NIDHAMU HUJENGA MAFANIKIO YASIYO NA UKOMO

Faraja Mndeme,
GK Contributor.


Huwezi kutenganisha mafanikio na mtu kwenye jambo lolote lile na nidhamu yake. Nidhamu ni jambo ambalo linajenga mafanikio yasiyo na ukomo na hudumu kwa muda mrefu hata usipokuwepo. Mfumo wa maisha yetu kwenye kila jambo umejengwa kwenye nidhamu. Ili ufanikiwe kwenye jambo fulani ni lazima uwe na aina fulani ya nidhamu.

Maisha ya mwanadamu yamejengwa kwenye mfumo wa nidhamu. Bila nidhamu kwenye mambo mbalimbali basi kusingekuwa na mfumo mzuri na bora kwenye maisha yetu ya kila siku. Ukiona maisha yanaendelea na vitu mbali mbali vinafanikiwa na kutokea, basi tambua kuna aina fulani ya nidhamu ilijengwa vyema juu ya nidhamu katika jambo husika. Mafanikio huendana na nidhamu.

Nidhamu huongeza siku za kuishi. Mara nyingi tumekuwa na maswali mbali mbali. Je ni namna gani wanadamu wa kale waliweza kuishi kwa muda mrefu zaidi kuliko binadamu wa sasa? Jibu naloweza kukupa haraka haraka ni aina ya nidhamu waliyokuwa nayo. Nidhamu hiyo ilikuwa imejengwa katika mfumo wa vyakula. Kuna aina fulani ya vyakula vililiwa na pia nidhamu kwenye namna ya kulinda afya zao. Nidhamu kwenye utumizi na ulinzi wa afya zao. Watu wa kale walijenga mfumo ambao nidhamu ilianzia kwenye familia hadi nje ya familia ndio maana hata mmoja wa wanafamilia alipokiuka taratibu za maisha basi alihukumiwa na kuadhibiwa na familia.

Nidhamu itakufanya usonge mbele haraka zaidi kuliko wengine. Mafanikio ya mtu ni nidhamu ya mtu. Ukimuona mtu amefanikiwa kwenye swala la fedha basi tambua kuwa mtu huyo kwenye swala la pesa amejenga nidhamu ya hali ya juu. Unaweza kumkumta mtu ni tajiri lakini fedha kwake haitoki kirahisi na mpaka uipate umefanya kazi ya ziada. Kiukweli si kwamba hapendi kutoa bali aina ya nidhamu aliyoijenga mpaka kufikia hatua ya kuipata hiyo fedha ndio inayomuongoza namna ya kutoa fedha. Huwezi kutofautisha nidhamu ya mtu kwenye maswala ya fedha na mafanikio yake. Nidhamu ya mtu aliyefanikiwa katika maswala ya fedha imejengwa katika sehemu kuu mbili; mapato na matumizi. Huwezi kumkuta mtu mwenye mafanikio ya fedha anatumia fedha hovyo hovyo bila kuwepo na bajeti ya matumizi.

Nidhamu kwenye Afya. Unapomuona mtu ana afya njema na haugui hugui kila wakati, basi tambua kuna aina fulani ya nidhamu ambayo amejijengea kwenye afya yake. Unaweza kumkuta mtu huyo kila jioni anafanya mazoezi, analala vyema na anakula vyema. Mtu huyu amezingatia kanuni na taratibu zinazofanya afya yake iwe muhimu. Huwezi kumkuta anavuta sigara au anakunywa aina fulani ya vilevi, si kwasababu havipendi, ila ameona afya yake ni bora kuliko vilevi hivyo. Mtu huyu ukimfwatilia utagundua mfumo mzima wa maisha yake umejengwa katika nidhamu iliyo thabiti na isiyotikisika ili kuiweka afya yake kwenye hali njema na salama.

Nimezungumzia maeneo machache kwa sehemu tu kuonyesha namna nidhamu ilivyo na sehemu kubwa na mchango mkubwa kwenye maisha yetu wandamu. Hauwezi kutenganisha maisha ya mwanadamu na mafanikio aliyo nayo na nidhamu yake. Ukiona mtu amefanikiwa katika ndoa, uchumi, kiroho, na hata kijamii utagundua kuna aina fulani ya nidhamu ambayo ameiwekeza kwa kiwango cha juu tofauti na watu wengine ambayo inafanya aende mbele zaidi ya wengine. Maisha ni nidhamu, na nidhamu ni maisha. Bila hivi hatuwezi kufurahia maisha wala hatutafanikiwa kwenye jambo lolote maana tumekiuka sheria za uhai wa mwanadamu na mfumo mzima na taratibu za kuishi.

Email : naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless You All
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.