SOMO: NGUVU YA NENO HAPANA

Faraja Mndeme,
GK Contributor.
©Clip Art Sheep
Hapana ni neno dogo na la kawaida tu kwenye maisha yetu ya kila siku. Neno Hapana ni neno jepesi sana ukilitazama kwa haraka haraka. Kuna watu wengi wamefanikiwa katika maisha yao kwa kujua matumizi ya neno hapana na wengine wameshindwa kufanikiwa kwa kutokujua umuhimu wa neno hapana. Kuna wakati kwenye maisha yetu tulipaswa kulitumia Neno HAPANA lakini Kinyume chake tulitumia neno NDIYO. Namna maisha yetu ya kila siku yalivyo yanakulazimisha utumie neno ndiyo au hapana; inachotegemea ni utashi wako wa kutumia maneno haya pia na uadilifu wako wa ndani kwenye utumizi wa maneno haya.

Faida za Kutumia Neno Hapana.


I. UTUMIZI WA NENO HAPANA HUKUTAMBULISHA WEWE NI MTU WA NAMNA GANI.
Wataalamu wa mambo ya saikolijia wanadai moja ya neno ambalo lina nguvu kuliko maneno mengine ni neno hapana. Neno hapana linaonyesha aina ya msimamo ulio nao na kuonyesha wewe ni mtu wa namna gani. Unapokua mtu wa kusema ndiyo kila wakati inatengeza watu kutokuelewa wewe ni mtu wa namna gani na je ni mtu kaliba gani. Mara nyingi tumefikiri kuwakubalia watu mambo kwa kusema ndio ni kutufanya tuonekane bora kwa wengine, lakini muda mwingine imekuwa kinyume. Neno hapana linapotumiwa linaweza kumsaidia mwingine kuweza kutambua na kufahamu aina ya mtu na inakuwa raisi kutambua aina misimamo na mitazamo binafsi uliyo nayo.
 
2. UTUMIZI WA NENO HAPANA HUHARIBU MINONG’ONO HASI YA NDANI YA MTU.
Kila wakati na kila mara kila mmoja wetu umekuwa akisikia sauti ya ndani yake mwenyewe ambayo ikimwambia mambo kadha wa kadha. Minong’ono ya ndani ni jambo ambalo linaweza kukusaidia kuvuka kutoka hatua moja kwenda nyingine au inaweza ikakuharibu kabisa. Kila mmoja wetu kwa wakati wake anaweza asiwe anaongea kwa njia ya mdomo kama tunavyofikiria na tukamuona yuko kimya. Lakini kiukweli ndani yake kuna mazungumzo yanaendelea kati yake mwenyewe na hakuna anayesikia. Ikiwa ndani mwa mtu huyu maondezi hasi yatakuwa yakiendelea bila kusema HAPANA kuna wakati atajikuta ni mtu wa kukata tama na kushindwa kufurahia maisha yake ya Kila Siku.Neno Hapana linathibitisha aina ya utashi na nguvu uliyo nayo hata kwa maongezi yako ya ndani na mazungumzo yote yanayoendelea.

3. UTUMIZI WA NENO HAPANA NI ISHARA YA KWAMBA UNAJITAMBUA.
Je umeshawahi kukutana na mtu ambaye kila unachosema yeye anakuitikia ndio tu? Unafikiri wewe utawazaje nafsini mwako? Unapotumia neno HAPANA pale unapopaswa kulitumia na ukalitumia pila kuyumbayumba na kujiuliza ni ishara ya kwamba unajitambua na unatambua nini unahitaji kwa wakati huo, na kitu gani hauhitaji kwa wakati husika. Unapotumia neno hapana pia linatoa utambulisho wako binafsi kwenda kwa upande wa pili. Upande wa pili unapata taarifa kwamba hiki kinawezakana au hiki hakiwezekanai. Ni muhimu kujifunza utumizi wa neno hapana pale panapohitaji, bila kusitasita na kujiuliza mara mbili mbili. Maana utakaposema ndio alafu kile ulichosema ndio hakikutekelezeka kitatoa picha ya namna nyingine kwa upande wa pili na kumbe sivyo ulivyo.

4. UTUMIZI WA NENO HAPANA HUDHIHIRISHA UJASIRI ULIO NAO.
Kila mmoja wetu hapenda kuonekana ni jasiri kwa upande mmoja au mwingine. Kwenye maisha yetu ya kila siku kuna wakati kuna maamuzi ulipaswa kusema hapana lakini wewe ulisema ndio pamoja na maumivu ambayo uliyaona yangekuwa na uwezo wa kuepukika lakini bado ulisema ndio ili kuridhisha mwingine.Unapotumia neno HAPANA pale panapohitajika na kwa wakati sahihi unawaonyesha wengine aina ya ujasiri ulio nao kuelekea mambo mengine mbali mbali ya kimaisha. Maisha ni safari ndefu ambayo haina mjuzi wala mjanja. Maisha ni safari iliyojaa kanuni na taratibu mbalimbali. Unapokiuka sheria na taratibu zake lazima kuna wakati kwenye maisha yako unaweza kuadhibiwa. Ni muhimu kujifunza kanuni na taratibu mbalimbali. Moja ya taratibu hizo ni kuweza kutumia neno HAPANA. Hakikisha unasema hapana pale unapopaswa kusema hapana.


Email : naki1419@gmail.com
+255788454585
God Bless You All
Share on Google Plus

About Gospel Kitaa

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.