"Usikae kimya tu. Kile usichokisemesha hakitabadilika kuwa vile unataka kiwe"
*Daudi alimsemesha Goliati (1Samweli 17:44-45).
*Yesu aliusemesha mtini ukanyauka (Marko 11:14-20).
*Yesu aliisemesha homa iliyokuwa inamtesa mama mkwe wa Petro (Luka 4:38).
*Yesu aliisemesha maiti iliyokuwa kaburini siku nne (Yohana 11:40-44).
*Yesu alisema tunaweza kuiambia milima ing'oke na ikatii (Marko 11:24).
*Ni muhimu ujue kuwa ULIMI NI MOTO na wewe mwenye nao ndiye unaamua unateketeza kipi, unasafisha kipi kwa moto ulionao kwenye ulimi (Yakobo 3:6a).

2. Izungumzishe nafsi yako na moyo wako.
-Wewe ni roho una nafsi na unakaa katika mwili. Kama usipopata "sapoti" ya nafsi yako kwenye hali yoyote unayopitia, na ukaacha nafsi yako iwaze na kufikiri na kutafakari kila wazo na fikira inayokuja ndani yako, hakika utapoteza vita.
Watu waliofanikiwa ni wale wanaoweza kuzitawala na kuzitiisha nafsi zao.
Kwanini kutiisha na kutawala nafsi yako?
Nafsi yako ni kiwanda kinachobeba mambo matatu makubwa uliyonayo: Hisia, akili na utashi.
Ebu fikiri upo katikati ya upinzani halafu "akili yako haiko sawa" au "hisia zako umeshindwa kuzithibiti" ama "umekosa utashi" wa kuendelea kupambana!

Kwenye Biblia, Daudi ni mfano hai wa watu waliokuwa wakijua siri hii ya kuiongelesha nafsi yake. Ifuatayo ni mistari michache aliyokuwa akiisemesha nafsi yake;

"Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya.
Tumaini langu hutoka kwake"
(Zaburi 62:5).

"Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA. Naam vyote vilivyomo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu"
(Zaburi 103:1).

"Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA, Wala usizisahau fadhili zake zote.
Akusamehe (wewe nafsi yangu) maovu yako yote, akuponya magonjwa yako yote.
Aukomboa uhai wako na kaburi, akutia taji ya fadhili na rehema..."
(Zaburi 103:2-4).

*Mzee Yakobo naye aliwahi kuiongelesha nafsi yake;

" Simeoni na Lawi ni ndugu; panga zao ni silaha za jeuri.
Nafsi yangu, usiingie katika siri yao,
Fahari yangu usiungane na kusanyiko lao..."
(Mwanzo 49:5-6).

Na wewe unaweza kuisemesha nafsi yako kwa maneno ya kujenga, ahadi za Mungu nakadhalika.
"Wewe ni nabii wa maisha yako. Usipofanya chochote Mungu hafanyi chochote"
-Inuka sogea kwenye kioo, jiangalie kwa dakika mbili tatu, jitamkie kupenya na kuvuka, jitamkie uhuru, jitamkie ushindi, jitamkie kibali, jitamkie upendeleo, jitamkie neema iliyozidi.
Usiruhusu kinywa chako kusema kinyume na maisha yako.
"Yale unayojiongelea na kujisemea yanaweza kukufingua au kukufunga"
(Mithali 6:2).

3. Muongeleshe Mungu kuhusu hilo jambo.

*Jizoeze kukata rufaa mbele za Mungu haraka sana unapogundua huna nguvu na akili za kibinadamu za kutatua jambo fulani (Isaya 38:1-8).

*Ni vema ujue Mungu huwatendea watu sawa na "walivyosema masikioni mwake" na si zaidi au pungufu ya walichosema (Hesabu 14:28).

*Ni vema ujue kuwa Mungu huwapa watu haki au hukumu kutegemea na walichosema kwake.
"Kwa maneno yako utahesabiwa haki (ukitumia vizuri ulimi wako kwenye uwepo wa Mungu), na kwa maneno yaki utahukumiwa (ukitumia vibaya maneno yako kwenye uwepo wa Mungu)" (Mathayo 12:34-37).

* Mungu anasubiri ukusudie Neno ili alithibitishe na Mwanga uziangazie njia zako (nguvu za Ufalme wake, Ufalme wa nuru zikusaidie kupenya)" (Ayubu 22:28).

* Mungu anasubiri umwambie ili ayaumbe matunda ya midomo yako (Isaya 57:19).

Hitimisho:
-Lisemeshe linalokusumbua
-Isemeshe nafsi yako
-Msemeshe Mungu

Mwl Dickson Cornel Kabigumila


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.