SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO (4)
SOMO: NGUVU YA MAONO KATIKA KUAMUA KIWANGO CHA HATMA YAKO
MNENAJI: Mwalimu Dickson Cornel Kabigumila.
Tulikoishia sehemu ya tatu;
KWANINI MUNGU HUTOA MAONO KWA WATU?
i) Ili kujifunua kwa wanadamu
ii) Ili kujitukuza mbele za wanadamu
iii) Ili kutatua changamoto na vilio vya watu
iv) Ili kuweka msingi kwa ajili ya vizazi vingi vijavyo
v) Ili kuyapa thamani na maana maisha ya mbeba maono
Niliyazungumzia kwa kina mambo haya, ili kujifunza zaidi tafuta somo hili sehemu ya tatu.

Sehemu ya nne;
Tabia za Maono ya Kimungu;
Utajuaje kuwa hayo maono uliyonayo ni maono ya Kimungu?
Zifuatazo ni tabia au sifa za maono yoyote ya Kimungu;
1. Huwa ni ya mtu mmoja na si kikundi cha watu;
Maono ya Mungu humjia MTU MMOJA na si kikundi cha watu.
*Ibrahimu aliona maono ya kuwa Baba wa mataifa na kuwa na uzao kama mchanga wa bahari akiwa peke yake, hata mkewe Sara hakujua.
* Nuhu alipata maono ya kujenga safina kwa sababu mvua kubwa ilikuwa ikija juu ya nchi na aliyapata peke yake, mkewe na watoto hawakuwepo.
*Isaka akiwa peke yake alipata maono ya kupanda mbegu wakati wa kiangazi na akavuna mno kiasi cha kuwa na uchumi mkubwa kuliko taifa zima la Wafilisti, mkewe Rebeka hakujua wala wanae Esau na Yakobo.
* Rebeka akiwa peke yake alipata maono kuhusu mimba ya mapacha aliobeba, ya kuwa mkubwa atamtumikia mdogo, mmewe Isaka hakujua na alitaka kumpa baraka Esau asiyestahili kwa sababu hakuwa ameyajua maono.
* Yusufu akiwa kijana mdogo aliona maono ya kuja kuwa mtu mkubwa kuliko ndugu zake na ya kuwa atawatunza, ndugu zake na wazazi wake hawakuona, na hata alipojaribu kuwashirikisha ilileta uadui.
* Musa akiwa peke yake anachunga kondoo wa Yethro mkwewe alipata maono ya kuwatoa nduguze kutoka utumwani Misri, mkewe Spora hakuwepo wala baba mkwe wake kuhani Yethro.
* Kahaba Rahabu akiwa peke yake bila kujali ya kuwa ni kahaba na mtenda dhambi aliyedharauliwa akiwa peke yake alipata maono na kujua kuwa Israeli watauangamiza mji wake, akafanya mikakati ba michakato ya kuwa rafiki yao na akajiponya yeye na ndugu na wazazi wake na kuingia kwenye orodha ya ukoo wa Yesu.
* Mariamu akiwa peke yake alipata maono ya kumzaa mwokozi wa ulimwengu na hakujiuliza itakuwaje mchumba wake Yusufu na wazazi wake watachukuliaje.
Sikiliza mpendwa wangu, Mungu huwa anafanya kazi na mtu mmoja anayemuelewa, halafu wengine huelewa baada ya kuona "mwanga" na "impact" ambayo yule mbeba maono ameanza kuileta.
(Zaburi 14:2, Ezekieli 22:30).
Jiandae, Watu hawatayapokea maono yako wala kuyakubali mpaka watakapoona nuru fulani imeanza kutokea;
Hakuna aliyekubaliana na Yusufu. Wazazi wake walimpinga, ndugu zake walitaka kumuua, na waliposhindwa walimuuza awe mtumwa.
Lakini Yusufu hakusubiri watu wakubali alichobeba, aliendelea kuamini ndoto yake na mwisho wa siku ilitimia.
Hakuna aliyekubaliana na Nuhu ya kuwa gharika kubwa itakuja. Hakuna aliyekubali kuwa watu wote wataangamia. Hakuna aliyewahi kuona chombo kikielea juu ya maji, walimshangaa na kumuona kichaa alipotumia miaka 40 kutengeneza safina ambayo hawakuwahi kuiona kabla.
Hakuna aliyemuelewa Musa aliposema ana maono ya kuwatoa Israeli utumwani. Hata Waisraeli hawakumwamini. Walimuona mzee wa miaka zaidi ya 80, atafanya nini huyu?
Mpaka walipoziona "ishara" alizokuwa nazo!
Hakuna aliyemuamini Daudi kwamba anaweza kumpiga na kumuua Goliati, wote walisema ni kijana mdogo, wote walisema huna uzoefu, wote walisema hayo maono yako yatakutokea puani kijana (1Samweli 17),
Mpaka alipowasimulia "aliyokwishaanza kufanya" (kuua dubu na simba akiwa machungani) ndipo wakaamini ana kitu!
Hata Yesu alipoanza kazi ya kutimiza Maono yake aliyobeba, Watu wa mji wake hawakukubali kuwa ana kitu cha ziada, hawakumpa mkono wa shirika. Walipoziona Ishara alizofanya ndipo walipoulizana "ameyapata wapi haya? Na hizi kazi anazofanya na hekima hii kubwa kaitoa wapi huyu mwana wa seremala?"
Cha kujifunza;
- Hakuna maono ya Kimungu yanayokubalika haraka.
- Kama Mungu amekupa maono, usipoyaamini wewe na kuyafanyia kazi hakuna atakayefanya kwa niaba yako.
- Usitake watu wakuelewe na kukuamini kwenye maono uliyobeba, wao hawaoni unachoona, hawana picha uliyonayo.
- Watu huanza kukukubali na kukupa mkono wa shirika pale wewe unapoanza kuyafanyia kazi maono yako na wakaona na kupata picha ya unachofanya.
- Ukisubiri watu wayakubali maono yako kwanza ndipo uanze utakufa nayo.
- Kama Mungu amekuamini na kukupa maono, wewe na Mungu mnatosha kuyafanya kuwa halisi, Msingi wa maono yoyote ya Kimungu hujengwa na mtu pamoja na Mungu aliyempa maono.
2. Maono ya Kimungu huinua vita na upinzani;
Maono yoyote ya Kimungu yamebeba suluhu kwa maelfu ya watu, yamekusudia kumtambulisha na kumuinua Mungu na Ufalme wake, yamekusudia kuweka msingi wa vizazi vingi, yamekusudia kumpa mbeba maono maana na heshima katika kizazi chake na dunia yake.
Na Shetani asingetamani haya yatokee. Atainua vita ya ajabu ambayo hukuitarajia.
Atawatumia hata ndugu zako wa damu na marafiki wa karibu kukupiga vita na kukuzuia kama ilivyokuwa kwa Yusufu na Daudi.
Atawatumia watu ambao walipaswa kukutia moyo na kukuonesha njia kuanza kukuzuia na kukuzima kama alivyofanya kwa Daudi akimtumia Sauli ammalize. Kama alivyomtumia Mfalme Herode kutaka kummaliza mfalme Yesu.
Utashangaa watu ambao ulitarajia watakupa msaada na kukuelewa ndio wamekuwa adui zako.
Maono huleta upinzani, Maono huleta maadui.
Ukiona hivi ujue tayari Ufalme wa giza umejua una kitu cha ajabu umebeba. Usipoteze muda kupigana na wanadamu au kuyaacha maono yako, ni wakati wa kuomba zaidi na kuendelea kufanya vitu kimya kimya.
Utashangaa baada ya muda Mungu amekomesha upinzani na umeanza kupenya.
Lakini ukiangalia upinzani utapoteza maono ambayo yamebeba thamani kubwa ya maisha yako.
Ili upate maziwa usiogope mateke ya ng'ombe.
Ili upate asali mzingani usiogope ukali wa nyuki.
Ili umuue Goliati na kupata heshima yako halisi usisikilize sifa ya Goliati na walioshindwa kumuua bali jikumbushe yale ambayo umewahi kuyafanya kwa mkono wa Mungu yawe chachu ya kukupa hatua nyingine!
3. Maono yoyote ya Kimungu hayasubiri uwe na kila nyenzo na rasilimali ya kuyafanya halisi, yanataka uanzie hapo ulipo ukiwa na mtaji wa Maono yenyewe kama ramani, Mungu aliyekupa maono, Imani katika Mungu, faraja ya Neno la Mungu, akili na ufahamu wako huohuo mdogo ulionao, watu wachache hao hao wanaoamini kuwa unaweza na muda wa masaa 24 uliyonayo kwa siku!
Huu ni mtaji mkubwa sana... Watu, pesa na fursa nyingine vitakujia ukichukua hatua ya kwanza!
Malaika alipomtokea Gideoni wakati amejificha akipepeta ngano hakumpa kila kitu, alimpa "cha kufanya" (kuwapiga Midiani), halafu akampa utambulisho wake halisi "Salaam Eee Shujaa Mkubwa" badala ya alivyokuwa akijichukulia na kuchukuliwa na watu wengine, halafu akamwambia "Enenda kwa uwezo wako huo" (hicho hicho ulichonacho) nawe utawapiga Midiani kama unapiga mtu mmoja (Waamuzi 6).
Mungu anataka "uanze hapo ulipo na hicho kidogo ulichonacho"
Ushuhuda wangu:
Mwaka 2009 nilikuja Dar kusoma chuo pale DIT, nikiwa pale nilijifunza kutumia kompyuta.
Mwaka ule baada ya kujifunza kutumia kompyuta nikakiunga na mtandao wa kijamii wa Facebook, wakati ule usingeona post hata moja ya Neno la Mungu.
Kwangu niliona ile ni fursa, nikaanza kuandika post zenye jumbe za Neno la Mungu, kwa zaidi ya Mwaka sikupata hata "Like" moja... Lakini hiyo haikunikatisha tamaa, nilijua kuna watu wanasoma na kuna watu wanabadilika. Baada ya muda Watu waliookoka walipoona ninachofanya nao wakaanza kupost jumbe za Neno la Mungu. Mapinduzi yakawa yametokea. Watu wakaanza kulike na ku-comment post zangu na ku-share na wengine!
Miaka miwili na nusu baadaye rafiki yangu niliyesoma naye "Chekechea" aitwaye Newton Deus (Admin wa website yangu ya www.yesunibwana.org) akanitafuta na kunishauri nifungue blog ili masomo yasije kupotea, nikamjibu nikamuambia sina utaalamu katika hilo! Huyu rafiki akaniambia nimpe tu jina la blog ninalotaka yeye atashughulikia kuitengeneza na kuhamisha post kutoka Facebook kwenda blog, na nisimpe chochote hiyo ni sadaka yake kwa Mungu! Na huu ndio ulikuwa mwanzo wa www.yesunibwana.org website ya kiswahili ya Neno la Mungu ambayo kwa mwaka jana imetembelewa na watu karibu 70, 000 kwa mwaka mmoja tu. Imetembelewa na watu kutoka mataifa zaidi ya 54 duniani... Kwa mwaka jana tu nimepata watu waliookoka baada ya kusoma mafundisho na kunitafuta zaidi ya 100, na mamia wengi waliokuwa wamerudi nyuma, wagonjwa, wenye shida na walioteswa na nguvu za giza waliofunguliwa.
Sasa nahubiri redioni, nafanya semina kubwa na makongamano mengi yanayogeuza maisha ya wengi.
Lakini nilianza na ukurasa wangu wa facebook. Sikusubiri kila kitu kiwe sawasawa!
Mwalimu Christopher Mwakasege aliwahi kusema, "Vijana wengi wanataka kuwa kama Mwakasege, wajaze viwanja namna hii lakini hawajui NILIANZA NA MTU MMOJA SEBULENI KWANGU"
Ayubu 8:7;
"Japokuwa mwanzo wako ulikuwa mdogo lakini huo mwisho wako ungeongezeka sana"
Ni muhimu ujue hili;
"Kila kilichozaliwa na Mungu huanzia chini na kukua kuwa kitu kikubwa cha baraka"
- Mbegu zote huanza chini mchangani kabla ya kuwa mavuno makubwa
- Watu wote maarufu na wakuu waliowahi kuishi duniani walianza kama mimba tumboni kwa mama zao.
- Jua halianzi na mionzi mikali na ya joto bali huanza kama nuru tu ya mapambuzuko lakini huzidi kukua na kuongezeka na kuwa jua kali.
Kila kilichotoka kwa Mungu huanza chini na kukua kuwa kitu cha baraka kwa wengi.
"Kama chembe ndogo ya haradali (ndogo kuliko ya mtama na ulezi), lakini hukua na kuwa mti mkubwa uletao kivuli kwa wanyama wengi wakubwa, na ndege huja na kujenga viota vikubwa juu yake"
Usisubiri upate kila kitu ili uanze kutimiza ndoto, mawazo na picha uliyonayo, anzia hapohapo ulipo!
4. Katika maono yoyote ya Kiungu upinzani na changamoto ni madarasa ni maandalizi kwa ajili ya hatua kubwa mbele;
Mungu hutumia upinzani, vita na changamoto anazopata mbeba maono kama njia ya kumsogeza karibu na Mungu, kujenga imani yake, kumfundisha uongozi, kumpa uzoefu, kumkosoa, kumuimarisha, na kumuandaa kwa hatua kubwa za utukufu mbele.
* Yesu asingekuwa bora kama asingepata upinzani toka kwa walimu wa dini, na wapinzani wake wengi, walimuongezea vitu vingi.
* Yusufu hakuwalaani na kuwakasirikia ndugu zake bali alisema, "Ninyi mlitumiwa na Mungu kunifikisha hapa... Mlikusudia mabaya lakini Mungu aliyatumia kunipa mema na kunifikisha kwenye hatma yangu"
* Daudi hakumchukia Mfalme Sauli wala hakupigana naye, alimchukulia kama darasa lake, alijifunza kwake, hata alipopata nafasi za kumuua hakumuua.
Alijua njia ya kwenda "next level" haihitaji watu ambao hawabebi misamaha na kuachilia. Alijua akianza kuwalipa mabaya adui zake atapanda mbegu mbaya itakayomsumbua.
Aliacha Mungu afanye hukumu.
(Warumi 12 ina mwongozo mzuri sana)!
Changamoto na hali unazopitia sasa zinakuandaa kwa hatua kubwa na bora za maisha yako!
"Ujapopita katika moto hautakuunguza, wala maji mengi hayatakugharikisha" (Isaya 43:2).
"Nijapopita katika bonde la uvuli wa mauti sitaogopa mabaya maana wewe u pamoja nami" (Zaburi 23).
Mistari yote hiyo miwili inatufunulia yafuatayao;
- Unapokuwa na maono hautapita "tambarare" tu utapita na mabondeni na milimani
- Kuna nyakati za kuumiza kama moto, na kuna nyakati unahisi unazama lakini Mungu hatakuacha kama wewe mwenyewe hautajikatia tamaa.
- Uzuri ni kwamba inasema "ujapopita" ikimaanisha "unapita" tu na hautakaa hapo milele, haleluya!
Unapita kaka, unapita dada, unapita mwanaume, unapita mwanamke... Barabara mbovu siku zote haizuii gari kwenda linapotakiwa kwenda... Barabara mbovu hutumia muda, mafuta na umakini mkubwa lakini kamwe haikatishi safari... Barabara mbaya ndicho kipimo bora cha dereva bora!
NB: Yarudie masomo haya mara nyingi uwezavyo, hautabaki ulivyokuwa...
Somo litaendelea.......

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.