SOMO: NGUVU YA MANENO, FAIDA NA ATHARI ZAKE (4)

Jumatatu iliyopita tulikomea kwenye vipengele vinavyosema habari za maneno ya Shetani, na athari zake. Leo napenda kujibu baadhi ya maswali magumu ambayo huulizwa kuhusiana na suala zima la kuwepo kwa Ibilisi na malaika zake na usumbufu wanaousababisha: Kusoma sehemu iliyopita BONYEZA HAPA

Askofu Sylvester Gamanywa

Maswali magumu juu
ya Mungu na Shetani

Huko nyuma tumejifunza kwamba, Mungu alimwumba Lusifa akiwa malaika mzuri ma mkamilifu mpaka siku uovu ulipoonekana ndani yake. Yeye ni mwasisi wa uovu. Uovu wake ulianzia katika mfumo wa mawazo na kisha akaupandisha ngazi ukaja kwenye mfumo wa maneno. Uovu uliposikika kwa sauti masikioni mwa malaika ulipandikiza “mawazo hasi” miongoni mwa malaika. Wako walioshawishika na kuona Lusifa ana hoja, na wako waliomkatalia. Katika mazingira hayo ilitokea vita kati ya malaika walioko upande wa Lusifa na malaika walioko upande wa Mungu.

Sasa, Yamekuwepo maswali magumu yanayoulizwa na baadhi ya watu wakidai kujua ni 1. Kwanini Mungu hakumdhibiti Lusifa tangu mwanzo ili asieneze uasi wake kwa malaika wengine? 2. Ni kwanini Mungu asimwangamize lusifa na malaika zake enzi hizo kabla hajaja kumdanganya binadamu wa kwanza? Kwanini Mungu ameendelela kumwacha Ibilisi na malaika zake kuendeleza uovu na uasi wake, na wengi kumwelekea yeye badala ya Mungu?
Maswali haya ni magumu sana. Kila mwenye kuthubutu kuyajibu ni lazima awe amepata ufunuo wa Roho wa Mungu ajuaye hata mafumbo ya Mungu. Lakini kujibu maswali haya kunategemea na kiwango cha ufahamu alio na mtu kuhusu elimu ya Mungu. Lakini maswali haya kutokujibiwa haina maana majibu yake hayapo. Ila yanahitaji hekima kuyawasilisha ili yasizalishe maswali magumu zaidi yasiyo lazima.
Katika mada hii, nataka kutumia ufahamu wangu mdogo kujibu maswali haya, na nina hakika majibu yake yatasaidia kuongeza ufahamu au kuzidi kutafakari zaidi ambako kutamfikisha mtu kwenye majibu yaliyokamilika.

Kwanini Mungu hakumdhibiti Lusifa
asieneze uasi wake kwa malaika wengine?

Enzi hizo kulikuwepo mfumo mmoja wa utawala wa Mungu. Utawala ambao ni mwema, usio na machafuko wala ghasia. Utawala wa amani, furaha na haki.

Malaika ni viumbe walioumbiwa nafsi wakiwa na akili, hisia na utashi. Hawakuumbwa kama “maroboti” wa kufanya kazi kama mashine zisizokuwa na uhai wala utambuzi wake binafsi.

Maswali ambayo wengi hujikwaa kwayo katika eneoo hili ni pamoja na:  “hivi uovu uliumbikaje ndani ya Lusifa?” Ulitokea wapi? Je Mungu hakujua kwamba uovu utajitokeza ndani ya Lusifa. Kama alijua kwanini basi aliuruhusu ujitokeze ndani yake wakati alikuw ana uwezo wa kuzuia kabisa?

Kujibu maswali haya kunahitaji ushahidi kamili wa kimaandiko. Majibu kamili hayamo katika Bibilia. Kwa hiyo si vizuri kujibu kwa mawazo ya kibinadamu. Lakini tunachoweza ni kutafsiri kile kilichoandikwa katika maandiko. Mathalan maandiko yanasema:

 “Ulikuwa mkamilifu katika njia zako tangu siku ile ulipoumbwa, hata uovu ulipoonekana ndani yako.” (Eze.28:15)

Kwa ushahidi huu tunajifunza kwamba, Lusifa “hakuletewa uovu” kutoka mahali fulani. Wala hakuingiziwa “mawazo ya uovu” ndani yake. Tunasoma kwamba, “Uovu ulibuniwa, uliasisiwa, ulizalishwa ndani yake mwenyewe”! Kwa maelezo haya, hata kama Mungu alikuwa anajua, lakini haikuwa ni sahihi au haki kwa kuzuia “mawazo yaliyobuniwa nafsini” hata kama ni mabaya. IKumbukwe kwamba, tunaposema uovu maana yake kuna uande mwingine wa “uzuri/wema”! Kitu alichozalisha Lusifa ni “kuleta mbadala ulio kinyume” na kilichokuwepo tangu mwanzo.

Lakini jibu langu la pili katika kujibu swali la msingi ni kwamba, Lusifa alijenga hisia kwamba, si halali Mungu peke yake ndiye aendelele kuabudiwa na akajenga hoja kwamba, ni lazima awepo mwingine anayestahili kukalia kiti cha uumbaji naye apate kuabudia kama Muumbaji.

Kwa hiyo mawazo ya kumpindua Mungu maana yake ni mashambulizi yaliyomlenga Mungu moja kwa moja, na kupima tabia zake za uungu wake, haki yake, na hekima yake. Iwapo Mungu angeamua kumdhibiti kwa mabavu Lusifa pale pale ili uasi na uovu wake usipate kuenea, bado Lusifa angepata “kiburi cha kuwa tishio dhidi ya Mungu” na Mamlaka ya Mungu ingekuwa imetumika “kujihami tu” badala ya kubakia kuwa mamlaka iliyo bora, sahihi, ya haki na isiyo mbadala wa uzuri wake!

Hatua yoyote ya kumdhibiti Lusifa ingempa kiburi zaidi kwamba yeye ni tishio dhidi ya Mungu. Lakini pia hata malaika wengine wangebaki na mawazo na hisia hasi yenye kuhoji uhalali na upekee wa mamlaka ya Mungu katika uumbaji wake.

Tatu, malaika walioasi walitumia fursa ya kimaumbile ya kuchagua kutii au kuasi. Na kila upande lazima upewe fursa ya kuonyesha tabia na uwezo wake dhidi ya upande mwingine. Kwa hiyo, Mungu hakumdhibiti Lusifa kwa sababu angemtia kiburi cha kujiona amekuwa tishio dhidi ya mamlaka ya Mungu; aidha, hata malaika wengine wangebaki na mawazo na hisia chanya kwamba, hata Mungu naye kuna jambo ambalo lingekuwa bora zaidi ya ubora wa mamlaka yake.

Mungu alipochagua kutomkumdhibiti Lusifa mara moja; pamoja na athari za uharibifu aliousababisha Lusifa na malaika zake, bado heshima, wema na uzuri vimebaki upande wa Mungu. Mungu anapendwa na kuabudiwa na viumbe wake kwa hiari na utashi kamili, lakini pia kuwa kutambua wema, zuri, ubora na ukamilifu uko upande wa Mungu peke yake.

Kwanini Mungu hakumwangamiza
Lusifa na malaika zake wakati ule walipoasi?

Suala la kumwangamiza Lusifa na malaika zake moja kwa moja, nalo linakuja kwenye sababu za majibu ya swali la kwanza. Tumekwisha kuona kwamba, Mungu hakutaka kujihami wala kuzuia uasi na uovu kwa kuwa havikutokana na Mapenzi yake mwenyewe.

Pili, kwa kuwa uasi ni mamlaka iliyo kinyume na mamlaka halali, Mungu ametumia hekima yake kuruhusu kuwepo kwa Lusifa na malaika zake ili nao waonyeshe mbadala wa ushawishi wa mawazo yao kwa viumbe wengine kuanziia malaika mpaka binadamu.

Mungu amekubali changamoto ya Lusifa na malaika zake kwamba, kile walichokiansisha kinaweza kutowesha uzuri na wema wa mamlaka halali ya Mungu? Mungu amekubali kutoa fursa ya viumbe wake kuchagua wenyewe, wanataka kuwa upande gani. Hii ndiyo sababa Mungu ameamua vizazi vyote vya binadamu hapa duniani kuanzia Adamu vipate fursa ya kuona pande mbili za mamlaka ya Mungu, na mamlaka ya Lusifa, na kisha wachague wenyewe wanataka upande gani

Ndiyo, maana, tunasoma nabii zinazotabiri habari za kuja kwa utawala wa Mpinga Kristo, ambaye atasimika serikali moja ya ulimwengu ambayo inaendeshwa kimabavu na kazi yake ni kuhamasisha, kuendesha maovu na uasi dhidi ya Mungu na wanaoitwa kwa jina lake duniani.


Aidha shetani na malaika zake wanajua hiyo fursa ya wao kupewa mamlaka ya kuitawala duniani ili wafanye maovu kwa viwango vya juu vya uasi dhidi ya kila kitu kinachoitwa elimu ya Mungu.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.