SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO (2)SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO

MNENAJI: Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila

MAHALI: MORAVIAN MOSHI MJINI

Tulipoishia sehemu ya kwanza;
*Mwanamke na mwanaume wote waliumbwa kwa sura na mfano wa Mungu/ asili ya Mungu ndani yao (Mwanzo 1:27).
Na hii "sura na mfano wa Mungu" ni asili ya Mungu ambayo inasukuma uwezo wa "kutengeneza picha na mawazo" ya kuifanya dunia na maisha yawe bora.

* Mungu alipotamka suala la kumilki, kutawala na kutiisha nchi na rasilimali zake hakumuongelea mwanaume tu, bali alitamka jukumu hilo kwa wote (Mwanzo 1:28).

* Mungu alipotamka "baraka" ya kuzaa (kufanya vitu vitokee) na kuongezeka (uwezo wa kufanya vitu vidogo vilivyobuniwa kwa mawazo na picha ndani ya mtu vikue na kugusa maisha ya maelfu hata mamilioni), hakuisema kwa mwanaume tu bali kwa wote mwanaume na mwanamke. Hii ina maana kwamba wote mwanamke na mwanaume linapokuja suala la kuzaa vitu (kuanzisha, kubuni, kutengeneza na kuzalisha mambo makubwa) wote wako sawa. Na pia linapokuja suala la kuongezeka (nguvu ya kupanuka na kuzidi) wote wanayo hiyo kitu ndani yao.

* Jumla ya yote hayo ni hii, "Linapokuja suala la Maono, ndoto na kusudi la maisha" hakuna kizuizi cha jinsia. Wote mwanaume na mwanamke kila mmoja ana maono. Kila mmoja ana ndoto. Kila mmoja ana kusudi kubwa na maalum asilokuwa nalo yeyote isipokuwa yeye tu.
Hivyo tunapojifunza hii shule ya maono ni vema kila mmoja akajua NINAZUNGUMZA NAYE KIBINAFSI NA BILA KUJALI JINSIA YAKO. Kusoma sehemu ya kwanza BONYEZA HAPA

Mwendelezo wa somo;

Mambo ambayo hayawezi kuwa kizuizi cha mtu kutimiza maono yake;

1. Jinsia
Jinsia si kizuizi cha wewe kufanya mambo makubwa kwa utukufu wa Mungu.
Wanawake wengi wameshindwa kufanya mambo makubwa kwa sababu "Mfumo wa kishetani" wa dunia hii unawagandamiza wanawake na kuwafanya waonekane kana kwamba hawawezi kufanya vitu vikubwa kuliko au sawa na wanaume.
Huu ni uongo wa Shetani. Kusudi la Mungu si mwanamke awe mnyonge na asifanye mambo makubwa.

Mungu anasema "kila alichokiumba (akiwemo mwanamke) ni chema" (Mwanzo 1:31).
Mungu anamtaja "mke kama KITU CHEMA NA MSABABISHA KIBALI KWA MWANAUME ampataye" (Mithali 18:22).
Mungu anamuita mwanamke "MSAIDIZI" wa mwanaume ikiwa na maana ni "RASILIMALI YA AJABU" iliyobeba vile asivyoweza mwanaume na asivyokuwa navyo mwanaume. Siku zote anayesaidia ANA UWEZO MKUBWA kuliko anayesaidiwa. Mwanamke ni chombo cha thamani na cha ajabu endapo atajitambua na kuji-define kwa NENO LA MUNGU linavyomuita na kumtaja na si uongo wa dunia unavyomtaja na kumuita.
Jinsia si kizuizi cha kukamilisha maono na kusudi kubwa ulilobeba.

2. Umri mdogo;
Wengi wanajitetea kwamba wao ni "wadogo" hivyo hawana uwezo wa kuleta IMPACT kwa dunia yao.
Wengi wanasema "nikikua" nitafanya moja, mbili, tatuu.... Lakini huu ni uongo wa Shetani kukuzuia usitimize maono yako. Anataka uendelee kuota ndoto tu halafu ukija kushtuka umri umekuacha na haukujipanga kuleta mapinduzi.

Mimi nina miaka 25 sasa... Kwa neema ya Mungu nagusa maisha ya maelfu kila siku, kila wiki na kila mwezi na mwaka... Sikusubiri niwe hivi nilivyo leo... Nilianza kufuatilia kitu cha utumishi nilichonacho tangu nikiwa darasa la saba... Niliokoka darasa la sita na darasa la saba tayari nilikuwa nawafundisha watoto wa sunday school... Sikusubiri mpaka nianze mikutano na semina kubwa kama Mwakasege... Ninakumbuka nilikuwa nakwenda makanisani kuomba nafasi ya kuhubiri... Wakinisikiliza tu mara moja, mlango unafunguka naanza kupewa matukio makubwa na hata kuandaliwa semina.

Nilianza kufundisha Neno la Mungu FACEBOOK mwaka 2009 mwishoni... Wakati wengine wakiiona kuwa SOCIAL NETWORK mimi kwangu ilikuwa madhabahu ya kutokea na kuwafikia wengi... Sikuwa na marafiki wengi niliowafahamu, hivyo nilikuwa NAJIPENDEKEZA kwa kutuma Friend request kwa marafiki wa marafiki zangu lengo likiwa WAKINIKUBALIA TU watayakuta masomo yangu na watapata kitu... Leo hii nina watu wanaofuatilia mafundisha yangu MAKUMI ELFU kule Facebook, WhatsApp, Viber, na kupitia website yangu ya www.yesunibwana.org .... Sikusubiri kila kitu kiwe sawa... Sikusubiri NIWE MKUBWA au nifikishe miaka 30 kama Yesu!!!

Nilikuwa nasoma Biography ya Benny Hinn, alianza utumishi na miaka 21.
Nilikuwa nasoma Biography ya Morice Cellulo, alianza huduma na miaka 14.
Nilikuwa nasoma biography ya T.L Osborn, Yeye na mkewe Daisy walianza huduma kama Wamishionari kule India akiwa na miaka 17 na mkewe miaka 16.
Nilikuwa nasoma biography ya Kenneth Haggin, alianza kazi ya Mungu akiwa na miaka 17 tu baada ya Mungu kumponya kimiujiza ugonjwa wa moyo uliolemaa na tatizo la damu lisiloponyeka.

Daudi alipakwa mafuta kuwa mfalme wa Israeli akiwa na miaka 16 tu.
Yusufu aliota ndoto (aliona maono) ya kuja kuwa mtu mkubwa na wa baraka kwa dunia yake akiwa na miaka 17 tu.
Katika kitabu cha Mambo ya Nyakati kuna Mfalme aliyeanza kutawala akiwa na miaka 8 tu, na akawa imara akatawala zaidi ya miaka 50.
Umri mdogo sio sababu ya wewe kutotimiza maono na ndoto kubwa uliyobeba.
Huu ndio muda wa kufanya mambo makubwa kijana mwenzangu.
Unabii wa siku za mwisho kwenye kitabu cha Yoeli 2:28, na Matendo 2:17 unasema "VIJANA WADOGO WATAONA MAONO" na wataongoza kizazi cha siku za mwisho kuleta mapinduzi makubwa katika SIASA, UCHUMI, HUDUMA, nakadhalika.

3. Umri mkubwa;
Kuna watu ambao kwa vile ana umri zaidi ya miaka 40 basi amekata tamaa, haoni kuwa anaweza kutimiza maono na ndoto kubwa alizobeba.
Huu ni uongo wa Shetani. Anataka akuzuie usiache alama kwa dunia yako. Anataka ufe na mbegu kubwa uliyobeba. Anataka ufe na hiyo biashara kubwa ndani yako. Anataka ufe na huduma hiyo kubwa unayoiona ndani yako. Anataka akuzuie usiishi hiyo ndoa uliyoiona na kuiota tangu ujana wako. Anataka ukate tamaa na kutoona kuwa kuna MLANGO WA KUTOKEA. Shetani anataka ujihukumu na kujilaumu kwa FURSA ULIZOPOTEZA ulipokuwa kijana na miaka kadhaa iliyopita.
Adui anajua ukianza kujilaumu, ukianza kujihukumu na kujilaani basi tena MKONO WA MUNGU hautakusaidia.
Shetani anaelewa kitu kikubwa anachokichukia Mungu ni KUKATA TAMAA, KUMUWEKEA MIPAKA, KUNUNG'UNIKA na MALALAMIKO.

Wewe si wa kwanza kufanya mambo makubwa katika UMRI MKUBWA.
Agenda ya Mungu ya SIKU ZA MWISHO katika Yoeli 2:28 na Matendo 2:17, WAZEE na WENYE UMRI MKUBWA wamejumuishwa.
Mungu anasema, "Wazee wetu WATAOTA NDOTO" na hapo wakithubutu kuzifanyia kazi zitatimia.

Nitolee mfano wa rafiki yangu na baba yangu Mchungaji wangu SOSTENESS LANGULA;
Huyu alikuwa na ndoto ya kuwa na degree... Akiwa na umri zaidi ya miaka 50 aliamua kurudi shule na mwaka jana amehitimu akiwa na miaka karibu 65.
Alifungua kanisa na kuanza kuchunga akiwa na miaka zaidi ya 55 baada ya kustaafu jeshini.
Kwa miaka zaidi ya 7 sasa amekuwa mchungaji kiongozi wa kanisa la EAGT Kiluvya Gogoni.

Kama baba yangu huyu ameweza kufanya vitu vikubwa katika umri wake huo mkubwa, kwanini wewe ujitetee kwa kutotimiza ndoto yako?
Biblia inasema "Wazee wataota ndoto"
Maadamu unaweza kusoma ujumbe huu, unaweza kupata picha kichwani/ moyoni ya kitu fulani cha kufanya; Hiyo ndoto, hilo wazo linaweza kuwa halisi.

*Kalebu akiwa na miaka 85 bado alikuwa na ndoto ya kumilki mlima uliokuwa urithi wake (Yoshua 14:6-13).
Na hakika alitimiza ndoto yake na kuwa mtu mkuu.

* Ibrahimu akiwa na miaka 75 alipoitwa na Mungu kufanyia kazi "Maono aliyonayo" (Mwanzo 12:1-4).
Na hakuna asiyejua mambo makubwa aliyofanya Ibrahimu.
Ukisoma kitabu cha Mwanzo utaona mambo mengi ya ajabu yalifanywa na "Mzee Ibrahimu";
- Ni mtu wa kwanza duniani kuanzisha "teknolojia ya kuchimba visima" kwa ajili ya umwagiliaji na kunywesha mifugo yake.
-Akiwa katika umri huo mkubwa aliongoza wafanyakazi wake na kuwapiga vitani wafalme wanne waliokuwa wamemteka Lutu mpwa wake (Mwanzo 14).
Katika umri wake huo mkubwa aliweza kuacha rekodi ya ajabu ambayo tunaisoma leo.

Hakuna sababu ya kutotimiza maono, kusudi na ndoto ya Mungu maishani mwako kwa sababu ya umri mkubwa... Kumbuka agenda ya siku za mwisho inasema "wazee wetu" wataota ndoto!
Kama Ibrahimu unaweza kuota ndoto.
Kama Kalebu unaweza kuota ndoto.
Kama Sarah unaweza kuota ndoto.
Umri mkubwa si kizuizi. Ukiacha kujilaumu na kujutia yaliyopita, Mungu atakupa hekima ya kukusaidia kuacha alama kwa dunia yako.
"Usiyakumbuke mambo ya kwanza na wala usiyatafakari mambo ya zamani. Kwa maana nitatenda jambo jipya nalo litachipuka sasa nanyi mtaliona..." (Isaya 43:18-19).

4. Kutokuwa na elimu au kuwa na elimu ndogo;

Kuna watu wamekwama kutimiza ndoto na maono makubwa waliyobeba kwa kisingizio cha elimu waliyonayo au kwa kutokuwa na elimu kabisa.

Mimi ni shabiki na mfuasi mkubwa wa elimu. Kama kuna fursa ya kuongeza elimu itumie ukasome. Ila kama hakuna uwezekano bado hilo si tatizo wala kizuizi cha wewe kutimiza maono na kusudi kubwa ulilobeba.

Nuhu aliyetengeneza Safina (meli ya kwanza) hakusoma kokote Marine engineering... Hakusoma "Law of floatation" wala "Archimedes principle" lakini hakushindwa kutimiza kusudi lake.
Maadamu una moyo wa kunyenyekea na unaweza kutega sikio lako na kutii anachokuambia Mungu, kama alivyofanya Nuhu, unaweza kutimiza ndoto zako kubwa na maono ya ajabu uliyobeba.

Smith Wigglesworth ni mtumishi mkubwa wa Mungu ambaye aliishi miaka ya mwishoni mwa 1800 na anajulikana dunia nzima kama "Mtume wa Imani" kwa sababu ya mafundisho yake, vitabu na hata audio zake na matendo makuu ya imani, miujiza na utendaji wa Roho mtakatifu katika huduma yake. Kwenye huduma yake Wafu zaidi ya 20 wamefufuliwa ikiwemo kumfufua mkewe Polly mara mbili alipofariki.
Lakini ndugu Wigglesworth hakuwa msomi. Hata kusoma na kuandika alifundishwa na mkewe!!
Lakini hiyo haikuzuia asitimize ndoto, maono na kusudi kubwa alilobeba kwa vizazi vingi.

Daudi hakuwa na elimu yoyote ya darasani. Alikuwa mchungaji wa kondoo alipopakwa mafuta kuwa Mfalme wa Israeli.
Na ndiye Mfalme Mkuu na anayeheshimiwa milele na Wayahudi.
Elimu haikumzuia kuacha alama kwa dunia yake.

Mtume Petro hakuwa na elimu yoyote ya maana ya darasani. Hata Nyaraka zake aliandikiwa.
Lakini hakuna asiyemjua Petro. Ni mtume aliyetukuka ambaye hata kivuli chake kiliponya wagonjwa.
Elimu si kizuizi cha kutimiza maono makubwa uliyonayo.

Somo litaendelea....
Mwl D.C.K
www.yesunibwana.org
+255 655 466 675
+255 753 466 675 
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.