KWA TAARIFA YAKO: JE HII NI DALILI YA KUNDI LA UPENDO GROUP KUWA LIMEKUFA RASMI?

Haya msomaji wetu wa Gospel Kitaa karibu katika kipengele chetu maalumu ''KWA TAARIFA YAKO'' ambacho kinakujia kila siku za alhamisi ndani ya GK kikiwa na lengo la kukupatia habari ambayo iliwahi kutukia lakini yawezekana huijui pia yawezekana ilitukia ukawa unaijua lakini GK ikawa imesahau mahali au kuna sehemu haina usahihi utapata fursa ya kusahihisha kwa kuweka comment yako chini kabisa kwenye habari husika. Karibu

Kutoka kushoto Albert, Lilian, Joshua pamoja na Esther waanzilishi wa Upendo Group


KWA TAARIFA YAKO ni takribani miaka mitatu sasa, kundi maarufu la muziki wa injili liitwalo Upendo Group limekuwa kimya katika tasnia ya muziki huo nchini Tanzania na kwingineko ambako walikuwa wakifahamika kwenda na kutoa huduma. Kundi hilo ambalo lilivuma sana miaka ya mwanzoni mwa elfu mbili lilikuwa likiundwa na takribani waimbaji saba na lilifanikiwa kuteka anga la muziki wa injili kwa kiasi kikubwa huku likiibua vikundi vingine vidogovidogo na hata kuamsha ari ya waimbaji binafsi katika muziki huu wa kumsifu Mungu.

Hata hivyo kimya cha Upendo Group kwa miaka hii minne kimezidi kuwaacha njia panda wapenzi wa kundi hili pamoja na mashabiki wa muziki wa injili ambako wengi wanajiuliza kama kundi hili limefikia tamati. KWA TAARIFA YAKO hali hii ya sintofahamu imeibuka tena hivi karibuni baada ya muimbaji mwingine mashuhuri wa kundi hilo Eliwinjuka Mafwenga akionekana kuhudumu katika kwaya yake ya zamani aliyoiimbia ya Uinjilisti Kijitonyama. Kwaya ya Uinjilisti ilialikwa kuhudumu katika uzinduzi wa album ya Boniface Mwaitege Diamond Jubilee Hall Jumapili ya tarehe 2 Agosti, uzinduzi ambao uliandaliwa na Msama Promotions.

Kitendo cha Eliwinjuka ambaye alikuwa mmoja wa waimbaji tegemeo wa Upendo Group kurejea katika kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama kimezua maswali sana na kuthibitisha kuwa huenda Upendo Group imemaliza muda wake, maana ni vigumu kutumikia vikundi viwili. KWA TAARIFA YAKO Ikumbukwe kuwa kabla ya kuanzishwa Upendo Group waimbaji wake walikuwa ni sehemu ya Kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama na kitendo cha wao kuanza kurejea kinaleta tafsiri nyingi kwa washabiki na wadau wa muziki wa injili nchini.

Eliwinjuka alipopanda madhabahuni mwaka juzi kwa mara ya kwanza na kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama wakisherehekea jubilei ya kwaya hiyo. 


KWA TAARIFA YAKO Eliwinjuka ambaye anafahamika sana kwa wimbo wa Bam Bam alioimba na Upendo Group alianza kuwika ndani ya miaka ya tisini akiwa na kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama ambako alikuwa mmoja wa waimbaji viongozi akishirikiana na Lilian Joshua. Ndani ya Uinjilisti Eliwinjuka alivuma na nyimbo kama Nikimbilie Wapi, Nakutafuta Mponyaji na Nafarijika. Uongozi wa Uinjilisti Kijitonyama ulipoulizwa ulithibitisha kumpokea muimbaji huyo mwenye sauti nyororo na kuwa ni kweli ameanza kuhudumu na kwaya hiyo tena.

Hali ya wasiwasi ya kumeguka kwa kundi la Upendo ilianza mnamo mwanzoni mwa mwaka 2011 ambapo muimbaji maaruufu wa kundi hili, Joshua Mlelwa aliamua kuachia ngazi na kwenda kuanza huduma ya peke yake. Duru za ndani ya Upendo Group zinasema Mlelwa aliaga rasmi baada tu ya kutoka safari ya huduma Ulaya. KWA TAARIFA YAKO hata hivyo katika mahojiano mbalimbali na vyombo vya habari Joshua amekuwa akisema kuwa alihama Upendo Group baada ya wingu kuhama hivyo alienda kutafuta wingu mahali pengine. Hata hivyo habari zisizo rasmi zinasema kulitokea mtafaruku baina ya Joshua na uongozi wa Upendo Group hasa pale ambapo uongozi haukuridhia Joshua kubaki Uingereza ambapo alikuwa ameomba abaki kwa muda kufanya shughuli binafsi.

“Kitendo cha kubaki Uingereza hakikuwafurahisha viongozi maana walijua Joshua ni nguzo muhimu hivyo kukosekana kwake kungezuia mambo Fulani Fulani“, kilisema chanzo kimoja cha karibu na kundi hilo ambacho kisingependa kutajwa jina kwa sababu kadha wa kadha.

KWA TAARIFA YAKO mtu wa pili kumeguka alikuwa ni mke wa Joshua anayejulikana kwa jina la Lilian ambaye aliachana na Upendo na kuungana na mumewe katika huduma ya pamoja. Wawili hawa wamebaki kuwa maarufu na wameonekana wakihudumu katika mikutano na matamasha mbalimbali ikiwamo semina za mwalimu Christopher Mwakasege. Joshua anatamba na album yake iitwayo Ni Wewe. Habari za kuaminika zilizoifikia Gospel Kitaa zinasema kuwa mkewe Lilian naye yuko studio akimalizia kutengeneza album yake ambayo mpaka sasa haijapewa jina.

Esther Castory

Ikumbukwe kuwa kuhama kwa Joshua na mkewe kulikuwa ni pigo kwani yeye ndiye alikuwa mtunzi, mwalimu na muimbishaji kiongozi lakini pia mkewe alikuwa ni mmoja wa vivutio vya kwaya hiyo sio tu kwa uimbaji na sauti nzuri bali hata uchezaji wake. Hata hivyo kuhama huko hakukuwazuia Upendo Group kuzindua album yao ya mwisho iliyokwenda kwa jina la Mungu wa Ushindi ambapo nyimbo nyingi zilianzishwa na Joshua na mkewe na baada ya hapo miaka mitatu baadae hakuna ambalo limesikika ndani ya kundi hilo, kuachana na huduma za hapa na pale.


“Waimbaji wamekuwa wazito, hawajiamini tena mara nyingi wanakataa kwenda kwenye huduma
maana wanaogopa kama watafanya huduma chini ya kiwango,“ kinasema chanzo kingine kilichoko karibu na kundi hilo. KWA TAARIFA YAKO, Upendo ilipata pigo lingine baada ya muimbaji wake Esther Castory, kuhamia Mbeya kimakazi kama wakili wa mahakama hivyo kufanya pengo lizidi kuwa kubwa ndani ya kundi hilo. Muimbaji pekee aliyebaki na kuonekana labda angeweza kumudu kulishikilia kundi hilo alikuwa ni Eliwinjuka ambaye naye sasa anaonekana kujitoa na kurudi makazi yake ya zamani yaani Kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama.Mashabiki wengi wanakaa mkao wa kusikiliza tena nini kitatokea na kama Eliwinjuka atawika tena ndani ya Uinjilisti Kijitonyama kama ilivyokuwa zamani alipokuwa akihudumu na kundi hilo ambalo nalo limejipatia umaarufu sana sio tu nchini Tanzania bali hata mipaka ya nje ya Tanzania.

Lakini pamoja na hayo, KWA TAARIFA YAKO ni muhimu kuombea waimbaji na makundi yote ya uimbaji nchini ili kuwepo na umoja wa kudumu katika kumtumikia Kristo Yesu BWANA wetu. Hilo litakuwa mfano kwa wale wote ambao hawajamjua Mungu ili kupata kuiga mfano wetu wana wa Mungu.

Na kwa kuwa pia hiyo ni huduma, na DVD pamoja na matoleo yanauzwa, basi ni vema viongozi wafikirie namna y akuwasaidia waimbaji wao kiuchumi.

MTAZAME ELIWINJUKA AKIIMBA WIMBO MAARUFU NA UPENDO GROUP


Uinjilisti Kijitonyama


Hiyo ni KWA TAARIFA YAKO vinginevyo tukutane wiki ijayo….

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.