SOMO: KUKOSA NIDHAMU YA MAISHA NI MAANGAMIZO YA HATIMA YA MTU (2)

Na Kelvin Kitaso,
GK Contributor.Wiki iliyopita tuliishia kutazama kipengele ambacho Daudi alikuwa anaomba, basi tuanzie hapo na tuendelee kwa wiki hii.

Daudi anamuomba Mungu na kumwambia “Basi utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima” na katika tafsiri ya The Living Bible usema “Teach us to number our days. And recognize how few they are, help us to spend them as we should,” utafsiri maneno haya kwa Kiswahili chake kuwa Utufundishe kuhesabu siku zetu. Tujue ni jinsi zilivyo chache, utusaidie kuzitumia jinsi itupasavyo.” Zaburi 90.12. Daudi kwa kuwa na hekima alifahamu kuna umuhimu sana wa kujua siku zake kuwa zi chache na kuna umuhimu mkubwa sana wa kuishi kwa hekima katika siku hizo. Ni dhahiri kuwa kama hujui kuwa una siku chache za kuishi duniani ni kazi kwako kuishi kwa hekima na hata kujua ni namna gani unapaswa kufanya hili afya yako iwe chache sana.
Kwa kujua kuwa una maono ya kufanya ni lazima umuombe Mungu akufunze kuzitumia siku zako vizuri ili uweze kufikia malengo yako ukiwa na afya njema. Ukiwa na maono ya maisha yako ni lazima uwe makini na namna unavyoyaishi maono yako, angalia aina ya vyakula unavyotumia na jiepushe na vitu hatarishi kwa afya yako. Zingatia sana matumizi ya maji ya kutosha maana ni ya msingi sana kwa afya yako iliyo msingi wa maono yako, epuka matumizi ya vyakula vya kemikali ambazo zinachangia mwili wako kuchoka mapema na tumia hata mazoezi kwa kuwa ni muhimu sana. Usitumie vitu ambavyo vitaufanya mwili wako uremae na kukufanya kuwa mzembe.

4. Ukosefu wa nidhamu katika kufanya kazi.
Mungu anataka watu tufanye kazi, na ndiyo sababu maandiko matakatifu usema kuwa, “asiyetaka kufanya kazi na asile” na pia Mungu usisitiza kuwa yeye ubariki kazi za mikono yetu, na kama Mungu anabariki kazi za mikono yetu basi ni wazi kuwa asiyefanya kazi hana sehemu ya kupokea Baraka kutoka kwa Mungu. Ni vyema kufahamu kuwa Mungu anafurahishwa sana anapoona watu wake tunafanya kazi kwa bidii na kujituma na ndiyo sababu tukasisitizwa kuwa lolote tutakalopewa kulifanya ni lazima tulifanye kwa nguvu zetu zote.
Suala si kufanya kazi tu. Ila ni kufanya kazi katika nidhamu, ni ukweli usiopingika kuwa kuna watu wengi wanashindwa kufanikiwa katika maeneo yao ya kazi za kuajiriwa au ya kujiajiri kwa sababu ya kukosa nidhamu katika kazi zao. Ni vyema kufahamu kuwa ni nidhamu ndiyo usaidia kufanya kitu sahihi, mahali sahihi na kwa wakati sahihi. Mfanya kazi mwenye nidhamu ufahamu ni wakati gani anapaswa kuwepo kwenye eneo la kazi zake, anafahamu nini afanye na nini asifanye katika eneo la kazi, anaishi kwa mahusiano mazuri na wenzake afanyao kazi nao, na ufanya mambo yake kwa ubora na utulivu.
Nyakati za sasa si ajabu kumkuta mtu wakati wa kazi ofisini, nyumbani au biasharani anatumia simu yake kuwasiliana ‘anachart’, au wakati wa kazi unaweza kukuta watu wanazungumza na kuhadithiana mambo ya kwao na maisha yao au kujadili watu wengine na hata wakija watu wa kuhudumiwa mhudumu anakuwa mzito kwa kujali mawasiliano na mazungumzo anayoyafanya na wakati mwingine ni mawasiliano yasiyo na msingi, ni vyema kufahamu kuwa nidhamu inatufundisha kuwa kila jambo lina wakati wake, wakati wa kazi ni vyema kufanya kazi na wakati wa kuwasiliana ni vyema kufanya hivyo. Au kumkuta mtu anakula wakati wa kazi au kalala wakati wa kazi na kazi za kufanya zipo nyingi, hii ni ishara ya kukosa nidhamu. 
Nidhamu ya kazi ni maandalio ambayo hayaanzii pale kwenye eneo la kazi bali uanza nje ya eneo la kazi kwa mhusika kufahamu kuwa yeye ni mfanyakazi na anapaswa kuwa kazini muda Fulani, na kufahamu akiwa kazini yupo kwa ajili ya kufanya kazi, na kwa kufanya hivyo atajifunza kujiwekea ratiba toka nje ya eneo la kazi ambayo itamsaidia kufanya kazi zake kwa usalama, maandalio hayo yanahusisha muda wa kupumzika na kulala ulio wa kutosha ambao utamsaidia kutochoka ovyo wakati wa kazi, aina ya chakula cha kutumia ambacho kitasaidia mwili kuwa salama na afya njema kuendelea na majukumu yake, pamoja na kujiepusha na vitu ambavyo vitamfanya awe na msongo wa mawazo wakati wa kazi.
Nidhamu sehemu ya kazi ndiyo usababisha watu wengine kupandishwa vyeo mara kwa mara na wengine kushushwa na kufukuzwa kabisa, na upande wa biashara ndiyo sababu ya biashara kukua na kuwa na wateja wengi na kujiongezea umaarufu na mipaka ya utendaji.
Mwalimu mmoja aliajiriwa kufundisha shule ya sekondari yenye wasichana na wavulana, kwa kukosa nidhamu ya kazi alikuwa akinywa pombe sana na kutembea na mabinti wengi waliokuwa wakisoma katika sekondari hiyo, suala hili lilipofahamika katika ngazi za juu lilisababisha wamfute kazi na kumlipa faini ya vitendo alivyofanya ambavyo licha ya kuharibu mabinti wa ile shule ilichangia kuchafua sifa za ile shule. Tatizo kwa mwalimu huyu ni kukosa nidhamu kulikompelekea kusahau mipaka yake. Nidhamu usaidia kufahamu mipaka yako na kuishi ndani ya hiyo mipaka. Kama mwalimu huyu angekua na nidhamu ni lazima angeheshimu mipaka ya kazi yake.
Nidhamu katika eneo la kazi ni pamoja na kufanya kazi kwa wakati na kumaliza kwa wakati na wakati mwingine kumaliza kabla ya wakati. Kumaliza kazi ulizopangiwa na kuagizwa kwa wakati ni nidhamu ambayo ukufanya uonekane ni mwaminifu na kukupa fursa ya kupanda juu kwa madaraja ya kikazi, ila nidhamu si katika kumaliza hizo kazi tu kwa wakati, bali ni kufanya kwa ufanisi na ubora wa hali ya juu. Ukimaliza kwa wakati uliopangwa na kazi isiwe bora hakuna kitu chema na cha tofauti ulichofanya ambacho kinaweza kukupa jibu. 
Watu walio bora mara zote ufanya vitu vyao kwa wakati, usahihi na wakiwa mahali sahihi kwa ubora wa hali ya juu. Na utofauti wao na wengine ni nidhamu yao ambayo uzaa vitu vilivyo bora.

Katika maeneo ya biashara pia, watu wengi wamekuwa wanafanya biashara ila hawana nidhamu ya kufanya biashara ambayo ingewasaidia kuvuta wateja wengi zaidi, unaweza kumkuta mhudumu wa biashara anagombana na wateja na wakati mwingine anaweza kuwa mzito pasipo kuwa na lugha nzuri kwa mteja wake, hii inamfukuza mteja na kumfanya asije siku nyingine; Upande mwingine wafanya biashara wamekuwa wakitoa huduma kwa kutazama matakwa yao kwanza kuliko jamii ya wateja wao, hii ni kutofahamu kuwa katika kuanza ni vyema kwanza kujitengenezea uaminifu na kutoa huduma bora sana ambazo zitawasababisha wateja wako wapende kufuata bidhaa zako mara kwa mara na hata kama itatokea umepandisha bei bado watu wataendelea kukufuata kwa kuwa wanavutiwa na huduma yako. Unapoanza jiwekee nidhamu ya kufanya vitu bora ambavyo vitakufanya utafutwe na hata watu  wa kutoka mbali watavutwa na kuifuata huduma huitoayo.
Mambo ya wizi na ufisadi katika eneo la kazi ni matokeo ya kukosa nidhamu ya kazi, kwa kuwa mwenye nidhamu ya kazi ni lazima awe makini na mipaka yake ya kazi.
5. Ukosefu wa nidhamu katika familia.
Ni ukweli kuwa familia nyingi zimekosa kufanikiwa na kuwa na mafanikio mazuri kwa sababu ya kukosa nidhamu ya pamoja kama familia, hii ni kwa sababu kuna mambo yakufanywa kwa pamoja kama familia na kuna mambo yakufanywa na mtu mmoja mmoja katika familia. 
Mfano familia inayokosa nidhamu katika eneo la kupanga pamoja na kuomba pamoja inakosa umoja wa kimwili na kiroho hata kama watu wako pamoja, itaifanya familia kuwa dhaifu kukabiliana na matatizo yajayo yakiwa ya kiroho au ya ulimwengu wa kawaida kwa sababu kila mmoja atapambana kwa sehemu yake pasipo umoja.
Familia inayokosa nidhamu huwa haina utaratibu wa kupangilia mapato na matumizi, na mara nyingi tabia hii hupelekea umaskini, njaa na uhitaji wa kudumu katika familia. Na ni nidhamu ya familia ndiyo inaweza kuwakuza watoto katika njia njema, kwa kuwa nidhamu itawafunza wazazi namna ya kuwa bora na kuwaongoza watoto wao.

Wiki ijayo tutaanza kwa kutazama kanuni nyingine ya nidhamu ya MAGAZIJUTO.

_____
Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.