UJUMBE: KIJANA USILALE,AMKA KWA KAZI YA BWANA - MTUMISHI MADUMLA

Mtumishi Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…

Ujumbe wa leo hauendi kwa vijana tu,bali na kwako pia. Nimetumia neno ” kijana usilale ” nikiwa na maana ya mtu mwenye nguvu anayepaswa kuitumia karama yake kuleta watu kwa Yesu Kristo. Mtu huyo asilale bali akaze kwa Bwana.

Neno “karama ” linamaana ya utendaji kazi wa Roho mtakatifu ndani ya mwamini aliyeokoka.Hivyo mtu aliye ndani ya Yesu hapaswi kukaa kihasara hasara pasipo kutumika katika ufalme wa Mungu Baba.

Wakati nasoma biblia yangu nalikutana na kisa cha kijana mmoja Eutiko,aliyesinzia sana hata akaelemewa na usingizi kiasi cha kudondoka na kufa. Nami nikaonelea nikushtue wewe kijana mahali ulipokaa kwamba uangalie usije ukasinzia kiasi kwamba usingizi huo ukakupelekea kifo.

Ngoja tusome kidogo,

Kisha nikuelezee japo kwa ufupi siku ya leo,Imeandikwa;

“ Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane. Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika.

Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa. Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake.

Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake. ” Matendo 20:7-11

Biblia inaanza kutuambia kwamba watu wa Troa walikutana “ siku ya kwanza ya juma ” hii ikiwa inamaanisha walikutana siku ya jumapili sababu siku ya kwanza ya juma ya kiyahudi kipindi kile ilikuwa ni siku ya jumapili.

“ Siku ya Bwana” imeelezwa pia katika 1 Wakorintho 16:2,hata ufunuo 1:10

Hivyo kuanzia hapo waamini wa Kristo waliendeleza kukutana siku ya Bwana kwa ibada.

Shida ya huyu kijana Eutiko haikuwa siku ya kuabudu,wala shida yake kubwa iliyopelekea mauti yake haikuwa kwa sababu ya makutano ya watu wengi. Bali ilikuwa ni kuelemewa na usingizi wakati yeye alipopaswa kuwa macho.

Sababu kama angeelemewa na usingizi kisha akaenda kulala zake basi asingelidondoka. Ila yeye Eutiko alielemewa na usingizi wakati alipostahili kuwa macho. Kwa lugha nyepesi mtu mmoja aweza sema Eutiko hakupaswa alale maana ule wakati ulikuwa si wa kulala.

Shida hii ipo hata katika makanisa yetu ya leo. Utakuta wakati wa ibada~ muhubiri awapo akinena madhabahuni,baadhi ya watu hulala. Ila akimaliza tu mahubiri basi yule aliyelala ujikuta akisema “ amen “pasipo kujijua kwa nini kasema amen,sababu hakusikia chochote kilichohubiriwa.

Je kulala wakati wa ibada hutokana na nini basi?

Zipo sababu zimfanyazo mtu kulala ibadani, wengine usema kwa sababu ya uchovu wa siku iliyopita.

Wengine usema wakishindwa kuelewa mahubiri hujukuta wakisinzia na kulala.

Nami nasema,

Sababu kuu sio hizo,ingawa sababu hizo zinaweza kupelekea usingizi ibadani. Lakini sababu kuu ni roho za nguvu za shetani alizoziachilia kwa watoto wa Mungu.

Adui shetani,kamwe hawezi kukuruhusu kusikia mahubiri kwa usahihi wake maana anajua pindi usikiapo neno la Mungu vizuri basi utaelewa kisha utampinga kwa neno kama vile Bwana Yesu alivyompinga kwa neno. Neno linasema kwamba usikiapo neno la ufame wa Mungu,neno hili linakwenda kupandwa moyoni mwako,lakini usipoelewa nalo huja adui kulinyakuwa. ( Mathayo 13:19 )

Hivyo basi utagundua siri kubwa ya adui ni KUKUFANYA USIELEWE NENO LA BWANA.

Ingawa shetani alikuwa na hila mbaya kumzuia Eutiko asisikie zaidi habari njema kutoka kwa Paulo. Mungu akafanya muujiza kupitia mikono ya Paulo,maana Paulo alimfufua kisha injili ikaendelea kuchapwa kama kawaida mpaka alfajiri (soma hapo juu Matendo )

Ndipo sasa nikajifunza kwamba shetani hawezi kuzuia kusudi la Mungu. Kusudi la Mungu kwake Paulo ilikuwa ni kuhubiri habari njema siku ya Bwana,lakini shetani akakorofisha akamsukumia Eutiko usinginzi mkali ili aanguke kisha ghasia zije ili Paulo yamkini ahairishe mahubiri,lakini shetani alishindwa sababu kijana alipokufa,Paulo akamfufua kudhihilisha nguvu ya Mungu aliye hai.

Neno lanapotolewa madhabahuni,basi ujue huyo ni Mungu mwenyewe anasema nawe kupitia mnenaji wake. Hivyo hustahili kulala hata kidogo.

Lakini kisa hiki cha Eutiko kimebeba mafunuo mengi kwa kanisa la leo.

Kwamba Eutiko pale alipojisahau akazidiwa na usingizi ndipo akadondoka,kisha akafa. Hivyo utaona kwamba kifo chake kilikuwa na hatua hadi hatua na mwishoe akafa. Hatua zenyewe ni kama ifuatavyo;

Hatua ya kwanza Eutiko alielemewa na usingizi sana,lakini hatua ya pili akaanguka, kisha hatua ya tatu akafa.

Na ndivyo jinsi ilivyo hata sasa.

Mtu yeyote aliyeelemewa na usingizi wa kiroho,yaani yule aliyekuwa na imani kwake Bwana Yesu tena kuwa na bidii hapo awali,kisha akajisahau asifanye bidii tena kwa Bwana. Mtu huyo ni sawa na Eutiko aliyeelemewa na usingizi sana.

Mtu wa namna hiyo hujikuta akipitia katika hatua ya pili baada ya kuelemewa na usingizi wa kiroho,hatua ya pili ni kuanguka ( kuanguka hata kiuchumi,kuanguka kiafya,kuanguka katika kila eneo la maendeleo yake )

Akianguka pasipo kurejea kwa Bwana kwa haraka,hujikuta akimalizia kupitia hatua ya mwisho ambayo ni kifo. Siku hizi mtu uanzia kufa kiroho kwanza kisha kama hatashtuka tena hufa kimwili.

Mungu akusaidie kijana,usije ukasinzia ukaanguka Pwa!

Wakati wa kuwa macho ndio sasa!

Wakati wa wokovu ndio sasa.Na ndio wakati wa kutumia karama yako sasa.

Tuwe macho kwa kuifanya kazi ya Bwana.

Kwa huduma ya maombi na maombezi nipigie kwa namba yangu hii;

0655~11 11 49.

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.