MAMBO MACHACHE YATAKAYOFANYA JINA LAKO LIWE NA SIFA NJEMA

Faraja Naftal Mndeme,
GK Contributor.


I.  UADILIFU.
Muda mwingi tumetamani majina yetu yazungumzwe vizuri kwenye maisha yetu ya kila siku hata baada ya sisi kufa, au kuwepo mbali na mahali husika ambapo jina lako linatajwa. Lakini ni watu wachache sana ambao wamejua mbinu ambazo zitafanya majina yao yawepo kwenye vinywa vya watu bila ukomo. Jina la mtu ni utambulisho wa mtu. Jina la mtu linaweza kuwa nguvu mahali husika hata bila yeye mwenyewe kuwepo katika eneo hilo. Uadilifu kwenye kila jambo na kwenye kila eneo la maisha yako kutafanya jina lako liendelee kudumu na kuwepo. Je Unaposikia jina kama Mwalimu Julius Kambarage Nyerere unakumbuka nini ingawa mwenywewe alishafariki zaidi ya miaka kumi iliyopita? Je Ukisikia Nelson Mandela unapata picha gani kichwani mwako? Jina lako tu linaweza kukupa kibali kwa mtu anayelisikia bila hata wewe mwenyewe kuwepo. Ni muhimu kuhakikisha unakuwa muadilifu kwa asilimia zote kwenye maisha yako.

II. UKWELI
Kuna watu wewe binafsi ukisikia majina bila hata wewe kuwepo kuna aina fulani ya tabia yao unaikumbuka. Jina la mtu ni utambulisho wa mtu. Kuna Mahali unaweza kwenda lakini sifa zako na jina lako zinakuwa zimeshakutangulia kwa namna tabia yao ilivyo. Kuishi maisha ya kweli kuna faida. Ni mara ngapi umesema uongo ukahisi unapata faida yako kwa mtu uliyemdanganya? Hasara ya kuishi maisha yasiyo na ukweli ndani yake ni kubwa zaidi kuliko ilivyo kawaida. Ni muhimu kujenga utaratibu ya kwamba kweli yako iwe kweli na hapana yako iwe hapana ili kujijengea jina ambalo litakumbukwa daima na hata usipokuwepo. Kumbuka jina lako ni urithi wa vizazi vijavyo. Unafikiri vizazi hivyo vitakumbuka jina lako kwa lipi?

III. UAMINIFU.
Je, jina lako linapotajwa linawakumbusha nini watu wanaolisikia? Je linawakumbusha maisha yako na hasara ulizowaletea kwa kukosa kwako uaminifu na maumivu tele mioyoni mwao? Uaminifu ni bidhaa ambayo huleta harufu nzuri ya manukato kwa wale wanaosikia jina kako. Jina lako linaweza likakupa kibali sehemu yoyote kutokana na namna unavyoendesha maisha yako ya kila siku. Unaweza ukahisi unapomtendea mtu mmoja vibaya watu wengine hawaoni, kumbe wanaona lakini hawasemi tu. Hakikisha unajenga haiba ya uaminifu ili kulijengea jina lako sifa njema. Jina lako linaweza likawa mtaji wa kibiashara. Jina lako linaweza kuwa urithi bora kwa vizazi vijavyo. Mfano Mzuri unaposikia Bill Gates au CocaCola na Pepsi unafikiri unaelewa nini? Majina haya yamejengwa katika uaminifu kwa jamii kiasi ukitaka tu kuyatumia lazima ulipe kodi kwa mwenye jina. Hasara ya jina baya si kwamba itakuathiri wewe tu bali itaathiri na watu wengine kwenye kizazi chako. Kuna majina kwenye nchi yetu (unayafahamu) yakitajwa tu kuna namna unajisikia moyoni, kwanini?

IV. HAKI
Haki imekuwa bidhaa adimu sana miongoni mwa wanadamu, lakini wewe hakikisha unamtendea haki kila ajaye kwenye maisha yako; mkubwa kwa mdogo. Haki pamoja na kuzunguzwa kwenye vinywa lakini hakikisha unaitenda. Mara nyingi tumehubiri haki lakini linapofika swala la utendaji imekuwa ni ngumu, sababu ya aina ya maslahi mabaya tunayopata kwa kutokutenda kwetu haki. Haki itakufanya uendelee kuishi hata bila wewe mwenyewe kuendelea kuwepo. Unaposikia  NYERERE unakumbuka nini kwenye hili taifa? Je hakuna viongozi wengine kwenye hili taifa? Jina lako likitajwa je linakumbusha dhuluma, ubabe na mambo mengi maovu uliyotenda? Jina lako litakumbukwa zaidi iwapo utatenda haki kwenye kila jambo. Jina lako linaweza kukupa fedha bila hata wewe kutumia nguvu, tunasikia mifuko mbali mbali ya kijamii ina majina ya baaadhi ya watu ambao wiliishi kwa haki. Jina likitajwa tu basi fedha hulifwata jina hilo. Je Wewe jina lako likitajwa sehemu ni nini kinatokea?

Mwisho
Jina lako linaweza kukupa kibali sehemu au kukunyima kibali kabisa. Kuna watu wamekosa kazi, fedha, kwasababu ya ubovu na ubaya wa majina waliyorithi kwenye maisha yao, hadi kuna wengine wameacha kuyatumia si kwa sababu hayana ladha nzuri yanapotamwaka bali ujumbe uliopo nyuma ya jina unaleta matatizo. Jina lako ni urithi kwa vizazi vijavyo. Ukilitumia vizuri basi kuna wakati vizazi vijavyo wanaweza kutumia jina lako kama mtaji kwenye maisha yao na wanaweza kufaidika. Jina lako linaweza kutumika kama nembo ya kibiashara. Fikiria jina lako limehusishwa kwenye wizi, uongo, dhuluma unafikiri likitumika kama nembo ya bidhaa kuna mtu atasogelea hiyo bidhaa? Jina lako ni mtaji unaodumu kizazi hata kizazi.

Email : naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless You All
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.