MASHAKA NA UOGA NI VIKWAZO VYA KUKUFIKISHA MAHALI UNAPOPASWA


Na Kelvin Kitaso,
GK Contributor.


Watu wengi wamekuwa wanatamani sana kuwa na maisha yaliyo bora na kuwa na hali njema kiroho lakini miongoni mwa vikwazo vya kuwa hivyo licha ya kile cha watu wa karibu yao/marafiki, changamoto nyingine ni uoga/mashaka.  
Uoga ni ile hali ya kusitasita kuthubutu kufanya mambo na kuweka mashaka kama matokeo yatarajiwayo yanaweza kutokea. Mara zote hali hii uambatana na maneno kama;

·    Sidhani.
·    Siwezi
·    Sijui.
·    Labda.
·    Nitajaribu badala ya nitafanya.

Kibiblia hii ni hali ya kukosa uhakika na ubayana juu ya mambo yatarajiwayo na mambo yasiyoonekana; yaani ni kukosa imani. Na kitendo hiki kinamfanya mtu wa Mungu kuishi maisha yanayomfanya Mungu asiwe na furaha kwa kuwa haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo kuwa na imani.

Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. 39 Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.”

Waebrania 10:6a “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza;…”

                Uoga ni kitendo cha kupungukiwa imani kwa kuingiwa na wasiwasi.

Marko 4:40 “Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”

Yesu anaweka uwiano wa maneno mawili ya ‘kuwa waoga’ na ‘kukosa imani’ Kwa kumaanisha kuwa wanafunzi waliogopa kwa kuwa hawakuwa na imani bado na kama wasingekuwa waoga ni matokeo ya kuwa na imani na kama wangekuwa hivyo Yesu angeweza kunena nao na kusema “hamkuwa waoga, mmekuwa na imani sasa”.

Wakati mmoja nikiwa natafakari neno pamoja na rafiki yangu tukafika mahali pa kutafakari ‘flexibility’ (kubadilika) kwa Mungu na kutafakari kuwa Mungu ni Mungu anayeweza kubadilika na uwezo wa kumfanya asibadilike (static) umewekwa mikononi mwetu wenyewe. Jinsi tunavyoweza enenda ndivyo tunaweza kumfanya Mungu atende yale aliyoahidi au asitende. Wana wa Israeli walipotolewa na Mungu katika nchi ya utumwa (Misri) waliambiwa wanaelekea Kanani (nchi ya ahadi) ila si kwamba  Mungu akupenda wao wafike Kanani bali ni wao wenyewe ndio waliuokuwa sababu ya kutofika kwao.

Waebrania 3:11-19 “ Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu.
12 Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.
16 Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?
17 Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?
18 Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?
19 Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.”

Kuna jambo Mungu anaapa tena kwa hasira na sababu kuu inayomfanya aape kwa hasira ni kukosa imani/uoga/kusitasita kwa watu wake hii ni kwa sababu alisema watu wake wanapaswa kuishi kwa imani na wakisitasita moyo wake hauna furaha nao.  

Watu wengi wamekuwa wakijifariji kuwa Mungu ameniahidia ni lazima itatimia ila ukweli ni kwamba ukiweka uoga na mashaka kamwe mambo hayo hayatatimia kamwe na itakuwa historia tu kama ilivyo historia ya wana wa Israeli kuwa waliahidiwa lakini hawakuweza kuingia Kanani isipokuwa uzao wao pamoja na Joshua na Kalebu.

Mpaka mtu anaogopa zipo sababu zinazomsababisha akaogopa na pengine zikawa ni sababu nzito, ngumu na za msingi sana za kumfanya mtu aogope, mara nyingi sababu hizo uwa kwa namna ya mazingira yanayomzunguka mtu kwa kutokuwa rafiki na yale ayatamaniyo, au jamii inayomzunguka si rafiki na hali aiendeayo na pengine unenewa maneno mabaya na kusikia mambo mengi ambayo yanamfanya yeye aogope.

“maneno ya wanadamu mara nyingi uleta uoga nakubomoa imani ila neno la Mungu uimarisha imani na kumpa mtu ujasiri”

Marko 4:35-40 “Siku ile kulipokuwa jioni, akaawaambia na tuvuke mpaka ng’ambo. 36 Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwa pamoja naye. 37 Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. 38 Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? 39 Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. 40 Akawaambia, mbona mmekuwa waoga? Hamna imani
Wanafunzi walizungukwa na mazingira yasiyotabiri kama watafika ng’ambo lakini wakasahau kuwa utendaji wa Mungu haufungwi na mazingira ambayo wapo.
Kumbukumbu la Torati 7:17-23 “Nawe kama ukisema moyoni mwako,mataifa haya ni mengi kunipita mimi;nitawatoaje katika miliki yao? 18 Usiwaogope; kumbuka sana Bwana Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote; 19 uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyooka, aliokutolea nje BWANA, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya BWANA, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa. 20 Tena BWANA, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.  21 Usiingie na kicho kwa sababu yao;kwa kuwa BWANA, Mungu wakoyu katikati yako, Mungu mkuu mwenye utiisho. 22 Naye BWANA, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu. 23 Ila BWANA, Mungu wako, atawatoambele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa”

Unaweza ukaona vita ni vikubwa sana kuliko vile ulivyo na wanaosimama kinyume nawe ni wengi kuliko ulivyo na hali hii ikatia uoga.

2 Wafalme 6:15,16 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake Yule mtu wa Mungu alipoondoka na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyaje? 16 Akamwambia, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”

Sababu ya kutokuogopa ni kuu sana ya zaidi ya sababu za kuogopesha, ikiwa Mungu yu upande wako uwezekano wa kushindwa ni asilimia 0% na kushinda ni 100%.

Hesabu 13:30-33 “Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. 31 Bali wale waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi, 32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya nchi waliyoipeleleza, wakasema, ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. 33 Kisha huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

Ni kweli uhalisia na muonekano wa adui zao ilikuwa ni sababu kubwa sana ya kuwasababisha kuogopa ila ule uzoefu wao waliowahi kumwona Mungu akifanya kazi toka Misri ilikuwa ni sababu kuu ya kuwafanya wasioogope, japo kuogopa kwa wale wengine kuliwasababisha wajione kama mapanzi na ndivyo walivyokuwa kwa kuwa ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Uonaji wa Mungu uko tofauti kwa kuwa Yeye aliwatazama kama mashujaa ila tatizo lilikuwa ni katika wao wenyewe kujiona kama mapanzi.

1 Samweli 17:8-11 “Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupinga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu akanishukie mimi. 9 Kama akiweza kupigana na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; name nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. 10 Yule Mfilisti akasema, nipeni mtu tupigane. 11 Basi Sauli na Israeli waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Pindi tu unapoingiwa na uoga ndipo unatoa mwanya wa kushindwa kwako. Ni vyema ukafahamu kuwa hakuna muoga ambaye alishawahi kufanikiwa katika maisha haya kwa kuwa waoga wote uogopa kuthubutu kufanya mambo kwa kuhofia kushindwa ila waliowahi kushinda ni watu waliokubali kufanya mambo pasipo kuogopa kushindwa na hata waliposhidwa walitumia kushindwa kwao kama fursa ya kuwapeleka katika hatua nyingine ya juu sana.

Wengine uogopa kufanya mambo kwa sababu tu walishawahi kuwaona watu wengine wanashindwa katika mambo hayo na katika fahamu zao wamekubaliana na mambo hayo, hii ni sawa na yale mawazo ya wale wapelelezi walioogopa kabla hawajaenda kutamalaki kwa wanefili. Waoga mara nyingi usema nitajaribu labda nitashinda lakini washindi mara zote usema nitafanya na nitashinda bila shaka kama walivyosema Joshua na Kalebu kuwa “tupande tukatamalaki kwa kuwa tutashinda bila shaka” lakini muoga ni rahisi kusema “siendi” au akasema “twendeni labda twaweza kushinda na sisi.”

Tofauti kati ya muoga na mtu jasiri ipo katika mitazamo yao juu ya mambo yanayowazunguka, katika jambo moja jasiri atafanya na kushinda ila mtu muoga ataogopa na akija ona matokeo ya mwenzie ubaki kutaamaki na kumwona menzie kuwa ni mtu wa tofauti sana ila siri ipo katika kuthubutu kufanya na si kukimbia kufanya.

Hakuna muoga yeyote aliyewahi kufanikiwa ila ni majasiri tu ambao uthubutu kugusa katika sehemu ambazo wengine hawagusi. Kwa mfano katika maeneo ya siasa wengi wamekuwa wakiogopa kuthubutu hata kugombea nafasi za ngazi mbali mbali kwa kuogopa kushindwa na wengine pia uogopa kuwa ni ngumu sana na zipo kwa ajiri ya watu wa tabaka fulani tu na uamini kuwa watu wa chini ni vigumu sana kuweza katika mambo ya siasa; ila uoga wa mtu ndio kushindwa kwa mtu mbona wapo wanaoweza kwa hiyo mtu muoga yeye ushindwa hata kabla hajaingia kwenye ushindani na jasiri ushinda hata kabla hajaingia kwenye mashindano.

Mfano kwenye mpira zikiwa zinacheza timu mbili kuna timu ambayo inacheza ili ishinde na kuna timu ambayo inacheza isishindwe, timu ambayo inacheza ishinde wachezaji wake wanakuwa na hali ya ushindi mara zote na ucheza kwa kushambulia wapinzani mara zote na ndiyo timu inayotazamiwa kushinda kwa kuwa ushindi wao ni hali iliyopo ndani yao kabla hawajaanza mchezo; ila mambo uwa tofauti kwa timu inayocheza ili isifungwe yenyewe ucheza kwa kujilinda sana kuliko kushambulia na wachezaji wake hali yao ni kujilinda wasije kufungwa na mara nyingi si watu wa kushinda. Ni vyema kujifunza kwa timu ichezayo kushinda.

Wiki ijayo tutaanza kutazama mambo ya msingi ili kuweza kuishinda hali ya uoga.
___
Somo hili ni sehemu ya kitabu cha Adui wa Mafanikio Yako ambacho tayari kimeshazinduliwa Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.