SOMO: KUKOSA NIDHAMU YA MAISHA NI MAANGAMIZO YA HATIMA YA MTU (3)


Na Kelvin Kitaso,
GK Contributor.
Wiki iliyopita tulimaliza kwa kutazama namna ambavyo familia zinakosa nidhamu na hivyo kushindwa kufanikiwa katika maisha, hiyo ni sehemu ya somo, bonyeza hapa kulisoma. Kisha tuendelee na wiki hii ambapo tunazungumzia kanuni ya nidhamu ya magazijuto.
KANUNI YA NIDHAMU YA MAGAZIJUTO
Katika Maisha kuna kanuni nyingi ambazo zinatumika katika kuleta au kutimiza ndoto za watu kwani ukiijua kanuni una 50% ya kupata, na ukiifuata vizuri na kwa umakini utakuwa na 50% zingine za kufanikisha malengo yako.
Hebu tujikumbushe kanuni moja ya Hesabu iitwayo MAGAZIJUTO ambacho kirefu chake ni
MA-Mabano
GA-Gawanya
ZI-Zidisha
JU-Jumlisha
TO-Toa
Hii ni kanuni ambayo inatufundisha kwamba ili uweze kupata jibu sahihi ni lazima kuwe na umakini katika ufuataji wa kanuni, kutokuwepo na umakini katika kufuata kanuni hakuwezi kuleta majibu sahihi.   Naomba ufuatilie kwa umakini mfano ufuatao
1+(28/4+5x2-3)

Usione ajabu kuona hesabu kwani wengi husema ni ugonjwa wa taifa, fuatilia kwa umakini mafunzo unayoyapata kutoka kwenye mfano huu ili upate ufahamu na akili katika kuzikabili changamoto za Maisha, na hivyo hesabu kuwa kinga ya taifa na sio ugonjwa.
Jibu tulilopata hapa ni tofauti na la kwanza japo swali ni lile lile, hii ni kwasababu ya utumiaji  wa njia tofauti. Lakini mpaka kumepatikana jibu kulikuwa kuna swali (ndoto/maono ambayo yapo ila yanahitaji kufanyiwa kazi) na kulikuwa na kazi (ambayo ni njia ya kupeleka maono yaliyo kama kitendawili na swali, hapa kama usipotumia kanuni sahihi hauwezi kupata jibu sahihi) na jibu ni (matokeo ya kuwa na swali na kufanya kazi). Zingatia kuwa si kila jibu ni sahihi na si kila njia itakuletea jibu sahihi bali ni njia sahihi tu, ambayo huleta jibu sahihi. 
·       Usipofuata kanuni kwa umakini, hauwezi kupata jibu sahihi.
Katika Maisha kuna nafasi mbalimbali ambazo kila mtu anatamani azifikie na pia kuna juhudi nyingi zinazofanywa ili kufikia nafasi hizo, ila imekuwa si kitu rahisi sana kwa sababu nyingi, lakini ngoja nikwambie sababu kuu inayofanya kutofikia ni kutokufuata utaratibu kwa usahihi(kukosa nidhamu).
Kama ulivyoona kwenye mifano hiyo hapo juu, alipojaribu kubadilisha kanuni, au kutunga ya kwake jibu alilopata si la ukweli na ni dogo kuliko jibu sahihi, na hata kama umebadilisha uanze na kuzidisha au kutoa, uwezekano wa kupata jibu sahihi ni mdogo sana. Na hata ukipata utakuwa umebahatisha, je! Kwanini uishi kwa kubahatisha wakati kanuni ipo? Usipoteze wakati fuata kanuni kwa umakini.
Pia katika ufafanuzi wa kina neno bahati iitwayo Lucky kwa lugha ya kiingereza, mwanafalsafa mmoja ameelezea kwamba “bahati inatokea kikamilifu pale mtu mwenye nia iliyojiandaa anapokutana na fursa” Na kujiandaa huko ni kikamilifu yaani asilimia 95 na asilimia 5 tu ni za kuiona hiyo fursa. Hivyo ni wazi kwamba kama mtu hajajiandaa akikutana na fursa uwezekano wa kuipata ni mdogo, na mara nyingi akiikosa watu husema hana bahati au ana bahati mbaya lakini ukweli ni huo hakujiandaa ipasavyo, hivyo ni vyema ujiandae mapema ili fursa ikukute wakati umejiandaa.
                 
Kuna mwimbaji mmoja ameimba kwa lugha ya kiingereza ya kwamba “There is a race I must run, there are victories to be won, give me power, every hour to be true” akimaanisha ya kwamba “Kuna mbio ambazo ninatakiwa nikimbie na kuna ushindi ambao uko mbele yangu, nipe nguvu, kila saa nifanye kwa usahihi na ukweli”. Nampongeza kwa sababu alijua ya kwamba kupewa nguvu peke yake hakutamsaidia kuupata ushindi, bali aliomba kitu cha ziada ambacho ni nidhamu ya kuifuata(kila saa) kufanya kwa usahihi ili aweze kuufikia huo ushindi wake.
Hivyo kama mtu mwenye maono makubwa na ya muhimu sana katika kizazi hiki na vizazi vijavyo, inapaswa utambue ya kwamba nidhamu ni muhimu sana katika kufanikisha malengo yako.
(i) Mabano (   ),
Yaani panga mipango yako, hata ikiwa mingi si mbaya kwani ni wewe uonaye mbele yako. Kama vile Mungu alivyomuuliza Yeremia unaona nini?
Yeremia 1:11,12 “Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, unaona nini? Nikasema, Naona Ufito wa Mlozi 12. Ndipo BWANA akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.”
Hii ina maana ya kwamba kila mtu, yaani kila mtu  amepewa uwezo wa ndani kuona mbele na kupanga, na nidhamu ya kufikia malengo hayo inategemeana na utendeaji kazi wa Neno la Mungu pamoja na uongozi sahihi. Ndio maana neno hai la Mungu katika kitabu cha Mithali 16:1,3 linasema ya  kwamba  “Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu, bali jawabu la ulimi hutoka kwa BWANA 3. Mkabidhi BWANA kazi zako, Na mawazo yako yatathibitika.” Kwamba kuna nafasi ya mtu kupanga, na nafasi ya Mungu kuthibitisha au kukuongoza lakini lazima uwe umemuomba.
Mshikishe sana Mungu katika yote uyapangayo na uwe tayari kuruhusu mapenzi yake kutimizwa katika yote uyapangayo. Kubali mapenzi ya Mungu yatimizwe na si kama wewe upendazyo.
(ii)Gawanya (/)                                                                 
Baada ya kupanga mipango au malengo yako, inamaanisha ya kwamba unaanza kushughulika na mambo yaliyopo ndani ya mabano.Hivyo hatua inayofuata ni kugawa katika makundi kwa kuzingatia vipaumbele(scale of preference), yaani yale ambayo ni ya muhimu na ni ya haraka, ya muhimu lakini siyo ya haraka, ni ya haraka ila si ya muhimu pamoja na mengine ambayo si ya muhimu wala si ya haraka.
(iii) Zidisha (x)
Fanya kwa bidii sana mambo yale uliyoyachagua kuwa  ya muhimu sana na yanahitaji kuwa ya kwanza kuyafanya ili uyatimize haraka(zidisha), upate muda  wa kuendelea na mengine.
Zidisha nguvu kazi ya utendaji wako na acha kufanya kwa kawaida.
(iv) Jumlisha (+)
Kisha yaongeze yale yanayofuatia kwa umuhimu, na uyafanye kwa ustadi na umakini ili uweze kufanya tathmini ya kazi yako au lengo lako.
(v)Toa (-)
Baada ya kumaliza kufanya vitu vya ziada na vya muhimu vilivyo ongezwa, inatakiwa ufanye tathmini ya kazi na kupunguza/kuondoa mambo ambao si ya muhimu na hayana haraka ili kupata matokeo au jibu lililokusudiwa. Fanya tathmini itakayokusaidia kuondoa vikwazo na vitu vyote visivyo na ulazima.
Kukosa nidhamu ya Maisha ni kipengele  ambacho kitakusaidia kubadilisha mfumo mzima wa Maisha na jinsi unavyokabiliana nayo.
Kuna msemo unaosema “kama hauridhishwi na matokeo, angalia na rekebisha  jinsi unavyotenda/unavyofanya” yaani itakusaidia kukipata kile unachokifanya. Usipofurahishwa na aina ya Maisha unayoishi, angalia jinsi unavyotenda (tumia kanuni ya magazijuto) ili ufanye tathmini na ubadilishe mtazamo pamoja na aina ya matokeo, na pia uweze kuishi maisha ambayo Mungu amekukusudia kwani alikujua kabla hajakuumba, na kabla hujazaliwa alikutakasa(ikimaanisha kuwa alikutenga kwa ajili ya kazi maalum) Yeremia 1:5
Pia kumbuka kuwa watu wote hapa duniani bila kujali eneo, taifa, rangi au lugha, Mungu ametupa  vitu vikuu vitatu vinavyofanana,
1.     Muda (masaa 24 kwa siku)
2.     Fursa (zisizopungua 100 kwa siku)
3.     Maamuzi (free will )
Yaani wote tumepewa muda sawa(yaani masaa 24 tu hakuna nchi iliyozidishiwa masaa kwamba yawe 25 au 30 kwa siku). Pia kila mtu kwa siku anaweza kukutana na fursa zisizopungua 100, na zaidi kila mtu ana uhuru wa kufanya maamuzi, kuamua nini afanye wakati gani kwa namna gani na mahali gani? Yote haya ni sawa kwa kila mtu bila kujali anaishi Marekani au Tanzania au sehemu yeyote ile ya dunia,
Tofauti ipo wapi? Kwanini watu wengine wameendelea kiuchumi na kimaisha kiujumla  wakati wengine bado? Nini sababu kuu ya  kutokuwa na uwiano sawa kimaisha? Jibu ni rahisi sana ambalo ni NIDHAMU. Hii ni siri iliyojificha ambayo ukiitambua, hautapoteza muda kufanya mambo ambayo siyo ya msingi na ambayo siyo wakati wake, na itakupa umakini sana katika utendaji kazi ya mambo yako kwani  itakuwa rahisi sana kuiona fursa na kuitambua. Haitoshi tu kuitambua bali utaitumia ipasavyo kwa kuwa sehemu sahihi, wakati sahihi na ukifanya kitu sahihi.
Nikudokeze kidogo kuhusu kuitambua fursa, kwani fursa ni nafasi ya kipekee anayoipata mtu kufanya kitu fulani mfano kupata fursa ya kusoma, kuwa na wazazi, kukutana na watu waliofanikiwa, kuwa na marafiki, kuwa mzima, kuokoka na zingine nyingi hizo ni fursa. Usipoitambua kuwa ni fursa utaitumia vibaya na badala ya kuifurahia, utaijutia. Hebu angalia baadhi ya mifano ya  fursa na matumizi yake.
Mfano mwanafunzi amepata fursa ya kusoma, ili apate ujuzi utakaomsaidia maishani, na akachezea shule, kwa kuwa na makundi mabaya, kutoroka shule na hatimaye kufeli au kufukuzwa shule. Wengi wanatamani kusoma, ila hawana uwezo wa kulipa ada au hawakufaulu vizuri, hii ni kutotambua umuhimu wa fursa hii. Kuwa makini! tambua kuwa kupata nafasi hiyo ni fursa, itumie kwa umakini nayo itakutumikia.
Pia niizungumzie fursa nyingine nyeti sana ya kumkiri Bwana Yesu kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako(KUOKOKA). Hiyo ni fursa ya kipekee ambayo mtu anaipata baada ya kulisikia neno hai la Mungu, na kuliamini moyoni mwake na kumkabidhi Yesu kuwa kiongozi wake, hivyo kufanyika Mwana wa Mungu. 1Yohana 5:1 “Tazameni ni pendo la namna gani? Alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu”  Lakini kuna watu wanauchezea wokovu kwa kutokuujali wakati wapo watu wengi wanatamani sana kuokoka lakini wanashindwa kwa sababu wamefungwa na nguvu za giza, Ewe mkristo, utapataje kupona usipoujali wokovu mkuu namna hii? Badilika na utambue kwamba ni neema tu(fursa)ya kwamba umeokoka, na hata kama hujaokoka hii ni fursa unayoipata kuokoka, Umpe Yesu maisha yako akubadilishe, nawe hautakuwa kama ulivyokuwa.
Fursa ya uchumi na kufanikiwa katika maisha, ipo katika kujitambua kwa mtu, na kwa namna gani mtu huyo anatumia muda wake na anafanya maamuzi ya aina gani katika maisha yake.
Kila mtu unayekutana naye kwa siku anaweza akawa ni fursa ya kukufanikisha katika maisha yako na ukaweza kuyafikia m,alengo uliyonayo katika maisha yako, ila fursa inategemea unatumiaje muda wako unapokutana na mtu. Angalia mazungumzo mnayoyazungumza kwa kuwa yanaweza kukufanya ufanikiwe au usifanikiwe katika maisha yako.
Unaweza kukutana na mtu mliyewahi kushirikiana nae au kuishi nae kwa miaka iliyopita, ila tofauti ya mtu anayejitambua katika mazungumzo yake atakuwa anatafuta fursa ya kufikia hatima ya maisha yake, ila kwa mtu asiye ishi kwa fursa ataishia kuzungumza mambo ya kawaida na kufurahi tu.
Kuna fursa nyingi sana katika ulimwengu huu tunaoishi, hata katika matatizo na adha zitokeazo na katika mambo ambayo wengine huyaogopa ndani yake kuna fursa kubwa ya mafanikio. Daudi katika tatizo lililosumbua wana wa Israeli yeye aliona fursa ya kuoa mtoto wa kifalme, kuingia ikulu na kuwa shujaa wa nchi. Katika jambo ambalo wengine wanakimbia jaribu kufanya kwa ujasiri kwa kuwa kwa kufanya hivyo utapata fursa na kung’aa zaidi ya wengine.

Mwisho.
_____
Somo hili ni sehemu ya kitabu cha Adui wa Mafanikio Yako ambacho tayari kimeshazinduliwa Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.