SOMO: NITATUMAINI WALA SITAOGOPA - ASKOFU KAKOBESOMO: NITATUMAINI WALA SITAOGOPA

NENO LA MSINGI:

ISAYA 12:2

“Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu; NITAMTUMAINI WALA SITAOGOPA; Maana BWANA YEHOVA ni nguvu zangu na wimbo wangu; naye amekuwa wokovu wangu.”

Tangu katika kitabu cha MWANZO mpaka katika kitabu cha mwisho cha Biblia, UFUNUO, mara nyingi mno Mungu amekuwa akiwaambia watu wake wasiogope. Katika MWANZO 15:1, Mungu alimwambia Abramu, “USIOGOPE, Abramu, Mimi ni ngao yako, na thawabu yako kubwa sana”. Katika UFUNUO WA YOHANA 1:17, Yesu Kristo alimwambia Yohana, “USIOGOPE, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho”. Nyakati zote, Mungu amerudia mara nyingi akiwaambia watu wake wasiogope. Hata leo, ujumbe wa Mungu ni huohuo kwa kila mtu aliyeokoka. Hupaswi kuogopa katika mazingira yoyote. Roho ya woga, haitokani na Mungu bali ni ya shetani. Biblia inasema katika 2 TIMOTHEO 1:7, “Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi”. Biblia inasema katika UFUNUO 21:8, kwamba waoga watatupwa katika ziwa la moto sawasawa na waabudu sanamu, waongo, wachawi, wauaji na wazinzi. Mtu aliyeokoka hapaswi kamwe kuogopa katika mazingira yoyote yanayomkabili. Unapoogopa na kubabaika, unakuwa umeshiriki kufanya mambo matatu ya hatari yanayosababishwa na woga.

MAMBO MATATU YA HATARI YANAYOSABABISHWA NA WOGA

1. KUOGOPA NI KUMPA NGUVU SHETANI YA KUKURARUA:

Shetani ni kama mbwa koko asiye na nguvu yoyote. Anachokifanya mbwa huyu ni kumtishia mtu na kubweka kwa sauti na kuunguruma. Kama mtu akiogopa na kuamua kurudi nyuma, mbwa yule anatiwa nguvu zaidi na kumfukuza mtu yule na hata kumjeruhi. Kama mtu yule asipoogopa na kuendelea kutulia na kutokubabaika, mbwa yule mara moja huamua kukimbia kwa woga mkubwa. Biblia inaeleza jambo hili kwa tukio lililompata Petro katika MATHAYO 14:30, “Lakini alipouona upepo AKAOGOPA, AKAANZA KUZAMA, AKAPIGA YOWE…….” Shetani aliunguruma kwa kutumia upepo mkali kumtisha Petro na aliogopa na kuacha kumtumaini Yesu alimwambia “Njoo”; mara ileile akampa nguvu shetani na akamzamisha majini. Mara nyingi watu waliookoka wameraruliwa na shetani kwa sababu ya woga wao uliompa shetani nguvu ya kuwazamisha. Shetani nguvu zake ni ndogo mno kwa mtu aliyeokoka. Ni nyoka ambaye amepondwa kichwa na kinachopigapiga huku na huku ni mkia tu. Nyoka huyu, alipondwa kichwa na Yesu Kristo pale msalabani, na sisi wote tuliookoka tumepewa amri au mamlaka ya kumponda kichwa, na kumkanyaga wakati wowote [MWANZO 3:15, LUKA 10:19].

2. KUOGOPA NI KUKOSA KUWA NA IMANI

Imani ndiyo ngao ya mtu aliyeokoka ambayo tunaitumia kuizima MISHALE YOTE YENYE MOTO ya yule mwovu. [SOMA WAEFESO 6:16] Mtu aliyeokoka anapoogopa, ni kwamba woga huo, unanyonya imani yote ya mtu huyo na kumuacha tupu; na ndipo mishale ya moto ya shetani inampiga kwa urahisi maana hana ngao yoyote ya kuizima. Angalia maandiko yafuatayo:

MARKO 4:40:

“(Yesu) Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”

MARKO 5:36:

“Lakini Yesu, alipolisikia lile neno likinenwa, akamwambia mkuu wa Sinagogi, Usiogope, amini tu.”

Kamwe, woga na imani, haviwezi kuwa katika furushi moja. Ni lazima woga ufukuzwe, ndipo imani ya kumshinda shetani iendelee kuwapo.

3. KUOGOPA NI KUMDHARAU MUNGU NA NENO LAKE

Unapokabiliwa na magumu yoyote na ukajaa woga na kuanza kubabaika na kukosa matumaini, kwa kufanya hivyo, umemdharau Mungu na Neno lake linalosema katika YEREMIA 32:27, “Tazama, mimi ni BWANA, Mungu wa wote wenye mwili; je! kuna neno gumu LOLOTEnisiloliweza?”

Ukimdharau Mungu na Neno lake, na kuona kwamba Mungu hawezi lolote, hana nguvu, hana uwezo, na kwamba Neno lake siyo kweli; basi ujue uko katika hatari kubwa. Shetani umempa nafsi mwenyewe ya kuendelea kukupiga, ukiwakimbilia waganga wa kienyeji, wachawi, wote hao ni maajenti wake, ndipo utakapopigwa zaidi bila msaada. Umemkataa mwenye nguvu ya kukusaidia kwa kumdharau, na kamwe huwezi kufanikiwa bali unatafuta kuangamizwa.

2 SAMWELI 12:9-10

“Kwa nini umelidharau neno la BWANA……….Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, KWA SABABU UMENIDHARAU“.

HESABU 15:31:

“Kwa sababu amelidharau neno la BWANA……….mtu huyo atakatiliwa mbali……….”.

HATUPASWI KUOGOPA, MUNGU MWENYE NGUVU YUKO PAMOJA NASI.

Yeye mwenye nguvu na uwezo wote yuko upande wetu watu tuliookoka. Kwa nini uogope? Kwa nini usimtumaini?

MWANZO 26:24, “…………… Usiogope, maana mimi ni pamoja nawe ………”

ISAYA 41:10, “Usiogope, kwa maana mimi ni pamoja nawe; usifadhaike, kwa maana mimi ni Mungu wako; nitakutia nguvu naam nitakusaidia, naam, nitakushika kwa mkono wa kuume wa haki yangu”.

TUNAPASWA KUMTUMAINI MUNGU NA KUMWOMBA
Tunapokabiliana na mazingira yoyote ya maisha, iwe ni mateso mwilini, magonjwa kwa watoto na ndugu, hali mbaya ya kibiashara, masimango kazini, kutokufanikiwa kikazi au masomoni, vitisho vya wachawi kwamba watatuua, au mazingira yoyote yale magumu, hatupaswi kuogopa bali kutumaini na kumwomba BWANA. Yeye ana nguvu za kutushindia. [SOMA ZABURI 31:13-15, ZABURI 3:4,6] Tutaendelea kumwomba BWANA kwa kutumaini huku tukiwa na moyo imara, na lazima tutawaona watesi wetu wakishindwa.

ZABURI 112:7,8:

“Hataogopa habari mbaya; moyo wake u imara ukimtumaini BWANA. Moyo wake umethibitika hataogopa, hata awaone watesi wake wameshindwa”.

KUNA BARAKA KUU KATIKA KUMTUMAINI BWANA ALIYETUOKOA

ISAYA 57:13:

“……. Anayenitumaini ataimiliki nchi, na kuurithi mlima wangu mtakatifu”.

MISTARI YA KUIWEKA MOYONI

ZABURI 91:2:

“Nitasema, BWANA ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini”.

KUTOKA 14:13-14:

“Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa BWANA atakaowafanyia leo; kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele, Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza kimya.”

ZABURI 20:7:

“Hawa wanataja magari na hawa farasi, bali sisi tutalitaja jina la BWANA, Mungu wetu.”Je! kuna jambo lililo gumu linalokukabili katika maisha yako? Je, ni ugonjwa ulioshindikana? Je ni vitisho vya Uchawi au kuachiwa “laana” na wazazi kwa ajili ya kuokoka? Je ni kutishwa kufukuzwa na mumeo au nduguzo sababu ya wokovu? Je ni masomo magumu? Je ni kukosa mtoto? Je ni vitisho vya kufukuzwa kazi? Je ni vitisho kwamba hutafanikiwa katika biashara yako? Ni nini? USIOGOPE, SIMAMA TU UKAUONE WOKOVU WA BWANA. Iambie nafsi yako na jirani yako pia, “NITAMTUMAINI, SITAOGOPA.”

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.