HOJA: INJILI YA UFALME WA MUNGU ILIYOPOTEA

Askofu Sylvester Gamanywa
WAPO Mission International.

Kila msomi wa maandiko matakatifu ya agano jipya, kama anataka kuwa mkweli katika nafsi yake, atakubaliana nami kwamba, injili ile iliyohubiriwa na Yesu Kristo mwenyewe na kisha kupokelewa na wanafunzi wake, sio injili ile ile inayohubiriwa katika ulimwengu wa leo. Na kama “injili ya leo sio ile ile “injili ya kwanza” sio ajabu kuona hatuoni ishara zile zile “injili ya kwanza”! Katika hoja ya leo, nachukua fursa hii kuirejea “Injili ya kwanza” ili yamkini wahubiri wa “Injili ya leo” tutubu na kurejea katika “Injili ya kwanza”

Injili ya ufalme wa Mungu
ndiyo injili ya kwanza na asilia

Injili ya ufalme wa Mungu ndiyo Injili ndiyo iliyohubiriwa na Yesu Kristo na akawaamuru wanafunzi wake waihubiri kila mahali baada ya kuondoka kwake. Injili ya ufalme wa Mungu ndiyo ilikuwa na “ujumbe muafaka” uliobeba taarifa muhimu kwa kila binadamu duniani. Kabla sijaingia kwa kina hebu tupate tafsiri fupi za misamiati ya maneno magumu yakiwemo  neno “injili” na pili neno “ufalme wa Mungu”!

1.    Msamiati wa neno “Injili”

Neno Injili tafsiri yake ni “habari njema”! Enzi za karne za Biblia, jamii ilizoea maisha ya vita vya kikabila. Wakati wa vita jamii ilikuwa katika hali ya maficho au wasiwasi wakati jeshi lake liko mstari wa mbele. Lakini jeshi moja liliposhinda maadui zake, mjumbe maalum alipelekwa kupeleka taarifa maalum kwenye miji ile ambayo jeshi lake limeshinda vita. Neno hili, “habari njema” (Injili) ndilo lilipigiwa mbiu kwa wenyeji walioshinda na furaha ikawashukia wakaanza kupiga vilegele na shangwe za amani.

Yesu Kristo alipoanza huduma rasmi, ujumbe wake wa kwanza, ulikuwa ni “Tubuni, ufalme wa Mungu umekaribia.” (Mathayo. 3:2). Kuanzia wakati huo, mahubiri na mafundisho yake yalihusu habari za “ufalme wa Mungu”! Hata baada ya kufa na kufufuka kwake, siku 40 za mwisho kabla ya kupaa, tunasoma alizitumia kuwakumbusha habari za ufalme wa Mungu.

2.    Msamiati wa neno “Ufalme wa Mungu”

Kwanza neno “Ufalme” maana yake ni eneo ambalo mfalme anamiliki na kutawala. Pili, “ufalme” ni mfumo wa utawala ambao mtawala ndiye mmiliki wa vitu vyote. Tunapokuja kwenye msamiati kuhusu “Ufalme wa Mungu” tunapata maana ya “mfumo wa utawala ambao Mungu ndiye mwumbaji na mmiliki wa vitu vyote” na ndiye “mwenye mamlaka ya juu na ya mwisho juu ya wote na vyote”

Enzi za karne ya kwanza, mfumo wa kifalme ndio mfumo uliokuwa unatawala ulimwengu wa nyakati hizo. Hata hivi sasa, bado yako mataifa na makabila ambayo tawala zake zimeendeleza mfumo wa kifalme, japokuwa sio kwa mikazo ile ile ya karne ya kwanza.

Kabla sijaingia kwa kina kuhusu mada kuu ya “injili ya ufalme wa Mungu” hapa duniani, ambayo nadiriki kusema kwamba imepotea kabisa; hebu kwanza niweke tofauti zilizopo kati ya “mfumo wa utawala wa duniani hii” na “mfumo wa utawala wa Mungu” unaotakiwa kuonekana hapa duniani:

Tofauti zilizopo kati ya “utawala wa
duniani hii” na “ufalme wa Mungu”

Zipo tofauti kubwa kati ya mifumo hii hususan kwa utawala wa Tanzania na “mfumo wa kifalme”! Kwa hapa Tanzania tunatumia “mfumo wa demokrasia ya vyama vingi vya siasa”. Huu ni mfumo ambao “utawala wake hupatikana kwa njia ya uchaguzi wa walio wengi; na pia  “utawala wa uwakilishi” wa walio wengi.

Tukirejea kwenye mfumo wa Ufalme wa Mungu kama tulivyokwisha kuchambua kwamba huo ni “mfumo wa utawala ambao Mungu ambaye ndiye muumbaji wa binadamu wote na viumbe vyote,, ndiye mwenye mamlaka ya juu na ya mwisho juu yake.” Kimsingi, asili ya mfumo huu wa “ufalme wa Mungu” sio wa hapa duniani. Hii iliwekwa bayana na Yesu mwenyewe pale alipokuwa akijibu swali la Pilato akasema:

“Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania, nisije nikatiwa mikononi mwa wayahudi. Lakini ufalme wangu sio wa hapa.” (Yh.18:36)

Kwa hapa napenda kutoa angalizo kwa jamii ya baadhi ya Wakristo ambao, kwa kutokujua tofauti zilizipo kati ya mifumo ya tawala hizi; wao wamekuwa wakichanganya itikadi zake na kulazimisha “mfumo wa kidemokrasia unaotawala Tanzania” ubadilike na kutumia itikadi za “mfumo wa kifalme” jambo ambalo haliwezekani. Na sio kwamba haliwezekani tu bali linachangia kupotosha maana sahihi ya “Ufalme wa Mungu” unaotakiwa kuonekana hapa duniani.

Ninatambua uwepo wa tafsiri mbali mbali zinazoshinikiza na kulazimisha kuwapata viongozi wa kisiasa, wenye sifa za kimungu kwa madai kwamba, tunahitaji kuongozwa kisiasa na wacha Mungu ambao watatawala kwa haki na kuzingatia miiko ya utakatifu. Hii ni shauku nzuri na yenye kusisimua. Lakini lazima tutambue kwamba, “kuwa na watawala wacha Mungu” ni tofauti kabisa na kuwa na “utawala wa Mungu” ndani ya “mfumo wa utawala wa duniani hii”!

Ni kweli mtawala anaweza kuwa mcha Mungu kama mtu binafsi, na akasaidia kutawala kwa hofu ya Mungu, lakini hii haimaanishi kwamba ataweza “kubadilisha mfumo wa utawala wa duniani hii” uanze kutumia misingi ya “ufalme wa Mungu” kama ndio sheria za kuongoza nchi.

Bila shaka unaweza kujiuliza kama “mfumo wa utawala wa Mungu” hauna nafasi ndani ya “mfumo wa utawala wa duniani hii”; Yesu alikuwa na maana gani aliposema tuombe kwamba “Ufalme wako uje…”? Jibu la swali hili la sehemu kuu mbili.

Kwanza, upo wakati maalum wa kinabii uliotabiri kuhusu “mfumo wa ufalme wa Mungu” utakapotawala duniani hii kwa 100%! Hiki kinajulikana kama kipindi cha miaka elfu moja maarufu kwa jina la “utawala wa milenia” ambapo Mtawala mwenyewe atakuwa ni Yesu Kristo mwenyewe. Sasa wakati huo haujafika bado mpaka hapo Yesu Kristo atakaporudi mara ya pili duniani.

Lakini kwa sasa, “mfumo wa utawala wa Mungu” unaotakiwa kudhihirika hapa duniani ni uwepo wa jamii ya wana wa ufalme kama watu binafsi waliovikwa mamlaka ya kifalme na wanaishi kwa kanuni za ufalme wa Mungu katikati ya jamii ya wana wa ulimwengu huu.

Itaendelea juma lijalo

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.