HOJA: JE, MUNGU NDIYE MTEUZI WA VIONGOZI WA KISIASA?

Askofu Sylvester Gamanywa.
Mwangalizi Mkuu, WAPO Mission International.

©People Triggers
Utangulizi

Leo naleta mada ambayo wengine wanaweza kuita ni “tata” na wengine wanaweza kutafsiri nimeileta kwa nia ya kufanya kampeni na kadhalika na kadhalika. Kwanza sifanyi kampeni kwa ajili ya mtu au chama chochote bali nataka kuchangia katika kuondoa utata ulioghubika jamii ya kikristo hususan katika suala zima la ushiriki wa Mungu katika kuteua watawala wa nchi hapa duniani.

Ninatambua kwepo kwa dhana mbali mbali zinazokinzana katika eneoo hili, na si kusudi langu kukubaliana na moja dhidi ya nyingine. Hapa nakuja na falsa nzima ya kibiblia kuhusu suala zima maandiko yasemavyo kuhusu utawala wa tangu Kitabu cha Mwanzo mpaka kitabu cha Ufunuo.

Na zaidi naileta mada hii kwa sababu kila ufikapo msimu wa uchaguzi zinatokeza tafsiri nyingi na nabii nyingi ambazo zinatoka zikiwalenga wagombea mbali mbali na nyingi hushindwa kutimia kama “manabii”  walivyo tabiri na hapo ndipo utata mkubwa kuwachanganya watu wengi waliokuwa wamesikia na baadhi wakaamini.

Mpaka hivi saa ninapoandaa makala haya, tayari kuna mzozo unaondelea katika jamii ya Kikristo kuhusu manabii na viongozi wa kikanisa waliotoa unabii wakiwatabiria baadhi ya watangaza nia kuwa watashinda kwenye uteuzi na hawakushinda na sasa wanatafutwa wajieleze ni Mungu yupi aliyewatuma na sasa unabii wao mbona haukutimia.

Japokuwa kuwa hili laweza kuchukuliwa kiwepesi tu kwa dhana za kisiasa, lakini nyuma yale iko roho nyingine ya Ibilisi inayolenga kuwafanya watu kukosa imani na maneno ya viongozi au mahubiri yao kwamba hayana ukweli; lakini pia kuwarudisha nyuma kiimani wengine wasiojua Mungu amesema nini hasa kuhusiana na suala la uteuzi wa watawala wa nchi.

Katika mada hii nataka kujibu maswali ya msingi ambayo hasa ndiyo yatakayotufungua ufahamu wetu na kupata kuyajua kwa usahihi vile maandiko yasemavyo!

1.     Mungu anatambua na kuridhia mifumo yote ya utawala wa kidunia?
2.     Vipi nchi zinazotawaliwa kijeshi au kidikteta Mungu anazionaje?
3.     Kwanini tunaombea chaguzi wa za kisiasa?
4.     Tutajuaje kiongozi fulani ameteuliwa na Mungu?
5.     Katika maombi tupendekeza kwa Mungu tunaowataka au tunamwomba atupe anayemtaka?

Je Mungu anatambua na
mifumo yote utawala?


Mifumo yote ya utawala iliasisiwa na Mungu

“Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake.” (Kol. 1:16)

Maandiko haya yanataja habari za aina mbali mbali za mifumo ya utawala hapa duniani, na kuweka bayana kwamba mwasisi wake ni Mungu na iliumbwa kwa ajili yake. Tukumbuke kwamba tunaposema mfumo hatuna maana ya mtu binafsi ndani ya mfumo au utaratibu wa kuingiza mtu kwenye mfumo. Kilichotajwa hapa ni mifumo ya utawala ambayo kwa asili yake ni mawazo na ridhaa ya Mungu kwamba mifumo hiyo iwepo kama ambavyo aliridhia uwepo wa vitu vingine vilivyopo pia.

Hii ndiyo ilimfanya Mtume Paulo awaandikie Wakristo waliokuepo Roma wasiache kutii mamlaka kwa kisingizio cha imani katika dini, bali watambue kwamba mifumo yote ya utawala iliyoko duniani chimbuko lake ni Mungu. “….vitu vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake….”


Kila mfumo wa utawala uliopo umekubaliwa na Mungu

“Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo imeamriwa na Mungu.” (Rum. 13:1)

Natambua kwamba maandiko haya yameleta mjadala mreeefu na mkubwa na kuzalisha makundi tofauti tofauti kila moja likitoa tafsiri yake ili kutetea mtazamo wake. Lakini hapa tunaendelea kutafuta majibu ya swali letu la msingi la kutaka kujua kama kweli Mungu anatambua mifumo ya utawala iliyopo duniani hivi sasa?

Kwa kifupi maandiko tuliyosoma yanajibu moja moja kwa moja kwamba Ndiyo! Mungu anaitambua na kuikubali mifumo ya utawala iliyopo. Lakini Mungu hahusiki moja kwa moja katika “taratibu za kuchagua na kuapisha viongozi kwenye mifumo husika”! Hili nitatolea maelezo yake baadaye kidogo.

Wakati maandiko kwa Warumi yanaandikwa, mfumo wa utawala uliokuwa ukitawala katika dunia ya wakati ule ulikuwa ni “mfumo wa kifalme”. Huu ni mfumo wa utawala wa mtu ambaye amekuwa mfalme kwa kuzaliwa kutoka kwenye ukoo wa kifalme. Huu ni mfumo tofuati na “mfumo wa Demokrasia” uliopo sasa ambapo viongozi wake wanapatika kwa kuchaguliwa na raia kwa njia ya kura. Bado mifumo yote hii inaendelea kutawala hivi sasa, japokuwa mfumo wa Demokrasia ndio umeshika dunia kwa sehemu kubwa.


Vipi nchi zinazotawaliwa kijeshi
 au kidikteta Mungu anazionaje?

Katika ulimwengu wa sasa ambao umetawaliwa na mfumo wa Demokrasia, “mifumo wa utawala wa kijeshi” haukubaliki kwa sababu haujatokana na ridhaa ya raia wa nchi husika. Lakini zamani, hata mfumo wa kifalme ulipanua mipaka ya utawala kwa kupigana vita na kuteka nchi nyingine. Kwa wakati huo huo bado mfumo huo uliruhusiwa kuwepo na Mungu. Swali letu linahoji kuhusu mtazamo wa Mungu kwa mifumo ya tawala za kijeshi.

Sasa itategemea sana na mazingira ya kila nchi husika. Katika Afrika tunazo nchi ambazo hata kama si Jeshi ndio linatawala nchi lakini marais wake ni wanajeshi na wameshika madaraka katika nchi zao wakitokea msituni.

Hata kama baadaye waliamua kuruhu mfumo wa Demokrasia kwa shinikizo tu la jamii ya kimataifa, lakini bado harufu inayoendelea kutawala bado ni “mamlaka ya kijeshi.”! Sasa Mungu anazionaje nchi hizi? Jibu ni kwamba anazitambua kama anavyotambua mfumo wa demokrasia.

Kwa kifupi, kuna nchi ambazo, asili ya watu wake, pamoja na tamaduni zao, wanaweza kutawaliwa na mifumo yenye mwelekeo wa kijeshi ili kudhibiti uasi na machafuko yenye kuendeleza vita vya kiraia. Kwa maneno mengine kila nchi na raia wake wanatawaliwa na aina ya mfumo ambao unafanana na tamaduni zao mahali walipo.

Itaendelea toleo lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.