SOMO: ROHO YA UMASIKINI - ASKOFU JOSEPHAT GWAJIMA

Askofu mkuu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima


SOMO: ROHO YA UMASIKINI
Yesu alipokuja hapa duniani aliwachagua watu wayashuhudie yale anayoyafanya ili wawe mashuhuda wa kazi na na mafundisho yake. Kati ya mambo ambayo Mkristo anatakiwa kuyafahamu ni majina yake halisi ya kwenye Biblia. Biblia inasema sisi ni wana wa Mungu kwa asili, ukitaka kumfahamu mtoto kama ni wa Baba yake aliyemzaa unaangalia kwenye vipimo vya DNA ndipo utagundua kwamba ni wa baba yake au siyo. Ukristo maana yake ni kuzaliwa Mungu kwasababu hiyo sisi ni wana wa Mungu.

 Kwa kawaida dunia imejaa taratibu zake za kiutendaji na kimtazamo lakini Yesu kristo alikuja duniani kupindua taratibu za kidunia na kuweka taratibu zake. Msomi mmoja aitwaye Nikodemo alimstaajabu Yesu kristo kwa jinsi alivyokuwa akiponya wagonjwa, vilema, kutoa pepo na kufufua wafu na kuwafanya watu waliofungwa kuwa huru, Yesu alikuja kwaajili ya masikini na wenye matatizo. Duniani watu wenye uwezo mkubwa wana madaraja ya juu, wenye uwezo wa kati wapo kwenye madaraja ya kati na masikini wapo madaraja ya chini lakini Yesu alikuja na kuwapenda masikini na kupindua tamaduni za kidunia zilizowakandamiza na kuwaweka juu.

“Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee? Aweza kuingia tumboni mwa mamaye mara ya pili akazaliwa? Yesu akajibu, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu. Kilichozaliwa kwa mwili ni mwili; na kilichozaliwa kwa Roho ni roho. Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho. Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya? Yesu akajibu, akamwambia, Je! Wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu?” Yohana3: 1 – 10
Mungu ni Baba wa roho yako na Baba na Mama yako ni wazazi wa mwili wako. Maana yake unapokuwa mtu wa kawaida ukapompokea Yesu ndani yako, Yesu anaingia ndani yako na unaanza kuitwa mtoto wa Mungu na unakuwa mwana wa Mungu kwa njia ya imani unakuwa umeokolewa, ile asili na Mungu inakuwa ndani yako na unakuwa alivyo Mungu ndivyo ulivyo wewe.

 “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake” YOHANA 1:12
“Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” YOHANA 4:24
Tuliomwamini Yesu na kumpokea kwenye mioyo yetu tupo kwenye ulimwengu huu lakini sisi si wa ulimwengu,
"Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu." YOHANA 17:16
“Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo. Nilipokuwapo pamoja nao, mimi naliwalinda kwa jina lako ulilonipa, nikawatunza; wala hapana mmojawapo wao aliyepotea, ila yule mwana wa upotevu, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu.” YOHANA 17:14
Sisi tunaomwamini Yesu Kristo tuna kazi ya kufanya hapa duniani, roho zetu tumetoka mbinguni na tukifa roho zetu hazifi bali miili yetu inakufa na tukirudi mbinguni tutakuwa na kumbukumbu zote kwamba tulishawahi kuishi mbinguni na tutakuwa tunakumbuka jinsi Mungu alivyotuagiza kuja kuzigeuza tawala za duniani ziwe za mwanakondoo Yesu kristo, kuja kufanya mapenzi ya Mungu hapa duniani.

Tunaweza kuongea lugha ya babeli lakini hatuli chakula cha babeli, tunaweza kuigusa mikono michafu kwa mikono mitakatifu na hakuna kitakachotubadilisha, tunaweza kuvaa na kuongea kama wasioamini lakini sisi sio kama wao, sisi ni mabalozi wa Ufalme wa mbinguni na hili sio swala la hisia kwasababu hisia zinaweza kubadilika kulingana na wakati. Tumepewa kazi ya kufanya hapa duniani. Mazingira yasitegemee furaha yako bali furaha yako imtegemee Bwana Mungu wa Majeshi.
Ufalme wa giza nyakati zake za kukaa duniani zinahesabiwa na mwanakondoo anatawala.
“Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tuna ukombozi, yaani, msamaha wa dhambi; naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.” WAKOLOSAI 1:13
Wokovu maana yake ni kunyofolewa kutoka kwenye ufalme wa giza na kuingizwa kwenye ufalme wa Mungu.

Duniani kuna falme mbili ambazo ni ufalme wa Mungu wa Mbinguni na ufalme wa shetani. Kama hujaokolewa shetani anaweza kukutumia na kukutupa muda wowote, kama upo kwenye ufalme wa shetani wewe ni “disposal” wa shetani hawezi kuumba kipawa, wala uzima bali huchukua wazima na kuwatumia na wakiharibika anawatupa lakini Yesu kristo yeye ni tofauti anakutumia na ukiharibika anakuambia yeye ni Bwana atoaye uzima hivyo anakupa uzima.
Unapompokea Yesu kwa kumkaribisha ndani ya moyo wako Yesu anaingia ndani yako na hapo ndipo unakuwa umezaliwa mara ya pili huwezi kusikia hisia yeyote ile au mabadiliko yeyote ile pale unapompokea lakini mabadiliko hayo yanafanyika rohoni. Unapookolewa unaondoka kabisa kwenye sheria ya giza na ukiingia kwenye ufalme wa Mungu kuna sheria zake zenye katiba ambayo ni Biblia Takatifu na ukitaka kuwa tajiri, kuoa, kufanikiwa ukiwa kwenye ufalme wa Mungu kuna sheria za kufuata na unapozifuata unafanikiwa.
Watu wengi tumehubiriwa sana injili ya wokovu mfano:- unahubiriwa kwamba mwamini Yesu utafanikiwa, jifunze neno la Mungu, hudhuria kanisani, toa fungu la kumi, umesamehewa dhambi na nafsi yako imekombolewa kutoka kwenye laana, ulikuwa huna mume umeolewa, ulikuwa unamagonjwa umepona, unanena kwa lugha, ulikuwa mwizi umeacha, huna fedha lakini ukinena kwa lugha unasikia amani moyoni maana yake roho mtakatifu ni mfariji unapokuwa na matatizo anakufariji lakini hakuondolei matatizo yako, hiyo ndio injili ya wokovu na ndiomaana watu wengi wanaokoka na kuacha wokovu kwasababu wanakuwa wanahudhuria kanisani, wanaimba na kupambana na nguvu za giza mpaka inakuwa mazoea lakini hayo siyo mapenzi ya Mungu kwetu hapa duniani.
Mapenzi ya Mungu ni wanadamu kuokoka na kufanikiwa kwenye maisha wakiwa ndani ya wokovu huku wakitimiza kusudi lao lililowaleta hapa duniani, lakini dunia inasema mtu ambaye hajaokoka akiwa tajiri ni kawaida lakini mtu aliyeokoka akimiliki nyumba kumi huyo anaitwa hajaokoka ni tapeli kitu ambacho sio kweli.
Dunia imewatengeneza watu kwamba wakifanikiwa sana wanaitwa wanapenda mali lakini watu ambao hawajaokoka wakiwa na ndege na makampuni hiyo inakubalika kitu ambachi sio kweli na sahihi. Kuna kanuni ukiingia kwenye ufalme wa Mungu `uwe na viwanda, magari au makampuni, hiyo niruhusiwa lakini uvipate ukiwa ndani ya kanuni za Mungu “sisi ni wana wa ufalme wa Mungu”, Dunia inashtuka inapoona unanena kwa lugha huku ukiwa unamali hapo unaanza kusakamwa na kulazimishwa urudi chini “uwe masikini”.
“Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake.” Zaburi 24:1
Dunia imetengeneza mkakati wa kumtumia mwanadamu na kumtupa mfano: umeajiriwa unafika kazini saa moja asubuhi na unatoka jioni kesho tena vilevile na haupati muda wa kutengeneza cha kwako, dunia inataka uende hivyohivyo mpaka uzeeke na upewe kiinua mgongo, maana yake wale waliokuajiri wamekutumia na wameona umechoka wanakutupa na baadae unajikuta unafariki haujafanya cha maana.
“Tajiri humtawala maskini, Naye akopaye ni mtumwa wake akopeshaye.” MITHALI 22:7
Mtu aliyeokoka anatakiwa we ana mali huku anamcha Bwana, mtazamo wa dunia ni kwamba wenye mali hao hawajaokoka nawasiona mali ndio wameokoka.
Mungu alikuleta duniani akiwa na lengo la kutengeneza koloni lake hapa duniani na vyote vikaavyo duniani ni mali yake. Ndani yako kuna hazina lakini umekosa mahala pa kuanzia. Sio elimu inayoleta nyumba au gari bali ni kuwa ndani ya ufalme. Kuna kazi unaweza kuzifanya zikakuletea utajiri haijalishi uwe mzee au kijana.
Ukiri:
“Mimi ni mwana wa ufalme nimehamishwa kutoka ufalme wa giza kwenda ufamle wa Mbinguni na Baba yangu ameumba mbingu na nchi na vyote vikaavyo ndani yake ni mali yake, Kwa jina la Yesu ninamiliki juu ya nchi”
“Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.” 2 Wakorintho 8:9
Kuokoka hakutuletei utajiri bali ni hatua ya kwanza ya kumjua na kumpokea Bwana Yesu, kwenye ufalme wa Yesu kuna namna ya kutenda ili tupate kufanikiwa, kujenga viwanda, kusafiri nchi za nje, kufanya biashara nk. Utajiri ni sehemu ya Ufalme wa Mungu lakini ukiwa tajiri sana hata walokole wenzako wanaanza kukushangaa sababu ya dunia imetengeneza utaratibu wa kuwa mtu tajiri si mtu wa Mungu.
“Naye Abramu alikuwa ni tajiri sana kwa mifugo, kwa fedha, na kwa dhahabu.” MWANZO 13:2
“Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti; ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.” Wagalatia 3:13
Yesu alilaaniwa msalabani ili Baraka ya Ibrahimu ya fedha, mali iwaendee mataifa.
“Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki.” AYUBU 1:1-
Zamani kwenye agano la kale watu wa Mungu walitambulika kwa utajiri wao. Shetani hatishwi na masikini sababu anajua hana madhara na kazi zake na mfumo wa dunia umetengeneza mfumo watu wenye dhambi wazidi kuwa matajiri halafu sisi tulio wa Mungu tuendelee kuwa masikini.
“Nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.” Isaya 45:3
Unatakiwa ufute kwenye akili yako kwamba kuwa na mali ni mpaka uwe hujaokoka. Mtu aliyeokoka ana akili nyingi na nguvu nyingi duniani lakini dunia imeweka mfumo wa kumfanya asimiliki utajiri wa Mungu wake.
Nakataa umasikini kwa jina la Yesu
ILI UMILIKI UKIWA NDANI YA UFALME WA MUNGU NI LAZIMA:-
1. Uamini ni mapenzi ya Mungu kwamba wewe uwe na mali, magari, nyumba, viwanda nk
2. Unaanza kuyasema yale unayoyaamini, kuamini bila kusema ni sawa na kutokuamini. Kwenye kitabu cha Mwanzo 1:3 – 30 Mungu alisema na akayaona yale aliyoyasema. Hii haijalishi umetoka kwenye familia ya utajiri au masikini ukiamini na kukiri lazima utafanikiwa.
Ukiri:
“Ninaamini kutoka ndani ya moyo wangu kwamba naweza kuwa tajiri nikiwa ndani ya Ufalme wa Mungu hakika Yesu amechukua magonjwa yangu, umaskini wangu na balaa zangu kwa jina la Yesu”
Usiseme hauwezi kama hauja jaribu mara milioni miamoja kwa siku, kweli kuna mashetani hasa majini ambayo yanakaa ndani ya mtu na kumfanya mtu awe wa kuibiwa (chumaulete) kwamba fedha inapokuja kwako inaenda kwa mtu mwingine badala ya kuja kwako. Mungu alipomuumba mtu alimpa ubunifu ndani yake na wanadamu wote ni waumba wenza sawasawa na Bwana.
Ukiri:
KWA JINA LA YESU NAKATAA UMASIKINI KWA JINA LA YESU.
“Mtu akizaa watoto mia, akaishi miaka mingi, nazo siku za maisha yake ni nyingi, lakini nafsi yake haikushiba mema; tena ikiwa, zaidi ya hayo, amekosa maziko; mimi nasema, Heri mimba iliyoharibika kuliko huyo” Mhubiri 6:3
Watu wengine wanatumia maandiko ili ukae kwenye kona ya umasikini uliyopo kwamba huwezi kuwatumikia miungu miwili kwa wakati mmoja lakini lile neno mungu kwenye kiebrania linamaanisha mungu mammon ambaye anawapa watu wenye dhambi fedha na inamaana kwamba huwezi kumtumikia Mungu Jehova na mungu huyu mammon kwa wakati mmoja. Ni rahisi kwa masikini kuingia mbinguni na kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mbinguni alimaanisha kwamba huwezi kukumbatia fedha na ukuacha kuwasaidia watu na kumwacha Bwana.
Ukitaka kujenga nyumba lazima uwe na fedha, ukitaka kumiliki gari lazima uwe na fedha na fedha hizo unatakiwa uzipate ukiwa ndani ya ufalme wa Mungu. Unapokuwa unaomba unasema “mimi ni tajiri” na milango ya kupata inafunguka Unaoomba mpaka maombi yako yanageuka na kuwa miliki juu ya nchi. Wasioamini na wachawi wanaogopa wakiona umeokoka na una mali na fedha sababu wanajua utawatawala na sisi ni watoto wa Mungu kwenye ufalme wa Mungu. Tunamiliki mali za Baba yetu wa mbinguni hapa duniani kwa jina la Yesu.
Maombi:
“Katika jina la Yesu Kristo Mimi ni Mwana wa Mungu namiliki juu ya nchi ninakataa umaskini wa kurithi kutoka ndani ya moyo wangu kwa jina la Yesu, nakataa umasikini wa kujitakia kwa Damu ya Yesu, namiliki juu ya nchi, namiliki fedha, namiliki elimu, namiliki makampuni, namiliki uongozi, namiliki utajiri wa fedha, namiliki utajiri wa dhahabu kwa damu ya Yesu, namiliki angani, namiliki ardhini, namiliki baharini kwa jina la Yesu” Amen.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.