UBATIZO NI HAKI YAKO (1) - MCHUNGAJI MADUMLA

Mchungaji Gasper Madumla


Bwana Yesu asifiwe…

Haki ya msingi kwako ni ubatizo. Haki hii ni kwa kila aaminie jina la Yesu Kristo,anapaswa abatizwe kama vile Yesu Kristo alivyobatizwa akionesha kielelezo cha imani yetu.Biblia inasema;

” Yesu akajibu akamwambia, Kubali hivi sasa; kwa kuwa ndivyo itupasavyo kuitimiza haki yote. Basi akamkubali.
Naye Yesu alipokwisha kubatizwa mara akapanda kutoka majini; na tazama, mbingu zikamfunukia, akamwona Roho wa Mungu akishuka kama hua, akija juu yake;” Mathayo 3:15-16

Hivyo basi ubatizo ni haki yako ya msingi. Na kwa sababu ubatizo ni haki yako ya msingi basi ujue shetani na mapepo yake hayatakupa mpenyo kuipata haki hii ya ubatizo kiuharisia wake,maana shetana na nguvu za giza zipo tayari kuregeza uzi ukayafanya mambo mengine ya kiimani lakini sio ubatizo!


Wabatizwa wakiwa katika mto Yordani-Israeli katika moja ya ziara yangu ( Katikati ni askofu wa jimbo la Tarime EAGT,Askofu Fransis Mbwilo )

Tafsiri nyepesi na iliyo sahihi ya ubatizo ni;

Ubatizo ni tendo la imani la kuuzika utu wa kale pamoja na mambo yake na kufufuka katika nguvu za Kristo Yesu./Au kufa na kufufuka pamoja na Kristo Yesu.

Neno linasema; ” Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?
Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.” Warumi 3:4

Biblia inaposema ”… Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake… ” maana yake tuliuzika utu wa kale wenye kuharibika.Kumbuka hili;huwezi kuzika mwili nusu,bali kinachozikwa ni lazima kiwe kitu kizima yaani ni chote, mfano mtu azikwapo-ni lazima azikwe mwili wote maana haiwezekani kuzikwa kichwa tu na kubakia kiwili wili,hivyo hata katika ubatizo mtu hawezi akabatizwa kwa kunyunyuziwa maji,bali apaswa azamishwe mwili mzima kuwakilisha tendo la kiimani la kuzikwa na kufufuka na Yesu Kristo.


~ Mkristo asiyebatizwa amekosa haki yake.

~ Mkristo aliyebatizwa kwa ubatizo mwingine uwaye yote isipokuwa ubatizo aliobatizwa Yesu Kristo amekosa haki yake pia.

~ Hakuna ujanja ujanja wa ubatizo wa kunyunyuziwa maji kichwani au njia nyingine yoyote ile,ubatizo halisi ni mmoja tu wa maji mengi uliovuviwa na Roho mtakatifu.

Ni afadhari sana upoteze haki nyingine kuliko kupoteza haki yako ya ubatizo. Kwa sababu ubatizo ni sehemu kubwa ya wokovu,yaani asemaye ameokoka sharti abatizwe.Maana imeandikwa;

“ Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa.” Marko 16:16

Ooh,kumbe!

~ Ubatizo huja baada ya kuamini. Kwa lugha nyepesi ni kwamba hakuna ubatizo pasipo kuamini. Na ndio maana nalikueleza kuwa ubatizo ni tendo la imani. Kama kuna suala la kuamini kwanza ndipo ubatizwe hii inahusishwa na uwepo wa mafundisho ya msingi juu ya ubatizo.

Biblia imeweka mkazo juu ya kuamini kabla kubatizwa, ” Aaminiye na kubatizwa ataokoka;…”

Mtu hawezi kubatizwa pasipo kuamini.

Imeandikwa;

“ Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe? [ Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.]Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza.” Matendo 3:36-38

Towashi alipoamini tu,akabatizwa saa ile ile. Na ndivyo inavyopaswa katika ubatizo,pale mtu anapoamini fundisho la Kristo Yesu juu ya ubatizo inafaa abatizwe saa ile ile. Towashi alikuwa darasani akifundishwa neno la Bwana kupitia kinywa cha Filipo,

Kama Towashi atuoneshavyo kwamba ili mtu abatizwe ni lazima apitie darasa la fundisho la ubatizo ili apate haki yake,kisha akiamini ubatizwa mara.

Sasa,unisikilize mpendwa; 

Kama kuna hali ya kupitia darasa kusudi uamini,ili hatimae ubatizwe basi mtoto mchanga hawezi kupitia darasa lolote lile,wala mtoto mchanga hawezi kuamini. Na kama hawezi hivyo vyote,basi ni dhahili hastahili ubatizo kabisa maana hawezi kuamini.

Bali kwa habari ya mtoto mchanga,anaweza kuwekwa wafku kwa Bwana kupitia mtumishi wa Mungu iwe katika ibada au hata nyumbani anaweza kupelekwa kwa Bwana kwa kuwekwa wafku,ikiwa na maana mtoto huyo anakabiziwa kwa Mungu mwenyewe.

Haki hii ya ubatizo ikifanywa kama mapokeo tu,haina maana na wala udhihilisho wa nguvu za Roho mtakatifu hautaonekana.

Sikia,hata kama watu watabatizwa kwa maji mengi,lakini kama ubatizo huo haukuambatana na mafundisho ya kina yenye kuuleta uwepo wa Roho mtakatifu na ikatokea kwamba Roho wa Bwana hakuhusika basi ubatizo huo utakuwa ni wa kimapokeo na wala utu wa kale kwa wale watakao batizwa hautavuliwa. Ngoja nikupe mfano kidogo;

Sauli kabla ya kuchaguliwa na Bwana awe mfungwa wa Kristo Yesu,yaana mtume wa Bwana-alibatizwa kwa ubatizo wa maji mengi na akaendelea kuwaudhi waamini wa Kristo Yesu. Mtu huyu alibatizwa kama mapokeo ya dini yao ya kiyahudi,lakini katika ubatizo huo hakukuwa na kuuzika utu wa kale maana bado aliendelea kuua. Imeandikwa;

” Enyi wanaume, ndugu zangu na baba zangu, nisikilizeni, nikijitetea mbele yenu sasa. Waliposikia kwamba anasema nao kwa lugha ya Kiebrania wakazidi kunyamaza; akasema,

Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi;nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake. ” Matendo 22:1-4

Paulo anawaeleza kwamba alipitia taratibu zote za sheria ya baba zake,ambapo sheria moja wapo ya dini ya Kiyahudi ni ubatizo wa Yohana. Ubatizo wa Yohana ni ubatizo wa maji mengi,sasa ingawa Paulo alibatizwa huko kwa maji mengi kama mapokeo ya kidini lakini bado aliendelea kuwa muuaji yaani utu wake wa kale haukufa!

Mpaka pale alipobatizwa tena kwa Roho mtakatifu ndipo akauzika utu wake wa kale na kuupata utu wa utukufu kwa ajili ya kazi ya Bwana. Ndio maana ninakuambia kila ubatizo ni lazima usimamiwe na kuongozwa na Roho mtakatifu mwenyewe ili nguvu za kuzika utu kale zionekane.

Makanisa ya leo,ipo shida hii;

* Wengi ubatiza kwa kufuata mapokeo pasipo kuongozwa na Roho mtakatifu,maana hata fundisho lenye nguvu hukosekana na hatimae ubatizo unakuwa hauna nguvu yoyote. Na ubatizo usio kuwa na nguvu yoyote ni sawa kama kuogelea tu katika maji kisha na kurudi nyumbani ukiwa vile vile.

* Makanisa mengi huwanyima waanio haki hii ya msingi . Maana huwazuia kwa kuwaambia ubatizo waliobatizwa awali wakiwa wachanga unatosha! Wengine bado huendelea kuwanyunyizia maji badala ya kuwazamisha kama ipasavyo.

Ifike wakati sasa waamini wajue kabisa kwamba katika ubatizo ndipo mahali sahihi pa kuzika magonjwa na kila aina ya udhaifu uliopo katika miili yetu…* Kwa huduma ya maombi na maombezi,nipigie sasa kwa namba hii;0655-11 11 49.

Mch.Gasper Madumla

Beroya bible fellowship church.

ITAENDELEA

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.