HOJA: MAOVU NA WAOVU - ASKOFU GAMANYWA

Mungu bado anachukia maovu na
pia anawachukia watendao maovu

Kuna dhana maarufu isemayo “Mungu anachukia maovu” lakini “anawapenda watenda maovu”. Dhana hii pamoja na kuwa maarufu sana lakini bahati mbaya haina ushahidi wa kimaandiko yenye kumaanisha kile ambacho dhana hii inataka wengi waamini:
Askofu Sylvester Gamanywa

Dhana ya Mungu “kuchukia maovu”
na “kuwapenda watenda maovu”

Nasema hivi kwa sababu dhana hii imebeba fumbo gumu kweli ambalo ni kuwepo kwa uzi mwembamba kati ya kumtenganisha mtendamaovu na maovu yake? Je Unaweza kuyaadhibu maovu pasipo kumwadhimu mtenda maovu?

Hivi kwani ni kipi kitakacho hukumiwa kwenda jehanamu ya moto? “Maovu ya mtu” au “Mtenda maovu”? Kama mtenda maovu ndiye anakwenda motoni kwa matendo yake maovu, kipi kimechukiwa na Mungu ni maovu ya mtendamaovu au mtendamaovu kwa maovu yake?

Haya mfano mwingine, hakimu au jaji mahakamani anapotoa adhabu hulenga nini? Mkosaji au makosa ya mkosaji? Kinachokwenda kutumikia kifungo ni makosa ya mtu au mtenda makosa? Unaona kitendawili hiki kigumu? Ni jinsi gani tunaweza kutenganisha au kuhusianisha hivi viwili?Majibu kamili japokuwa ni magumu ni kwamba Mungu anawachukia wenye dhambi kwa sababu ya dhambi zao na sio kwamba anachukia dhambi zao peke yake. Hebu tusome baadhi ya maandiko yafuatayo:“Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.” (LAW. 20:23) Unaona jinsi ilivyoandikwa? “…kwa ajili ya hayo niliwachukia..


“Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; Naam, viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo, Na mikono imwagayo damu isiyo na hatia; Moyo uwazao mawazo mabaya; Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; Shahidi wa uongo asemaye uongo; Naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.” (MIT. 6:16-19)

1.     Macho ya kiburi na sio kiburi peke yake
2.     Ulimi wa uongozi na sio uongo peke yake
3.     Mikono imwagayo damu na sio umwagaji damu peke yake
4.     Moyo uwazao mabaya na sio mabaya peke yake
5.     Miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu na sio maovu peke yake
6.     Shahidi wa uongo na sio uongo peke yake
7.     Mpanda mbegu za fitina kati ya ndugu na sio fitina peke yake

Je Maandiko haya ni makali na magumu? Mungu anachukia dhambi. Lakini anapoadhibu haiadhibu dhambi peke yake bali humwadhibu mtenda dhambi. Dhambi yenyewe haishikiki na kufungwa na kutupwa kwenye kapu la uchafu na kuchomwa moto peke yake. Dhambi ni uasi unaofanyika ndani ya moyo wa mtu na kuhusisha utashi wake binafsi. Kwa hiyo, Mungu analazimika kumwadhibu mwenye dhambi kwa sababu ni matunda ya maamuzi yake ya uasi. Kesho tutaendelea na kipengele cha pili ambacho ninatetea dhana ya Mungu kuwapenda watenda maovu kwa maandiko ya Mungu kuupenda ulimwengu hata akamtoa Mwanawe pekee ili kila amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.

Mungu alipoupenda ulimwengu
hajaa kuwachukia watenda maovu

Dhana inayotetea kwamba Mungu alikwisha kuacha kuwachukia watenda maovu na ndiyo maana alimtuma Mwana wake pekee kwa ajili ya kuwakomboa watenda maovu bila masharti. Na maandiko yanayotumika kutetea dhana ni haya yafuatayo:

 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.  Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.  Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.” (YN. 3:16, 18, 19)

Maandiko haya na mengine yenye kufanana na haya yametumika sana kuhalalisha dhana ya Mungu kuwapenda watendao maovu isipokuwa anachukia maovu peke yake. Lakini tukisoma huu mstari wa 18 wenyewe unafunua siri ya Mungu kwachukia watendao maovu pale tunaposoma kwamba……

“…Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu….”  Unaona nini? “asiyeamini amekwisha kuhukumiwa..” na kisa cha kuhukumiwa kwake ni nini? Tumesoma kwamba: Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu.”
Asiyeamini ni mtu kupenda giza kuliko nuru; na kupenda giza ndiko kupenda kutenda maovu! Kwa hiyo, kwa mujibu wa maandiko tuliyosoma ya Mungu kuupenda ulimwengu, hakuna maana ya kupenda watendao maovu bali anawapenda waliotubu na kuacha maovu. 

Tukumbuke kwamba tukio la Mungu kuupenda ulimwengu lilimgharimu “kumwadhibu Mwanawe adhabu kali na akamalizia hasira zake zote juu ya Yesu Kristo pale msalabani. Unaona? Yesu aliadhibiwa kwa sababu ya maovu yetu! Kwanini? Ili sisi tukiitambua na kutubu kwa kuomba utakaso wa damu ya Yesu, tuokolewe bure pasipo kupata adhabu ambayo tuliistahili tangu mwanzo

Pili tutofautishe Mungu kuwa “mvumilivu kwa watendao maovu” na dhana “kuwapenda watendao maovu”. Ukweli unabakia kwamba, pamoja na Yesu kujitoa dhabihu kwa kila mtenda maovu ili afikie toba na kuokolewa; bado mhusika asipotubu tayari amekwisha kuhukumiwa kwenda jehanamu ya moto.

Ni kweli Mungu hafurahi kifo cha mwenyedhambi! Lakini haimaanishi kwamba amewaondolea hukumu ya adhamu ya jehanamu ya moto kama wasipotubu! Ndiyo maana tumesoma kwamba huyo  “asiyeamini” amekwisha kuhukumiwa sio kwamba ni “mtenda maovu” bali zaidi ni “mpenda maovu”! 

Tuache kuwafariji watendao maovu kwamba Mungu anawapenda. Ni muhimu sana wajue na kutambua kwamba bado Mungu anawachukia watendao maovu kwa sababu “wanayapenda maovu” kuliko kumpenda Mwanawe aliyekubali kuadhibiwa kwa niaba na kwa ajili yetu.

Mwisho
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.