SOMO: INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA - MCHUNGAJI MADUMLANa Mchungaji Gasper Madumla 

Bwana Yesu asifiwe…

Imeandikwa;

” Ingieni kwa kupitia mlango ulio mwembamba; maana mlango ni mpana, na njia ni pana iendayo upotevuni, nao ni wengi waingiao kwa mlango huo. Bali mlango ni mwembamba, na njia imesonga iendayo uzimani, nao waionao ni wachache. ” Mathayo 7:13-14

Mtazamo wa kawaida kabisa kuhusu mlango mwembamba ni mlango unaopitisha mtu mwembamba,ni vigumu sana mtu mnene wa miraba mnne kupita katika mlango mwembamba. Kwa lugha nyepesi ni kwamba mlango mwembamba hupitisha yule asiyekuwa na mizigo.

Mfano ; Fikiria mbele yako kuna mlango mwembamba,na wewe una mizigo mikubwa na papo hapo unataraji kuingia kupitia mlango huo. Unafikiri utaweza kuingia wewe pamoja na mizigo?

Ndiposa ninaposoma andiko hilo hapo juu, ( Mathayo 7:13-14 ) ninagundua kumbe hatuwezi kuingia katika mlango mwembamba tukiwa tumeshikilia mizigo yetu,bali kila atakaye kuingia katika mlango mwembamba ni sharti aubwage na kuuachilis mizigo ili aweze kuingia katika mlango mwembamba.

Roho mtakatifu amenichukua mpaka katika moja ya merikebu iliyoshehena mizigo huko baharini. Merikebu hiyo ni kubwa,na imejaa shehena za kutosha kisha gafra bahari ikachafuka kiasi cha kuizamisha meli. Ndiposa naodha ikabidi awaagize watu wote wajaribu kupunguza shehena zao za mizigo ili wasije wakangamia na tufani. Kadri wanavyoitupa baharini ndipo unafuu unapatikana,na mwishowe wakafanikiwa kuitupa mizigo mingi baharini.

Merikebu ikapata unafuu,lakini kumbe bado ikawa inaelemewa ndipo naodha akajiuliza kwamba yamkini iko mizigo iliyobakia,akajuliza na wataalumu wenzake pasipo kupata jibu.

Baadaye wakagundua kwamba kulikuwa na vijimzigo vidogo vidogo walivyoficha watu wakidhani kwamba ni vidogo sana kiasi kwamba havitaweza kuzamisha Merikebu. Kumbe vile vimzigo vidogo dogo ndivyo navyo vilikuwa vikichangia kwa kiasi kikubwa kwa kuzama ile merikebu.

Sasa,tunajifunza nini kwa mfano huo ?

Salama ya maisha yao wale wa merikebu ilikuwa ni kuitupa mizigo,kwamba walikuwa hawawezi kuokoka pamoja na mizigo yao maana njia yao ilikuwa imesonga kwa mchafuko wa bahari. Katika tafsiri nyepesi,mizigo ya ni dhambi. Hakuna aingie katika mlango mwembamba akiwa amebeba dhambi.

Watu wa merikebu,kama wakezidi kuidharau ile mizigo midogo midogo kwamba wasiitupe baharini basi ni dhahili kabisa wangelizama baharini. Salama yao ni kuitupa mizigo yote,na ndivyo wengi leo walivyo wenye kushikilia dhambi wakidhani ya kwamba ni dhambi ndogo ndogo kwamba hazina shida,kumbe hizo hizo wazionazo ndogo ndogo ndizo zitakazowazamisha na kuwafanya wasiuone mlango mwembamba. Ifahamike kwamba hakuna dhambi kubwa wala dhambi ndogo bali dhambi ni dhambi.

Tuangalie biblia tena inasemaje kwa habari ya mfano wa Merikebu,imeandikwa; ”

” Na kwa maana tulikuwa tukipigwa sana na ile tufani, siku ya pili yake wakaanza kuitupa shehena baharini.

Siku ya tatu wakatupa vyombo vya merikebu kwa mikono yao wenyewe. Jua wala nyota hazikuonekana kwa muda wa siku nyingi, na tufani kuu ikatushika, basi tukakata tamaa ya kuokoka. ” Matendo 27:18-20

Hii ni habari ya akina Paulo walipokuwa katika merikebu iliyokuwa imekumbwa na dhoruba baharini. Ilibidi nao washushe shehena za mizigo baharini ili waokoke na maisha yao. Laiti kama wangelikataa kushusha shehena zao za mizigo basi wasingelipona kabisa. Paulo aliliona hilo. Mlango wao wa kuokoka ni kuingia mlangoni pembamba kwa kutupa mizigo waliyoibeba.

Biblia inasema kuwa mlango mwembamba,na njia imesonga iendayo uzimani,nao waionao ni wachache. Njia iliyosonga ni njia ambayo imefichika,ambao wachache sana wataweza kuiona njia hiyo. Na biblia imeweka wazi kabisa ya kuwa njia hiyo ni wokovu tu. Ambapo si wengi wataingia katika njia hiyo maana katika wokovu si wengi wenye kuuona,wengi hukataa kuokoka tena katika njia hii hauitajiki kubeba mizigo yaana dhambi na kuwa mnafiki. Maana hakika hutaweza kuiona njia.

Leo tunafundishwa kuwa,tukihitaji kuingia katika mlango mwembamba,njia iingiayo uzimani basi hatuna budi kuyaacha yote kwa ajili ya Kristo Yesu,maanaYeye ndio njia, kweli na uzima.

▪ Yesu ndiye njia,na kweli na uzima hakuna aendaye kwa Baba pasipo njia hiyo ( Yoh.14:6)

Njia ya Yesu haibadiliki badiliki,bali njia ni ile ile ya kumpokea Yeye awe Bwana na mwokozi wa maisha yako. Watu wengi wanafikiri kwamba waweza ingia katika mlango hali wamebeba shehena za mizigo ya dhambi. Tena hujifariji kwamba watatubia baadaye au kesho,kumbe hawajui kuhusu hiyo baadaye wala kesho. Maana wakati wa wokovu ndio sasa ( 2 Wakorintho 6:2 )

Mpendwa kataa vyote,lakini usikatae wokovu,okoka leo maana Yesu yupo kwa ajili yako.Hii ndio njia iendayo uzimani,mtu akiwa nayo amepata jambo jema. Hakika tunastahili kuingia katika njia nyembamba iendayo uzimani.

▪ Kwa huduma ya maombi,nipigie 0655111149.

Mchungaji Gasper Madumla.

Beroya bible fellowship church ( Kimara,Dar-Tanzania )

UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.