SOMO: YAKUPASA KUMPENDA JIRANI YAKO

Mchungaji Gasper Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…
Siku moja katika pita pita zangu nalimuona binti mmoja,binti huyu alikuwa na tabia ya kuwachukia watu hata ambao walikuwa hawafahamiani nao,maana akiona mtu labda kapita mbele yake basi umuangalia mtu huyo kisha na kuanza kumtoa kasoro kwa vile aonekanavyo.Mfano anaweza kupita mdada mwenzake kisha ukamsikia akisema ;

”…Yaani huyu mjinga kweli! sasa ndo amevaaje hivyo! gauni baya,alafu hata kiatu alichokivaa akiendani na gauni wala bag…” Au kama mtu akipita na gari mbele yake anaweza akaliangaliaaa,kisha usema ” Gari yenyewe mmh! bayaa,sijui kwa nini kanunua gari kama hili,hata hivyo litaharibika tu,we subiri tuone,kwanza gari yenyewe ni ya bei rahisi…” N.K
Sasa,kinachoonekana kwa huyu binti ni roho ya chuki iliyo ndani yake,kwa sababu huwezi kumchukia mtu usiye mfahamu kabisa. Ile namna ya kusema ” Huyu mjinga kweli,sasa ndio amevaaje !!!…” Hiyo pekee inatambulisha roho ya uasi iliyo ndani ya huyu binti.Huu ni mfano mdogo wa mtu mmoja tu kati ya wengi wenye kufanana naye.
Leo hii wapo watu wengi wa namna hii,tena cha ajabu ni pale unapokutana na mpendwa katika Bwana akiwa amejawa na roho ya chuki kwa wengine hata kama hawajamkosea.Huko makanisani ndio balaa ! Sasa mimi najiuliza hivi; Ikiwa kama hatuna upendo,ukristo wetu unathamani gani? Au Ikiwa kama hatuna upendo thamani ya wokovu wetu ni nini?
Tuangalie jambo hili kibiblia zaidi.

Amri ya kwanza katika amri zote ni kumpenda Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote,kwa roho yako yote,kwa akili zako zote na kwa nguvu zako zote. Then Biblia inatuambia sasa ” Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi.” Marko 12:31
Ndiposa nami nikasema kwamba yakupasa umpende jirani yako. Kwa maana huwezi kumpenda Mungu,ikiwa unamchukia ndugu yako. ( 1 Yoh.4:20 ) Au huwezi kumpenda Mungu ikiwa unamchukia rafiki,jirani yako. Yeye ampendaye Mungu ni yule ampendaye jirani yake na kuwapenda wale wote wenye maudhi.
Siri kubwa ya kuwa mkristo safi ni kuwapenda watu wote pasipo kuangalia itikadi za dini zao,wala imani zao.
Mara nyingi Bwana Yesu amezungumza juu ya upendo akisisitiza tupendane. ( Yoh.13:34,Yoh.15:12) Bwana Yesu hakuwa mjinga kusisitiza upendo wa udugu,jirani,maana hakika palipo na upendo wa thati basi ujue upo umoja wa nguvu.Ndio maana hata maombi ya Yesu yalikuwa sisi tuwe na umoja.
Ukisoma katika Yoh.13:34,utaona Bwana Yesu akisisitiza tupendane kama alivyotupenda sisi. Ikumbukwe kuwa Yeye alituvumilia mno,akatupenda mno hata sasa tu mali yake. Anasema nasi tupendane kwa upendo huo,tuvumiliane,tuchukuliane na kuwaona wengine ni bora kuliko sisi. Tukiweza kuishi hivyo,basi ujue thamani ya maisha yetu ya wokovu yatakuwa na maana.
Shida iliopo katika kanisa la leo,ni kuchukiana. Hatuna upendo wa dhati kwa majirani,wala kwa ndugu tena huko makanisani utakuta mchungaji wa kanisa amesimama na kumsema mchungaji mwenzake wa kanisa jingine huku akiwa madhabahuni na cha kushangaza basi utakuta na wachungaji wenzake walioketi wakimsikiliza wanashangilia ujinga anaoongea mwanzao. Hii si sawa,na wala hatukuagizwa kufanya hivyo.
Bwana Yesu ametuagiza kuwapenda maadui zetu na kuwaombea wanaotuudhi. ( Mathayo 5:43-44 ). Hakuagiza tuwasema vibaya madhabahuni,wala hakuagiza tuwachukie bali tuwapende na kuwaombea.
Leo kumezuka aina mbaya ya maombi ya kuwapaka mavi wale wote wanaotuudhi. Utakuta mchungaji akiongoza maombi hayo ya kuwapaka mavi maadui zao,na wanamaombi uendelea kuomba,kwamba fulani ni adui yetu,basi nampaka mavi,namchafua…N.K
Au namfarakanisha,namlipua kwa moto…. Ukiuliza chanzo cha maombi hayo utaambiwa huyo wanaemuombea hivyo aliwaudhi. Sasa jamani ! Hapo ndipo nauliza,Neno linasemaje lakini? Neno si linasema tuwapende maadui zetu,na kuwaombea,kulikoni sasa kumpaka mavi,kwa toka wapi?!!!
Asili au chimbuko la maombi ya namna hii ni kutokuwa na upendo kwa wenzetu na kushindwa kulifahamu neno la Mungu linasemaje. Emu tuwaangalia wanafunzi wake Yohana na Yakobo ambao kuna kipindi walihitaji kuomba maombi ya maangamizo ya namna hii,
Wanafunzi hawa waliudhiwa na watu wa Samaria,sasa badala ya kuwapenda wale waliowaudhi,wakawachukia na kuanza kuowaombea vibaya kama wengine wenye kuwaombea vibaya wanauwaudhi,tusome;
Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya] ” Luka 9:54
Wanafunzi hawa walitaka kuwateketeza kwa moto maadui zao wanaowaudhi,wakati Yesu hakuja kuziangamiza roho za watu bali kuziokoa. Hivi ndivyo tuombavyo makanisani kwa habari ya maadui zetu,tunatamani wafe kwa sababu wametuudhi tu. Ikiwa tunawaombea mabaya ya namna hii,kuwapi kuokoka kwetu?
Mungu wa mbinguni atusaidie sana…
Wakristo wa leo wamesahau kuwapenda watu wote. Bali huchagua watu wa kuwapenda na wengine wakiwachukia. Sasa ipo faida gani ya kumpenda yule akupendaye tu na kumchukia akuchukiaye,maana hata watu wa mataifa hufanya hivyo. Bali sisi yatupasa kupenda zaidi,kuwapenda watupendao na kuwapenda watuchukiao.
Biblia inasema; ” Nasi tumelifahamu pendo alilo nalo Mungu kwetu sisi, na kuliamini. Mungu ni upendo, naye akaaye katika pendo, hukaa ndani ya Mungu, na Mungu hukaa ndani yake. ” 1 Yohana 4:16
Mungu wetu ameanza kwa kujitambulisha ya kwamba Yeye ni pendo. Biblia inasema,yoyote akaaye ndani ya pendo amekaa ndani ya Mungu,na Mungu pia hukaa ndani yake,kwa lugha nyepesio kabisa ni kwamba yeye asiyekaa katika pendo hawezi kukaa ndani ya Mungu.
Kwa lugha hiyo tunaweza sasa kumjua vizuri mtu wa Mungu ni mtu wa aina gani.Mtu wa MUNGU ni yule aliyekaa katika pendo. Tena nami nasema leo kwamba,ukiona mtu yeyote yule asiyekaa katika pendo basi ni dhahili kabisa hajakaa ndani ya Mungu,na kamwe hawezi kuwa mtumishi wa Mungu.
Nasema nawe mpendwa katika BWANA,thamani ya ukristo wako ni kukaa katika pendo kwa sababu pasipo pendo hakuna utakatifu. Tena pasipo pendo la kweli hakuna utumishi wa kweli wowote ule sana sana tutadanganyana tu! Biblia imeweka wazi,kwamba; ” Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao; ” Waebrania 12:14
Neno ” kuwa na amani ” ni kuwa na pendo. Msingi wa kuwa na amani ni kuwa na pendo,kwa sababu kama mtu akitafuta amani hana budi kutafuta pendo kwanza,kwa sababu amani ya kweli hutegemea pendo la kweli.Huwezi kuwa na amani na mtu ikiwa unamchukia,basi yeye mwenye amani ya kweli ni yule aliyekaa katika pendo. Kabla ya kuombea amani basi ombea tupendane kwanza.
Ikumbukwe kwamba upendo ni amri kuu,kwa sababu kila amri ya MUNGU hutimzwa katika pendo. Marko 12:28-33
Shida iliyopo leo katika makanisa yetu ni waamini kutokukaa katika pendo. Utakuta kuna hali ya malumbano baina ya mtu kwa mtu,kiongozi kwa mwamini,N.K
Haipaswi kabisa kuwachukia wenzeko kwa sababu ya udhaifu wao,bali tuwapende ili thamani ya wokovu wetu ionekane.

UBARIKIWE.
Kwa mawasiliano ya maombi na maombezi,nipigie 0655111149.
Mch. Gasper Madumla,
Beroya bible fellowship church.
MWISHO.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.