SOMO: NGUVU YA MANENO, FAIDA NA ATHARI ZAKE (3)

Askofu Sylvester Gamanywa


Nguvu ya Maneno , faida na athari zake-3
Wiki iliyopita tulianza mchakato wa kupitia sura tatu za Neno la Mungu ambapo tulianza na sura ya neno katika mfumo wa “Andiko”. Humo tulijifunza kwamba nguvu ya “andiko” ni kuelimisha, kuelekeza na kumpa msomaji ufahamu wa mambo ambayo hayako machoni pake kwa wakati huo, au kuwepo katika mawazo yake. Nguvu ya andiko ni kutunza kumbukumbu ya maneno yaliyotamkwa ili yatumike wakati wowote wa sasa na kwa vizazi vingi vijavyo.  Kusoma somo la wiki iliyopita BONYEZA HAPA. Leo tunakwenda kuchambua sura ya pili ya Neno la Mungu ambayo ni “sauti” na kuendelea:
Sura ya Neno la Mungu
kupitia mfumo wa Sauti

Sura ya pili ya Neno la Mungu ni pale linapotamkwa na kusikika kwa sauti. Sauti ya Neno la Mungu kazi yake ni kulifanya Neno hilo lifahamike kwenye masikio ya asili katika ulimwengu wa asili. Lakini, sauti ya Neno la Mungu ndimo ilimo nguvu ya uumbaji.
Maana yake, kabla ya ulimwengu kuwepo ulitungwa katika mfumo wa wazo la Mungu kwanza. Kisha Mungu akalitamka kwa sauti hilo wazo likawa neno na ndipo ulimwengu ukapata kuwepo. Maandiko yanaposema kwamba “hata vitu vinavyooonekana havikufanyika kwa vitu vilivyo dhahiri,” maana yake ni kwamba, kabla ya vitu havijakuwepo vilianza katika mfumo wa mawazo katika Nafsi ya Mungu. Kisha Mungu akatamka kwa sauti kila wazo ili liumbike kuwa kitu halisi katika ulimwengu wa asili.
Kama tujuavyo ni kwamba, Neno katika mfumo wa “andiko” tunalisoma kwa kutumia mlango wa maarifa wa macho. Lakini neno linapokuja kwa mfumo wa “sauti” mlango wa maarifa unaotumika ni ”masikio” yetu. Sasa, Maandiko yametujuza kwamba,, hata imani yetu kwa Mungu ili ipate kuumbika ndani yetu, ni lazima kwanza “tusikie” Neno la Kristo kwa njia ya “sauti”:“Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo”(Rum.10:17)
Nguvu ya uumbaji wa Neno
katika mfumo wa Sauti

Kwanini lazima “kusikia” na sio “kusoma”? Nguvu ya andiko hugusa fahamu na hisia za ndani ya msomaji; lakini kusoma hakuwezi kuathiri kitu kwa nje katika ulimwengu wa asili. Lakini neno linapotamkwa kwa sauti, humo ndipo Mungu ameweka nguvu ya uumbaji wake! “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanyika kwa vitu vlivyo dhahiri.” (EBR.11:3)
Neno la Mungu linapotamkwa na kusikika kwa sauti, ndimo ilimo nguvu ya kulifanya wazo la jambo kufanyika kitu halisi kilichotamkwa na kikaonekana kwa macho, au kutambulika waziwazi katika ulimwengu wa asili.
 “Maana Neno la Mungu li hai, lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyambua mawazo na makusudi ya moyo.” (EBR.4:12)
Hapa tunathibitisha kwamba Neno la Mungu linapotamkwa linakuwa lina sifa muhimu zifuatazo: Linakuwa ni “hai” maana yake lina uzima wa roho na mpaka afya ya mwili; pili lina “nguvu” kwa maana “utendaji wa miujiza ya uumbaji”; tatu ni “kali” maana yake uwezo wa kujibu na kudhibiti mashambulizi ya Ibilisi na mapepo yake; nne ni “linachoma” maana yake moto wa kuteketeza nguvu ya dhambi na tamaa mbaya za Ibilisi, na tano li “jepesi” kuzigundua hila za Ibilisi na kuzifuchua hadharani.
  

Maneno ya Shetani kwa mujibu
 wa Maneno ya Yesu Kristo

Haitakuwa ni sahihi kama tutaishia tu kwenye maneno ya Mungu peke yake. Tunahitaji kujua kwa kifupi habari za “Maneno ya Shetani”! Najua Watu wengi hawajui kwa usahihi habari juu ya Shetani, na hata jamii ya watu wa Mungu hawapendi kujua habari zake wakidhani ama ndipo waathirika au watampa sifa asizostahili. Miye naomba tumwangalie Yesu Kristo mwenyewe alihusiana vipi na Shetani na alimchambua vipi. Naamini tukifuatilia nyazo za Yesu katika kumjua Shetani ndipo tutakuwa salama zaidi maana tutakuwa tunatafakari Neno la Kristo na sio maneno ya Shetani peke yake

“Ninyi ni wa baba yenu Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo.” (YH.8:44)

1.         Mwenye tamaa ya kuabudiwa sawa na Mungu

Maneno ya Yesu yamemchambua Shetani kuwa ana asili ya tamaa. Anasema “tamaa za baba yenu….”! Kwa kifupi, Shetani alipokuwa bado ni malaika mbinguni alijaa tamaa ya kutaka kuwa sawa na Mungu, na kuabudiwa kama Mungu. Tunapata taarifa zake kwenye maandiko yafuatayo: “…nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu…”(ISA.14:13a) “Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na yeye Aliye juu.” (Isa.14:14:14)

Kutokana na tamaa hii, alianzisha vita mbinguni ambapo alishindwa na kutolewa yeye pamoja na malaika zake aliowashawishi kuwa upande wake: “….Yule joka akatupwa, Yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye.” (Ufu.12:9)

2.         Shetani ni Mwongo:

Sifa ya pili ambayo Yesu alimchabua Shetani ni tabia yake ya “kutunga na kusambaza uongo” wa kupotosha fikira zimwelekee na kumwabudu Ibilisi. Yesu alimtambulisha Shetani kuwa ndiye mwasisi wa uongo. Na ukweli uko dhahiri kimaandiko kwani uongo wa kwanza wa Shetani ulianzia kwa malaika aliowashawishi kufanya mapinduzi dhidi ya serikali ya Mungu mbinguni.

Uongo wa pili wa Shetani unapatikana pale alipomdanganya binadamu wa kwanza akimwambia Eva: “…Hakika hamtakufa….” (MW.3:4b) “….siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu…..”(MW.3:5) Kuanzia hapo Shetani akafaulu kuudanganya ulimwengu mzima kama maandiko yasemavyo kwamba; “…audanganyaye ulimwengu wote….”

3.         Shetani ni Mwuaji

Yesu Kristo alimchambua Shetani kuwa ndiye mwasisi wa mauaji, yeye akiwa mwuaji wa kwanza; “…yeye alikuwa Mwuaji tangu mwanzo…” (YH.8:44). Biblia haijasumulia Shetani alianza mauaji kwa binadamu au malaika. Lakini tafsiri ya neno Mwuaji maana yake ni mwenye kusababisha mauti. Yeye ndiye chimbuko la umwagaji damu ya kwanza ya binandamu, mtoto wa Adamu aliyeitwa Habili aliyeuawa na kaka yake Kaini.

Mfumo wa maneno ya Shetani

 Baada ya kutambua dhahiri sifa kuu za Shetani kama alivyochambuliwa na Yesu Kristo, sasa turejee kwenye hoja ya msingi wa mada hii inayotaja “mfumo wa maneno ya Shetani” ambayo yamekuwa yakisababisha athari kubwa katika fahamu za viumbe kuanzia malaika aliowarubuni mpaka kwa binadamu tangu mababu zetu waliotutangulia.

Mfumo wa maneno ya Shetani unashabihiana sana na tabia zake mwenyewe. Kama ujuavyo kwamba, maneno ndiyo utambulisho halisi wa tabia ya chanzo chake. Kwa kurahisha maelezo, tunakwenda kujifunza maeneo matatu ya mfumo wa maneno ya Shetani kama ifuatavyo:1.         Uongo

Kama tulivyokwisha kutambulishwa hapo awali katika mada, tunajua kwamba “uongo” ni maneno yasiyo na ukweli; ni maneno yaliyobeba ulaghai na upotofu.

Uongo wa kwanza wa Shetani ulianzia kwa malaika mbinguni hata akafaulu kushawishi theluthi moja ya  malaika wa Mungu. Uongo wa pili ni pale alipomdanganya Eva kwamba akila matunda ya mti uliokatazwa hatakufa bali atafanana na Mungu.

Uongo mwingine anaoueneza ulimwenguni kwa jamii ya wasioamini ni “kuwapofusha fahamu wasimpokee Yesu Kristo na kuokolewa”. Uongo kwa jamii ya waaminio wasijitambue wao ni nani katika Kristo na pia wasitambue kwa yupo na anawanyemelea ili kuwatoa katika imani sahihi. Kwa hiyo, ukisikia neno lolote lenye mwelekeo usiolingana na tafsri sahihi ya Maandiko matakatifu tambua kwamba hiyo sauti ya Shetani

2.         Hasi

Sehemu ya pili ya mfumo wa maneno ya Shetani ni “maneno hasi” Tafsiri ya msamiati wa neno “hasi” maana yake ni “..enye kupinga jambo bila kutoa pendekezo bora la njia ya kulifumbua tatizo.” Maneno ya shetani yote yako katika mfumo kinyume, yenye kupingana na kutokubaliana na maneno ya Mungu ambayo mfumo wake ni chanya.

Maneno hasi ya Shetani ndiyo chimbuko la roho ya kutokuamini kwa sababu yanatilia mashaka na kutokuamini ukweli wa Neno la Mungu na uaminifu wa Mungu kwa ahadi zake. Kwa hiyo, unaposikia “kutokuamini” tambua kwamba chanzo chake ni “kusikia maneno hasi ya Shetani.” Na kila unapisikia neno lolote lenye mwelekeo ulio hasi wenye kukinzana na Neno la Mungu jua hiyo ni sauti ya Shetani

3.         Ubaya/uovu

Sehemu ya tatu ya mfumo wa maneno ya Shetani ni asili ya “ubaya” au “uovu”. Kimsingi ni maneno yasiyo mazuri. Na hapa ndipo asili ya majina yote ya huyu kiumbe mwovu kuitwa Shetani, Ibilisi, Joka nk.

Lakini kama nilivyotangulia kudokeza awali kwamba, Shetani alikuwa malaika mzuri sana kwa jina la Lusifa na aliumbwa akiwa mkamilifu mpaka uovu ulipoonekana ndani yake: “..ulikuwa mkamilifu siku ulipoumbwa”……. “….hata uovu ulipoonekana ndani yako….” (Eze.28:15)

Uovu wa Shetani ulianza katika mfumo wa mawazo alipotamani kuwa sawa na Mungu “…nitapanda mpaka mbinguni, nitakiinua kiti changu juu kuliko nyota za Mungu…”(ISA.      14:13a) “Nitapaa kupita vimo vya mawingu, nitafanana na yeye Aliye juu.” (Isa.14:14:14) Hapa tunagundua kwamba “Uovu” wa mawazo ndio ulizaa “maneno ya uovu”, ushawishi kumpindua Mungu… kama maandiko yalivyonukuu…”  Kwa wingi wa uchuuzi wako….”

Maneno ya uovu ni maneno ya kudharau/kashfa/usengenyaji/yenye kujikinai na          kujitenga na mamlaka halali iliyoko chini ya utawala wa Mungu. Ukisikia neno lolote lenye mwelekeo wa upinzani dhidi ya mamlaka halali tambua hiyo ni sauti ya Shetani!


Itaendelea wiki ijayo….

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.