SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO (1)SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO.
MNENAJI: Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila.
MAHALI: KANISA LA MORAVIAN MOSHI MJINI
Utangulizi
Mungu alipoumba mwanadamu, hakumuumba kama viumbe wengine.
Alimuumba mwanadamu kwa "sura yake" na kwa "mfano wake".
Mungu hakumuumba "mwanaume" akiwa bora kuliko mwanamke!
Mungu aliwaumba mwanamke na mwanaume siku moja, na wote aliwaumba "roho zao" kwa sura na mfano wake (Mwanzo 1:27).

Na alipotangaza majukumu na uwajibikaji, wa "kutawala, kumilki, kutiisha na kusimamia rasilimali alizoziumba" hakusema hilo kwa mwanaume pekee! Hilo lilikuwa la wote- Mwanaume na mwanamke (Mwanzo 1:28).
Mungu hana jinsia linapokuja swala la Maono, Ndoto, Mipango na Kusudi.
Ndani yao wote- Mwanaume na mwanamke kuna "sura na mfano wake" ambao ndio hasa unaobeba NGUVU YA MAONO.
Mfumo wa dunia na wa kibinadamu ndio ulioleta maswala ya tofauti za kijinsia na kushusha kiwango cha ubora wa mwanamke kutoka "mtu aliye na sura na mfano wa Mungu na mwenye wajibu wa kutawala na kumilki na kutiisha akiwa bega kwa bega na mwanaume" na kumfanya kuwa kiwanda tu cha kutotoa watoto na kitu duni kuliko mwanaume.
Shetani anajua "mwanamke" amebeba nguvu kubwa ya "Usaidizi" ambayo kama akipewa nafasi na kuaminiwa atamsaidia mumewe/ mwanaume kutimiza kila kusudi la Mungu.
Ili kumkwamisha mwanaume asifanye vema na kufanikiwa, amemfanya amuone mkewe si kitu na hana cha kufanya zaidi ya kuzaa watoto na kulea tu watoto!
Mungu anamuita mwanamke "msaidizi" kwa maana "anayesaidia" ni bora au ana nguvu kuliko "anayesaidiwa" !
Shetani alijua nguvu kubwa iliyowekezwa ndani ya mwanamke na akajua ili kuharibu kila kusudi na mpango wa Mungu lazima kwanza afanikiwe kumharibu mwanamke!
Hakuanza na Adam, alianza na Eva mkewe (Mwanzo 3).
Alipofanikiwa kumshinda "mwenye nguvu- Msaidizi" akamtumia kumharibu msaidiwa- Adam.
Shetani anachikifanya ni kuwaaminisha wanadamu kuwa mwanamke "hana kusudi" lolote, ili Yeye (Shetani) amtumie huyohuyo mwanamke mwenye nguvu kuimaliza dunia na kila kusudi la Mungu.
Mungu anajua nguvu iliyomo ndani ya mwanamke na ndio maana tangu siku Adam na mkewe walipoanguka, alitoa unabii kuwa "Uzao wa mwanamke" utakiponda kichwa cha nyoka (utaharibu mission na plans zote za Shetani)!
Nilitarajia Mungu angesema "uzao wa mwanaume" utakiponda kichwa cha nyoka... Kwa sababu watoto hutoka katika viuno vya baba zao na matumbo ya mama ni kiwanda tu cha kuumbia miili yao!
Mungu hakukosea kutoa tamko hilo, Mungu alijua ili mwanaume alete mabadiliko ya maana duniani anahitaji nguvu kubwa iliyomo ndani ya mwanamke!
Ndio maana jukumu la ukombozi wa mwanadamu akalifunga kwenye "uzao wa mwanamke/ uzao wa tumbo lake" na hili kuthibitisha nguvu kubwa ya mwanamke- Yesu alizaliwa kupitia MWANAMKE BIKIRA bila kumshirikisha mwanaume.
Hii yote ni kutuonesha kuwa Kibiblia mwanamke si chombo dhaifu bali ni mbeba kusudi kubwa na aliyepewa nguvu ya kufanya mambo makubwa yatokee endapo ataheshimiwa, kuaminiwa na kupewa nafasi ya kumsaidia mwanaume!
Biblia inasema apataye mke (mwanamke aliyemuoa) apata KITU CHEMA (Mithali 18:22).
Mungu anajua amewekeza ndani ya mwanamke HAZINA ZA AJABU MNO ambazo mwanamke huyu anaweza kuzitumia KUJENGA nyumba, kanisa, taifa na dunia endapo atapewa nafasi na kuaminiwa kama msaidizi mwenye nguvu na madini mengi ndani yake (Mithali 14:1).
Point:
*Linapokuja suala la kusudi halizuiwi na jinsia, kila mtu mme na mke wote wana kusudi na maono ya kutimiza.
*Mwanamke si dhaifu na asiye na sauti; Mwanamke ana nguvu kubwa ambayo ikiheshimiwa na kupewa nafasi itazaa miujiza ya kupita kawaida.
* Mungu tangu mwanzo alikusudia "mwanaume na mwanamke" washirikiane kutimiza maono na hatma njema aliyowakusudia na si mwanaume pekee.
* Shetani baada ya kuona wanadamu wamekubali uongo kuwa "mwanamke si kitu" Yeye akaanza kumtumia mwanamke huyohuyo kuharibu kila kitu duniani.
Mfano: Watu wanauza magari lakini wanaweka picha za wanawake wakiwa na sidiria na chupi tu. Unajiuliza kuna uhusiano gani kati ya gari linalouzwa na mwanamke aliye nusu uchi na ufunguo wa gari mkononi.
Angalia miziki na movie zote, wanawake ndio wanaotumika "kuleta mvuto" ili kuwapata wengi na kuwaharibu.
Shetani amejua na anaelewa mwanamke si duni bali ni "kitu chema" tena "msaidizi" (maana yake mwenye nguvu kuliko anayehitaji msaada) hivyo anamtumia vibaya kuharibu mambo makubwa ya Mungu.
Katika Biblia kuna wengi sana ambao maisha yao yaliharibiwa na wanawake kwa vile tu Shetani alijua nguvu yao na kuwatumia kuharibu maono, mipango na makusudi makubwa yaliyopaswa kutokea duniani.
Alikwama kwa Yusufu baada ya Yusufu kujitambua "Yeye ni nani" la sivyo ndoto na maono yake makubwa yangeishia kwenye mapaja ya mke wa Potifa (Mwanzo 39:1-9).
Lakini alimharibu Rubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo kwa kulala na kimada wa babaye.
Akamharibu Samson kupitia Delila.
Akamharibu Suleimani kupitia wanawake.
Akamharibu Ahabu kupitia Yezebeli mkewe.
Hii ni mifano ya mwanamke alivyo na nguvu kubwa kuliko ambavyo Shetani amewadanganya wengi ili kupitia mwanamke huyuhuyu amtumie kuiharibu dunia na makusudi makubwa ya Mungu.
*Mwanamke na mwanaume wote wana maono na makusudi makubwa yanayoweza kuigeuza dunia yao.
Somo litaendelea.....
Mwl D.C.K
www.yesunibwana.org
+255 753 466 675
+255 655 466 675
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.