SOMO: SADAKA IGUSAYO MOYO WA MUNGU

Na Kelvin Kitaso,
GK Contributor.


“Utoaji ulio mwema ni mlango wa mafanikio na uponyaji wa kimwili, kiuchumi, na kiroho”

Dhabihu igusayo moyo wa Mungu ni mlango wa baraka yako.

Watu wengi wamekuwa wakitamani sana kubarikiwa na Mungu ila si wepesi kutaka kujua ni kwa namna gani au zipi ni kanuni za Mungu kwa mafanikio yao. Wengine kwa kutojua utaratibu wa Mungu wameamua hata kuvutwa na makanisa yanayotangaza kuwa wana ibada za kuombea watu Baraka na utajiri, ila Mungu yeye ni wa utaratibu na ukimgusa katika maeneo yake aliyoamuru yafanywe ni lazima utabarikiwa hata pasipo kuombewa na mitume na manabii, Ni muhimu sana kwa kila mtu kujifunza njia za Mungu na kujua ni kwa namna gani Mungu anawabarika watu wake.

Nyakati za leo ni rahisi sana kukuta mtu anamdai Mungu mambo mengi na Baraka ila ukitazama maisha yake jinsi yalivyo hakuna utoaji na si mwepesi kufanya mambo yanayobariki moyo wa Mungu.

Vipo vitu vinavyougusa moyo wa Mungu moja kwa moja, na vipo vitu vinafanyika na vimebeba sura nzuri ila si vyote vinavyougusa moyo wa Mungu. Katika sadaka kuna sadaka inayougusa moyo wa Mungu moja kwa moja na kuna dhabihu itolewayo katika madhabahu ya Mungu ila haina sifa ya kugusa moyo wa Mungu.

Maandiko matakatifu yanatueleza kuwa utoaji ulio wa moyoni pasipo kushinikizwa ni sababu ya watu kubarikiwa na pia kukosa roho ya utoaji ubaki kuwa sababu ya watu kutobarikiwa.

Kitabu cha Marko 5:30-32 “Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, na wewe wasema ni nani aliyenigusa?” Watu wengine waliokuwa katika eneo lile walimpapasa Yesu ila hakuona mguso wowote, tofauti ni kwa Yule mama ambaye aligusa kwa mguso wa kudhamilia ambao uligusa moyo wa Mungu moja kwa moja na ukamfanya Mungu aingilie kati suala la Yule mama na kumponya.

Si kila agusaye ana mguso wa kugusa moja kwa moja, kuna wengine wanapapasa tu ila hawagusi ila kuna wengine wanagusa kabisa mpaka wanatoa mshituko na muitikio wa tofauti kwa mguswaji, mpapasaji hana athari yoyote ile ila mgusaji anaathari kubwa sana, na mgusaji aweza patiwa mambo mengi sana kwa kule tu kugusa kwake.

Marko 12:44-44 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. 42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. 43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; 44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Suala si kutoa ila suala ni kutoa dhabihu igusayo moyo wa Mungu kwa moja kwa moja, mtu unayeweza kumpima kwa viwango vyako vya kawaida kuwa yuko chini sana ndiye anaweza kuwa mtu afanyaye mambo yanayougusa moyo wa Mungu na kumfanya ajisikie vizuri.

Aidha katika eneo la sadaka kuna watu wengi watatoa dhabihu zao kama wapapasaji, ila kuna mmoja atatoa dhabihu ambayo itaugusa moyo wa Mungu moja kwa moja na kumfanya Mungu asiwe na kimya na ashuke na kusababisha uponyaji wa maeneo yote kwa huyo mtu.

Dhabihu itolewayo kwa moyo na kupenda mbele za Mungu uwa inasema na kumkumbusha Mungu mara zote kwa habari yetu na maisha yetu. Ni kweli kuwa maombi tuyaombayo uzungumza sana mbele za Mungu, ila dhabihu tuzitoazo kwa moyo zinapaza sauti njema sana mara zote mbele za Mungu huku zikimkumbusha Mungu kuwa imempasa hatubariki. Kweli kuna wakati aweza kaa kimya kabisa ila akitazama moyo wako wa kumtolea na kujitoa mbele zako ni lazima aitike na kufanya hata zaidi ya yale uyaombayo. Maandiko usema yeye ufanya zaidi ya yale tuyaombayo, ushawahi kujihoji ndani yako kuwa ni nini kinamshawishi afanye zaidi ya yale tuyatamkayo katika kuomba kwetu? Ni kweli kuwa kuna neema ila pia dhabihu uzitoazo zinadai ulinzi, uponyaji, utajiri na mali, na heshima mbele za Mungu kwa maisha yako.

Mfano Kornelio sadaka alizokuwa akitoa kuwasaidia watu wengi wenye shida zilifika mbele za Mungu na kumkumbusha Mungu kuwa inapaswa afanye jambo kwa mtu wake Kornelio.

Mwanzo 4:3-5 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. 4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama, BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; 5 bali Kaini hakumtakabali wala sadaka yake, Kaini akagadhabika sana, uso wake ukakunjamana.” Suala si kutoa tu ila suala ni kutoa dhabihu yenye kupendeza mbele za Mungu. Kaini alikuwa anatoa tena sana ila tatizo alikuwa anatoa ziada za vile alivyonavyo na tena si vile vizuri, nadhani hakufahamu kuwa, “kipimo kile kile upimacho  ndicho utapimiwa”. Tofauti kwa Habili ni ya kuwa yeye alitoa kila kilicho bora mbele za Mungu, kile ambacho ni kizuri na chenye kupendeza ndicho alichochagua kumpa BWANA, maandiko yanaeleza kuwa Mungu aliikubali na kuipokea sadaka ya Habili na akaikataa sadaka ya Kaini.

Kama si mtoaji au unatoa sadaka mbovu usijadili sana kwa nini mambo yako hayako vizuri. Jawabu unalo kuwa Mungu anakubali sana sadaka itolewayo kwa moyo na yenye kupendeza.

Ni dhahiri kuwa kukosa roho ya utoaji na kuwa na tabia ya kumkadiria Mungu katika yale tuyatoayo ni sababu kubwa sana ya kutopokea baraka za Mungu.

Watu wengi sana huwa na tabia njema ya kupenda kutoa kama ilivyokuwa kwa Kaini na Habili, ila katika kupenda huko wengi hutoa ziada ya vile walivyonavyo na wakati mwingine uchagua vitu ambavyo wanaona kwao vimepoteza thamani na ndivyo uvitoa kwa wengine. Kutoa ziada ya vitu ulivyonavyo na kuchagua kibovu katika vizuri kamwe hakuwezi kugusa moyo wa Mungu hata akageuka kama alivyogeuka kwa mama Yule aliyemgusa.

Wengine usema kuwa mimi ninatoa sana ila naona kama sibarikiwi, jiulize kama unatoa kwa namna njema inayoweza kumgusa moyo wa Mungu.

Itaendelea wiki ijayo...

Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia  0769190019/0713804078, kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.