SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO (3)SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO.

MNENAJI: Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila.

Huu ni mwendelezo wa somo hili ikiwa ni sehemu ya tatu ya somo.
Tulichojifunza sehemu ya pili ya somo:
"MAMBO AMBAYO HAYAWEZI KUZUIA MAONO YATIMIE" na nikazungumzia;
i) Jinsia
ii) Umri mdogo
iii) Umri mkubwa
iv) Kutokuwa na elimu au kuwa na elimu ndogo ya darasani.
Nilichambua kwa kina na kwa mifano ya kibiblia na mifano ya kawaida ya watu waliofanikiwa. Ni somo lililokuwa limesheheni sana, kama hukulipitia tafadhali lisome litakufungua sana. kusoma sehemu ya pili BONYEZA HAPA, chini ni mwendelezo wa somo sehemu ya tatu

Somo la tatu la leo;

KWANINI MUNGU ANATOA MAONO?
Mungu ni Mungu wa faida, hafanyi jambo lolote bila kukaa chini na kuangalia faida gani na kiasi gani atapata.
*Kabla ya kuumba nuru alitafakari na kuangalia faida ya nuru ukilinganisha na giza.
*Kabla ya kufanya wingi na utele kwanza alitafuta faida yake zaidi ya ukiwa na utupu uliokuwepo.
*Kabla ya kuumba nchi kavu kwa kusukuma maji yajitenge na nchi kavu na kujikusanya alishaangalia na kujua faida ya kuwa na nchi kavu na nini itampatia kuliko akikaa na maji tu.
Tangu mwanzo, Mungu hafanyi chochote anachofanya bila "kusudi" na bila faida kubwa ndani yake.
Hii inatusukuma kulipitia Neno la Mungu ili kutafuta KWANINI Mungu anatoa MAONO kwa wanadamu.

 Zifuatazo ni sababu/ kusudi la Mungu kutoa maono kwa wanadamu;
1. Ili ajifunue katikati ya wanadamu;
Biblia inatuambia kuwa "Mungu ni Roho" (Yohana 4:24), na hivyo haonekani kwa macho ya kawaida.
Njia mojawapo anayoitumia kuipnesha dunia kwamba "yupo" ni kwa kuwapa watu maono ambayo wanaopewa na wanaoyaona yakitimia wote wanakiri kwamba HAKIKA KUNA MUNGU NYUMA YA HILO JAMBO.

 Kuanzia wazo au picha ndani ya mtu, mchakato mzima wa kulifanya liwe halisi, kudhihirika kwake nje na faida yake kwa mbeba maono na wote wanaoguswa na maono husika.
Biblia inasema, "Hakuna aliyewahi kumuona Mungu wakati wowote bali MWANA akaaye kifuani pake ndiye aliyekuja KUMFUNUA/ KUMDHIHIRISHA" (Yohana 1:18).

Kama ilivyokuwa kwa Bwana Yesu kumdhihirisha Mungu na upendo wake kupitia MAONO YA WOKOVU aliyokuwa amebeba, ndivyo ilivyo kwetu pia.
Tunamfunua Mungu na hekima yake kupitia MAONO aliyotupa na tukayatimiza dunia ikayaona kwa utukufu wake.
Biblia inasema "Sisi Wanadamu (hasa waliozaliwa mara ya pili) tu BARUA ZINAZOSOMWA NA WATU WOTE zilizoandikwa na Roho mtakatifu" (2Kor 3:2).
Kwa lugha nyepesi; Mungu ameandika ujumbe wake kupitia maisha ya mwanadamu, ukiuelewa na kuutendea kazi watu wataona uhalisi wa uwepo wa Mungu kupitia kile ulichoweza kufanya kugusa dunia yako.

 Mungu ni mme wa wajane lakini hatumuoni akipeleka mahitaji yao physically, anatumia watu.
Mungu anaitwa Baba wa yatima lakini hatumuoni akilipa ada zao na mahitaji yao physically bali ameweka huo mzigo ndani ya watu ili wafanye hayo kwa wanadamu.
Mungu anasisitiza kuhusu elimu anasema tusiiache tuishike sana, anasema tuyanunue maarifa na tusiyauze lakini hatumuoni akijenga mashule na vyuo bali anafanya hayo kupitia watu.
Mungu akitaka kujifunua katikati ya watu hupitia MAONO ALIYOMPA MTU.

Je, uko tayari Mungu akutumie kufanya mambo makubwa ambayo yatamfunua na kumtambulisha kwa wanadamu wengine?
"Bali WATU WAMJUAO MUNGU WAO watakuwa hodari na kutenda MAMBO MAKUU (kutimiza maono na ndoto kubwa kuliko uhalisia wao)" (Danieli 11:32b).
2. Ili atukuzwe katikati ya wanadamu;
Mungu anapompa mwanadamu anataka kupitia hayo maono, Yeye Mungu atukuzwe katikati ya wanadamu.

 "... Ili baba atukuzwe ndani ya mwana" (Yohana 14:13).
Mungu anataka dunia irudishe utukufu kwake kupitia kile unachokifanya kugusa na kuchangia kwenye maisha ya dunia yako.
"Mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, UMPATIAO MUNGU SHUKURANI kupitia kazi yetu (yale maono tuliyonayo na kuyatekeleza)" (2Wakorintho 9:11).
Kama ukiyatendea kazi maono uliyopewa na Mungu na yakaanza kugusa na kubariki maisha ya watu wengine, mwisho wa siku hao watu WATAYAONA MATENDO YAKO/ KAZI YAKO NJEMA NA KUMTUKUZA MUNGU (Mathayo 5:16).

Maono ni sauti na maelekezo ya Mungu ndani ya mtu. Ni kile ambacho kama Mungu angekuwa dunia angekuwa anafanya lakini anamchagua mtu mmoja aliye tayari na kumtumia kukifanya na mwisho wa siku utukufu wote hurudi kwa Mungu juu mbinguni.
"Kwakuwa ni Mungu atendaye kazi ndani yetu, Kutaka kwetu na kutenda kwetu kwa ajili ya kusudi lake jema" (Wafilipi 2:13).
Mungu anataka (will) na kutenda (do) kupitia sisi na mwisho wa siku anatukuzwa kwa vile tuzaavyo sana/ tuongezekavyo/ tustawivyo/ tuzidivyo na kuleta impact kwa dunia yetu (Yohana 15:8).
Sababu kubwa ya Mungu kumpa maono mwanadamu ni ili Mungu atukuzwe kutokana na ile alama ambayo huyu mtu anaiweka.

 "... Chipukizi nililolipanda mimi Mungu mwenyewe, ili Mimi NITUKUZWE" (Isaya 60:21).
Hivi ni kweli huna kitu unachoweza kufanya na kugusa maisha ya watu na wakamtukuza Mungu au kumshukuru kwa sababu yako?
Ni wakati wa kuamka na kufanyia kazi hilo wazo, ni wakati wa kuwa baraka kwa watu, amka ufanye kitu, usikubali kukaa na hilo wazo wala hiyo ndoto, acha Mungu atukuzwe kupitia alama unayoweka kwa watu wengine!
3. Ili atatue changamoto walizonazo watu au kujibu uhitaji wao;
Mungu husikia kilio cha wanadamu duniani. Na hili kukijibu HUWEKA SULUHU KUPITIA MTU na suluhu hii huwa ni maono ndani ya mtu.
Mtu hupata picha ya kitu ambacho akikifanya kitagusa na kutatua changamoto za watu. Na hilo huwa ni jibu la Mungu. Huwa ni Mungu akitatua changamoto.
"BWANA akasema, Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimesikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi wao; maana nayajua maumivu yao. Nami nimeshuka niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe katika nchi ile, hata nchi njema, kisha pana, nchi ijaayo maziwa na asali..." (Kutoka 3:7-8).

Ukisoma hilo andiko hapo juu utagundua ni "agenda" ya Mungu kugeuza na kuboresha maisha ya watu na kutatua changamoto zao. Anaona mateso yao. Anasikia kilio chao. Na anayajua maumivu ya wanadamu. Na amekusudia kuyatatua yote yanayowaumiza na kuwapa maisha mazuri lakini hafanyi hayo physically, HUSEMA NA WATU KUPITIA MAONO (Mawazo na ndoto fulani za kujenga na kugeuza maisha ya wengi)!
Kila wazo la kuanzisha huduma, biashara, kipindi fulani cha TV au radio, au kufanya chochote cha kuwahusisha watu kwa namna chanya ni JIBU LA MUNGU KWA KILIO CHA WATU WAKE ambao wewe ndio target yako!
Ukishakuwa na ufahamu kuwa hilo jambo jema unalotaka kufanya ni jibu la Mungu kwa dunia yako hauwezi kuogopa maana Mungu mwenyewe ata-back up hilo wazo na hiyo ndoto iwe halisi.
"Nisikilizeni enyi visiwa; tegeni masikio yenu enyi kabila za watu mlio mbali sana, BWANA ameniita tangu tumboni; Toka tumboni kwa mamangu amenitaja jina langu. Naye anifanya kinywa changu kuwa kama upanga mkali..." (Isaya 49:1-2).

Mungu amekuumba duniani ili akutumie kuleta masuluhisho kwa wanadamu.
Wewe ni silaha ya Mungu katika kuleta suluhu kwa dunia yako.
Wewe ni kimbilio la mjane, ni jibu la yatima, na ni mvika walio uchi (Mathayo 25:31-41).
Mungu amekupa hilo wazo na hayo maono ili ulete suluhu juu ya watu wanaolia na walio matesoni wakitaka suluhu katika hilo eneo la maisha unalojisikia kujikita hapo; Inaweza kuwa biashara, huduma, kufundisha aina fulani ya watu, kuandaa events mbalimbali zinazowajenga na kugeuza maisha ya wengi, huduma na kingine chochote unachokiona ndani yako.

 "Roho wa BWANA yu juu yangu, naye amenitia mafuta kuwahubiria masikini habari njema, kuwafungua waliofungwa na kuwaweka huru waliosetwa..." (Luka 4:18).
Ni aidha una habari njema kwa dunia yako au una kitu kikubwa kitakachofungua na kugeuza maisha ya wengi.
Wewe si mtupu, wewe umejaa majibu na suluhu kwa dunia yako.
Usikubali kukaa tu na hayo majibu moyoni yatoe nje, washirikishe watu sahihi, omba ushauri kwa waliofanikiwa, ongeza ujuzi kuhusu hilo jambo.
"Dunia yako inasubiri udhihirike na kuleta suluhu iliyosubiriwa vizazi vingi" (Warumi 8:19).
4. Ili ajenge msingi kwa ajili ya vizazi vingi vijavyo;
Mungu anapompa Mwanadamu maono ni ili aweke msingi kwa ajili ya vizazi vingi vijavyo.
Mungu alipoweka wazo la simu ndani ya Alexander Bell, ni wazo hilohilo ambalo limekuja baada ya mamia ya miaka kuendelezwa na kuwa simu zetu smartphones tulizonazo.

 Kupitia kwa Alexander Bell Mungu aliachilia kitu kwa ajili ya vizazi vingi vijavyo.
Wright Brothers ambao ni waasisi wa wazo la "vyombo vya anga" yaani uwezekano wa kuwako vyombo vinavyoelea angani, waliweka msingi kwa ajili ya vizazi vingi vijavyo. Na kizazi chetu kimetumia maono yao kutengeneza vifaa vya namna nyingi vya anga.
Maono yao yametumika kujenga msingi wa vizazi vingi baada yao.
Hii ndiyo sababu ya Mungu kutoa maono. Anataka kuachilia mbegu kwenda vizazi vingi vijavyo.
Ndani yako kuna mbegu ya vitu ambavyo vizazi vijavyo watavihitaji. Usipovifanyia kazi na kuruhusu vifie ndani yako utakuwa umewadhulumu haki yao.

 " ... UTAINUA MISINGI YA VIZAZI VINGI..." (Isaya 58:12).
Huu ni wajibu wako. Ni wajibu wangu. Ni wajibu wetu kuinua misingi ya vizazi vingi.
Hayo maono, hayo mawazo, hiyo ndoto itatumika kujenga na kurahisisha maisha ya vizazi vingi vijavyo.
Umebeba mbegu ya muhimu sana kwa dunia yako ijayo. Usikubali kuwa mtu wa kawaida, una kitu cha kuchangia, usife nacho tafadhali.
"Utaiinua misingi ya vizazi vingi"
5. Ili ayape maana na thamani maisha ya mtu;
Unajua hakuna hata mtu mmoja ambaye ameumbwa bila kazi duniani. Kila mmoja wetu una kitu ndani yako cha kipekee unachopaswa kuipa dunia yako.
"Kabla hujazaliwa Mungu alikujua na alikutenga kwa kazi maalumu" (Yeremia 1:4-5).
"Mungu alikuita kwa jina lako hilo ukiwa bado hata wazazi hawajajua jinsia yako" (Isaya 49:1-2).
Wewe si bahati mbaya. Wewe ni mtu maalum sana. Una kitu cha pekee na hazina za ajabu za kuipa dunia yako toka kwa Mungu.

 Kila chema unachokiona ndani yako kinaweza kutimia na kutokea na kukupa heshima na thamani kati ya wanadamu.
Mungu anapokupa MAONO anataka dunia ijue kwamba nawe upo. Maono hayo uliyobeba ndiyo yatakayokutambulisha kwa dunia yako na kukutoa uliko kuwa mtu mkuu na mwenye heshima.
Mungu hutumia maono aliyokupa ukiyafanyia kazi kukupa heshima na kukuinua katikati ya waliokudharau (Isaya 49:7).

 Mungu ameshakupa kitu cha kukupa heshima na kukufanya "mtu kati ya watu" na hicho kitu ni hayo mawazo, ndoto na picha ulizonazo ndani, chukua hatua na Mkono wa Mungu utakusaidia.
Mungu aliyekuita tangu tumboni kwa mamako hataki uwe mtu mdogo, anataka kukufanya kuwa "ishara na ajabu" kwa dunia yako zitokazo kwa Bwana akaaye Sayuni (Isaya 8:18).
Kazi ni kwako kuamua kuipa dunia hicho ulichobeba. Tunasubiri kuiona thamani yako kubwa iliyokuwa imefichika. Wakati wako umefika.

 "Inuka uangaze kwa maana nuru yako imekuja na utukufu wa Mungu umekuzukia" (Isaya 60:1).
Ni wakati wako wa kung'aa!
Somo litaendelea......
Mwl D.C.K
www.yesunibwana.org
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.