SOMO: "SIKUTAMANI FEDHA WALA DHAHABU,WALA MAVAZI YA MTU ”


Na Mchungaji Gasper Madumla.
Bwana Yesu asifiwe….


Paulo anawaambia wazee wa kanisa kutoka Efeso,kwamba ” Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.” Matendo 20:23 Hii inatuonesha kwamba Paulo hakuwa na tamaa juu ya mali ya mtu mwingine katika utumishi wake. Lakini pia Paulo anatufundisha kuwa hakuwa na tamaa ya kujinufaisha binafsi mahali popote katika utumishi wake aliyoitiwa.

Hivyo utagundua kwamba tamaa ni roho kamili itendayo kazi ndani ya mtu. Paulo hakuwa na roho ya tamaa ya fedha,dhahabu wala mavazi ya mtu kwa kujinufaisha.

Kati ya jambo moja baya katika huduma ya Mungu apewayo mtu ni kutamani fedha,dhahabu au mavazi kutoka kwa watu,ikumbukwe kuwa tamaa inaua huduma kabisa. Ninachokiangalia leo si kazi aliyoifanya Paulo kwa mikono yake na kupata kitu cha kujisaidia na kuwasaidia wale aliokuwa nao,bali ninachokiangalia ni ile namna ya kuishinda tamaa ya fedha katika huduma ya Mungu.

Wapo watumishi wa Mungu wenye kujawa na tamaa za pesa kutoka kwa waamini wao kinyume kabisa na neno la Mungu,watu hawa wameshindwa na tamaa ya kupenda pesa kwa kupindukia.Wakiamini kwamba mapato yote wanayoyakusanya ni sahihi mbele za Mungu kumbe sivyo,kwa maana mapato mengine ni kwa ajili yao ya kujinufaisha tu.

Mfano mdogo ni huu hapa;utakuta mtumishi wa Mungu anawalazimisha waamini wake watoe kiasi kikubwa cha pesa kisha wambariki mtumishi pasipo kuwafundisha kwa usahihi njia za mbaraka.

Paulo angeliweza kuwaagiza watenda kazi wake wamletee pesa,au dhahabu,au mavazi. Lakini hatuoni akiwaagiza hao watu wafanye hivyo. Paulo hakutaka kupata mapato ya aibu kuitukanisha huduma ile aliyokabidhiwa na Yesu Kristo Bwana wa utukufu.

▪ Kutamani fedha,dhahabu au mavazi kutoka kwa waamini ni mapato ya aibu.

~ Ninaposema ” mapato ya aibu ” nina maana hii; ni malipo ambayo mtu huyapokea pasipo kustahili kuyapokea. Ni mapato yanayotokana na tamaa na ushawishi wa kimwili. Mtumishi wa Mungu akishawaka tamaa za kimwili,hujikuta akitumia nguvu nyingi sana kuwashawishi waamini hata mara nyingine husema ametumwa na kuagizwa na Mungu kuwaomba watu pesa kwa kiwango fulani cha juu sana kwa lengo la kutimiza matakwa yake.

Mfano aweza akawa anahitaji pesa hizo kwa ajili ya starehe na anasa zake mwenyewe na wala hakutumwa na Mungu kufanya changizo kanisani. Sasa changizo ya namna hii,ni mapato ya aibu!!!

Huduma ya mtu yeyote afanyaye hivi,siku zote haiwezi kuhubiri kweli ya Mungu. Kwa sababu kweli ya Mungu,au injili halisi haipatikani wala kusimamiwa na fedha wala dhahabu bali injili ya Kristo Yesu husimamiwa na kuongozwa na Roho mtakatifu.

▪ Laiti kama Paulo angelitalaji fedha au dhahabu katika huduma yake ni dhahili kabisa asingeliongozwa na Roho mtakatifu.

Ikumbukwe kuwa;Sisemi ya kuwa watumishi wa Mungu wasitegemezwe kwa sadaka au pesa kutoka kwa waamini wao au washirika wao. Bali ninachokisema ni hile hali ya kuwa na roho ya tamaa katika huduma zao, roho ya tamaa katika pesa,dhahabu na mavazi ndio jambo baya la kulikimbia kabisa kama vile Paulo alivyolikwepa.

Mfano mwingine huu hapa;Nalimuona mchungaji mmoja ambaye huvaa mavazi makukuu sana,hula kifahari pia na kuwa na gari za kifahari ambazo zote zimetokana na huduma. Kumbe yule mchungaji alikuwa anawalazimisha waamini wake watoe pesa nyingi kwa ajili ya kumpendezesha yeye na mke wake. Sasa kuna kipindi anazidi na kupitiliza michango yake maana hata katika kuhubiri kwake uhubiri kutoa ili ubarikiwe,tena utoe na kujiungamanisha naye kwa pesa sio kwa moyo.

Hakuna hapingae kwamba kutoa ni chanzo cha kubarikiwa,lakini basi iwe kutoa kwa moyo mkunjufu kwa kuelewa lakini sio kutoa kwa kulazimishwa kwa ajili ya matakwa ya mtu binafsi. Cha ajabu kwa mchungaji huyu ni kwamba waamini wake wamefulia yaani hawajafanikiwa kiuchumi hata kidogo,

Karibia wote wana hali ngumu kiuchumi,tena kuna wahitaji kama vile wajane wapo hapo hapo ambao na wao wamekamuliwa vijisenti vyao vya kula ugali na kuvitoa kwa mtumishi ambaye mtumishi huyo kaenda kujinunulia pea ya viatu vya mtoko. Ukiangalia kiundani utagundua kuwa mchungaji huyu alipaswa awasaidie wahitaji katika huduma yake na sio kuwakamua hata hao kwa matakwa yake.

Huduma yoyote ya Ki-Mungu ikiendeshwa katika roho ya tamaa ya kupenda pesa,kamwe haina mafanikio ya kiroho. Mungu wetu hakututuma tufanye huduma iwe biashara za kujinufaisha nafsi zetu,ndio maana haiwezekani huduma ya kweli ya Mungu isimame katika kupenda pesa kupindukia.

Ikiwa wachungaji wakirejea katika misingi ya kanisa la kwanza la akina Petro,watagundua kuwa hawakuwa hivi tulivyo leo. Bali wao walikuwa na vitu vyote shirika kwa utukufu wa Bwana. Leo haiko hivyo,maana wapo watumishi wenye kuwaka tamaa za mali waweze kujilimbikizia huku ndimi zao zinatoa udenda waonapo penye mali. Yaani mimi nakereka jamani!!! Sijui wewe unajisikiaje ?

Utakuta mtumishi labda ni muimbaji au mchungaji anapoalikwa kuhudumu basi kitu cha kwanza anaanza kunegosheiti bei/ yaani anaanza kupanga kwamba watamlipa Tshs ngapi,na akiona hazina maslahi haendi au la! Kama akienda nakwambia ataenda na mistari yake ya kutaka watu wamtolee pesa,na wala mistari hiyo ya biblia utakuta ilikuwa haielezi kuhusu pesa. Hii ni mbaya sana katika huduma ya Kristo Yesu.

Nami nasema leo wazi wazi mahali hapa ya kuwa ikiwa mtumishi wa Mungu akifanya mabaya haya ya kupenda pesa kinyume na mpango wa Bwana,basi ni lazima atahukumiwa na atapigwa na Mungu mwenyewe.

Ifike wakati sasa na wewe uzichunguze roho za watu wa namna hiyo,ili kama ni kujiengua katika huduma zao basi ujiengue maana sio dhambi kuhama huduma ambayo sio sahihi isiyoongozwa na Roho mtakatifu.▪ Kwa huduma ya maombi na maombezi,usisite kunipigia simu yangu hii;0655111149.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church ( Kimara,Dar-Tanzania )

S.L.P 55051 Dar.

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.