HOJA MPYA: NGUVU YA MAWAZO FAIDA NA ATHARI ZAKE - ASKOFU GAMANYWA

Askofu Sylvester Gamanywa, Rais wa WAPO Mission International

Nguvu ya mawazo faida na athari zake


Leo naleta mada mpya ambayo itakuwa ikizungumuzia kwa kina habari za nguvu ya mawazo, faida na athari zake. Hii ni sehemu ya ujumbe ambao nimekuwa nikuota kwenye vipindi vya alfajiri ya saa 11.00 alfajiri katika kipindi cha WAPO Radio FM cha TUAMKE PAMOJA, na nimeombwa niuchapiche kama makala kwenye gazeti Msemakweli.

Utangulizi

Mawazo ni fikira za mambo ambayo yamo katika akilini kama kumbukumbu. Lakini tafsiri hii ni finyu sana kama tutaishia kufikiri kwamba mawazo ni kumbukumbu za mambo yaliyomo akili mwetu. Kwa asili, mawazo ndiyo chimbuko la kila jambo. Hakuna jambo linalotendeka bila wazo. Maamuzi mengi hufanywa kutokana na mawazo. Maneno na matendo yote yanayoendelea kusikika na kuonekana vyote asili yake ni “Mawazo” yaliyotokea akilini mwa binadamu.

Jambo jingine muhimu kulifahamu kwamba, mawazo yaliyoko akilini mwa binadamu yamegawanyika kwenye sehemu kuu mbili. Kuna “mawazo chanya” ambayo ni “mema na mazuri”, na pili kuna “mawazo hasi” ambayo ni “mabaya na maovu”  yenye mtazamo kinyume!

Aidha, mgawanyiko wa mawazo haya una chimbuko lake maalum. Mawazo chanya ambayo ni mema chimbuko lake ni Mungu ambaye amejitambulisha katika maandiko matakatifu ya Biblia; na mawazo hasi ambayo ni mabaya na maovu chimbuko lake ni Shetani na Ibilisi.

Ninaposema chimbuko la “mawazo chanya” ambayo ni mema asili yake ni Mungu, hii ni kwa mujibu wa Biblia jinsi alivyomtafsiri Mungu kwamba anayo mawazo anayotuwazia binadamu wake kama livyoandikwa: “Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema BWANA, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.” (Yer.29:11)

Aidha ninaposema “mawazo hasi” ambayo ni mabaya na maovu asili yake ni Ibilisi na Shetani, hiyo nayo ni kwa mujibu wa Biblia kama Yesu alivyomtambulisha Shetani kwetu akisema: “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yee ni mwongo na baba wa huo.” (Yh.8:44)

Unaona maneno kama haya ya “yeye ni mwuaji tangu mwanzo…” na “…asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa sababu yeye ni mwongo na baba wa huo…” haya yote ni mambo mabaya, ambayo chimbuko lake ni “mawazo hasi” yaliyomo katika “mfumo wa mawazo” katika akili za Ibilisi.

Sasa basi, ili kukujengea mtiririko mzuri wa uelewa katika hoja hii makini, sina budi kukujulisha pia kwamba, hata mambo ya kiroho yanayohusu  imani kwa Mungu, au kutokuamini Mungu nayo pia yako katika mfumo wa mawazo! Biblia inaposema imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yalisiyoonekana, maana yake “hayo mambo yatarajiwayo” yako katika “mfumo wa mawazo”. Mawazo huonekana akilini na rohoni tu. Na hakika juu ya mawazo yaliyoko moyoni nayo inategemea na akiba ya “mawazo ya Neno la Mungu” iliyoko ndani ya moyo wa mtu.

Haya, hali ya “kutokuamini” nayo iko katika mfumo wa mawazo moyoni mwa mtu. Ndiyo! Kutokuamini ni akiba ya “mawazo hasi na yaliyo kinyume neno la Mungu”! “Kutokuamini” ni “mtazamo kinyume na kufanikiwa kwa kutegemea njia za Mungu na kanuni zake”.

Kwa hiyo, “Imani kwa Mungu” na “kutokuamini” vyote viko katika mfumo wa mawazo lakini, moja liko kwenye fungu la mawazo chanya kwamba ahadi za Mungu ni kweli na ndivyo ilivyo; na “kutokuamini” ni fungu la mawazo hasi yaliyojaa mashaka na wasiwasi juu ya uaminifu wa Mungu na ahadi zake. Kupitia makala haya, tutakwenda kuchunguza ukweli kuhusu nguvu za mawazo, faida na athari zake katika maisha ya binadamu hapa duniani.
Ngome za mawazo

Sasa baada ya kupata utangulizi kuhusu tafsiri pana ya mawazo, mgawanyiko wake na chimbuko la mgawanyiko huo, ni bora sasa tuingie sehemu nzito kuhuzu mawazo ambayo yameitwa ngome katika maandiko matakatifu kama ilivyoanidkwa:

 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)  tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo; (2 KOR.10:4-5)

Hapa tumesoma maneno ya “silaha za vita”, “kuangusha ngome” na “kuangusha mawazo”. Kabla sijaingia uchambuzi wa ngome za mawazo hebu nitoe tafsiri ya msamiati wa neno “ngome”.  Ngome ni ukuta mnene uliojengwa kwa madhumuni ya kuzuia kuingia ndani, hasa maadui kuingia ndani kwa urahisi. Kabla ya kuingia ndani ya mji/nyumba ili kupigana na kuteka waliomo/vilivyomo ndani kazi ya kwanza ni "kuangusha ngome za kuta”

Haya, tuje kwenye tafsiri ya msamiati wa “ngome za mawazo” kwa mujibu wa maandiko tuliyosoma hapa juu. Kwa kifupi, maandiko yalichokuwa yana kilenga hapa ni

1.     “Falisafa za kibinadamu” zilizotungwa kwa kusudi la kupingana na elimu ya Neno la Mungu m.f nadharia ya mabadiliko inapopingana na “sayansi ya uuumbaji”

2.     “Nadharia potofu ya kidini” yaliyotungwa kupingana na kweli ya Neno la Kristo m.f hakuna kuokoka wala kuwa mtakatifu duniani, Roho na karama zake vilikwishakoma

Kwa mujibu wa maandiko tuliyosoma, tunagundua mara moja kwamba Ibilisi ndiye mwasisi na mjenzi wa “ngome za mawazo” na mikakati yake siku zote ni kutanguliza mapema “Mawazo yake hasi” katika fahamu za watu ili kuwejengea “Falsafa za kibinadamu” zilizo kinyume na elimu ya Mungu pamoja na “mafundisho potofu ya kidini”

Hapa, kusudi la Ibilisi la kuwajengea mapema watu “ngome za mawazo” ni ili ziwazuie waathirika kuipokea Injili ya Kweli na Neno la Mungu (Biblia) na kupata kuokolewa na kujazwa Roho Mtakatifu. Na ndiyo maana sababu kubwa ya watu wengi kutokuiamini Injili sahihi ya wokovu ni kwa kuwa Shetani alitanguliza kwenye akili zao hizi i) Falisafa za uongo uliohalalishwa kijamii na ii) Injili za uongo zilizohalalishwa kidini!


Itaendelea toleo lijalo
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.