MASHAKA NA UOGA NI VIKWAZO VYA KUKUFIKISHA MAHALI UNAPOPASWA (2)

Kelvin Kitaso,
GK Contributor.

Wiki iliyopita tulianza kwa kutazama dhana nzima kuhusu uoga na vikwazo. Unaweza kubofya hapa ili kuisoma. Kwa wiki hii tutatazama namna ya kuushinda uoga.


Mambo ya msingi ili kuweza kuishinda hali ya uoga:

1. Usiogope.

2 Wafalme 6:15-16 “…………………………, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyaje? Akamwambia, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”
Neno usiogope ni neno lenye maana kubwa sana nimeelezea kwa undani katika kitabu cha ‘uungu wa mwanadamu na maisha yenye kibari mbele za Mungu’ na popote ulionapo neno hili limetumika ujue nyuma yake ipo/zipo sababu za kuogopa japo vijana wengi upenda tumia kama neno la kawaida katika mazungumzo yao ila matumizi sahihi ni pale kunapokuwa na sababu za kuogopesha.

Na Mungu anaposema neno hili usiogope umaanisha mengi na haina maana kuwa haoni kuwa yapo yanayoogopesha ila yeye anaona sababu za kukufanya wewe usiogope ni nyingi na kubwa kuliko zikufanyazo uogope nazo ni kama:
·    Yupo pamoja nawe nyakati zote hata ukamilifu wa dahari.
·    Anaweza juu ya jambo linalokusumbua.
·    Hakuna neno gumu asiloliweza.
·    Ameona na kutazama kuteseka kwako na yupo apate kukusaidia.
·    Hakuna liwezalo kusimama mbele zako likafanikiwa.
·    Tulia tu ili atende kwa uweza wake, n.k

Pia neno hili usiogope lina maana sawa na ile ya kuwa hodari na moyo wa ushujaa. Ni taarifa njema kufahamu kuwa neno usiogope kwenye biblia lipo kwa hesabu za siku za mwaka mzima kwa maana ya kwamba kila siku ina ‘usiogope’ moja, kila uamkapo lipo neno la BWANA lisemalo usiogope  kwa kuwa waweza kutana na yaogopeshayo ila kila siku tumia moja hata mwaka uishapo na kuanza mwingine kwa namna hiyo hiyo.

2. Usienende kwa kuona bali enenda kwa imani.

2 Wakorinto 5:7 “(Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona)”
Kwa maana nyingine ni kusema kuwa mazingira usema kuwa haiwezekani ila imani ambayo chanzo chake ni kusikia neno la Mungu usema kuwa “nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu, Filipi 4:13.” Ni vyema kutoangalia kwa macho ya damu na nyama na kukubaliana na ile hali uliyonayo ila ni busara sana kutazama nini Mungu anatazama kwako.

Kwa kutazama Yese alimwona Daudi kama kijana mdogo sana na hakuona kile kitu kilicho ndani ya Daudi ila Mungu yeye hakumtazama Daudi kama mchunga kondoo tu, bali aliona zaidi kwa kumwona mtu mkubwa na mpakwa mafuta wake wa kusimama kama mfalme.

Usikatishwe tamaa na mazingira uliyonayo leo pengine ni magumu sana na yanakupa mashaka kama utakuja kuwa mtu mkubwa fahamu kwamba hayo uonekana tu ila kwa imani utakuwa kama vile Mungu akuonavyo. Ni vyema sana kujifunza kwa ndugu zetu walio tangulia katika biblia nao walianza sehemu mbaya sana lakini hawakutazama mazingira yanatabiri nini kwa habari yao bali walitazama nini Mungu anasema kwa habari ya maisha yao.

Watu watakutazama kama mtu mdogo sana kama walivyo mtazama Daudi ila Mungu anakutazama kama mtu mkubwa na mfalme juu ya watu wake; watakuona mfungwa ila Mungu anaona waziri mkuu kama alivyomuona Yusufu. Kamwe usikubaliane na watu wakutazamavyo kwa kuwa akuonavyo Mungu si kama watu waonavyo, wao wanaweza kukuona wa kawaida ila Mungu anakuona mtu mkubwa.

I Samweli 16:7 “Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa, BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje bali BWANA huutazama moyo”

Mungu kamwe hatazami umbo, historia, mali za mtu bali uangalia moyo wa mtu. Alipotazama kule porini na machungani alimuona Mfalme mkubwa wa taifa la Israeli japo Yesse aliona mchunga wanyama aliye na thamani ndogo kuliko ndugu zake wengine. Alipotazama gerezani alitazama na kuona mtu mkubwa wa kuwa waziri mkuu japo Potifa yeye aliona mfungwa na mtumwa. Alipoangalia Midiani aliona mkombozi wa wana wa Israeli kutoka Misri aitwaye Musa japo Yethro kuhani wa Midiani aliona mchunga mifugo. Aonavyo Mungu si kama vile wanadamu wengine wawezavyo kuona kwa kuwa wao waweza kukuona si kitu ila Mungu akaona mtu mkubwa sana ndani yako.

Mungu kamwe haangalii umezaliwa kwenye familia ya namna gani au ulitoka kwenye tumbo la mama wa namna gani au viuno vya baba wa namna gani ila anaangalia kusudi lake juu yako ambalo lilikuwepo kabla ya uwepo wako katika tumbo la mama yako.

Mithali 23:7a “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.”
Ona vyema kama Mungu aonavyo huku ukitambua ya kuwa uonaji wako ndicho kipimo cha hatima yako, kwa maana ya kuwa utakuwa kwa namna ile ujionavyo nafsini mwako. Kuna msemo wa Kiswahili usemao “mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake” na ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa mtu uwa kwa upana wa utazamaji wake na kamwe mtu hawezi kuvuna asichopanda kwa kuwa apandacho mtu ndicho avunacho ni rahisi kusema alichokibeba mtu ndani yake ndicho atakacho kitoa kwa kuwa haiwezekani mtu atoe kitu kisichokuwa ndani yake na pia ni wazi sana kuwa yamtokayo mtu ni yale yaujazayo moyo wake na si yalio nje yake.

Mazingira na watu pia uweza sema  wewe hauwezi kufanikiwa, kupata kazi, kuwa mtu mkubwa, kuwa na ndoa nzuri, kupata mchumba,nakadharika ila Mungu naye usema kuwa mambo yote hayo kwake yanawezekana na hakuna lisilowezekana kwake na anahitaji uwe na imani tu kwa kutotia shaka.

Matendo ya mitume 4:19 “Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe”
Ni bora kumsikiliza Mungu katika mambo magumu unayoyapitia maana kwa kusikiliza watu ni rahisi sana ukarudi nyuma na kushindwa kuyatimiza makusudi ya Mungu.

Marko 10:27 “Yesu akawakazia macho, akasema, kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yanawezekana kwa Mungu”
Wakikukatisha tamaa wewe sema “kwa wanadamu kama nyinyi/wewe haiwezekani lakini kwa Mungu inawezekana”

Luka 1:37 “Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu”
Wewe fanya yale yakupasayo kufanya ili upate kufanikiwa kwa kuwa hakuna limshindalo Mungu.

Kwenye hili eneo la Imani bado watu wengi wamekuwa na mtazamo hafifu na si wa kiMungu kwa kuwa wengine usema kuwa namwamini Mungu atatenda tu ila hawafanyi kazi yoyote ili wapate kufanikiwa, ni jambo jema kufahamu sana kuwa Mungu hapendi watu wasioshughulika kwa kuwa yeye hafanyi kazi na mkono mlegevu kwa hiyo hata kama utakiri sana kuwa itakuwa ila kama haufanyi juhudi zozote usidhanie kuwa utapata kufanikiwa. Mungu ameahidi kubariki kazi za mikono ya watu wamchao na ni vyema kufahamu kuwa kama ukifanya kazi ndipo Baraka za Mungu ukutana na wewe huko ili apate kuzidisha yale uyafanyayo.

3. Dharau tatizo na kuliona kuwa dogo kwa kuwa aliye upande wako ni mkuu kuliko tatizo lililo kinyume nawe.

Hesabu 14:7-9 “wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuipitayo kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. 8 Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. 9 Lakini msimwasi BWANA, wala msiogope wala wenyeji wan chi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope.”

Sehemu hii ya maandiko nimekuwa nikiipenda sana na kuifurahia kila wakati napoitazama kwa kina zaidi. Joshua na Kalebu wanaonyesha ushujaa wa hali ya juu sana ambao kama ukisoma kwa kawaida tu hauwezi pata undani mkubwa wa yale waliyoyasema, cha kwanza wanaliona taifa kubwa lililotia uoga na mashaka taifa la Israeli kuwa kama chakula kwao yaani kwa maana nyingine ni kuona kuwa ni kitu kidogo sana ambacho unaweza kukila si kikudhuru bali kikutie nguvu ya kusonga mbele, Joshua na Kalebu wao waliona mbali zaidi ya kuwa wanasafari ndefu sana na kama wasipopata chakula kama wanefili ambacho ni chakula chenye nguvu watateseka na njaa katika safari waiendeayo. Wao waliona fursa katika matatizo, chakula katika matatizo na sina maana ya kwamba walimaanisha kuwa wawale nyama yao ila waliona ni kitu kidogo sana kwao. Lakini jambo jingine wanaona ule uvuli uliokuwa ndani yao umeondolewa, yaani ule utiisho au kile kinachowafanya waogopeshe kimeondolewa ni sawa na kumwona simba atishaye sana ila hana meno na kucha ambazo zaweza kukudhuru ndivyo walivyoona Joshua na Kalebu kwa wale Wanefili.

Kwako leo inawezekana wapo wanefili wasumbuao ila ni vyema kuona kama mashujaa hawa walivyoona. Yaani kuona fursa katika tatizo na si kuona adha katika tatizo lililo mbele zako na kujua katika kila tatizo linalojitokeza mbele zako ipo fursa (chakula chako) ila ni swala la wewe kuwa jasiri na kutumia fursa hiyo.

Mithali 28:1b “……Bali wenye haki ni wajasiri kama simba” Wenye haki wa Bwana ni majasiri kama simba na hakuna la kuwatisha.

1 Samweli 17: Inaelezea kwa kina sana mwanzo wa tatizo na hata mwisho wa tatizo na jinsi kijana Daudi anavyopambana vyema na kuzidi hata kwa mfalme Sauli.

Tofauti ya Sauli na Daudi katika tatizo lililotokea ni:
·    Sauli alitazama tatizo kama lilivyo na kulitukuza; ila Daudi aliona tatizo ni dogo sana na kumshusha sana mfilisti.

·    Sauli alipomtazama Goliathi akaona kama ‘giant’ (shujaa/shupavu) asiyepigika; ila Daudi akamtazama kama ndege ndo mana akabeba silaha za kuulia ndege. Ni bora angemtazama kama dubu au simba angebeba mkuki na siraha kubwa ila yeye alimuona kama ndege.

·    Sauli alitegemea akili zake mwenyewe bali Daudi alimtegemea Bwana.

·    Sauli alikwenda kwa kuona ila Daudi alikwenda kwa Imani, 1 Wakorinto 5:7.

·    Daudi alimsikiliza Bwana na kumtii kwa kile Bwana aonavyo ila haikuwa hivyo kwa Sauli, Matendo 4:19.
Hata kama tatizo ni kubwa kiasi gani kwako, kwa Mungu ni dogo tu, wewe mwamini Mungu na umtarajie yeye naye atafanya.

Zaburi 37:5 “Umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini naye atafanya.”

4. Inuka na utende uyaogopayo kwa imani bila kuogopa.

Jitie ujasiri juu ya hicho kitu ukiogopacho, na uinuke na kukifanya kwa ujasiri huku ukimuomba Mungu akusaidie.

Kuna wengine wamekuwa wakisema kuwa hawawezi hata kama bado hawajajaribu kufanya. Mara nyingi kitu ambacho unaona uwezi kwanza ni vigumu sana kukifanya ukafanikiwa ni kwa sababu: Kumbukumbu la torati 7:17 “Nawe kama ukisema moyoni mwako,mataifa haya ni mengi kunipita mimi;nitawatoaje katika miliki yao?”


Ukiona kushindwa usidhani kama Mungu atasimama. Mungu utenda kazi katika mazingira na viwango ulivyomwekea na ukimwekea mazingira madogo madogo ufanya kwa mazingira hayo hayo na ukiweka makubwa aweza fanya kwa viwango hivyo.

2 Wafalme 4:3-6 “Akasema nenda ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. 4 Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, nay eye akamimina. 6 Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma”

Katika chombo cha mama mjane mafuta yalijaa kwa kadiri alivyoandaa vyombo angeandaa vidogo angepata vidogo na angeandaa vingi zaidi bila shaka angepata vingi zaidi. Ni vyema kwa mtu wa Mungu kumjengea Mungu mazingira ya kutenda mambo makubwa hata kama u mtu mdogo sana. Ikiwa ni biashara, kazi, masomo, inuka na utende kwa ujasiri maana Mungu anatenda kazi na majasiri na wasioogopa. Fanya tu ukishindwa mara ya kwanza usikate tamaa rudia kufanya tena na tena hata ukafanikiwa huku ukikumbuka kuwa mkono wenye juhudi utawandishwa.  

5. Amini kuwa unaweza.
Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”
Ikiwa watu wenye mafanikio makubwa duniani na walio na hali ya chini sana hapa duniani wote wana masaa 24 kwa siku, swali ni je, Nini kinaleta tofauti kati yao?

Hii pia ni sababu kubwa ya wao kufanikiwa kwa kuamini kuwa wanaweza wakafanya na hatimaye wakafanikiwa kuthubutu na kutenda.

Ukijenga imani ya kuamini kuwa unaweza kufanya una nafasi kubwa sana ya kufanikiwa katika lile ulitendalo.

Dr Myles Munroe anasema “watu waliofanikiwa katika ulimwengu huu ni watu waliotoa kabisa neno haiwezekani katika kamusi zao na kuliacha neno inawezekana.”

Hii ni kuonyesha kuwa katika kuamini kuwa inawezekana hapo ndipo mafanikio ya mtu yamewekezwa. Lipo neno jema sana Bwana Yesu alisisitiza na kusema kuwa “mambo yote yanawezekana kwake yeye aaminiye”


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.