SOMO: NGUVU YA MANENO, FAIDA NA ATHARI ZAKE (5)

Na Askofu Sylvester Gamanywa,
Mwangalizi Mkuu, WAPO Mission International.

Jumatatu iliyopita tulipitia vipengele vinavyojibu maswali magumu juu ya Mungu na Shetani ambayo yalikuwa ni “Kwanini Mungu hakumdhibiti Lusifa asieneze uasi wake kwa malaika wengine?” na “Kwanini Mungu hakumwangamiza Lusifa na malaika zake wakati ule walipoasi?” Soma hapa Leo tunaingia kwenye kipengele cha nguvu ya vita katika maneno:


Nguvu ya vita iko katika maneno

Mtiririko wa mada hautafaulu kama sitaweka mkazo kwenye mambo ambayo ndiyo yameshika uzito wa juu. Falsafa nzima ambayo tumeipitia madhumu yake hasa ni kutuleta kwenye kujua nguvu ya vita ya maneno jinsi ilivyo kubwa na kila aina ya vita inayohusisha silaha za moto na za maangamizi,, zote zinaendeshwa kwa nguvu ya maneno.

Tunapotumia msamiati wa neno vita, tunalenga hali ya uhasama na uadui ulioko pande mbili au zaidi, na yako mashindano hasi ya upande mmoja kuuondosha na kuutawala upande mwingine. Haya ndiyo mashindano ambayo tumeyaona yanayoendelea kati ya Shetani dhidi ya mamlaka ya Mungu.

Tumesoma historia ya uasi wa Shetani kwamba ulitokana na kiburi kilichoanzia ndani yake na kutamani kuabudiwa kama Mungu. Huu tumesoma kwamba ni “uovu ulioonekana ndani yake.” Lakini uovu hauu haukua na nguvu mpaka pale ambapo “shetani alitunga maneno hasi” dhidi ya mamlaka ya Mungu ambayo aliyasambaza kwa malaika.

Inasadikiwa kwamba maneno ya Ibilisi kwa malaika yalikuwa na ahadi za mgao wa vya utawala kwa malaika watakaomuunga mkono katika harakari zake za mapinduzi dhidi ya Mungu. Ushahidi wa dhana hii, ni jinsi hata baada ya kampeni yake kushindwa mbinguni hata alipotupwa, aliunda serikaii yake ya giza na kugawa vyeo kwa malaika wake waliokubalika kuanguka pamoja naye.(Efe.6:12)

Kwa hiyo, hata katika migogoro ghasia na vita vya kiraia vilivyoko hapa duniani, asili ya nguvu zake iko katika maneno. Matumizi ya silaha huwa ni matokeo ya wahusika kuathiriwa na kudhibitiwa na nguvu za mameno ambayo ama ni amri za wakubwa au vishawishi vya wenye kuongoza mapinduzi.

Samahani ninaomba tafsiri ya uasi na mapinduzi dhidi ya mamlaka halali ikomee kwenye mipaka ya “utawala wa Mungu” na “utawala wa shetani” ambazo ni moja ni mamlaka halali na nyingine ni haramu japokuwa imeruhusiwa kuwepo kwa hekima ya Mungu mwenyewe. Hapa tuko katika kujifunza habari ya vita vya kiroho ambavyo mamlaka zenye udhibiti wa vita hivi ziko katika ulimwengu wa roho. Na ni kwa jinsi gani mamlaka hizi za kiroho zinavyoathiri kila kinaofanyika katika ulimwengu wetu wa asili.

Sasa ni muhimu tujue kwamba, vita ya kiroho iliyopo iko katika nguvu ya maneno. Mathalan, Shetani ambaye ni mwasisi wa kiburi na uasi, yeye ndiye mwenye kutumia “maneno ya uchochezi” yenye kupanda mbegu za “mawazo hasi” dhidi ya Mungu na utawala wake.

Na kazi yake katika kampeni zake za kueneza kiburi na uasi hutumia maneno yenye ushawishi unaopanda mawazo hasi, mabaya dhidi ya upande wa mamlaka halali ili ionnekani haina uhalali wa kuheshimiwa na kufuatwa. Kisha anayo maneno ya ushawishi wa uongo kwamba yeye Shetani ndiye mwenye uwezo na mamlaka ya kumfanya mtu aishi maisha ya furaha na mafanikio tena yalisyo na masharti ya kimaadili. Hebu sasa tupitie kwa ufupi jinsi shetani anavyoendesha vita vyake wa kuhamasisha kiburi na uasi

Shetani anashindana
kwa kiburi na uasi

Huko nyuma katika mada hii tulijifunza jinsi shetani alivyomwendea binadamu wa kwanza na kumshawishi ale matunda ambayo Mungu alikataza yasiliwe. Kwa hivi sasa kuna vitu muhimu nataka kuviweka wazi ili tupate kuziona mbinu za shetani za kueneza kiburi na uasi.

“Nyoka akamwambia mwanamke, hakika hamtakufa, kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya.” (MW.3:5)

Kwanza, maneno haya yamebeba “uchongezi” na “uchochezi” na “kashfa” dhidi ya Mungu aliyewakataza binadamu kula matunda ya mti husika. Kule kusema “hakika hamtakufa” wakati Mungu ndiye aliyetangulia kusema “Mkila takufa hakika” ni sawa na kumfanya Mungu mwongo na mwenye kuficha mema kwa bidanamu wake.

Pili, kwa kupitia maandiko haya tunaweza kuona sura za maneno yaliyotumika katika kumshawishi mwanamke. “…..hakika hamtakufa…”, “mtakuwa kama Mungu…”. Haya maneno yamebeba ahadi zenye ushawishi, lakini Shetani aliyeyasema hakuwa na mamlaka ya kutekeleza ahadi zilizomo kwenye maneno yake.

Tatu, Mwenye tamaa ya “kuwa kama Mungu” ni Shetani mwenyewe, na ndiyo dhambi kuu iliyomfukuzisha mbinguni. Tamaa ile ile ya “kiburi” ameiambukiza kwa binadamu ambaye alijua tayari ndiye “ameumbwa kwa mfano wa Mungu na sura ya Mungu”; na sasa kwa kuihamasisha tamaa ya kuwa kama Mungu ni ili binadamu aamue kujitwalia mamlaka ya kuwa kama Mungu kwa kuasi amri ya Mungu.

Hatuwezi “kupokea na mamlaka” kwa “kuasi mamlaka” ile ile ambayo tunatafuta mamlaka yake. Kanuni ya kuinuliwa na kukwezwa ni kuwa “tunapokea mamlaka” kutoka kwa “mwenye mamlaka ya juu aliye juu yetu” na si vinginevyo. Kutaka kuwa na mamlaka ya aliye juu yetu, pasipo ridhaa yake, ni usaliti na mapinduzi haramu.

Kwa kifupi, maneno ya shetani yamejaa kiburi na kujisifu, kujidai, kujivuna, na ahadi za uongo ambazo haziwezi kutekelezeka kwa sababu shetani hana mamlaka ya kutoa mamlaka ambayo yeye yuko kinyume nayo. Kiburi ndicho huzalisha uasi ambao ni mtazamo hasi dhidi ya mamlaka halali na unaotoa maneno ya ushawishi wa kufanya mapinduzi haramu dhidi ya mamlaka halali

Yesu Kristo alimshinda Shetani
 kwa unyenyekevu na utii

“Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu.” (Mt.11:29)
Kwa kupitia maandiko haya, tunapata picha kamili ya ujio wa Yesu Kristo duniani. Alikuja sio kutukomboa kwenye utumwa wa kiburi na kuasi peke yake, lakini kwa yeye kuwa mfano halisi ili sisi tujifunze kutoka kwake.
Unyenyekevu umejaa maneno ya upole, staha, adabu, na kuheshimu mamlaka halali.

Kwa kuwa binadamu tulishindwa na shetani kwa udanganyifu wa kiburi na kuasi, Yesu alikuja kupigana vita kwa niaba yetu ili amshinde shetani na kutukomboa lakini atupe fursa pia na sisi kumpinga na kumshinda shetani kwa kufuata nyazo za Yesu Kristo.

Mwisho
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.