SOMO: HUWEZI KUINGIA KANANI PASIPO FARAO - MCHUNGAJI MADUMLA

                                                                                                                                 ©Mosaicmagazine
Mchungaji Gasper Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…

Ilikuwa ni vigumu kwa wana wa Israeli kuiendea njia ambayo Bwana amewaagiza pasipo Farao.Ni ukweli usiopingika kwamba Mungu aliwakusudia mema sababu alisikia kuugua kwao,kilio chao kilimfikilia Bwana Mungu. Na ndivyo tusomavyo;

” Mungu akasikia kuugua kwao, Mungu akakumbuka agano lake alilolifanya na Ibrahimu na Isaka na Yakobo. Mungu akawaona wana wa Israeli, na Mungu akawaangalia.” Kutoka 2:24-25

Kwa kuwa Mungu aliwapenda sana wana wa Israeli akamwinua Musa ili aende mbele yao,awatoe na kuwaongoza kuelekea Kanani yao ( Kutoka 3:9-10 ). Mateso waliyoyapata waisraeli huko utumwani hayakuwa mateso madogo madogo,bali yalikuwa ni makubwa tofauti kabisa na vile unavyofikilia.

▪ Ingawa Bwana Mungu aliwefanyia njia watoto wake watoke utumwani Misri,lakini bado Farao alihitajika.

Shida kubwa iliyokuwako kwa wana wa Israeli ni kuzoelea utumwa,kwamba hali ya utumwa ilikuwa imeganda akilini mwao mithili ya gundi igandavyo katika karatasi,maana haikuwa rahisi kuwachia utumwa kisha wao waendoke zao,bali waliona kana kwamba haiwezekani kuishi bila utumwa.

Na ndivyo ilivyo sasa,maana wapo watu wenye kuona kwamba hawezi kuishi bila kuwa watumwa wa dhambi. Kumbe inawezekana kuishi kwa kumtegemea Yeye Mungu katika jina la Yesu Kristo.

Kwa habari ya wanaisraeli huko utumwani Misri,si kana kwamba hawakuelekezwa njia iwapasayo kuiendea wawe huru,bali walipokea maelekezo yote kutoka kwa Musa na kama vile wakisema kwa midomo yao kwamba tutafuata njia hiyo tuwe huru lakini kumbe rohoni wamesema haiwezekani jambo hili la sisi kuwa huru eti kuondoka pasipo kutumikishwa,tukifia huko je ?

Tunasoma hapa; ” Neno hili silo tulilokuambia huko Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa jangwani. ” Kutoka 14:12

Waisraeli,hapo walikwisha sahau kwamba Mungu aweza kuwaokoa kutoka katika mikono ya wamisri,macho yao yalikuwa yameelekea katika woga wa kufa na wala sio kuelekea katika ukombozi waachane na utumwa. Hakika farao alihitajika sana kuwasukuma kuvuka.

Mimi huwa nikisoma hapo napata picha hii kwamba kama Musa angeliwaambia wale wenye kutaka kuvuka bahari ya shamu kwa hiyari yao wenyewe basi wakae upande wa kulia,na wale wasiotaka kuvuka bahari ya shamu kwamba wanataka kubakia Misri ili wawatumikie wamisri maisha yao yote na vizazi vyao vyote wakae upande wa kushoto.

Naona kama vile wote wangeenda upande wa kushoto. Lakini alipokuwa anakuja farao na jeshi lake kwamba yeyote asiyevuka na kubakia alipo ni lazima auwawe papo hapo,hapo ndiposa waisraeli walipoona bora wangie majini,wavuke bahari maana wasipovuka watauwawa na farao. Chezea farao weye!! Utavuka mwenyewe upende usipende!!!

▪ Upo wakati ambao tunamuhitaji farao atusukume ili tuvuke ngapo ya pili ya mafanikio,maana pasipo yeye akili zetu zinagoma kusonga mbele.

~Farao wa leo anaweza kuwa ni ugonjwa,adha,dhiki,udhia,chuki,au mlima wowote ule katika maisha yako,au Adui. Sasa,haiwezekani ukasonga mbele uingie kanani yako pasipo kuinukiwa na kimoja wapo au vyote.

Mfano mdogo tu nikupe,fikiria kwamba unaokoka na kuishi pasipo na ukinzani wa shetani, yaani hakuna shetani wala nguvu yoyote ile ya giza,isipokuwa dhambi tu ndio ipo,yaani pako shwariii~ hakuna shetani,vinyamkera vyake,mapepo,falme ya giza duniani.

We unafikiri utafanya mazoezi ya kiroho ? ( Kwamba utafunga?au utajibidiisha kuomba? Au utasoma neno na kukaa uweponi? Au utamtafuta Mungu ? ) hali ukijua ya kwamba hakuna ukinzani wowote ule. Hakika utabweteka na hutaweza kuingia katika ufalme wa mbinguni kwa maana hayupo wa kwenda kinyume naye.

Biblia imeeleza wazi wazi ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. (Matendo 14:22)

Hivi unajua kwamba hata Penina alihitajika kwa Hana. ( 1 Samweli 1:1-2 ). Kama asingelikuwa Penina basi yawezekana kabisa Hana asingeliomba kwa mzigo namna ile ili apate mtoto. Biblia inasema;

” Hana akajibu, akasema, Hasha! Bwana wangu, mimi ni mwanamke mwenye roho ya huzuni, mimi sikunywa divai wala kileo, ila nimeimimina roho yangu mbele za Bwana.

Usimdhanie mjakazi wako kuwa ni mwanamke asiyefaa kitu; kwa kuwa katika wingi wa kuugua kwangu na kusikitika kwangu ndivyo nilivyonena hata sasa. “ 1 Samweli 1:15-16

Baada ya Hana kusimangwa kwa farao wake mke mwenza,Penina~ akaamua kukaza kwa Bwana katika kuomba na hatimaye akapokea muujiza wa kumzaa Samueli nabii wa Bwana.

Na hivi ndivyo ilivyo hata sasa katika maisha yetu. Hatuwezi kuingia nchi ya ahadi pasipo farao. Wapo watu waliookoka baada ya kufukuzwa na farao. Yamkini ugonjwa ulikuwa ni farao ukamfanya mtu amkimbilie Yesu sababu kama asingemkimbilia Bwana asingeokoka,na hakika angekufilia mbali huko.

Au wachawi mtaani kwake wamefanyika kama farao,kisha wachawi wanapomfuatia mtu basi mtu huyo salama yake ni kuokoka tu kwa kumpokea Yesu awe Bwana na mwokozi wake.

Kumbuka hili; sio wote waliokoka leo walifukuzwa na farao la hasha! Bali wapo waliokoka kwa sababu ya upendo wa Mungu kwao maana sote tunaokoka kwa neema kwa njia ya imani ( Waefeso 2:8 ). Lakini baada ya kuokoka hapo farao ni lazima ukujie ili uweze kuimarika katika wokovu wako na kuingia katika hatma ya maisha yako ukiwa pamoja na Yesu Kristo Yeye aliyeushinda ulimwengu. ( Yoh.16:33 )

Sijajua farao wako ni nini? Yamkini umejitahidi kushindana naye lakini bado hujamshinda ipasavyo kuyafikia yale mafanikio yako. Na inawezekana nguvu unayoitumia sasa kupingana naye ni ndogo kwamba unahitaji kushilikiana na mtu mwingine ili kwa pamoja farao aanguke.

Basi mimi nipo hapo kwa ajili yako mpendwa katika Kristo Yesu. Waweza kunipigia kwa namba yangu ya simu hii; 0655111149.

Mchungaji Gasper Madumla.

S.L.P 55051,Dar es salaam.

Beroya bible fellowship church ( Kimara,Dar~Tanzania )

UBARIKIWE.
Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.