TUACHE KUHUKUMIANA BALI TUONYANE KWA UPOLE

Na Askofu Sylvester Gamanywa,
Mwangalizi Mkuu, WAPO Mission.


Ninatambua kwamba kila mtu ana uhuru wa kutoa maoni, mawazo, maelekezo na inapobidi kupinga maoni, na mawazo ya wengi ambayo kwake anaona hayako sahihi kwa mtazamo wake. Pia natambua kwa Mkristo halisi ni wajibu wake kumshuhudia Yesu Kristo kwa wengine ili mradi afanye hivyo kwa kuzingatia sheria za mamlaka zilizopo. Na pia natambua kwa wale ambao “tunashiriki imani moja, ubatizo mmoja, na Bwana mmoja” kama “familia moja ya kiroho” bado tunao wajibu wa kimaandiko wa kufundishana na kuonyana kila mara maadamu iiitwapo leo. Sasa, pamoja na hayo, kwa nyakati zetu za sasa, hususan katika enzi za “utandawazi wa kikristo” hali imebadilika sana kiasi kwamba, imeibuka kasumba ya watu “kuhukumiana” badala “kuonyana” ambayo imepitiliza mipaka yake. Mada ya leo nataka kuchangia maoni yangu kuhusu vile inavyotakiwa kuwa hasa kwa mujibu wa Biblia:

Utangulizi
“Msikuhumu nanyi hamtahukumiwa; msilaumu nanyi hamtalaumiwa; achilieni nanyi mtaachiliwa.” (Luk.6:37)
Kama haya yasingelikuwa ni maneno yaliyosemwa na Yesu moja kwa moja ambayo yamenukuliwa sio na Luka tu bali hata kwenye Injili za Mathayo na Yohana; pengine ingeliniwia vigumu kuwasilia mada hii. Lakini Bwana Yesu asifiwe ambaye alisema kwamba mbingu na nchi zitapita lakini maneno yake hayatapita milele.
Katika Injili ya Mathayo Yesu amenukuliwa akisema: “Msihukumu, msije mkahukumiwa…” (Mt.7:1); na katika Injili ya Yohana Yesu amenukuliwa akisema: “Basi msihukumu hukumu ya macho tu, bali fanyeni hukumu iliyo ya haki.” (YH.7:24)

Neno “kuhukumu” kibiblia linamaanisha kutoa uamuzi wa kimahakama, au kukosoa na kumtia mtu hatiani kwa kuweka waziwazi makosa yake. Hapa kuhukumu kunaonekana ni kitu kikali na chenye uzito wa juu ambapo Mwenye haki, anayestahili “kuhukumu mtu” ni Mungu peke yake.
Kuhukumu hatua ya juu ya mwisho kuhusu makosa ya mtu. Ni tamko dhidi ya mkosa ambaye anastahili adhabu moja kwa moja. Kwa uzito huu Yesu aliwaonya wanafunzi wake wasihukumiane kwa sababu viwango vya kufanya hukumu ya haki kama Mungu hatuna.

Tofauti kati ya kuhukumu na kuonya
Sasa, nataka tutofautishe kati ya “kumhukumu mtu” na “kumuonya mtu kwa maana ya kurejesha” katika njia sahihi.  Kuhukumu ni pale ambapo “unamlaumu na kumtakia adhabu mkosaji”. Kuhukumu hapa ni kumtia mtu hatiani. Ni kumtamkia mabaya na adhabu inayomtahili. Lakini hapa kuhumu kunajumuisha “kumfanya mosaji aonekane kuwa hafai kitu mbele za wengine”!

Lakini upande wa pili ambao ni “kuonya” wenyewe una mtazamo chanya kuhusu mkosaji katika jitihada za kumfanya atambue makosa yake, na madhara ya makosa hayo, na kumshawishi kutubu kujisahihisha kwa njia ambayo bado heshima yake imetunzwa.

Hapa wengi tunashindwa kutofautisha. Tunaacha “kuoanyana” kwa hofu ya “kutokuhukumiana” na mahali pengine “tunahukumiana” kwa kisingizio cha “kuonyana”.  Tumekatazwa “kuhukumiana” kwa maana ya kukosoana kwa dharau na kuumbuana na kutumia makosa ya wahusika ili kuwavunjia heshima zao; na bila kuwasiliana nao kuamua kuwatamkia adhabu kama sis indo tumekuwa mahakimu wa maisha yao. Lakini tumehimizwa “kuonyana kila iitwapo leo” ili asiwepo hata mmoja wetu atakayeikosa mbingu.

Kigezo cha kupima tofauti kati haya mawili, “kuhukumu” na “kuonya” ni “upole”. Maandiko yamesisitiza sana umuhimu wa kuoanyana kwa upole:

“Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.” (GAL. 6:1).  Hapa tunaupata ushahidi wa moja kwa moja, pale ambapo mmoja wetu, aitwaye ndugu anapokuwa “ameghafilika katika kosa lolote” kwamba tujihadhari sana kwa jinsi tunavyomwendea. Tutahadharishwa “kumrejeza upya mtu huyo kwa roho ya upole” huku tukijichunga wenyewe tusije kuanguka katika makosa yale yale.
Kana kwamba hii haitoshi, bado tumehimizwa kuwa watu wa tabia isiyo ya ugomvi bali kuwa wanana kwa watu wote, wakiwemo hata wapinzani wa imani yetu: 
“Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu;  akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli;  wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake. (2 TIM. 2:24-26)

Hapa tunaelimishwa kutokuwa wagomvi dhidi ya wale wanaoshindana kinyume na sisi, na badala yake tunaagizwa “kuonya kwa upole” wao washindanao nasi. Nia hasa ni kuwashawishi watubu na kuijua kweli, na kwamba wamenasa katika mtego wa Ibilisi.

Mwongozo wa kimaandiko umetupa picha kamili kwamba, tuna haki na uhuru wa kuonyana, lakini kwa roho ya upole. Labda unaweza kusema nitajuaje kwamba sasa naonya wa upole? Upole unaanzia katika mtazamo unaokuwa nao dhidi ya huyo unayemwona kakosea. Ukiwa na mtazamo hasi huwezi kumwonya kwa upole. Maana wakati huo tayari umeshamweka katika kundi la waovu wanaostahili adhabu. Yaani umeshahukumu tayari. Huwezi kuonya kwa upole wakati tayari maneno unayotamka ni ya kulaani na ya kikosoa kwa kulaumu. Kwanza huwezi kumrejeza huyo ndio unampoteza kabisa.

Katika mazingira tuliyomo hivi ambayo maadili yamemomonyoka vibaya kuanzia madhabahuni mpaka mitaani; ni muhimu sana kujua ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu hasa kwa walio wacha Mungu mbele ya wasioamini. Ni wajibu wetu kuonyana kwa nia kurejeshana katika njia sahihi. Lakini tusivuke mipaka kwa kuwavunjia watu heshima zao kwa kisingizio cha kuonya. 
Kumbuka kwamba, kila mmoja wetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu na sio za wengine. Hakikisha kwamba hatufanyi uzembe wa kuacha wakosaji wanaendelea kwa kuogopa kuwaonya ili wasitulaumu kuwa tunawahukumu. Lakini ukweli ubaki pale pale kwamba tusiwadhalilishe kwa kutumia makosa yao kwa kisingizio cha kuwaonya.
“Msikuhumu nanyi hamtahukumiwa; msilaumu nanyi hamtalaumiwa; achilieni nanyi mtaachiliwa.”
Itaendelea toleo lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.