SOMO: NAMNA YA KUMLEA MTOTO KATIKA NJIA IMPASAYO (5)

Kelvin Kitaso
GK Contributor.

Mara ya mwisho tulitazama malezi ya Samweli (bofya hapa kusoma) katika mfululizo wa somo hili linalolenga kutoa majibu ya namna gani mtoto anapaswa kukuzwa katika BWANA, na ni kwa namna gani mzazi anaweza mtengeneza mtoto kuwa katika misingi iliyo myema na ya kupendeza kwa kufuata misingi ya biblia.
Makuzi ya Yesu Kristo akiwa ulimwenguni.
Picha ya mchoro wa Mtoto Yesu hekaluni ©IDS
Nikiwa nazungumza na rafiki yangu nikamuuliza swali juu ya makuzi ya Yesu Kristo wakati akiwa mdogo kuwa, je Yesu wakati akiwa ulimwenguni alichapwa viboko na wazazi wake kama njia njema ya kumsababisha afanye vyema,? Swali hili halikuwa swali rahisi lakini kwa kutafakari utagundua kuwa Yesu tangu angali mdogo alikuwa anatenda vyema kama mfano bora na kuonyesha ni kwa namna gani watoto wanavyopaswa kuwa. Kusema moja kwa moja kuwa alikuwa anachapwa kama watoto wengine si sahihi na haina ukweli ndani yake kulingana na mwenendo wake ulivyokuwa safi huku akiwa mfano ni kwa namna gani watoto wanapaswa kuishi wakiwa wadogo.

Licha ya kuyaangalia malezi ya Samweli ambayo upata kujifunza mambo mengi sana kama mtu aliyelelewa mbali na nyumba ya wazazi wake, chini ya mwalimu makini aitwaye Eli, yaani alikuwa katika shule ya bweni; yupo mwingine ambaye kwetu ni Baba ila alifunuliwa kwa namna ya mwili na kuchukua umbo la mtoto na katika umbo hilo aliishi na wazazi wake ila kama ni aina ya shule inatofautiana na ile ya Samweli kwa kuwa huyu alikuwa kwa wazazi wake yaani ya kwenda na kurudi (day school and not boarding school) 


Luka 2:41-52 “Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya pasaka. 42  Alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; 43 na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, Yule mtoto alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. 44 Nao wakadhani yumo katika msafara ; wakaenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; 45 na walipomkosa wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46 Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. 47 Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. 48 Na walipomwona walishangaa na mama yake akamwambia, Mwanangu mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. 49 Akawaambia, kwani kunitafuta? Hamkujua kuwa imenipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu? 50 Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. 51 Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, alikuwa akiwatii; na mamaye akiyaweka hayo yote moyoni mwake. 52 Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima, kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.”   


Maandiko matakatifu yanaeleza sehemu ya maisha ya Yesu ambaye ndiye mfano mkubwa wa kuiga akiwa mtoto, na katika maisha yake yapo mambo mengi sana ya kujifunza na wazazi wanaweza kuyatumia kama ni kigezo bora cha kukuzia watoto.


Jambo la kwanza kulitazama ni tabia njema ya wazazi wa Yesu kama Viongozi, marafiki, walimu, na wapaji; Wazazi wa Yesu wanaonyeshwa wao wenyewe walikuwa ni wacha Mungu na watu wanaoheshimu sana mambo ya ibada na ilikuwa ni desturi yao kuwepo ibadani katika kipindi ambacho wanapaswa kuwa na ndiyo maana mstari wa 41 na 42 anasema “Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya pasaka. 42  Alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu;” Hii inaonyesha ibada kwa wazazi wa Yesu ilikuwa ni desturi yao na ni kitu chenye kipaumbele na ndivyo walivyomkuza mtoto wao kwa kumfunza na kumzoeza jambo hili na ndiyo maana mama yake anapolalamika kumtafuta yeye anajibu ya kuwa hamkujua kuwa imenipasa kuwepo nyumbani mwa Baba yangu, kama mtoto licha ya kuzungumzia ule UUNGU wake ila sehemu hii inaonyesha kuwa alijua umuhimu wa kuwepo mbele za Mungu na ndiyo maana aliwashangaa wazazi kumtafuta.


Ni wazi kabisa ukimfundisha vyema mtoto umuhimu wa kuwa katika nyumba ya Mungu hatohitaji kuhimizwa kwenda katika nyumba ya Mungu bali uweza kujisimamia mwenyewe na wakati mwingine kukuzidi wewe uliyemfundisha na pindi utakapomkataza au kumzuia atakushangaa kwa kuwa umemfundisha kuwa katika nyumba ya BWANA. Si katika kuwa nyumbani mwa BWANA tu, bali katika kufanya mambo mema yote pia.


Jambo jingine la kufikirika ni juu ya ile hekima kubwa iliyoonyeshwa na mtoto wa miaka 12 mbele ya walimu wa sheria, mbali na kuvuta hisia ya kuwa ni kwa sababu yeye ni Mungu na ndiyo maana aliwasikiliza na kuuliza maswali, ila kuna mchango pia wa wazazi waliopewa dhamana ya kumlea kwa kuwa katika kusikiliza kwake kwa makini ni matokeo ya kuwa msikivu mbele za wazazi wake, kwa kuwa ingekuwa ngumu sana kuwasikiliza walimu kama si msikivu kwa wazazi wake, ila kuuliza maswali ni ishara ya kuwa ni mtoto ambaye alikuwa akifundishwa nyumbani mambo mengi na ndiyo maana alikuwa akiwahoji sana waalimu, suala hili ni vyema kwa wazazi kulifahamu kwa kuwa na madarasa nyumbani na kuwafundisha watoto wao mambo mengi sana kwa kufanya hivyo yatawafanya kujua mambo mengi sana na kuwajengea ujasiri hata wa kusimama mbele za wakubwa. Kuwa na vipindi vya shule ya maandiko na wakati mwingine kuwapa nafasi ya kusoma na kutafsiri neno kutawafanya kuwa na hekima kubwa na maarifa makubwa.


Mtoto alelewaye vyema ni sifa njema kwa wazazi wake, ni wazi kabisa kwa ile hekima aliyoionyesha kule hekaluni ilikuwa ni sifa njema pia kwa wazazi wake, ila kama angefanya mambo ya kipumbavu ingekuwa ni aibu na fedhea kwa wazazi wake. Kuna Mama mmoja alipaza sauti yake na kumwambia Yesu, “……heri tumbo lililokuzaa na matiti uliyonyonya” Luka 11:27, hii ni matokeo ya kumlea mtoto katika njia ipasayo.  


Ni vyema kujihoji kuwa watoto uliowazaa wanasababisha upate Baraka na hata watu wakasema, “libarikiwe tumbo lililokuzaa, au wamekuwa wakikuletea laana kwa ajili ya tabia mbaya waliyonayo.
Uzuri wa tabia ya mtoto ni uzuri na sifa kwa mzazi, ubaya wa tabia za mtoto ni aibu na ubaya kwa wazazi

Ni dhahiri kabisa katika umri mdogo alikuwa na ujasiri mkubwa ambayo ni sababu pia kwa walimu kumshangaa na hii ni kwa sababu shuleni alipokuwa(nyumbani kwa wazazi wake) alikuwa akifundishwa mengi yaliyompa kujiamini.
Kama mtoto Yesu aliwatazama wazazi wake wafanye wajibu wao ila habari njema ni kwamba wazazi wake walikuwa ni watu wema waliojua kuufundisha wema huo kwa mtoto wao, ila kitu cha tofauti ndani yake ni katika kuwasikiliza kwa umakini na kutii maagizo yake ndiko kulimfanya kuwa watofauti na wengine.
Vipo vitu vinne ambavyo vinatajwa katika mstari wa 52, ya kuwa alizidi kukua katika hekima, kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. Kukua katika hekima ni matokeo ya umakini wake wakujifunza mambo yale afundishwayo na wazazi wake na walimu wengine na si kujifunza tu bali kutendea kazi yale ajifunzayo, kwa kuuliza maswali na njia nyingine mbali mbali, ndizo zilimfanya Yesu akue katika hekima, kukua katika kimo ni matokeo ya malezi mazuri na kupata chakula ambacho usaidia sana ukuaji wa mtoto awaye yeyote, kumpendeza Mungu ni katika kuyafanya yale aliyofundishwa kuwa ni mapenzi ya Mungu kwake; na kuwapendeza wanadamu ni matokeo ya mwenendo safi alionao mbele ya watu wanaomzunguka.
___
Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0769190019/0713804078, kitasokelvin@gmail.com


Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.