SOMO: NAMNA YA KUMLEA MTOTO KATIKA NJIA IMPASAYO (2)

Kelvin Kitaso,
GK Contributor.


Somo hili linatoa majibu ya namna gani mtoto anapaswa kukuzwa katika BWANA, na ni kwa namna gani mzazi anaweza mtengeneza mtoto kuwa katika misingi iliyo myema na ya kupendeza kwa kufuata misingi ya biblia. Kama hukusoma sehemu ya kwanza ya somo hili BONYEZA HAPA kabla ya kuendelea na sehemu ya pili.
NAFASI YA MZAZI
Wazazi wengi wamekuwa na imani kuwa kazi yao kubwa ni kuzaa, kwa kutimiza lile kusudi la Mungu la kuzaa na kuongezeka na kusahau kuwa baada ya kuzaa na kuongezeka kuna kazi ya ziada ambayo inapaswa kufanywa na wazazi kama watu waliopewa dhamana ya kumiliki uzao wao.  Mzazi yeyote ili kuwa mzazi bora ni lazima aige ni kwa namna gani Mungu analea watoto wake kwa kuwa Mungu ni Baba, ni vyema kwa kila mzazi kuangalia ni kwa namna gani Mungu kama Baba anafanya mpaka watoto wake huwa na tabia njema ambayo haifanani kabisa na ya watoto wengine.
Kitabu cha Isaya 48:17 “……..Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.” Kitabu hiki cha Isaya Mungu anajitambulisha kwa watoto wake ni nafasi gani aliyo nayo kama mwalimu na kama kiongozi mbele za watoto wake. Nafasi hizi ndizo alizo nazo mzazi mbele ya wanae.
Zipo nafasi ambazo anazo mzazi katika malezi ya mtoto nazo ni kama:
  1. KIONGOZI
Mzazi ni kiongozi katika familia na chini yake anao wafuasi wake ambao uitwa watoto na viongozi hawa uwa ni katika ngazi kuu mbili, yaani kiongozi mkuu (mwenyekiti) ambaye mara zote huwa ni baba na msaidizi wake ambaye ni mama (katibu). Viongozi hawa ndio wakuu ambao huanzisha taasisi yao na katika taasisi yao hupatikana watoto, hakuna taasisi isiyo na maono, hivyo viongozi hawa uhusika kutoa mwelekeo kwa wafuasi wao ni kwa namna gani taasisi yao inapaswa kuwa na washirika wa hiyo taasisi wanapaswa kuweje. Kuna nyakati kiongozi huwa na demokrasia lakini kuna wakati ulazimika kufanya maamuzi ya kidikteta kulingana na aina ya wakati uliopo. Ndivyo ilivyo kwa wazazi kwa kuwa kuna wakati watakuwa na hali ya demokrasia na kuna wakati watakuwa na hali ya udikteta ili kuhakikisha mambo yanaenda vyema katika familia. Mzazi akifaulu kuelewa kiongozi hupaswa kuwaje ni lazima atakuwa mtu wa tofauti kuwasaidia watoto wake kufanya vizuri.
Kiongozi ni mtu anayejua njia, anatembea katika njia na kuonyesha njia kwa wafuasi wake. Na ndiyo nafasi kuu waliyonayo wazazi katika familia kama kiongozi.

Kujua njia
Kujua njia ni sehemu ndogo tu, ila ni ya msingi sana kwa mzazi yeyote yule kuijua njia ipasayo kupitiwa, na ni muhimu kufahamu kuwa kama kiongozi hajui njia ni rahisi sana kuwapoteza watu wake na kuwafanya wakapotea njia. Yesu Kristo ni njia na kweli na uzima, Yesu ambaye ni njia uitwa neno. Njia ni neno la Mungu. Maandiko yanasema kuwa ‘kipofu hawezi kumuongoza kipofu mwenzake kwa kuwa watatumbukia wote shimoni,’ watoto uwa kama vipofu na uhitaji kupata mtu wa kuwashika ili wasiweze kutumbukia shimoni. Mzazi aliye kipofu ni lazima ataishia kuwatumbukiza watoto wake katika shimo.
Yohana 3:16 inazungumzia juu ya Mungu ambaye ni kiongozi bora na kiongozi makini  na katika uongozi wake anaona ni muhimu kupata kiongozi wa kuongoza familia yake na anamtoa mwanae pekee ili kila anaemwamini na kuwa chini ya uongozi wake hasipotee. Kupotea kwa watoto ni matokeo pia ya kukosa viongozi bora na viongozi wanaoijua njia.
Laweza kuwa fumbo kubwa kulifumbua juu ya kuijua njia ila kuijua njia katika sehemu hii umaanisha kufahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu kwako kwanza kama mzazi na kisha kufahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Mungu kwa watoto wako na pia kuangalia kuyafanya hayo yaliyo mapenzi ya Mungu; na pia kuijua njia ni kufahamu njia ambayo itamsaidia mtoto kukua katika makuzi yaliyo mema na kufahamu nini kama mzazi ufanye ili kuimalisha makuzi mema katika familia yako.
Ni vyema kufahamu kuwa kiongozi/mzazi hana njia moja tu katika kumkuza mtoto bali huweza kutumia njia mbalimbali kuhakikisha mtoto anakuwa katika makuzi yaliyo mema na salama mbele za Mungu. Anaweza tumia njia ya kidemokrasia pale inapobidi na kutumia njia ya kidikteta pale inapobidi, ila kutumia njia moja tu kwa kila jambo ni makosa na ni kukosa kuijua njia kama kiongozi.
Hautoweza kuongoza familia yako kama haujui njia kwa kuwa hasiyeijua njia ni kama kipofu na kipofu hawezi kuongoza kipofu mwenzake. Ila ni vyema kujua kuwa njia njema ni neno la Mungu, kwa kulisoma na kulitafakari kama mzazi na kuliweka ndani linakupa ufahamu wa kuijua njia ili uweze kuwasaidia na wengine kuijua njia.
Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, ni mwangaza wa njia zangu.” Ni kwa kulifahamu neno na kuliweka ndani ya moyo ndipo kiongozi anaweza kuwaongoza na washirika wake wakaijua njia sahihi.
Nafasi ya mzazi katika kuijua njia ni nafasi ya kutafuta yeye mwenyewe kujifunza ili aweze kuwafundisha na watoto wake. 
Kimtokacho mtu ni kile kilichoujaza moyo wake, ni busara kwa mzazi kujaa neno la Mungu ili kuwasaidia watoto wake na pia hauwezi kutoa kitu ambacho wewe mwenyewe hauna ndani yako, ila waweza kutoa ulichonacho tu, wayapokeayo na kujifunza kwako ni yale uliyonayo.

Kutembea katika njia
Haiishii katika kuijua njia ila inakwenda mbali zaidi katika kutembea katika hiyo njia, yaani kuyafanya yale uyajuayo. Katika kutafuta kuyajua yapi ni sahihi na yapi si sahihi ni vyema kwa kiongozi kuyatenda yale hayajuayo kuwa ni sahihi. 

Maxwell anasema kuwa, “wafuasi umwamini kiongozi na kumfuata kuliko vile wanavyojiamini wao wenyewe,” 

jambo hili ni vyema sana kwa mzazi kama kiongozi kulifahamu kuwa mara nyingi watoto uwaamini wazazi wao na kupenda kuwaiga hata kama hawako sahihi kwa kuamini kuwa kama yanafanywa na wazazi wao haina shida kwa wao kuyafanya, hata ukiwauliza watajibu mbona hata Baba/Mama anafanya. 
Nimeshawahi kuhojiana na watu wengi sana na wengine wakiwa wakubwa kabisa na ukiwaambia kwa nini unafanya kitu Fulani wao utoa jibu kwa kusema, “hata wazazi wangu walifanya hivi hivi.” Kazi ya mzazi ni kuishi katika njia iliyo sahihi ili watoto wake wapate kuona na kujifunza kwa kuiga kutoka kwao. 
Wengine wanasema “fuata maneno yangu, usifuatishe matendo yangu,” msemo huu utumiwa na jamii ya watu walioshindwa kufanya yale yaliyo mema na yawatokayo vinywani mwao. Baba mmoja wa kiroho aliyewaongoza watu wengi aitwaye Paulo kwa ujasiri alisema, “nifuateni mimi kama mimi navyomfuata Kristo” kwa maana nyingine yeye kama mzazi alijua na kufahamu kuwa ni jukumu lake kutembea katika njia na akahimiza watoto wake watembee katika njia kama yeye anavyotembea. Na pia mtume Paulo anasema juu ya watu waongozoa kuwa waigwe mwenendo wao ulivyo mwema katika Kristo, na waongozwao waangalie sana mwisho wawaongozao kwa vile wanavyoenenda. Ni vyema sana kwa wazazi kufahamu njia na kutembea katika njia na kuwa makini katika yale wasemayo yaendane na yale wayatendayo.
Wazazi wengi wamekuwa na kasumba ya kuwakemea watoto wao wanapokosea na kuwapa vitisho vikali kwa yale mabaya wanayokuwa wameyafanya, na wengine husema. “ukirudia tena nitakuchapa,” ila watoto wanaporudia maneno hayo ya mzazi hayatekelezwi na mara nyingi wazazi uishia kupiga kelele na kutoa vitisho tena na tena, hali hii ya kushindwa kutembea katika maneno ayasemayo mzazi uwasababisha watoto kuwazoea wazazi na kutoona uzito katika mambo wayasemayo ila jambo la msingi ni kwa mzazi kutimiza kile alichokisema kwa kuwa itamsababisha aaminike katika yale ayasemayo na kumtia hofu mtoto kila anapofanya kosa. Na si katika upande huu tu wa adhabu bali hata upande wa ahadi njema umfanya aamini kuwa wewe ni mtu makini na mtekelezaji wa yale uliyomuahidi.
Wazazi wangu walitulea kwa namna ya kutufanya kuogopa sana kukosea na kuwa makini sana katika mambo tuyafanyayo kwa sababu ya ule ukali waliokuwa nao pale tulipokuwa tunafanya makosa, wakati Fulani mimi na kaka yangu tulifanya kosa na Mama akatuambia kwa kuwa mmefanya hilo kosa leo hamtolala ndani, na alikuwa akimaanisha sana katika adhabu aliyoadhimia na katika kuadhimia huko alifunga mlango na sisi tulikuwa tumekaa muda mrefu nje, tukisubiri labda aweza fungua ila hakufungua mpaka tukaamua kutembea usiku kwenda kulala kwa dada  (binamu) yetu, kwa kupokea adhabu ya namna hiyo ilitufanya tumuone mama kuwa ni mtu anayemaanisha sana na ilitupa kuwa makini sana na kukosea tena. Na alipokuwa akitisha tena tulikuwa makini maana tulijua atafanya.
Mfano wa Mungu kama kioo cha wazazi akiahidi ni lazima atatenda, na akisema ni lazima atafanya na hii ni sababu inayozidi kumfanya Baba yetu kuonekana ni Mungu amaanishaye.
Mtoto akikosea usiache kumpa adhabu ili aogope kurudia tena, hii ndiyo staiki ya mtoto na ndiyo njia bora ya kumkuza mtoto.
Kuonyesha njia
Kazi nyingine kubwa na ya msingi sana kwa mzazi ni kuonyesha njia kama kiongozi kwa kuwa kiongozi bora ni lazima aonyeshe njia kwa wale anaowaongoza, haishii kuijua njia ila uzidi kwa kuionyesha njia kwa wale anaowaongoza. Kuonyesha njia ni kwema na ni tendo ambalo si la siku moja au mwaka mmoja bali uwa ni tendo endelevu kwa nyakati zote ambazo mzazi huwa pamoja na mtoto wake. 
a..
Kielelezo no: 1 Mfano wa picha ya mzazi akiwa kiongozi kwa mwanae na mtoto kuvaa kama vile alivyovaa mzazi wake. Baba anaijua njia, anatembea kwenye njia na anaonyesha njia. (Like a father, like a son)
Isaya 48:17 “……..Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.” Mungu kama mzazi mkuu anaonyesha mambo yenye uwiano kwa kufundisha njia ili upate faida na kuionyesha njia ipasayo, hii ni kusema kuwa yeye uhifahamu njia ndiyo maana uionyesha lakini pia anatembea katika njia.
Namna mzazi anavyoweza kuonyesha njia kwa mtoto akiwa kama kiongozi.
  • Kwa matendo yako.
Kama mzazi ni muhimu sana kuwa makini sana na matendo unayoyafanya kwa kuwa katika yale unayoyafanya unaweza mjenga au kumbomoa mwanao/wanao. Maandiko yanasema kuwa, “alivyo mchungaji ndivyo walivyo watu wake.” Watoto wao huwa na tabia ya kuiga sana na hupenda na wakati mwingine hujisikia fahari sana kufanya yale ambayo hufanywa na wazazi wao, wengine wakiwa katika michezo na marafiki zao huweza kurudia yote waliyoyaiga kwa wazazi wao, kuwa makini kuijenga tabia ya watoto wako kwa kufanya yaliyo mazuri machoni pao ili waweze kuiga yale yaliyo mazuri kutoka kwako kama kiongozi wao. 
Katika matendo kuwa makini sana na aina ya mavazi unayoyavaa kwa kuwa watoto pia hupenda kuiga wazazi wao au watu wakubwa wanavaaje na ni mara chache sana wakaweza kujisimamia katika maamuzi ya wavaaje, haswa kwa wale walio juu kuanzia miaka 12 na kuendelea. Kama mzazi unapenda kuvaa vimini/vinguo vifupi vifupi na vyenye kubana, na vionyeshavyo baadhi ya maungo nje; ni rahisi sana kwa mtoto wako kuiga hiyo tabia na kuanza kuvaa hovyo hovyo na kushindwa kujizuia katika mavazi ayavaayo. Kiongozi anayevaa vibaya ni rahisi kwa wafuasi wake kuvaa vibaya ila kwa kuvaa vizuri usababisha hata wafuasi wake kuvaa vyema. 
Hauwezi kubadilisha mtu kama wewe mwenyewe haujabadilika, kama mzazi ni mvaaji vibaya ni vyema akabadilika kwa kuwa yeye ni muonyesha njia kwa kuvaa vibaya uonyesha njia ni kwa namna gani watoto wake wanapaswa kuvaa. Si mavazi tu bali katika maeneo mengi sana ya maisha mzazi ana nafasi kubwa ya kumsaidia au kumharibu mtoto kwa matendo yake, kwa mfano vipindi vya redio, au television uviangaliavyo kama muonyesha njia ndivyo unaweza mjenga au mharibu mtoto wako. 
Kama muonyesha njia jitahidi watoto wako wajue misimamo yako kama kiongozi wao na uwawekee mazingira ya kuifuata misimamo yako kwa kuwa wewe ndiye mtoa dira ya ni kwa namna gani wanapaswa kuwa.
David Oyedepo anasema, “wazazi wanapaswa kuwaongoza watoto wao kwa wao wenyewe kuwa mfano kwa matendo yao kwa kuwa watoto uiga sana kile kinachofanywa na wazazi wao.”
  • Kwa maneno.
Ulimi ni kiungo kidogo sana ambacho kinauwezo mkubwa wakuharibu na pia kinauwezo wa kujenga, kwa ulimi wako kama mzazi waweza mjenga au kumharibu mtoto wako. Chiriku ni aina ya ndege mwenye uwezo wa kuiga sauti ya mwanadamu kwa jinsi anavyoongea japo hushindwa kutaja maneno katika kuiga huko. Ndivyo alivyo mtoto kwa kuwa ni mtu ambaye hupenda kuiga sana maneno yanayosemwa na wazazi wake, wakubwa na hata wadogo wenzake na ayasikiayo kwenye vyombo vya habari. Ni muhimu kwa mzazi kuwa makini kwa maneno anayosema mbele za mtoto, na pia kumjengea mazingira ya kutosikia maneno machafu yanayoweza kuharibu tabia njema.
Kwa nyakati za sasa imekuwa ni kawaida kuona mtoto anatoa maneno mazito na mengine huwa machafu, na ni kawaida sana kuona mtoto anashinda kijiweni na wakubwa na kutaniana nao na kuwatukana matusi makubwa na wao kumtukana matusi makubwa pia, sababu kubwa ni kuwa, watoto hupenda kuiga na katika kuiga kwao uathiriwa na aina ya yale maneno wanayoyaiga.
1 Wakorinto 15:33 “Msidanganyike; Mazungumzo mabaya uharibu tabia njema”. Mazungumzo mabaya yanaweza yakawa katika familia au nje ya familia ila huwa na mchango mkubwa sana wa kuharibu tabia njema. Kama kiongozi wa mtoto ni lazima uangalie kumsaidia mtoto kutosikia sikia maneno mabaya ambayo yanaweza haribu tabia yake na hata akawa mtu mbaya.
Wapo wazazi ambao hupenda kuwatamkia watoto wao maneno mabaya na ya kuwakatisha tamaa, kwa mfano, wengine uwaita watoto wao ‘mbwa,’ ‘kenge,’ ‘nyau’, ‘chizi’, ‘mwehu’ na majina mengi mabaya kwa sababu ya kuudhika na makosa ya watoto wao, na wengine uwatamkia ‘sura mbaya’ au kuwakosoa katika baadhi ya maumbile yao kuwa ni wabaya. Wakati wanayasema hayo wao uona ni kawaida sana ila kwa mtoto mambo yale uenda ndani ya mioyo yao na wakati mwingine ujirudia rudia ndani yake na kujiona kuwa hawana hata thamani kabisa kwa kule kufananishwa kwao na vitu visivyo na thamani. Kuna wengine wameamua kuuza utu wao kulingana na kule kutamkiwa kuwa ni wabaya na wenye maumbile mabaya na hawakuona thamani yao ndio maana ikawa ni rahisi kwao kuuza utu wao na miili yao kwa kuwa kwao  kitu cha kawaida na hakina thamani. Kwa maneno ya namna hii wapo ambao ukumbuka hata katika ukubwa wao na kusumbuliwa sana na maneno hayo hata ije neema ya Kristo iwatoe.
Katika jambo kama hili ni muhimu sana kwa wazazi kuwa makini sana na vile wanawatamkia watoto wao kwa kuwatamkia maneno mazuri, mazito na ya kuwatia moyo, ambayo yanawasababisha kujiamini na kuwa watu watofauti hata mbele za wenzao. Watamkie Baraka na mafanikio na maneno mazuri kwa kuwa yatasababisha kujiona wao ni watu wakubwa na watofauti katika ulimwengu huu, wafanye waijue thamani yao na thamani ya miili yao itawafanya waifunike vyema na kuiheshimu ili wengine waiheshimu na kuiogopa. Maneno unayoyatamka yanawatengenezea kesho yao au katika utu uzima wao watakuja kuwa watu wa namna gani, watamkie wao wakisikia na zaidi watamke mbele za Mungu.  
Ni wewe ndiye unayeweza kuwafanya wajijue wao ni wakina nani na wanathamani gani katika ulimwengu huu na miili yao ina thamani gani, kwa kufanya hivi utatengeneza watoto wenye kujiheshimu sana na kujiheshimu kwa watoto ni utukufu na heshima kwa wazazi na Mungu, ila kutojiheshimu kwao ni aibu kubwa kwa wazazi na hata kumuaibisha Mungu aliyewaumba. Kwa mfano mtoto anayevaa vibaya na kuacha maungo yake yapaswayo kufunikwa wazi ni sawa na kuwaweka wazi wazazi wake kwa kuwa hata watu wanaponyooshea kidole utaja kuwa Yule ni mtoto wa Fulani, uzinzi na kila aina ya uchafu aibu yake uenda kwa wazazi wake, mlee mtoto vyema aje kukuletea heshima. 
Nimeshawahi kuona wazazi wanaofurahia watoto wao wanapozini, wanapopigana na watu nakuwashinda(ugomvi), na mambo mengine kwa kuamini kuwa kwa kufanya hivyo ni ujanja na kwenda na wakati na wengine wakiona wanavaa vibaya huona kuwa wanaenda na wakati ila si kweli kwa kuwa kwa kufanya hivyo mtoto uingia katika aina ya tabia ambayo si njema, na huweza kumfanya mtu kuharibikiwa na kupoteza muelekeo wa maisha yake.
  • Katika uchaguzi wa marafiki
Mtoto katika utoto wake bado hutegemea sana uongozi wa wazazi wake katika uchaguzi wa marafiki kwa kuwaelekeza kuchagua ni marafiki wa aina gani wanapaswa kushirikiana nao na kuwa pamoja nao. Kuna umuhimu wa uhusika wa moja kwa moja wa wazazi kwa kuwa katika hali ya utoto mtoto huweza kuambatana na chochote kile ila kwa muongozo wa wazazi anaweza kujua ni yapi ya kuambatana nayo, na ni yapi ya kuachana nayo.
Tabia ya watoto wote ni kupenda kucheza na katika kucheza huko huweza kukutana na wenzake wenye tabia mbalimbali na wakachangia kwa kiasi kikubwa kuharibu tabia njema aliyotoka nayo nyumbani. Kama mzazi kuwa makini sana kuona mtoto wako anashirikiana na marafiki wa aina gani akiwa nyumbani, shuleni, kanisani na maeneo mengine mengi. 
Usimzuie kucheza kwa kuwa kucheza ni sehemu ya msingi sana kwa mtoto, ila muongoze katika usahihi wa watu wa kucheza naye, mfanye kufahamu anapaswa kucheza na watu wa aina gani.

Somo Litaendelea

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.