SOMO: SADAKA IGUSAYO MOYO WA MUNGU (2)

Na Kelvin Kitaso
GK Contributor.
"Utoaji ulio mwema ni mlago wa mafanikio na uponyaji wa kimwhili, kiuchumi, na kiroho"

Wiki iliyopita tulitazama sehemu ya kwanza ya namna ambavyo wengi wanapapasa tu, lakini wachache wanamgusa Mungu kwa utoaji wao. Unaeweza kuiona tofauti hiyo (bofya hapa kusoma) kwenye hilo toleo. Wiki hii tunaenedelea na namna ya kuugusa moyo wa Mungu.

Nakumbuka siku moja nikiwa nimesafiri kuelekea mahali pa faragha kwa ajili ya maombi binafsi, nikiwa huko nilipata mguso wa tofauti sana wa kutoa mavazi yote ya thamani niliyokuwa nayo nimpatie mtu wa Mungu ambaye nilimkuta katika eneo hilo, suala hili lilikuwa gumu sana, haswa ukizingatia nami sikuwa na mavazi mazuri na ya kupendeza zaidi ya yale, nilishindana na ile sauti ya kufanya jambo hili, ila mwisho nikaona ni vyema niitii ile sauti na kutoa, haikuchukua muda mrefu kuna mama mmoja alikuja nyumbani na kuleta nguo nyingi zaidi ya zile nilizotoa na kupata viatu vizuri, kwangu hii ni uaminifu wa Mungu asemaye, “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa kifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakacho pimiwa”

Dhabihu inayougusa moyo wa Mungu ni dhabihu inayouma katika moyo wa mwanadamu, yaani kutoa kitu ukipendacho na ukionacho kuwa bora kuliko vyote na wapenda kukitumia ila kwa ajili ya BWANA unaamua kutoa si jambo rahisi na kufanya hivyo ni ishara ya upendo sana kwa Mungu na huonyesha kuwa unamjua unayemtumikia. Yaani dhabihu ambayo yaweza kuugusa moyo wa Mungu hata wewe mwenyewe ukitoa unaona umetoa kitu mbele za BWANA na wakati mwingine hata nafsi yako yagoma kabisa kwa kuwa nafsi ina tabia ya kujipenda yenyewe.

Mwanzo 22:2 “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.” Mungu anamtaka Ibrahimu atoe mtoto pekee aliye naye na ampendaye, si jambo rahisi kwa watu walio wengi kufanya hivi. Kwa mfano huu ni sawa na umehangaika kupanga miaka mingi sana halafu unapata tu nyumba yako mwenyewe ukasikia Mungu anakuambia nataka utoe hiyo nyumba uliyonayo umpatie mtu Fulani, au umetembea muda mrefu sana kwa miguu halafu umepata gari zuri la pekee na ulipendalo sana halafu ukasikia Mungu anakuambia toa hilo gari umpatie mtu fulani si jambo rahisi.

Kumtii Mungu ni jambo la msingi sana katika maisha yetu, akisema hata kama jambo ni gumu sana wewe tii tu kwa kuwa kamwe hafanyi jambo hili kumkomoa mwanadamu, ila yeye hufanya yote kwa utukufu wake na ili kumfanya mwanadamu afurahie wema wake. Kwa Ibrahimu ukiendelea kusoma utaona kuwa Mungu anamuambia kwa kuwa hakumzuilia mwanae pekee ni lazima ambariki.

Sauti ya Mungu wakati mwingine inakuja kinyume na wewe ulivyo na waweza jiuliza mbona mimi nina vichache sana kwa nini amechagua mimi nitoe na si wale wenye navyo, ila jawabu ni kuwa Mungu amekuheshimu na amechagua kukubariki ndiyo maana amekuchagua wewe kati ya wengi.

Kijana mmoja katika Mathayo 19:21-22 “Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, Nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. 22 Yule kijana aliposikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” Kutoa na kuacha unavyomiliki kwa ajili ya Mungu ni suala la kujikana, kwa yule kijana alipoambiwa atoe alivyonavyo awape maskini aliondoka kwa kuhuzunika na akaona kuwa Mungu hamtakii mema kwa kumuagiza kutoa vitu vyake, ila laiti angejua siri iliyomkuta Ibrahimu na mjane wa Sarepta basi angetoa naye kwa kuwa angepata maradufu ya vile alivyokuwa navyo.

Mfano mwingine ni kitabu cha 1 Wafalme 17:13-16 “Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. 15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. 16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilonena kwa kinywa cha Eliya.”

Kutoa si kuwa navyo vitu vingi sana ila hata vile vidogo ulivyonavyo Mungu anataka umtumikie navyo, mjane wa Sarepta alidhani kuwa kutoa kwa ajili ya mtumishi wa Mungu ni mpaka awe na vitu vingi sana ila sivyo Mungu anavyotaka kwa watu wake. Kutoa ni moyo na wala si wingi wa vitu ulivyo navyo.

Kutoa ni muhimu sana kwa kuwa ni kujiwekea hazina mbinguni ambapo nondo na kutu hawali, kama isemavyo katika Mathayo 6:19-21 “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; 20 bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; 21 kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.”

Kutoa mbele za Mungu unajiwekea hazina mbinguni mahali ambapo utakuwa ukiishi milele, mfano mmoja aliutoa Mzee Moses Kulola kwa kusema “unakuta mtu anajisifu kuwa ana milioni kumi (10) benki ana mali nyingi sana ila hana hazina yoyote mbinguni na ni bahiri katika kutoa, ukimuuliza mtu huyu anaenda mbinguni, akifika bila shaka hata mahali pake kama atapata bahati hiyo hakutakuwa na hazina halizojiwekea.” Ukifahamu kuwa wewe duniani unapita kuelekea mbinguni weka juhudi katika siri hii pia. Kutoa katika hali ya kawaida ni kama kupoteza ila ni njia ya kujazwa vingi zaidi, ndiyo maana biblia usema kuwa “amfadhiliye/amsaidiaye maskini amkopesha BWANA”  

Mungu anataka watu wake kujitoa kwa ajili ya kuifanya kazi ya injili na ana thamini sana wote wanaojitoa kwa ajili ya injili. Hagai 1, Na BWANA uumizwa sana na watu wanaothamini mambo ya nyumba zao na kusahau kazi ya nyumba ya BWANA.

Alisema nami mama yangu kuwa imenipasa kujisikia vibaya na kuona aibu sana pale napopendeza na kuonekana nipo vizuri sana huku wakitazama familia yangu na wazazi wangu hata kwa sehemu ndogo sana hatufananii, yaani nimewaacha mbali sana na hata aibu kutambulisha kuwa ni wazazi wangu. Lengo la nasaha hii kwangu ni kunihimiza kuwa nina wajibu wa kuwafanya wazazi wangu wang’ae na kupendeza hata watu wakitazama waone namna ninavyo jali.


Sehemu  tatu za sadaka igusayo moyo wa Mungu

       Kutoa miili yetu kama sadaka na dhabihu takatifu iliyo hai.
       Kutoa muda wako kama dhabihu takatifu iliyo hai ili ikamfanyie yeye manukato.
       Kutoa mali na fedha zako kwa ajili ya kumtumikia BWANA.

Katika maeneo yote haya Mungu alifanya ili mwanadamu afurahie uzuri na uaminifu wa Muumba wake, na anafurahi sana kuona mwanadamu anashiriki pamoja naye na kumshirikisha katika kila jambo ampalo.

Itaendelea wiki ijayo...

Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.