KWA TAARIFA YAKO: BINTI WA MCHUNGAJI ALIYEKATAA KUMKANA KRISTO KISHA KUUWAWA NA BOKO HARAM

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu.


KWA TAARIFA YAKO hii leo tupo nchini Nigeria, kumbuka suala zima la kundi linalojiita la Boko Haram ambalo limekuwa maarufu duniani kwa vitendo vyake vya mauaji kwa Wakristo wasio na hatia huko nchini Nigeria wakitaka dini ya kiislamu itawale nchi hiyo. Lakini kubwa zaidi ambalo liliwaacha watu wengi duniani midomo wazi, ni kitendo cha kundi hilo kuteka mabinti zaidi ya 300 asilimia kubwa kutoka shule ya sekondari ya Chibok na kuwaficha sehemu ambayo hata serikali ya Nigeria na vikosi vyake enzi za utawala wa Rais Goodluck Jonathan kushindwa kuwarudisha mabinti hao.

KWA TAARIFA YAKO ni kwamba licha ya kampeni kubwa kufanywa na wanawake kwa waume zikiongozwa na watu maarufu duniani akiwemo mke wa Rais Barack Obama bibie Michelle Obama kutaka kundi hilo kuwarejesha mabinti hao bila mafanikio. Taarifa mbalimbali zilidai kundi la Boko Haram liliwateka wasichana hao kwaajili ya kuwaozesha kwa wapiganaji wao huku pia kwa wale ambao ni wakristo walitakiwa kubadilisha dini zao na kuwa waislamu kinguvu. Miongoni mwa mabinti hao ambao kwasasa inadaiwa ni marehemu ni Monica Mark ambaye baba yake ni mmoja wa wachungaji huko nchini Nigeria.Video ya baba na mama mzazi wa Monica wakieleza kwa ufupi


KWA TAARIFA YAKO kwa mujibu wa habari ambazo wazazi wake walipewa ni kwamba Monica aligoma kubadili dini na kuwa mwislamu kitendo ambacho kiliwafanya wapiganaji wa Boko Haram kuchimba shimo lefu na kumfukia binti huyo na kuacha sehemu ya kichwa tu ikionekana na kuanza kumpiga kwa mawe mpaka umati ulipompata. Kitendo cha kuuwawa kwa binti yao kimewauma wazazi hao ila pia kimewafurahisha kwa jinsi alivyoweza kuitetea imani yake mpaka mauti kwa kutomkana Yesu mbele ya wapiganaji hao.

KWA TAARIFA YAKO toka Rais Goodluck Jonathan atoke madarakani pamekuwepo na maendeleo ya haraka ya kuokolewa kwa watu mbalimbali hususani wanawake waliokuwa wametekwa na kundi hilo chini ya utawala wa Rais mpya wa nchi hiyo Muhammadu Buhari. Taarifa zinasema kati ya wanawake wengi waliopatikana wamethibitisha hali ilivyokuwa huko hasa suala la kupigwa mawe hadi kufa kwasababu ya kukataa kubadili dini na kuwa waislamu.

Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO kwa leo, endelea kuwaombea watu mbalimbali waliopo vifungoni kwasababu tu ya kumkiri Kristo kuwa BWANA na MWOKOZI wa maisha yao, kwamba wasitetereke   bali wakisimamie imani yao mpaka mwisho..


Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.