SOMO: FIMBO NI INJILI YA MTOTO

Kelvin Kitaso,
GK Contributor.


Kwa wakati wa sasa adhabu ya viboko imekuwa gumzo kubwa sana na zimeanzishwa mamlaka kubwa sana zinazohusiana na haki ya watoto na katika mamlaka hizo za kimataifa zimekuwa na kampeni ihusianayo na kuzuia adhabu ya viboko kwa watoto kwa madai ya kuwa ni unyanyasaji kwa mtoto. 

Kuna haki za watoto kutoka umoja wa mataifa na katika haki hizo usisitiza kuwa adhabu ya viboko siyo sahihi kwa mtoto ila suala hili bado linamkanganyiko mkubwa sana na mvutano mkubwa kwa kuwa zipo jamii na dini mbali mbali zinazo amini kuwa viboko ni njia ya kumtengeneza mtoto katika maadili yaliyo mema.

Licha ya hii sheria ya umoja wa mataifa bado kuna mvutano mkubwa sana kati ya wazazi wao wenyewe kwa kuwa wapo wanaoamini kuwa kumchapa mtoto anapokosea ni sawa na kumnyanyasa, na wengine uamini kuwa ni njia njema ya kumfanya mtoto kukua katika malezi safi.
Katika sura ya kwanza tulitazama kwa kina ni nafasi gani wanayo wazazi katika familia, na katika kuzitazama nafasi hizo tukaona ni vyema sana kuangalia nafasi ya Mungu na nafasi ya wazazi na kugundua kuwa wazazi wanapaswa sana kuiga nafasi ya Mungu vile afanyavyo kama kiongozi, rafiki, na mkufunzi asemaye, “Mimi ni BWANA, Mungu wako, nikufundishaye ili upate faida, nikuongozaye kwa njia ikupasayo kuifuata.” Na kama mzazi ufuata nafasi ya Mungu kwa kujifunza kutoka kwa Mungu ni vyema kuona ni kwa namna gani Mungu anafanya pale watoto wake tunapokosea, kwa kuwa husema, “Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi, basi uwe na bidii ukatubu (Yohana 3:19).” Kumbe Mungu mwenyewe hupenda kutoa adhabu kwa watoto wakoseao kwa sababu ya upendo alio nao, basi ni jambo la busara zaidi kwa mzazi kutoa adhabu kwa mtoto wake anapokosea, Mithali 13:24 “Yeye asiyetumia fimbo yake humchukia mwanae bali yeye ampendae humrudi mapema”

Fimbo kwa mtoto si mbaya na wala si kitu cha kubeza kwa wazazi kukitumia ila ni mbaya kama itatumika vibaya. Na ni njia kuu ambayo inatajwa kwenye biblia kama njia ya kumfanya mtoto akue katika njia ipasayo, maandiko yanasema, katika Mithali 23:13-14 “Usimnyime mtoto wako mapigo; Maana ukimpiga kwa fimbo hatakufa. 14 Utampiga kwa fimbo, Na kumuokoa nafsi yake na kuzimu.” 

Biblia inatoa tafsiri ya wazi ya neno ‘injili’ katika Warumi 1:16 kwa kusema, “ni uwezo wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye,” napenda kuifananisha fimbo na injili kwa kuwa ni kitu ambacho kimeandikwa kwenye Biblia na ni kitu ambacho kinapaswa kutendewa kazi. Kiboko kwa mtoto uleta wokovu wa nafsi yake kwa kila akipataye. 

Kumlea mtoto kama alelewavyo mtu mzima ni kosa kubwa sana na si kwamba unampenda bali unamsababishia maangamizo makubwa sana katika maisha yake ya baadae. Waebrania 12:7-10 “Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? 8 Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. 9 Na pamoja na hayo tulikuwa na baba zetu wa mwili walioturudi, nasi tukawastahi; Basi ni afadhali sana kujitia chini ya Baba wa roho zetu na kuishi? 10 Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vyema wao wenyewe; bali kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake. 11 Kila adhabu wakati wake haionekani kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye uwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.”

Yapo mambo ya msingi sana ambayo Mtume Paulo anayazungumzia mambo hayo uonyesha juu ya umuhimu wa adhabu kwake akoseaye, na anamfananisha mwana asiyerudiwa au kupewa adhabu na Baba yake ni sawa na yeye asiyependwa, kwa tafsiri hii ni kusema kuwa kama haukumrudi/kumuadhibu mwanao akoseapo ni sawa na kutompenda na kumtakia maisha mabaya katika kukua kwake; maana Paulo anamfananisha yeye asiyeonywa ni kama mwana haramu/asiye na thamani/ asiye na haki sawa na watoto wengine. Mstari wa tisa (9) Paulo anaonyesha ni kwa namna gani alikuwa akikuzwa kwa kusema kuwa naye alikuwa akirudiwa lakini katika kurudiwa kwake alikuwa akiwastahi wazazi wake, ni sawa na anasema kuwa, ‘nilikuwa nakubaliana na kukupokea kule kurudiwa’. Ila jambo pia la msingi anasisitiza Paulo ni kusema kuwa kule kuadhibiwa kulikuwa ni kwa faida yake yeye mwenyewe, japo mtoa adhabu alipata faida ya kule kubadilika na kufanya vizuri kwa mtoto ila zaidi ilikuwa ina faida kubwa kwa mtoto. Kila adhabu itolewapo uonekana ni kitu kibaya na kisicho furahisha na uleta huzuni pia kwake yeye aipataye adhabu hiyo ila ni kitu chenye maana kubwa sana kwake aliyezoezwa kupata.

Wiki ijayo tuatazama kwa nini adhabu ya viboko ni muhimu kwa mtoto. _____
Mwalimu Kelvin Kitaso anapatikana kupitia 0767190019 / 0713804078 na pia kupitia barua pepe; kitasokelvin@gmail.com

Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.