SOMO: JE WEWE NI KUKU AMA TAI

Elie Chansa,
GK Staff Writer.

©Smarty Brain
Rafiki yangu mmoja alinigusia kuhusu hadithi ya tai na kuku, nikahamasika kuifuatilia zaidi, ikanifunza jambo na kunifunua. Nimebarikiwa kukufikishia ujumbe huu.

Hapo zamani kulikuwa na tai ambaye alilelewa kwenye familia ya kuku, yaani tangu kuzaliwa (kutotoka kwenye yai) hadi akawa mkubwa, hakuwahi kuwa nje ya familia ya kuku.

Mama kuku alikuwa mwenye upendo sana, na alimlelea pasi na tofauti yoyote. kifufupi alikuwa mtoto wake. Alifunzwa kula kama kuku, kujinyoosha kama kuku, kunywa kama kuku na kutembea kama kuku. Zaidi ya rangi na umbile, hakuwa tofauti na kuku wenzake. Amecheza nao, amekua nao, na anaishi nao kama kawaida.

Siku moja yule tai (hebu tumuite kadogoo) katika cheza cheza yao na parua parua ya kusaka chakula kwenye udongo na majalalani, aliona kitu chenye kupendeza sana kikipita angani, akakipenda sana. Akauliza wenzake, ile ni nini? Akaambiwa, wale ni ndege aina ya tai, wao maisha yao ni ya namna hiyo, wana nguvu kubwa mno tofauti na sisi kuku, hatuwawezi katu.

Na hata Kadogoo alipotaka kuonesha shauku ya kuuliza zaidi kwa nini ni kama anafanana nao, alishutumiwa vikali na baadhi ya wenzake, wakimwambia; “mbona wewe huna shukurani, umekosa kitu gani hapa nyumbani hadi utake kujifananisha nao, wewe ni kuku tu, na utabakia hivyo”.

Na kweli yule tai akaridhika, maisha yakaendelea akiwa kuku, na si tai tena. Aliishi maisha yake mazuri tu, na alikuka kufa akiwa kuku.

Kuna jambo ambalo Mungu ameweka ndani yako na anataka ulitimize, lakini kuna kuku wanakuambia kwamba hiyo si saizi yako, ina wenyewe. Kwamba umri wako haukurushu kuwa diwani ama mbunge, kwamba asili yako huwezi kufanya kazi ya aina fulani. Kwamba elimu yako haitakufikisha popote, kwamba ule mradi unaotaka kuanza utakutia hasara kubwa - na kwamba usithubutu katu. Haya yote umeridhika kuyasikia kwasababu unaishi 'good life', bila kufahamu kwamba unastahili "a better life’. Ukisalia kwenye good life, utakufa na good life na kuku ‘wenzako’ bila ya kutambua kwanini Mungu alikupa mabawa makubwa yenye kukufanya uruke juu sana na kuelea angani kinyume na uelekeo wa upepo.

©Google Maps

Hutajua kwanini Mungu alikupa macho makali ya kuona umbali mrefu sana na kuchambua bidhaa iliyo njema dhidi ya bidhaa chakavu. (tai huweza kumuona sungura umbali wa kilomita 3.2, yaani kwa lugha rahisi anaona kutoka Ubungo hadi Mwananchi), ama kama hujui hiyo njia, basi ni kutoka Ubungo - Mlimani City iache uende mbele zaidi karibu na wanapochonga vinyago. Ndipo umbali huo). Ana uwezo wa kujinyonyoa mabawa na kujawa na nguvu mpya licha ya uzee.

Hizi zote ni baadhi tu ya ahadi za Mungu kwetu, maana tunatambua ya kwamba sisi tu washindi zaidi ya washindi (We are MORE THAN CONQUERORS.) Na pasi na shaka tunayaweza yote kupitia yeye (Mungu) atutiaye nguvu. Sasa wewe aliyekuambia better life si kwa ajili yako ni nani hata ukamkubalia na kuridhika? Unaweza kuwa vile utakavyo. Asitokee mtu akakueleza kwamba wewe huwezi kufanya jambo fulani kwa sababu kadha wa kadha - nawe ukamkubalia.

Muigizaji maarufu duniani, Arnold Schwarzenegger amepitia mengi katika safari yake hadi kutoka kwenye tasnia ya filamu huko Hollywood, Marekani. Katika safari yake akiwa bado mbeba vitu vizito, amewahi kuambiwa, "you are nothing but a bunch of muscles", kwamba yeye si kitu bali ni jamaa tu kama boya lililojaa misuli, mara kwamba lafudhi yake ni kituko, hatoweza kuongea mbele ya watu.. na kila aina ya dhihaka.

Lakini alichokifanya Schwarzenegger ni kufanya tofauti na kile ambacho watu wanasema. Aliamua kudhihirisha kwamba maneno yao si mawazo aliyokuwa nayo Mungu kwa ajili yake. Hakufikia kukata tamaa kwenye hararakati zake, na katika kuonesha juhudi anasema, "nilikuwa nafanya mazoezi mara kwa mara, na kitu ambacho watu walisema sitaweza kukinyanyua, basi mi niliamua kutilia mkazo ili niwaache mdomo wazi pale nitakapofanikiwa."  Mwisho wa siku Arnold amepata tuzo kadhaa kwenye uigizaji, ushindi kadhaa kwenye unyanyuaji wa vitu vizito, na hata kufanikiwa kuwa gavana wa jimbo la California kwa vipindi viwili, 2004-2011. Mifano iko mingi ambayo ningeweza kuelezea, lakini nukuu mojawapo ambayo huwa anaifanyia kazi ni, "you can not climb the ladder of success with your hand in the pocket". Yani kwamba huwezi kuikwea ngazi ya mafanikio ukiwa umeweka mikono yako mfukoni.

Chochote kilichopo ndani yako, anza sasa kukifanyia kazi kwa bidii bila kujali kuku wanakusemaje ama wanakutazamaje. Unaweza kufanikiwa, maana Mungu ameweka kitu ndani yako, usife nacho kama tai aliyeaminishwa na maneno ya watu akashindwa kutumia kile alichopewa. Uwe na safari yenye mafanikio.


UKIRI
___
BWANA Yesu ahsante kwa ufunuo huu, niwezeshe kuishi kulingana na mapenzi yako. Badili ninavyofikiri BWANA. Ninaomba uandae watu watakaoambatana nami, ili kusudi lako juu ya maisha yangu lipate kutimia. Ninaomba haya kwa Jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu, Amen!
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.