HOJA: JE MUNGU NDIYE MTEUZI WA VIONGOZI WA KISIASA? (2)

Askofu Sylvester Gamanywa,
Mwangalizi Mkuu, WAPO Mission International.

Jumatatu iliyopita (bofya hapa) tulianza hoja mpya ya kujibu swali la kama Mungu ndiye mteuzi wa viongozi wa kisiasa. Humo tulianza na utangulizi na kasha tukapitia vipengele vinavyochambua kama Mungu anatambua mifumo ya tawala zilizopo duniani hivi leo; na hasa zikiwemo zile za kidiktena na kijeshi. Tunajifunza kwamba Mungu anatambua na kuridhia na leo tunaingia kwenye vipengele vingine muhimu tukianza na “uhuru wa kuchichagulia viongozi’:

Alitoa uhuru wa kujichagulia

Leo napenda kufafanua kuhusu uhuru wa kujichagulia ambao Mungu ameutoa kwa habari ya kuwapata viongozi wa kijamii. Kwa hapa nataka kuweka bayana kuhusu ni kwa jinsi gani Mungu anamchagua kiongozi anayemtaka ili awaongoze watu katika nchi au eneo husika.

Kwa mujibu wa maandiko matakatifu, tunajifunza kwa Musa pale alipowaaiza wana wa Israeli wenyewe ndio wajichagulie viongozi kutoka miongoni mwao:

“jitwalieni watu wenye akili na fahamu, watu wanaojulikana, kwa kadiri ya kabila zenu, name nitawafanya wawe vichwa vyenu. Nanyi mkanijibu mkaniambia jambo ulilonena ni jema la kufanya. Basi nikatwaa vichwa vya kabila zenu, maakida elfu elfu, na maakida mia mia, na  maakida ya hamsini hamsini, na maakida ya kumi kumu, na wenye umri, kwa kadiri ya kabia zenu…” (Kumb.1:13-15)

Kwa maandiko haya tunajifunza kwamba, Musa aliwapa uhuru wana wa Israeli kujitwalia watu miongoni mwao. Isipokuwa Musa alitoa vigezo na sifa za kuwasaidia kuwatambua hao viongozi wanaohitajika. Hapa tunazipata sifa zifuatazo:

1.              wenye akili na fahamu

Hawa watu wenye akili na fahamu kilicholengwa ni ujuzi na elimu ya nyakati hizo. Haina maana kuna watu wasio na akili na fahamu. Wakti wakiwa utumwani Misri, wapo watumwa ambao walipata fursa ya mafunzo ya kusimamia wengine, na wengine walifanya huduma kwenye himaya za Farao.

2.              Wanaojulikana

Kujulikana ni mojawapo ya sifa ya kumpata kiongozi. Ni maana ya kujulikana. Hapa kililengwa kipaji cha ushawishi. Mtu mwenye kipaji cha ushawishi ni yule ambaye amejaliwa hekima ya kutoa mawazo yenye uzito na kukubaliwa na wengi wanaomzunguka.

 Hata kama hana cheo chochote, lakini anajulikana na kila mtu kwamba ni mtu mwenye ushawishi kwa hoja zenye nguvu. Kwa hiyo, kujulikana kwa namna hii ndiko ambako kulitumika kama sifa ya kuteuliwa kuwa kiongozi wa wengine ambao wanategemea hekima na busara zake ambazo wote wanajikubali.


3.               Wenye kuwakilisha kabila

Sifa nyingine muhimu ya kumpata kiongozi ilikuwa ni lazima awe anatokana na kabila husika. Hi ni kwa sababu aina ya uongozi uliokuwa umependekezwa ni wa mfumo wa uwakilishi. Mfumo huu uliwapa fursa kila kabila kumpata kiongozi wao ambaye anafahamu mahitaji ya watu wake na apate kusimamia maslahi ya watu wake.

Kwa kupitia sifa zilizotajwa hapa juu, wana wa Israeli waliwachagua watu watakaokuwa viongozi wao katika

Mfumo wa uongozi wa makundi

Kama ukichunguza aina ya mfumo wa uongozi kwenye maandiko tuliyosoma, tayari tunapata kujua kwamba mifumo mingi ya tawala zilizopo hivi leo nyingi zimeiga kutoka kwenye Biblia. Hapa ndipo tunakupata mfumo wa uongozi wa makundi unaonzia na nyumba kumi na kuendelea mpaka kuongoza maelfu. Mfumo huu pia unatumika kwenye majeshi.

Uzuri wa mfumo huu, ni kwamba, unasaidia kuwa na viongozi kulingana na uwezo wao wa kuongoza. Kiongozi mwenye kusimamia watu mia maana yake anao uwezo mkubwa kuliko mwenye kusimamia kundi la watu kumi.

Lakini pia mfumo huu ulisaidia katika kufikisha huduma za kila mtu mmoja mmoja, na pale mahitaji yake yalipokuwa mazito yaliwasilishwa ngazi ya juu kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi.

Jambo jingine muhimu ambalo lilishughulikiwa katika mfumo wa makundi, ni kukumbuka kwamba, hawa walikuwa ni kundi kubwa la mamilioni ya watu ambalo lilikuwa kwenye msafara wa miaka jangwani. Hawakuwa na makazi ya kudumu na kwa hiyo mahitaji au matatizo yao yalikuwa magumu kwa sababu ya mazingira magumu waliyokuwemo.

Viongozi wa makundi walitumika pia kusuluhisha migogoro iliyokuwa inajitokeza miongoni mwao. Binadamu hulka yake ni kutokuridhika, kulalamika na kulaumu. Katika mazingira magumu binadamu anakata tama upesi na kushuka moyo na hata kufanya maamuzi yaliyo dhaifu yenye kumwathiri yeye mwenyewe. Kwa hiyo mfumo wa uongozi wa makundi ulisaidia kusikiliza na kutatua malalamiko ya watu kuanzia ngazi ya watu kumi na kuendelea.

Katika uchambuzi huu, tunapata kujifunza kwamba, kwa habari ya kuwapa viongozi wa watu, Mungu alitoa uhuru kwa watu wenyewe kushiriki kujichagulia watu ambao wanawatambua wanazo sifa zinazokubalika kushika uongozi au usimamizi wa mambo kwa niaba ya wengine.

Hata ndani ya kanisa la kwanza, iilipojitokeza tatizo la kijamii, ambalo halihusiani kabisa na mambo ya huduma za kiroho, mitume walitumia mfumo huu huu wa kuwapa uhuru waaminii kujichagulia watu miongoni mwao watakaosimamia mambo ya kijamii wakiwakilishi makundi yaliyokuwemo ndanii ya kanisa:


“Basi ndugu chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia neno.” (Mdo.6:3-4)

Kwa maandiko haya tunakutana tena na utaratibu wa kuwapata watu wa kusiimamia mambo ya kijamii ndani ya kanisa ulikuwa na vigezo vya sifa za kuwatambua walengwa; lakini uhuru wa kuwachagua ulikabidhiwa kwa waamini wenyewe.

Inaendeleo toleo lijalo
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.