HOJA: JE MUNGU NDIYE MTEUZI WA VIONGOZI WA KISIASA? (Sehemu ya mwisho)

Askofu Sylvester Gamanywa,
Mwangalizi Mkuu, WAPO Mission International.
©Moore Head Foundation
Jumatatu iliyopita tulifanya uchambuzi kuhusu uhuru wa kujichagulia viongozi (soma hapa) ambao ulitolewa na Mungu katika maandiko. Tukajifunza kwamba, Mungu alitoa mwongozo tu wa vigezo vya kuwapata viongozi wanaofaa, lakini wenye kupendekeza ni watu wenyewe. Kisha tuligusia habari za mfumo wa uongozi wa makundi ambao unalenga uwakilishi katika usimamizi wa mambo ya wengine. Leo napenda kuja kwenye msingi wa swali la mada ambalo linataka kujua kama Je! Mungu ndiye mteuzi wa viongozi wa kisiasa? Tuendelee…

Biblia isemavyo kuhusu kupiga kura

Kura kwa tafsiri ya kawaida ni uchaguzi unaofanywa kwa kusudi la kumpata kiongozi atakayeshika wadhifa fulani na lazima tendo hilo hufanyika kwa siri. Hata hivyo, mtindo wa kupiga kura ni utamaduni wa kale na ulitumika hata kwenye utawala wa Israeli katika kufanya maamuzi. Lakini hata Biblia imeandika mifano mingi kuhusu matumizi ya kura katika mambo mengi lakini kwa hapa nitawasilisha mifano michache tu ili kuweka mkazo katika mada.

Jambo la kwanza Biblia inatoa sababu ni kwanini kura hutumika kwenye maamuzi yanayotaka uchaguzi. Mtunga mithali anasema kwamba: “Kura hukomesha mashindano; hukata maneno ya wakuu.” (Mith.18:18) Hapa tunashuhudia kwamba kazi kubwa ya kura ni “kukomesha masindano”!!!! Ni “Kukata maneno ya wakuu.”!! Kwa maelezo mengi kazi ya kura ni “kuondoa ubishi wa nani anastahili zaidi au anahitajika zaidi au afaa zaidi nk.

Mfano wa kwanza wa kura tunakuta kwenye kitabu cha Hesabu pale ilipofikia wana wa Israeli wameingia katika nchi ya Kanaani waliyoahidiwa miaka mingi, na iliyoeagharibu zaidi ya miaka 40 jangwani na kizazi cha kwanza kulichotoka Misri kikaishia jangwani.

Happa tunakuta mwongozo kuhusu mgao wa ardhi hiyo kulingana na idadi ya makabila 12 ya wana wa Israeli. Inaonekana kwamba ungekuwepo ubishi wa kila kabila kutaka kuchua ardhi ya upande fulani kwa sababu ya uzuri wake kuliko maeneo mengine.

Hapa kumaliza ubishi huu, mwongozo ni kupiga kura ili kuona kila kabila linashinda kupewa eneo gani: “Lakini nchi itagawanywa kwa kura; kwa majina ya kabila za baba zao, ndivyo watakavyopata urithi. Kama kura itakavyokuwa, ndivyo urithi wao utakavyogawanywa kati yao, hao wengi na hao wachache.” (Hes.26:55-56)

Mfano wa pili ambao ningependa kuuzumgumuzia ni mtindo uliotumika kumpata kuhani Mkuu wa kufukiza uvumba mahali pa Patakatifu pa Patakatifu. Utaratibu wa kila mwaka ulikuwa ni kuchagulia kuhani mmoja atakayeingia huko kwa mujibu wa taratibu za kutoa dhabihu hekaluni. Tunasoma kwamba wakati ule ulipokaribia ujio wa Yesu Kristo duniani, mtu mmoja kuhani jina lake Zakaria alipata kura nyingi na kuchaguliwa kuingia Patakatifu pa Pataakatifu:

“Basi ikawa alipokuwa akifanya kazi ya ukuhani katika taratibu ya zamu yake mbele za Mungu,, kama ilivyo desturi ya ukuhani, kura ilimwangukia kuingia katika hekalu la Bwana ili kufukiza uvumba.” (Luk.1:8-9)

Mfano wa tatu na wa mwisho ninaopenda kuutoa ni ule ambao mitume wa Kristo, kabla ya kujazwa Roho Mtakatifu walifanya uchaguzi wa kuziba nafasi ya Yuda Iskkariote aliyemsaliti Yesu na kasha akaishia kujinyonga. Tunasoma kwamba: “Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja.” (Mdo.1:26)

Kwa ushahidi wa maandiko tuliyopitia tunajua kwamba, utaratibu wa kupiga kura unatambuliwa na Mungu na hivyo ni mapenzi yake kuwachagua viongozi wa kijamii kwa uchaguzi.Chaguo la Mungu hujulikana vipi
wakati ni watu wanajichagulia wenyewe?

Kujibu swali hili ni kitendawili kigumu sana. Hakuna mwenye majibu yaliyo kamili. Lakini sio kwamba majibu sahihi hayapo. Yapo. Ugumu upo kwenye kuyatambua na kuyakubali. Mimi pia napenda kutoa mchago wangu katika kujibu swali gumu. Lakini nataka kuanza kwa kuchambua dhana ambazo zinatumika na wengine kujibu swali hili. Mwisho nitajibu nionavyo mwenyewe. Hebu tuanze na “Dhana zilizopo katika jamii ya waamini dini”:

1.   Mungu hutumia ushawishi wake kupitia akili za wapiga kura

Hii ni dhana maarufu hasa katika jamii ya waamini wa dini ya Kikristo ambao huamini kwamba, “Mungu hutumia ushawishi wake kwa kuwaingizia akilini wapiga kura kwamba ni nani anayewafaa kuwa kiongozi wao. Dhana hii inatokana na itikadi kwamba, wacha Mungu wakimwomba Mungu ili awasaidie wapiga kura kumchagua kiongozi ambaye ni chaguo lake, basi Mungu hujibu sala zao kwa njia hii ya ushawishi maalum unaoingia katika akili za wapiga kura ili wapate kumchagua anayestahili.

Hata hivyo, watu wasioamini katika mambo ya dini, wanaweza kupinga ukweli wa dhana hii kwa madaia kwamba, wagombea wa nafasi za uongozi ndio wenye kushawishi akili za wapiga kura kwa kutoa ahadi za mambo watakayowafanyia na kwamba hayo ndio ushawishi unaowaongoza wapiga kura kuwachagua au kutokuwachagua.

2.     Mungu hutoa mvuto maalum kwake amtakaye akubalike kwa wengi

Dhana hii nayo inabeba sehemu kubwa ya waamini katika jamii ya Kikristo kwa kuona mvuto anaokuwa nao mgombea kwa kupata washabiki wengi sana kwenye mikutano ya kampeni. Dhana hii inaamini kwamba, mtu anayekubali kwa Mungu lazima atakuwa kivuo kwa watu wengi ili wapate kumpigiia kura za ndiyo kwa kigezo hicho tu.

Kama ilivyo dhana ya kwanza ya ushawishi maalum, hali kadhalika na hii ya mvuto maalum kwa watu wengi. Wasioamini katika dhana hii wanapinga wakisema, wako wagombea ambao walikuwa na mvuto mkubwa lakini hawakuchaguliwa na wengi kama ilivyokuwa imetabiriwa. Na wako waliochaguliwa kwa sababu ya mvuto lakini baada ya kushika madaraka wakapoteza mvuto huo kwa jamii.

Hizi zote ni dhana. Zinaweza kuwa na ukweli kiasi fulani, lakini hakuna ushahidi wa kimaandiko wa kuthibitisha yasemwayo. Ni dhana. Kwa wengine wanaita ni imani tu.

Maoni yangu binafsi

Ninatambua na kukubali kwamba Mungu anautambua uchaguzi kama njia ya raia kuwapata viongozi wao. Na nina imani kwamba, Mungu anao uwezo wa kumwezesha yule ambaye ni chaguo lake, hata kwa mfumo wa kupiga kura kumfanya achaguliwe na watu wake mwenyewe.

Lakini pia natambua kwamba, Mungu hategemei kura za wengi ili mtu wake apite. Kura za wengi ni matokeo ya mapenzi ya Mungu kwa yule aliyemridhia kushika madaraka ya utawala. Pamoja na udhaifu wa binadamu katika harakati za kuchakachua utaratibu wa uchaguzi, bado yule ambaye ni chaguo la MUngu ndiye atakayepita na kushika madaraka.

Na kama Mungu hamtaki mtu hata kama anapendwa na wengi hatapita. Na yule aliyeteuliwa na Mungu hata kama wengi hawamtaki bado atapita. Yote hayo yanawezekana kwa Mungu. Ili mradi niweke angalizo hapa. HAKUNA AWEZAYE KUSHKA MADARAKA AMBAYE HANA RIDHAA YA MUNGU. HAKUNA.

MWISHO

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.