SOMO: NITAWEZAJE KUISHINDA ZINAA - MCHUNGAJI MADUMLA


Na Mchungaji Gasper Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…

Kati ya dhambi yenye kusumbua watu wengi leo katika jamii ya watu mbali mbali tena hata kwa wapendwa makanisani ni dhambi ya zinaa,ambayo ni dhambi yenye matokeo mabaya kuliko dhambi ziwayo zote ingawa dhambi zote zi sawa. Hukumu ya dhambi zote ni katika ziwa la moto,hivyo dhambi zote zinafanana katika hukumu,lakini dhambi hutofautiana kwa matokeo yake kwa kila dhambi.

Mfano matokeo ya mtu adanganyaye ni tofauti na matokeo ya mtu afanyaye zinaa sababu dhambi nyingine hazihusishwi na agano isipokuwa zinaa. Matokeo ya dhambi yenye kufungamanishwa na agano ni mabaya sana,sababu agano linadai uhalali wa ile dhambi. Mfano mtu yeyote alalaye na mwanamke asiye mke wake,watu hawa huungamanishwa kwa lile tendo la zinaa,nao huwa mwili mmoja. Ndivyo ilivyoandikwa;

” Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. ” 1 Wakorintho 6:16

Kinachomfanya mtu kuungwa na mwingine ni agano lililopo kati ya wawili kuwa mmoja,agano lina nguvu ya kuyaleta mawili na kuyaunganisha kuwa ni mamoja.Kumbuka pia agano linaweka mshabiano wa tabia za wawili kufanana.

Ndio maana hata kwa wanandoa kwa kipindi fulani hufanana tabia hata sura zao pia.(Tazama mke na mume si wawili tena bali ni mwili mmoja,Mwanzo 2:24 ).Agano hili linakamilishwa na la tendo la kujamiiana. Mtu akijiungamanisha na kahaba,ujue naye atakuwa ni kahaba tu,sababu ya agano.

Tazama mfano mwingine wa matokeo ya dhambi hii yenye agano la wawili kuwa mmoja. Biblia inasema;

” Yesu akamwambia, Nenda kamwite mumeo, uje naye hapa. Yule mwanamke akajibu, akasema, Sina mume. Yesu akamwambia, Umesema vema, Sina mume; kwa maana umekuwa na waume watano, naye uliye naye sasa siye mume wako; hapo umesema kweli. ” Yoh.4:16-18

Huyu mwanamke si kana kwamba aliolewa na wanaume wote sita kama vile wanawake wanavyoolewa leo kanisani kisha sherehe,hapana. Bali alishiriki zinaa na wanaume hao sita. Kwa kitendo cha kujamiiana na wanaume hao sita,tayari kimewaunganisha kuwa mwili mmoja ingawa hakuolewa nao.

Kwa sababu ya agano liliopo kati yao,wanaume hawa wana haki ya kudai uhalali wa dhambi ya zinaa kwa mwanamke huyo,hata kama yeye hataki. Hapo ndipo mwanamke wa namna hii hujikuta akiendelea kushiriki nao zinaa ingawa hapendi kabisa,kwa sababu ya ile nguvu ya agano la zinaa.

Hali ya namna hii imewakamata watu wengi mno si wanawake,wala wanaume,wote wote. Na ndio maana unakuta mtu hufanya zinaa,mpaka inafika wakati kila mmoja anamshangaa tena mtu mwengine hataki kabisa zinaa lakini hujikuta akiendelea kufanya hali akiugua moyo wake sana.

Huko makanisani ndio hali inatisha hivi sasa,maana wengine hawapendi kufanya zinaa ila wanajikuta wakishiriki alafu baadae wanajutia kwa toba fulani hivi,alafu tena kesho yake hufanya. Kwa hiyo imekuwa kama kamchezo fulani hivi ka kuigiza.

Ndiposa mtu mmoja alipoona yamemshinda,maana kila alipojaribu kuacha zinaa hakufanikiwa akauliza nitawezaje kuacha zinaa?

Swali la namna hili limekuja kwa sababu ya mtu ambaye amejaribu kuacha dhambi ya zinaa lakini ameshindwa,kila akijaribu anajikuta akinguka katika dhambi hiyo hiyo ya zinaa,mtu huyo anaweza akawa ni wewe. Maana zinaa si lazima kufanya manualy bali hata kwa kuwaza tu katika hali ya kumtamani mwanamke/mwanaume.

Kwanza,waweza kujiuliza mbona natumia neno zinaa na nisitumie neno uzinzi,au uasherati katika maelezo yangu yote ya hapo juu.

Jibu linapatikana endapo tutajua ni nini maana ya zinaa,uzinzi na uasherati. Na tufanyeje basi kuyaacha haya yote maana ni dhambi za machukizo kwa Bwana.

ZINAA.

Neno zinaa linawakirisha uzinzi na uesharati. Hivyo mtu asemapo zinaa ni sawa na kusema ” uzinzi na uesharati.” Katika maelezo yangu mahali pote nimezungumzia zinaa nikiwa na maana ya uzinzi na uesharati.Sasa Uzinzi ni nini? Na uesharati ni nini?

UZINZI.

~Uzinzi ni tendo la kujamiana kwa mwanandoa na yule asiyekuwa na ndoa. Mfano mwanamke mwenye ndoa akichepuka kwa kujamiana na mwanaume asiyeoa basi mwanamke huyu amezini. Alikadhalika kwa mwanaume ni vile vile kwamba mwanaume mwenye ndoa akichepuka akazini na mwanamke asiye na ndoa basi… …mwanaume huyo amezini.

Sasa hiyo ni maana ya kwanza ya uzinzi. Maana ya pili ni mwanaume au mwanamke mwenye ndoa akajamiana na mwanaume au mwanamke mwenye ndoa nyingine Mfano. Mwanaume katika ndoa akatoka akalala na mke wa mtu,basi mwanaume huyu huitwa mzinzi. Mwanamke naye ni vivyo hivyo.

” Basi wakati awapo hai mumewe, kama akiwa na mume mwingine huitwa mzinzi. ” Warumi 7:3a

Hivyo uzinzi ni lazima uhusishe ndoa~kwamba mmoja katoka katika ndoa yake,naye mtu huyo huitwa mzinzi. Uzinzi katika biblia una maana mbili, maana ya kwanza ndio hiyo iliyopo katika zinaa.

Maana ya pili ya uzinzi ni ile hali ya kumuacha Bwana ambaye Yeye Bwana amekuwa kama mume kwetu sababu tuna agano naye katika Kristo Yesu. Ikiwa kama tutaiacha imani yetu kwake Mungu,basi tumekuwa wazinzi ( Warumi 7:3-4) pia tunasoma ;

” Ingawa wewe, Israeli, unafanya uzinzi, lakini asiasi Yuda; nanyi msiende Gilgali wala msipande mpaka Beth-Aveni, wala msiape mkisema, Aishivyo Bwana. ” Hosea 4:15

UASHERATI.

Ni hali ya kujamiana kwa yule asiyekuwa na ndoa kwa asiyekuwa na ndoa mwenzake au hata yule asiyekuwa na ndoa kujamiiana kwa mwenye ndoa.

Mfano. Binti au kijana wa kiume akijamiiana na mtu mwenye ndoa au siyekuwa nayo,basi binti huyu au kijana huyu huitwa mwesharati.

Zinaa inayo dawa,ambayo kwa dawa hiyo utaweza kuishinda kabisa. Hizi nikupazo hapa chini ni dawa zitakazoweza kukufanya uwe mbali na uzinzi na uasherati ukiwa umeokoka kwanza.

Na ikiwa bado hujaokoka basi anza kuokoka kwa kumpokea Bwana Yesu Kristo,awe Bwana na mwokozi wa maisha yako kwa kutubia dhambi zako zote sawa sawa na atakavyoongozwa na mchungaji wako na kuombewa,kisha ndipo utumie dawa hizi hapa chini;

Kuikimbia zinaa. 1 Wakorintho 6:18.

~ Kuikimbia zinaa ni kujitenga mbali na mtu anayekufanya udondoke katika zinaa pia ni kujitenga na kila aina ya mazingira hatarishi,na tabia zote hatarishi.

Mfano; Wewe ni kweli umeokoka na unampenda Mungu,lakini bado una namba za simu za aliyekuwa boy friend au girl friend wako wa zamani ambaye wala sio mchumba kusema mtaoana kwa sasa.

Sasa kipindi hicho mlipokuwa duniani mlikuwa mkifanya dhambi ya uasherati,lakini sasa umeokoka na bado una mawasiliano yake ya karibu~ anakupigia,nawe wampigia~ tena umejidanganya kwamba utamuombea ili abadilike lakini ukaribu wenu unaamsha hisia za kipindi kile cha uasherati,gafla unajikuta badala ya wewe kumbadilisha,wewe ndio unabadilishwa imani yako kwa uasherati.

Au mke umeolewa na mume mwingine lakini bado una mawasiliano ya karibu na aliyekuwa akikutaka kukuoa na huko nyuma alikuchezea,bahati nzuri ukaolewa na mwingine aliyeletwa na Bwana. Kumbe! Mawasiliano yenu ya ukaribu yanawasogeza karibu,hatimaye unaanguka katika dhambi ya uzinzi.

Na mwanamume naye ni vivyo hivyo,kwa yule mwenye mawasiliano ya karibu naye anaweza kudondoka katika uzinzi.

Ujitenge mbali na mazingira chochezi pamoja na tabia. Mfano leo kumeibuka makanisani tabia ya kutaniana taniana kitamaa kati ya binti na mwanaume.

Wengine hudiliki hata kushikana shikana wakati wakitembea au hata kama wamekaa. Mambo haya ni machukizo ambayo hupelekea kufikiria zinaa kwamba ” ….aahaa tuzini kidogo alafu tutatubu bhana…” Hatua hii ya kwanza ni ya kuishinda zinaa ni kukimbia kama ukoma…

Bwana Yesu asifiwe…

Njia ya pili ambayo itakuwezesha kuishinda zinaa ni;

Kujitengamanisha na roho ya zinaa.

~Wapo watu ambao wamefungamanishwa na roho za zinaa pasipo kujijua,wanajikuta wakiwaka tamaa katika miili yao. Mfano shetani anaweza akawa amekutafuta katika kila kona ya maisha yako akuangushe,akiona amekushindwa anajaribu akuletee zinaa,hapo sasa anakuja binti/kijana mwenye vishawishi vya hali ya juu akikuanzia mbaliiii kiasi kwamba huwezi kumshtukia kwa haraka na anajua ya kwamba ukidondoka katika dhambi hii si rahisi kuinuka mara moja ikiwa hujadhamilia kikamilifu kwa sababu ya uwepo wa agano la zinaa.

Watu wengi wanazini na kufanya uasherati si kana kwamba wana penda,wengine ni miroho michafu ya zinaa inawasukuma kufanya. Mfano unaweza kukuta binti alinayedondoka dhambini mara kadha wa kadha na ukimuuliza anakujibu ya kwamba hata yeye mwenyewe hajui kwa nini amezini na mtu huyo.

Hili ni tatizo kwa watu wengi,kukumbwa na roho za zinaa. Kanisa la leo nalo limevamiwa na roho ya zinaa,baadhi ya watumishi wamedondokea huko. Dawa ni kujitengamanisha mbali na roho za zinaa,kwanza kwa kuchukia dhambi hii. Kisha kumsihi Roho mtakatifu achukue nafasi ya kuziondoa roho hizi,katika maombi rasmi kabisa ya kuvunja nira ya roho ya zinaa.

Kukaa uweponi mwa Bwana.

~ kukaa uweponi ni hali endelevu ya kudumu katika fundisho muda wote hata kama ukiwa unafanya kazi zako binafsi lakini muda wako mwingi una mawasiliano na Mungu. Ni hali ya kushughurika na mambo ya Mungu katik kiwango cha juu. Mtu yeyote mwenye ushirika na Bwana Mungu ni mtu aliyekaa uweponi.

Mfano mdogo ni huu; kama vile bawabu ilivyoungamanishwa na mlango wa chumba. Kiasi kwamba ukiingia chumbani yenyewe unaikuta pale pale,na hata kama ukitoka bado unaikuta pale pale imengangana katika mlango wa chumba,ndio maana Daudi akasema;

” Hakika siku moja katika nyua zako Ni bora kuliko siku elfu. Ningependa kuwa bawabu nyumbani mwa Mungu wangu, Kuliko kukaa katika hema za uovu. ” Zab.84:10

Sasa,ukiweza kujibidiisha kukaa uweponi mwa Mungu kama bawabu ilivyoshikamanishwa na mlango,ndivyo mawazo ya zinaa hukosa nafasi na ndivyo hata roho za zinaa hukosa mlango w kukuvamia. Siku zote roho chafu hukaa mahali pachafu,ikiwa hema ya moyo wako ni safi basi ni dhahili kabisa hakutakuwa na zinaa yoyote ile itakayotajwa kwako.

Shida kubwa ni kwamba watu wengi wapo uvugu uvugu katika imani zao,kwa hali ya kuwa uvugu uvugu kwamba unaamini lakini huku bado unaonja onja dhambi hapo ndipo zinaa nayo inakungangania. Bali dawa ya yote hayo ni kukaa uweponi full time.

Ikiwa roho ya zinaa imekukamata kiasi kwamba umejaribu kukimbia lakini hukufanikiwa,tafadhali nipigie basi ili tuombe pamoja ili Bwana akuhudumie.
Kwa huduma ya maombi nipigie sasa kwa namba 0655111149.
Mchungaji Gasper Madumla.
Beroya bible fellowship church.(Kimara,Dar-TZ)
UBARIKIWE.

Share on Google Plus

About Ambwene Mwamwaja

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.