ACHA KUISHI MAKOSA YAKO YA JANA LEO

Faraja Mndeme,
GK Contributor.


Hauwezi kuifanikisha kesho yako kwa kuangalia jana yako. Jana imepita na haiwezI kubadili yaliyopita. Hakuna mtu ambaye hajawahi kufanya makosa kwenye hii dunia, kila mmoja kwa wakati wake amefanya makosa ya aina yake. Huwezi kulibadilisha kosa la jana ili uwe wema wa kesho, maana tayari jana ni historia. Muda wa jana hauwezi kufanana na muda wa kesho, matukio ya jana ,hayawezi kufanana na kesho. Muda mwingi tumeisha kwa kujutia makosa ya jana kwa sababu yametufanya tuwe hivi tulivyo leo. Lakini tunashindwa kutumia muda mwingi kuweza kuitengeneza leo ili tuwe na maisha mazuri ya kesho.

Kuishi makosa ya jana katika leo kunaweza kukufanya usiwe na wakati mzuri wa kuweza kujenga kesho yako nzuri. Ni muhimu kuhakikisha kwamba tayari jana ilishapita na haitarudi tena, haijalishi ni makosa ya namna gani ulifanya lakini tayari imeshakuwa ni historia. Leo ndio wakati pekee unaoweza kuwekeza katika ubora zaidi ili kuepuka majuto ya kesho. Hakikisha unatumia leo yako vyema kama msingi bora wa kesho yako, maana jana haina maana tena, leo ndio wakati mwafaka wa kuijenga kesho yako bora.

Kuishi makosa ya jana leo hakubadili matokeo yako ya kesho. Maamuzi yako ya leo ndio yanaweza kuamua kesho yako iwe ya namna gani. Ni muhimu kuhakikisha unawekeza vyema katika mfumo wako mzima wa maamuzi, maana maamuzi yako yanaamua vitu vingi kwenye maisha yako binafsi na wanaokuzunguka. Boresha mfumo wako wa kufanya maamuzi. Iwapo jana ulitumia namna fulani ya kufanya maamuzi na ikakuletea matokeo mabaya basi badilisha mfumo wako maana tayari umeshajua namna ya matokeo ambayo yatatokea iwapo utatumia mfumo ule ule wa maamuzi.

Kuishi makosa yako ya jana leo ni kupoteza muda, Muda ni jambo huwa halirudi kwenye maisha ya mwanadamu iwapo muda umepita tayari umepita hauna namna ya kuurejesha. Kuendelea kuishi makosa ya jana leo ni kuendelea kuishi wakati uliopita wakati leo imefika. Miaka ya nyuma tulikuwa na simu kubwa sana kama miche ya sabuni lakini leo tuna simu ndogo ndogo sana. Kuishi makosa yako ya jana ni kama kuishi wakati wa simu kubwa zenye umbo mithili ya miche ya sabuni wakati leo tupo na simu ndogo ndogo. Usipokuwa makini unaweza kuhisi unaishi mwaka 2015 kumbe bado unaishi mwaka 2013. Ni muhimu kuhakikisha unaboresha namna unavyotumia muda wako leo ili kesho yako njema na yenye afya ikujie kwa furaha na amani.

Kuendelea kuishi makosa yako ya jana leo ni dalili kwamba kichwa chako hakijajifunza kitu kipya katika leo yako. Makosa ya jana ni ya jana na huenda yalikupa somo fulani ili usirudie makosa yale yale katika leo yako wakati unaendelea kuelekea kesho yako. Ni muhimu kuhakikisha unajifunza mambo mapya kila siku maana yatakupa upeo mpana zaidi, na kuweza kufahamu namna unavyoweza kutengeneza kesho yako kwa ubora wa namna ya hali ya juu kwa kuitumia leo yako. Leo yako ni mtaji wa kutosha kabisa wa kuweza kuifanya kesho yako iwe bora. Maisha ni mchakato na kila jambo lina kanuni na taratibu zake. Unapovunja kanuni na taratibu fulani kwenye maisha maana yake ujiandae kupata matokeo mabaya na adhabu kutokana na kuvunja aina fulani muhimu kwenye maisha yako ya kila siku.

Ukiona unaendelea kupata matokeo yale yale kwenye maisha yako ni ishara ya kwamba bado unaishi jana katika leo yako. Ukiona haujafanya kosa jipya ni dalili kwamba bado unauuguza vidonda vya jana. Jana imeshakuwa historia lakini leo ndio inaweza kuimarisha kesho yako. Makosa ya jana yatabakia kuwa ya jana hakuna anayeweza kurudisha nyuma jana na kuweza kuondoa kila kosa ulilofanya jana. Hakuna mtu anayeweza kubadilisha wakati uliopita bali unaweza kubadilisha wakati wako ujao kwa kupitia leo yako. Jenga utamaduni na utaratibu wa kujifunza na kuwekeza kila kilicho bora katika leo yako. Maisha yamefungwa kwenye mfumo na taratibu za msingi. Ukivunja taratibu na kanuni za msingi basi matokeo ya kile unchokitarajia unaweza usikipate, na hata ukikipata kinaweza kuwa dhaifu zaidi.

Email : naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless You All

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.