KWA TAARIFA YAKO MWALIKO WA PAPA FRANCIS ULIVYOMUWEKA MATATANI MWIMBAJI NYOTA WA INJILI

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu
KWA TAARIFA YAKO imekuwa kawaida kwa waumini wengi wa dini ya kikristo duniani kupenda kuwahukumu waumini wenzao kwa mambo ambayo hawana uhakika nayo ama kwakufuata mkumbo wa marafiki zao na kujikuta wakianza kazi za kuchambua makosa ya watu kama wenyewe wanavyodhani bila kujua hasa sababu za mlengwa kufanya hivyo. Hii inatokea kwa baadhi ya waumini wa kanisa ama huduma fulani kuanza kuwanyooshea vidole waumini wa makanisa mengine kwamba hawana Mungu, hawafundishwi maneno ya Mungu huku wakijiona wao ndio wamesimama kuliko mtu yeyote.

KWA TAARIFA YAKO hapana shaka unamfahamu mwanamama Darlene Zschech aliyewika kama kiongozi wa sifa wa kanisa la Hillsong lenye makao makuu yake Australia kabla ya mwanamama huyo kuachana na kanisa hilo na kwenda kusimamia huduma yake pamoja na mumewe huko huo nchini Australia takribani miaka saba sasa. Mwanamama huyu ambaye alipata jaribu la ugonjwa wa kansa ambao hata hivyo Mungu aliweza kuingilia kati na kuweza kuudhibiti kwa kiwango kikubwa na kumfanya awe salama na kuendelea na huduma yake kwasasa. Darlene alijikuta katika wakati mgumu mapema mwezi huu akihukumiwa kwa kitendo chake cha kukubali mwaliko wa kwenda kuimba Vatican nchini Italia ambako alipewa mwaliko na Wakatoliki waliookoka.

Darlene akisalimiana na Papa Francis katika tukio hilo
KWA TAARIFA YAKO Darlene kupitia blog yake aliandika makala aliyoipa jina Changes (Mabadiliko) ambapo alianza kwa kuwa na shukrani kubwa kwa muda alioupata wa kwenda Rome Italia kuhudumu, huku akidai kwamba licha ya kuacha mialiko mingi anayoalikwa kwenda kutoa huduma. Amesema yeye na mumewe walimuomba Mungu juu ya tukio hilo lililoandaliwa na waumini wa kanisa Katoliki waliookoka 'Catholic charismatic renewal' na kupewa baraka na Papa Francis.

KWA TAARIFA YAKO
Darlene aliweka wazi kwamba lengo kuu la tukio hilo lilikuwa kuwakutanisha wafuasi wa Kristo kutoka madhehebu mbalimbali pamoja ili kuiombea dunia. Ingawa Darlene aliona jambo jema na kuwa na amani nalo kuhudhuria, kwa bahati mbaya wafuasi wake katika mitandao ya kijamii waliamua kuonyesha hasira zao kwa mwimbaji huyo kwa kitendo chake chakukubali mwaliko huo hali akijua kanisa Katoliki halifuati misingi bora ya Kikristo.

KWA TAARIFA YAKO jumbe za kumhukumu kutoka kwa wafuasi wake hao, ikabidi mwanamama huyo aamue kuandika makala hiyo na katika moja ya ujumbe wake aliandika "Imenibidi niseme, sikutarajia kupata jumbe za kuhukumu na kunikosoa kwa uamuzi wangu wakushiriki tukio hili, bila kujua ni kwanini au sababu gani zilinifanya niwe pale, au kwanini nilijisikia ilikuwa muhimu kwamimi kuwepo pale. Sikushiriki lile tukio hili nihukumu, sikuwa pale ili niwe Mkatoliki, sikuwa pale kwaajili ya kutalii. Bali nilikuwa pale kuliinua jina la Yesu…. bila kusita au maelewano nje ya hilo…. kwasababu nimejifunza miaka mingi kwamba Yesu anapokuwa katikati ya jambo lolote linaweza kutokea" aliandika Darlene.KWA TAARIFA YAKO
mwimbaji na mtunzi huyo wa nyimbo maarufu za injili aliendelea kuweka uzito zaidi pale aliposema alibarikiwa katika tukio hilo. "Ndiyo nilikutana na Papa Francis, na nikweli nimeshuhudia Mungu wa miujiza, anayetutafuta sisi bila kujali madhehebu yetu, utaratibu wa ibada zetu,liturugia, umri au upendeleo wowote… Ukweli wa mioyo yetu katika kumtafuta yeye ndicho anachokiangalia" alisema Darlene. Aidha mwimbaji huyo alitumia vifungu mbalimbali vya Biblia kuwajibu wafuasi wake hao kuonyesha ni kwa jinsi gani wanahitaji kubadilika na kuacha vitendo vya kuwahukumu watu kwakuwa hiyo siyo kazi yao bali ni kazi ya Mungu.Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO wiki hii, vinginevyo tukutane wiki ijayo….

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.