TUJIFUNZE KUPITIA HABARI YA MTEGO WA PANYA

Na Faraja Naftal Mndeme,
GK Contributor.


Katika nchi ya Taknah kulikuwa na mkulima mmoja ambaye alikuwa akilima kwa bidii na muda wa mavuno ukifika huvuna na kuyatunza kwenye ghala maalumu aliloliandaa kwa ajili ya mazao hayo. Baada ya muda mrefu kupita aligundua mazao yake yalikuwa yanaharibiwa na panya mkubwa ambaye alikuwa akija kula na kuondoka, na ilikuwa ngumu kumkamata kawaida.

Baada ya muda kupita aliamua kwenda kununua mtego kwa ajli ya kumtega panya huyo ambaye alikuwa mharibifu wa mazao yake ambayo aliyapata kwa taabu baada ya kazi ya kuchosha. Lakini akiwa kwenye harakati za kwenda kununua mtego huo aliamua kumshirikisha mke wake ili iwapo ana wazo la ziada ampe. Wakati majadiliano yanaendelea kuhusu mtego kumbe yule panya alikuwa ndani ya ghala la mazao akiwasikiliza kwa umakini. Baada ya majadiliano kwisha yule mkulima alienda sokoni kununua mtego kama walivyokubaliana na mke wake. Panya naye aliamua kuondoka mbio maana alisikia kitu ambacho kinafuata iwapo mkulima angerudi kwenye lile ghala.

Panya alipoondoka kwenye lile ghala aliondoka kwa huzuni kubwa maana hakuwa na namna ya kupata chakula cha kutosha  kwa ajili yake na familia yake. Akiwa njiani alipata wazo la kupita kwenye banda la kuku ambapo kulikuwa na jogoo mmoja, kwenda kupata ushauri. Alipofika na kumweleza Jogoo kutaka msaada juu ya yale yaliokuwa yanamkabili Jogoo alimjibu mtego huo mimi haunihusu ni kwa ajili yako wewe ,Mimi siwezi kujiingiza.

Baada ya muda mfupi aliamua kupita kwa rafiki yake mwingine ambaye ni mbuzi kutaka ushauri na msaada wake juu ya mtego ambao ulikuwa unamkabili, na hali yake kwa ujumla na namna ambavyo mtego huo ulikuwa hatarishi kwa ajili yake binafsi na familia yake kwenye swala zima la upatikanaji wa mlo. Mbuzi akamjibu kwamba mimi haiwezekani kujiingiza maana haunihusu kabisa labda atafute msaada sehemu nyingine.

Akiwa anakaribia nyumbani alikutana na rafiki yake mwingine aitwaye ng’ombe. Akamweleza kwa kina na namna anavyoona mtego huo ulikuwa hatarishi kwake na kwa familia yake. Baada ya kumshawishi ng’ombe ili amsaidie iwapo mtego huo ungewekwa. Ng’ombe alimjibu, "sitoweza kujihusisha na kitu kidogo kama hicho, labda utafute msaada sehemu nyingine." Kwa sasa alikuwa anakabiliwa na mambo mengi sana.

Panya akaenda nyumbani kwake kwa huzuni kubwa huku nyuma mkulima alirudi na kuweka ule mtego kwenye ghala lake la chakula ili iwapo panya yule angerudi ungekuwa mwisho wa uhai wake. Baada ya muda wa siku kadhaa kupita mke wa mkulima alienda kuangalia ule mtego iwapo tayari umemnasa panya aliyekuwa amekusudiwa. Alipofika kwenye mtego akaingiza mkono bila kuangalia na ndipo alipogongwa kwenye mkono na kupata maumivu makali. Kumbe mtego ule ulimnasa nyoka badala ya panya.

Baada ya saa kadhaa kupita, mke wa mkulima alikimbizwa hospitali kwa sababu alipoteza fahamu kutokana na sumu kali ya nyoka aliyekuwa amemgonga. Muda ulipopita mke wa mkulima alizinduka na alikuwa hawezi kula kingine chochote, ndipo mkulima alipotuma ujumbe kwa watoto wake nyumbani wamchinje yule jogoo mkubwa na walete supu zahanati alipolazwa mke wake na mama wa watoto wake.

Baada ya siku kadhaa mke wa mkulima aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya matibabu kuisha zahanati. Mke wa mkulima alirudishwa nyumbani. Wageni, majirani, marafiki na ndugu walikuja kutoa pole  kwa habari walizozisikia zimpempata mke wa mkulima. Ndipo mkulima alipoamuru kwamba yule mbuzi mkubwa achinjwe ili wageni wapate kunywa supu na kufurahia pamoja na mkulima na familia yake baada ya muda wa kitambo wa kukaa zahanati wakimuuguza mke wake. Basi ndipo mbuzi yule alichinjwa na watu walikula nyama na kunywa supu yake kwa furaha kuu.

Usiku ule hali ya mke wa mkulima ilibadilika na kupelekea kupoteza uhai wake. Usiku ule ulikuwa wa taharuki kuu na kilio kikuu kutokana na kifo cha mke wa mkulima. Watu wengi walikusanyika kuweza kuomboleza kifo cha mke wa mkulima. Ndipo Ilipoamriwa kwamba yule ng’ombe mkubwa achinjwe kwa ajili ya Shughuli nzima ya msiba iliyokuwepo pale nyumbani kwa mkulima. Ndipo yule ng’ombe alichinjwa na watu walikula nyama yake na supu yake mpaka siku za msiba zilipokwisha.

1. Je Unahisi iwapo jogoo, mbuzi, ng’ombe wangemsaidia yule panya kuhusu mtego unahisi haya yote yangetokea ?

2. Je Unafikiri umejifunza nini kutokana na hadithi hii?


3. Je kuna umuhimu wa kuwasaidia wengine?


E-mail: naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless Y’All

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.