SOMO: NAMNA YA KUMLEA MTOTO KATIKA NJIA IMPASAYO (4)

Kelvin Kitaso,
GK Contributor.

Somo hili linatoa majibu ya namna gani mtoto anapaswa kukuzwa katika BWANA, na ni kwa namna gani mzazi anaweza mtengeneza mtoto kuwa katika misingi iliyo myema na ya kupendeza kwa kufuata misingi ya biblia. Soma sehemu iliyopita kwa kubofya hapa

MAKUZI YA SAMWELI

Kama lipo jambo jema ambalo wazazi wanapaswa kutafuta kujifunza kwayo ni malezi aliyolelewa Samweli na malezi aliyolelewa Yesu Kristo, Wawili hawa wanatajwa kwa namna ya tofauti sana katika maandiko kwa namna ile waliyokuwa wakikua. Utofauti wao ni kuwa Samweli hakulelewa na wazazi wake mwenyewe ila alilelewa kwa muda mwingi na Kuhani Eli, lakini Yesu alilelewa na wazazi wake waliopewa dhamana ya kumlea hapa duniani.

Kielelezo no 7: Mfano wa mtoto akuaye kwa hekima, kimo, kumpendeza Mungu, na wanadamu.
1 Samweli 2:26 “Na yule mtoto, Samweli akazidi kukua akapata kibali kwa BWANA, na kwa watu pia,” maandiko haya ueleza ni kwa namna gani Samweli alikuwa akikua; katika biblia ya New Internationa Version inasema, “And the boy Samwel continued to grow in stature and in favour with the Lord and with men” kwa tafsiri ya kuwa “mtoto Samwel akazidi kukua katika kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.” Kuna vitu vitatu vinatajwa katika maandiko haya navyo ni kimo, kumpendeza Mungu na kuwapendeza wanadamu.
Anapozungumzia kimo ni makuzi ya kawaida ambayo yanaonyesha makuzi ya kimwili, ila anapozungumzia kumpendeza Mungu ni matokeo ya mafunzo ambayo ameyapata yamfundishayo kumpenda na kumtumikia Mungu na ni matokeo wa yale yote aliyofundishwa na kuhani Eli na wazazi wake, lakini si kufundishwa tu bali kutii na kuyatendea kazi mafundisho ajifunzayo; na kuwapendeza wanadamu ni matokeo ya mwenendo mzuri aliokuwa nao mbele ya watu wakubwa na wanajamii kwa ujumla.
Ipo tofauti kubwa sana kati ya makuzi ya Yesu na makuzi ya Samweli na katika kuyatazama haya wazazi wanaweza kujifunza mambo mengi yaliyo ya msingi sana; Samweli baada ya kukua kidogo tu alipelekwa kwa Kuhani Eli ili apate kukua huko, 1 Samweli 1:24 “Naye alipokuwa amekwisha kumwachisha maziwa, akamchukua pamoja naye, na ng’ombe watatu, na efa moja ya unga, na chupa ya divai, akamleta nyumbani kwa BWANA, huko Shilo; na Yule mtoto alikuwa mtoto mdogo,” hii inafanana sana na familia nyingi za wazazi wa leo wanaopenda kuwapeleka shule za bweni/kukaa huko huko mara tu wanapokuwa wadogo na kuwakabidhi kwa walimu ili wapate kulelewa huko, ndivyo ilivyokuwa kwa Samweli alipoacha tu kunyonya akachukuliwa na kupelekwa kwa mwalimu ambaye ni Kuhani Eli ambapo alikuwa akifundishwa utumishi kama somo kuu. Zaburi 92:13 “Waliopandwa katika nyumba ya BWANA Watastawi katika nyua za Mungu wetu”  na inaonyesha kuwa Samweli alipandwa katika nyumba ya Mungu ndiyo maana akakua katika BWANA.
Kumpeleka mtoto akuapo katika shule za bweni ni njema ila ni vyema kuangalia ni walimu wa namna gani watakao mlea mtoto wako, Samweli alikuwa vyema kwa kuwa mwalimu wake alikuwa vizuri sana na mwenye kumpenda Mungu sana na alimsaidia sana Samweli kumjua Mungu na kujua ni kwa namna gani anaweza kumsikiliza Mungu. 
Jambo la msingi kuzingatia ni kuangalia kama ni katika mikono salama umemuacha mtoto, kwa kuwa unaweza kumuona anakuwa imara na hodari katika elimu ya dunia hii, ila si katika kumjua Mungu, angalia sana kama hakuna usalama wa walimu wa maadili ni bora kujilelea wewe mwenyewe kama alivyofanya Mariam na Yusufu kwa mtoto Yesu.
Wazazi wema, watoto waovu.
1 Samweli 2:12 “Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali BWANA.”
Ni jambo la wazi sana kuwa wazazi wanaweza wakawa ni wema sana machoni pa Mungu na kwa wanadamu pia ila tatizo kubwa likawa ni watoto wao. Kwa nyakati za sasa limekuwa ni jambo la kuzungumziwa sana ndani ya kanisa kuwa watoto wa watumishi ndio wanaongoza kwa kuwa na maadili mabaya na wenye maadiri mazuri ni watoto wa mbali tu kama ilivyokuwa kwa Samweli, hili limekuwa changamoto kubwa sana kwa watumishi na wakati mwingine ikisikika kuwa watoto wa watumishi ndio watu maarufu katika miziki ya kidunia, uigizaji, ulevi na mambo mengine. 

Kielelezo no 8: Mfano wa mtoto mwenye kiburi ©Getty

Katika suala hili kila mmoja amekuwa akijaribu kutoa maoni yake juu ya hili na wengi wamekuwa wakitafuta ni nani alaumiwe katika uovu wa watoto wa wazazi wafanyao vyema. Ni vyema kufahamu kuwa watumishi wa Mungu wapo katika vita kali na watoto wao pia huwa katika vita hivyo, na mara nyingi shetani akishindwa kwa wazazi utafuta kupiga watoto ili kuharibu huduma ya wazazi.

Hizi ni sababu zinazochangia jambo hili kwa kuangalia pande zote mbili:
  • Watoto wenyewe kutokuzingatia mafundisho ya wazazi wao na kutotaka kuwasikiliza, 1 Samweli 2:22-25 “Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisreli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. 23 Akawaambia, mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote. 24 Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA. 25 Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa BWANA ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya Baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuua.”
Tatizo kubwa ambalo lilikuwa kwa watoto wa Eli ni kukosa usikivu baba yao alipokuwa akizungumza nao. Na huwa ni tatizo pia kwa watoto wengi waharibikiwao kukosa usikivu wa maneno ya wazazi wao.

  • Makundi mabaya ambayo watoto ushirikiana nayo, na wakati mwingine ni vitu wajishughulishavyo kuvitazama kwenye runinga na hata kuvisikiliza. Kama kiongozi kwa mtoto kuwa makini sana na hili eneo kwa kuwa lina uangamivu mkubwa sana kwa mtoto kimaadili, eneo kama hili ukiona mtoto anajishughulisha nalo ni ufa, na kama hautoziba ufa ni lazima utajenga ukuta na si rahisi kuujenga huo ukuta ikiwa umebomoka, chukua tahadhari mapema.
  • Kutomjali BWANA na kutoheshimu kazi yake/kumzoea Mungu na kazi yake.
1 Samweli 2:12,17 Basi, hao wana wa Eli walikuwa watu wasiofaa kitu; hawakumjali BWANA.”  17 “Hivyo dhambi yao wale vijana ilikuwa kubwa sana machoni pa BWANA; kwa maana hao watu walidharau sadaka ya BWANA.” Mbali na watoto wa kuhani Eli ila jambo hili uendelea kutenda kazi kwa watoto wengi wa watumishi kwa kushindwa kumthamini na kumuheshimu BWANA bali wengi uona kutenda kinyume na mapenzi ya Mungu ni kawaida. Na huizoea kazi ya BWANA na kuiona ni kawaida tu na wengine ufanya kazi ya Mungu huku njia zao zikiwa mbali na Mungu. 
  • Wazazi kutozingatia sana kuwa na muda wa kutosha na watoto wao kama wazazi ili kuweza kuwafundisha mambo mengi. Hii ni kwa sababu watumishi wengi uzani kuwajibika kwao ni katika huduma tu na si katika familia zao na utoa muda mdogo sana wa kukaa na familia zao. Jim Murphy anataja vipaumbele vitatu kwa watumishi wa Mungu ambavyo ni 1. Uhusiano na Mungu, 2. Uhusiano na familia, 3. Uhusiano na huduma.
  • Watumishi wengine hushindwa kuwakemea watoto wao kwa ukali na hata kutumia viboko pale wakoseapo.

Kuhani Eli alikuwa akikaa karibu kabisa na hema ya kukutania na ndipo familia yake ilipokuwa inaishi lakini pamoja na ukaribu huo na hema ya kukutania haikuwa sababu ya watoto wake kuwa karibu na Mungu anayepatikana katika hema ya kukutania. Kumpenda Mungu kwa Eli kulikuwa ni kwa viwango vikubwa sana na inaonyesha ni mtu ambaye Mungu alimpenda ila alikataa uzao wake kwa sababu uzao wake haukuwa ukimcha Yeye. Ni vyema kufahamu hili kuwa kama watoto wa watumishi wa Mungu watashindwa kwenda katika njia za haki, basi Mungu atajitwalia mwingine kutoka mbali kabisa ili amtumikie yeye.

Watoto wengi wa watumishi wamekuwa wakisimama kuhudumu na kufanya huduma mbalimbali lakini si katika usafi wa mioyo kama ilivyo kwa wazazi wao hii ni kutokana na kuzoea huduma na kuchukulia huduma kama kitu cha kawaida sana.

___
Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0769190019/0713804078, kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.