SOMO: JIFUNZE KWA DHAHABU

Na Kelvin Kitaso,
GK Contributor.
"Akisha kunijaribu, nitaoka kama dhahabu", Ayubu.
Ni wazi kabisa kuna siri ambayo ilikuwa wazi mbele za Ayubu juu yake na juu ya dhahabu. Kwa kuitazama dhahabu na maisha ya ujumla ya mwamini kuna jambo kubwa la kujifunza. Yapo mambo kadhaa ya msingi ambayo mwanadamu amepaswa kujifunza kwayo kwa kuwa mwamini pia ufananishwa na dhahabu, mambo hayo ni kama:

 1. Dhahabu imefichwa ardhini chini sana.

Mwamini yeyote Yule kabla hajaokolewa uwa chini sana au kwa lugha nyingine ni uwa katika maisha ya dhambi ambako ni sawa na matopeni na chini huko ufunikwa na miamba mbalimbali iliyo migumu na iliyo myepesi, ila Yesu Kristo akaamua kulipa gharama na kuvunja miamba yote iliyo migumu na myepesi na kumtoa ardhini. Hivyo mwamini yeyote kabla hajaokolewa alikuwa mafichoni chini sana na hakuonekana kabisa katika ulimwengu wa roho kwa kuwa yuko chini sana na amefunikwa na mengi.

Lakini pia hatima yako uwa imefichwa chini sana na si rahisi kuipata hata ukaamua kujitoa na kuanza kuvunja miamba yote/ ugumu wote ili kuifikia hatima yako.

 1. Dhahabu itolewapo ardhini huwa na uchafu mwingi.

Kwa mwamini pia atolewapo ardhini uwa na uchafu mwingi sana kwa kuwa sehemu atokayo ni chafu.

 1. Dhahabu husafishwa kwa maji na moto.

Isaya 43:2 “Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.”
Zaburi 66:12 “Uliwapandisha watu Juu ya vichwa vyetu. Tulipita motoni na majini; Ukatutoa na kutuleta kunako wingi.”

Kwa kuwa u dhahabu ni lazima upite kwenye moto na kupita kwenye maji pia. Dhahabu itolewapo ardhini huwa chafu na hatua ya kwanza ni lazima ipitishe kwenye maji na si maji machache bali ni maji mengi ili ipate kusafishwa na kutolewa matope na ndiyo maana katika maandiko anaanza kwa kusema “upitapo katika maji mengi” kabla ya kupitishwa kwenye moto na ipitapo kwenye maji matope utakata ila bado inakosa kung’aa.

Hii umaanisha mtu wa Mungu ni lazima atolewapo dhambini/matopeni ni lazima apitishwe kwenye majaribu mengi/maji mengi kwa lengo la kutomzamisha ila kwa lengo la kumsafisha na ule uchafu na kumthibitisha imani yake.
Hatua nyingine ni kupitishwa kwenye moto na si moto wa kawaida bali ni moto uliomkali sana na katika hatua hii ndipo dhahabu hupimwa kama ni dhahabu au ni jiwe la kawaida, na kama ni jiwe la kawaida halitoweza kumudu ukali wa moto bali litayeyuka ndani ya moto huo na kupotelea huko huko.

Kwa kuwa dhahabu upenda kung’aa na kuwa safi/takatifu sana ni lazima ivumilie makali yote ya moto yanayoisibu.

Majaribu yanachoma kama moto ila yameruhusiwa ili kujaribu imani ya mwamini na hatimaye akimudu ukali wa moto huo ni lazima atoke aking’aa sana. Kuna msemo wa Kiswahili unasema “usione vyaelea ujue vimeundwa,” ni ukweli usiopingika kuwa waweza ona mtu anang’aa ila ukifuatilia mwenendo wake hata kufikia kung’aa huko utakuta huyu mtu alikubali kupita kwenye moto ili ang’arishwe.

Ni katika kipindi hiki wale wasio halisi(dhahabu) uyeyuka kwenye moto yaani hushindwa kumudu moto ila walio halisi huvumilia tu kwa kuwa wanajua baada ya moto huo watatoka waking’aa kama dhahabu, Ayubu 23:10b “…………..Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.”

Neno moja BWANA alinena na kusema “uonapo mambo magumu ujue mwisho umekaribia”. Ni ukweli wa mambo kuwa mara nyingi vitu vinapo fikia mwishoni uwa ni vigumu na wakati mwingine huleta majuto na wengine ukata tamaa wakiwa mwishoni kabisa. Kwa kumtazama mama mjamzito hapatapo ujauzito uweza furahi kwa kuwa na matazamio ya kupata mtoto na anapokaribia kujifungua huchoka sana na uchungu umshika sana na wengine hujuta na kuahidi kuwa hawatarudia kubeba mateso hayo ila ukweli ni kwamba mambo yawapo mwishoni ndipo ugumu uzidi, kikubwa ni kujitahidi na kukazana tu. Na baada ya kushinda kipindi hiki ni rahisi sana kusahau.

Kwa dhahabu jifunzeni, kwa kuwa mchimbaji kila akaribiapo dhahabu iliyopo ardhini hukutana na miamba mingi sana, wengine huoji kuwa “mbona mara ya kwanza haikuwa ngumu hivi?” jawabu ni kwamba unakaribia kukutana na dhahabu ndiyo maana ugumu/miamba huonekana sana. Usikate tamaa jua ushindi wako hupo njiani huku ukikumbuka neno lisemalo “Uonapo mambo magumu ujue ushindi umekaribia”.

Wakati huu ni vyema kufanya mambo haya:
 1. Kutembea katika mapenzi ya Mungu/kuishi utakatifu.
Ayubu 23:11 “ Mguu wangu umeshikamana sana na hatua zake; Njia yake nimeishika, wala sikukengeuka.”

 1. Kutokata tamaa na kurudi nyuma/songa mbele.
          Ayubu 23:12 “Sikurudi nyuma kuiacha amri ya midomo yake; Nimeyatunza maneno          ya kinywa chake zaidi ya riziki yangu,”
 
 1. Mtukuze Mungu kwa kutambua uwezo wake juu ya hali unayopitia.
Ayubu 23:13-14Lakini yeye ni mmoja, ni nani awezaye kumgeuza? Tena nafsi yake ilitakalo, ndilo afanyalo. 14 Kwani yeye hulitimiliza hilo nililoamuriwa; Tena mambo mengi kama hayo ya pamoja naye”

 1. Kiri utashinda na kutoka katika ugumu uliopo.
Ayubu 23:10b “Akisha kunijaribu, nitatoka kama dhahabu.”

 1. Usiogope kwa maana yupo pamoja nawe na hajakuacha.
Isaya 43:1-2 “………..Usiogope, maana nimekukomboa; nimekuita kwa jina lako, wewe u wangu. 2 Upitapo katika maji mengi nitakuwa pamoja nawe; na katika mito, haitakugharikisha; uendapo katika moto, hutateketea; wala mwali wa moto hautakuunguza.”

 1. Dhahabu hung’aa sana.
Ni dhahabu iliyopitishwa kwenye moto tu ndiyo inaweza kung’aa kuzidi mawe mengi. Mawe ina maana pana ya kifasihi kwa kumaanisha walimwengu/wasiomjua Mungu, popote pale alipo mtu wa Mungu halisi aliyepitishwa kwenye moto ni lazima ang’ae kuliko watu waliopo mahali pale.
Hakuna dhahabu inayofanana na mawe ya kawaida na ukiona dhahabu ipo kama mawe ya kawaida ni wazi kusema kuwa dhahabu hiyo ni chafu. Hakuna mkristo halisi afananaye na watu wa mataifa/wasio na Mungu
Isaya 60:1-3 “Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia. 2 Maana, tazama, giza litaifunika dunia, Na giza kuu litazifunika kabila za watu; Bali Bwana atakuzukia wewe, Na utukufu wake utaonekana juu yako. 3 Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.”

Dhahabu inaweza kuangaza kwa kuwa inang’aa kwa kule kupitishwa kwake kwenye maji na kisha moto; na biblia inasema kuwa mataifa na wafalme wataijia nuru yako na mwangaza wa kuzuka kwako hii ni kwa sababu ya kule kung’aa zaidi yao.
Mathayo 5:14 “14 Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.
 15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani. 16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni.”

Mwamini kama dhahabu ni nuru ya ulimwengu ipasayo kung’aliza ulimwengu ili watu waonapo matendo mema wamtukuze Mungu.
 1. Dhahabu ina thamani kubwa.
Mbele za Mungu mwamini ni mtu mwenye thamani sana kwa kuwa Mungu mwana aliacha enzi na utukufu na kufanyika dhabihu ili aweze kumuokoa mwanadamu. Na hii ni sababu Mungu anatazama watu wake kama mboni ya jicho lake kwa kuonyesha kuwa ni watu wa thamani sana mbele zake.
Pia dhahabu ni miongoni mwa jiwe lenye gharama kubwa kuzidi mawe mengi na ndivyo ulivyo uthamani wa mtu wa Mungu. Na ni vyema kwa mtu wa Mungu kulifahamu jambo hili ili kuepuka kuishi maisha ya kujirahisisha rahisisha na yasiyo na uthamani.
 1. Dhahabu ina mvuto kwa waitazamao.
Watu walio na Mungu ndani yao wanamvuto kwa jumla ya maisha yao jinsi wanavyoishi ambayo uwashawishi hata wale wasiomjua Mungu kuvutwa na imani yao, mtu aliyeingia ndani ya wokovu halafu dunia ikawa inamvuto kwake kuliko mambo ya Mungu hupoteza sifa za kuwa dhahabu halisi. Baadhi ya maeneo yenye mvuto ni kama:
*  Muonekano wako wa kujiheshimu na kumuheshimu Kristo.
Balozi anayekuwa na mwenendo mbaya ni aibu kwa nchi yake na raisi wake, hata mtu wa Mungu asiyejiheshimu hata katika kuvaa kwake ni aibu kwa Yesu wake, mbingu, kanisa na yeye mwenyewe.
*  Imani yako.
*  Usemi wako.
*  Tabia yako na mwenendo wako.
*  Elimu yako,n.k
Ni vyema sana kwa mwamini kuifahamu siri hii ambayo imebeba jumla ya maisha yake kiroho na hata kimwili pia.
______
Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.